Somo la 2: Katikati ya Vinara vya Taa
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, ungependa kufahamu mustakabali wako? Wasiwasi ni kwamba unaweza usiupende mustakabali wako! Somo letu juma hili linatumia njia tofauti kidogo. Badala tu ya kutupatia taarifa juu ya mustakabali wetu, linatuambia kwