Vazi la Harusi

(Mathayo 21-22)
Swahili
Year: 
2011
Quarter: 
2
Lesson Number: 
11

 

Utangulizi: Mathayo 21 ina visa ambavyo vinafunua kuwa Mungu ana maadui miongoni mwa wanadamu. Tatizo la hawa maadui ni kwamba mwanzoni hawaonekani kuwa wapinzani, wanaonekana kuwa wategemezaji/wasaidizi. Juma lililopita tulijifunza kisa cha mwana mpotevu  na kujifunza kuwa wokovu wa mwana mkubwa “mwema” ulikuwa kwenye hati hati. Visa vyote havijatukalia vizuri sisi Wakristo “wema,” na vinatusukuma kuielewa injili vizuri zaidi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuwe na uhakika kwamba hatupo kwenye kambi ya  maadui wa Mungu!

 

I. Majibu Mawili

A. Soma Mathayo 21:28-29. Kama Yesu anaelezea kisa cha Ufalme wa Mbingu, je, huyu ni mtu wa aina gani? (Mtu ambaye anamkataa Mungu, lakini baadaye maishani anabadili mawazo yake na kumfuata Mungu.)

B. Soma Mathayo 21:30-31. Je, huyu ni mtu aliyemo kanisani? (Huyu ni mtu anayekubali kuwa mfuasi wa Yesu, lakini aidha anasema uongo kuhusiana na hilo au baadaye anabadili mawazo yake.)

1. Je, unakubaliana na jibu lililotolewa na wasilikizaji wa Yesu?

2. Kama unakubaliana na hili jibu, inawezaje kuwa kweli kwamba watoza ushuru na makahaba wanaingia kwenye Ufalme wa Mbingu? Hawa sio watu wanaofanya mapenzi ya Mungu! Au, je, wanafanya?

C. Soma Mathayo 21:32. Je, ni aina gani ya “kufanya mapenzi ya Mungu” wanayoweza kudai makahaba? (Awali tulipoanza hiki kisa, suala lilikuwa ni kufanya kazi kwenye shamba la mzabibu. Sasa, tunaitafuta “kazi” angalao kwa kuanzia – ni kuamini na kutubu.)

1. Tatizo kwa wale ambao hawakumwamini Yohana Mbatizaji ni lipi? (Hawakuamini kile alichokizungumzia Yohana “njia ya haki.”)

a. Je, hiyo inapaswa kutufundisha nini? (Kwamba ni muhimu kuwa na uelewa sahihi wa njia ya haki ya Mungu. Watu ambao ungewatarajia kuielewa na kuikubali hawakufanya hivyo. Badala yake watu ambao hawakutarajiwa waliielewa na kuikubali.)

b. Je, njia ya haki ni ngumu kuielewa? Je, ni kama hesabu ngumu? (Hapana. Tatilo lilikuwa ni mojawapo ya imani, sio tatizo la uelewa.)

II. Mwaliko wa Awali

A. Soma Mathayo 22:1-2. Je, tunataka kujifunza nini hivi punde? (Jibu la swali tulilojadili hivi punde lilikuwa la msingi sana – njia ya haki ya Mungu ni nini?

B. Soma Mathayo 22:3-5. Je, hawa watu walioalikwa ni marafiki wa Mfalme? (Labda. Wanachukuliwa kustahili kualikwa kwenye sherehe ya harusi ya mwana wa Mfalme. Kwa hakika Mfalme ana uhusiano nao wa aina fulani.)

1. Je, Mfalme anasimamia/anatilia mkazo mwaliko wake? (Ndiyo. Anawakaribisha mara mbili. Alipaswa kujisikia kufedheheswa kwa kukataa kwao kwa awali, lakini badala yake anarudia tena mwaliko.)

2. Kwa nini marafiki wa Mfalme wanamkatalia? (wana mambo mengi sana ya kufanya kuhusiana na shughuli nyingi za maisha yao. Biashara zimeteka mawazo yao.)

C. Soma Mathayo 22:6. Je, hawa “marafiki” wana mtazamo wa aina gani? (Hawaenendi kama marafiki. Wanawatenda vibaya na kuwaua watumwa wa Mfalme.)

1. Je, unamtendeaje mchungaji wa kanisa lako? Vipi kuhusu viongozi/maafisa wa kanisa?

2. Je, unaweza kuelezeaje kile “marafiki” walichokifanya? (Walijisikia kusumbuliwa/kubughudhiwa na kukasirishwa na mwaliko wa mfalme.)

D. Soma Mathayo 22:7. Mfalme inawezekana alikuwa mvumilivu na si mwepesi wa hasira, lakini je, yeye ni mdhaifu? (Hapana. Anatekeleza adhabu kwa “marafiki” wake walioenenda kama maadui.)

1. Kisa cha Yesu kinaelezewa muda mfupi kabla ya kuteswa/kusulubiwa kwake. Je, kisa hiki kinaashiria nini mawazoni mwetu? (Viongozi wa dini walimtuhumu Yesu na wakashauri mamlaka ya Kirumi imuue. Muda mfupi baada ya hapo, mji wao, Yerusalemu, uliharibiwa/iliangamizwa na Warumi.)

III. Mwaliko wa Pili

A. Soma Mathayo 22:8. Kwa nini wale walioalikwa “hawakustahili” kuja? (Hawakujisikia kuja. Au, hawakujisikia kuja na badala yake walijisikia kufanya masuala mengine yahusuyo maisha yao.)

B. Soma Mathayo 22:9-10. Orodhesha njia ambazo hili kundi jipya la wageni waalikwa linatofautiana na kundi la wageni waalikwa wa kwanza? (1. Mfalme hawafahamu. 2. Sio watu wa kawaida kualikwa kwenye sherehe ya Mfalme kwa sababu hakuna kitu chochote maalum kuwahusu. Ni mchanganyiko wa kundi la watu wema na waovu. 4. Wako radhi kuja.)

1. Kati ya hizo tofauti nne, ipi iliyo ya muhimu zaidi? (Wako radhi kuja!)

C. Soma Mathayo 22:11-12. Muda mfupi uliopita tulijifunza hiki kisa na niliita kundi la pili la wageni waalikwa kuwa "Walmart shoppers" (Yaani wanunuzi wa kwenye maduka kama ya Kariakoo). Kwa nini huyu mtu “atekewe” (bila kuwa na kisingizio) kama alikwenda moja kwa moja kwenye sherehe ya harusi akitokea Kariakoo? (Njia pekee hii inaweza kuleta mantiki kama Mfalme alikuwa anatoa mavazi ya harusi kwa hawa wageni wote. Kwa wazi kabisa, hakuna mnunuzi hata mmoja wa Kariakoo anayevaa vazi lake la harusi ya kifalme na kwenda nalo kufanya manunuzi!)

IV. Uchambuzi wa Awali

A. Tuna taarifa za kutosha kuhusu maana ya injili, njia ya uzima wa milele. Kama ukiweka kisa chetu cha kwanza kuhusiana na wana pamoja na kisa cha pili kuhusu sherehe ya harusi, je, jibu gani la pamoja tunalolipata kwenye swali: “Je, ninaingiaje kwenye uzima wa milele?” (Katika miktadha yote miwili, suala la msingi lilikuwa ni kwenda/kuja. Kwenda kufanya kazi kwenye shamba la mzabibu. Kwenda kwenye sherehe ya harusi.)

B. Kama suala la kivitendo, je, inamaanisha nini kwa sisi “kwenda/kuja” kwa Mungu?

1. Huenda njia rahisi ya kukabili suala hili ni kubainisha kinachohusisha kutokuja/kutokwenda kwa Mungu . Nini kilichowazuia watu wasimwendee Mungu kwenye visa viwili tulivyojadili hivi punde?

a. Hebu tuanze na kisa cha wana wawili. (Kuliongelea tu haikuwa inatosha. Ulipaswa kutenda jambo fulani kuhusiana nalo. Kwa hakika, kuliongelea yaweza kuwa ni mtego. Kama unasema kuwa unakuja, lakini huji, unaweza kuwa umejipotosha. Kwa kiwango cha chini, chochote kile walichosema wale wana hakikuhusiana kabisa na matokeo.) 

b. Vipi kuhusu kisa cha sherehe ya harusi?  (Mathayo 22:5 inatuambia kuwa kutokumjali/kumpuuzia Mungu, kuweka kazi zetu au biashara zetu mbele dhidi ya Mungu, ni kikwazo cha kotokuja. Mathayo 22:6 inatuambia kuwa uhasama kwa mawakala wa Mungu ni kikwazo cha kutokuja.Wanunuzi wa Kariakoo hawakuwa na uhasama kwa wasaidizi wa Mfalme, na walifurahiwa zaidi na sherehe ya haruzi kuliko wanavyofanya manunuzi Kariakoo.) 

c. Kwa hiyo, suluhisho letu kuhusu kile ambacho “kuja” kwa Mungu inamaanisha ni: a) Inamaanisha kutenda, sio kuzungumza tu; na b) Inamaanisha kuwa na mtazamo sahihi – kuwa radhi kumweka Mungu wa kwanza.

 

V. Kusalia Kwenye Ukaribisho
 
A. Soma tena Mathayo 22:11-13. Huyu ni mgeni mchunguzi sana. Aliitikia wito wa Mfalme, akaondoka Kariakoo, na kuja kwenye sherehe ya harusi. Lakini alitupwa nje katika “giza.” Je, tunaweza kuupoteza wokovu wetu? (Kama kuja kwenye sherehe kunamaanisha kuokolewa, basi huyu bwana “hakuokolewa.”)
 
1. Je, tunaepukaje majaaliwa ya huyu mtu? (Kufikiria kwamba mavazi yetu ya Kariakoo ni mazuri vya kutosha. Tunahitajika kukubali zawadi ya bure ya vazi la haki la Mfalme.)
 
2. Hebu mfikirie huyu mtu kidogo. Anaweka mwaliko wa Mfalme juu ya biashara yake, hakuwa na uhasama na mawakala wa Mfalme, alikuja kwenye sherehe ya harusi. Alifikiria tu kwamba haki yake ilikuwa bora vya kutosha. Je, maelezo haya yanaweza kuwa yanakuelezea wewe?
 
VI. Uchambuzi wa Mwisho 
A. Soma Mathayo 22:14. Kama ungekuwa unafanyia kazi hili chapisho kwa kushirikiana na Mathayo, je, ungesema nini kuhusu usahihi wa hii kauli? (Sehemu ya kwanza ni sahihi – watu wa aina zote walialikwa kwenye sherehe ya harusi ya Mfalme. Lakini, sehemu ya mwisho ina makosa ya wazi kabisa – Mfalme alimchagua kila mtu. Hata pia aliwaalika wanunuzi wa Kariakoo! Kwa vile tunajua kuwa Biblia ni Neno la Mungu la uhakika, je, unaelezeaje hili? (Njia pekee hii inaleta mantiki yoyote ni kusema kuwa “Mungu anawachagua wale wanaochagua kuja kwake.”) 
1. Kwa kuzingatia kile tulichojifunza, je, njia ya uzima wa milele ni ipi? (1. Kutubu (uamuzi wa kuweka mwaliko/wito wa Mungu juu ya matamanio yetu ya ubinafsi); 2. Kuja (kuitikia mwaliko/wito wa Mungu, kuwa na mtazamo sahihi; na 3. Kukubali vazi la Mungu la haki (kutegemea haki ya Yesu badala ya haki yako).)
 
B. Soma Mathayo 22:15. Je, unaelezeaje hii? (Yesu alikuwa anaharibu hadhi yao maalum. Walikuwa wachaguliwa. Yesu anawakubali wanunuzi wa Kariakoo wanaokuja kwake.)
 
C. Rafiki, unaweza kudhani kuwa wewe ni rafiki wa Mfalme, unaweza kudhani kuwa wewe ni mtu maalum sana, lakini haya mafumbo (hivi visa) yanaonyesha kuwa kuongea hakumaanishi kitu chochote. Mtazamo mbaya ni kikwazo. Mtazamo wako wa kuweka mambo ya Mfalme mbele, kukubali wito/ukaribisho wake, na kukubali vazi lake la haki ndio ufunguo. Je, utatubu, hivi sasa na kuingia kwenye Ufalme wa Mungu?
 
VII. Juma Lijalo: Vielelezo Zaidi vya Mavazi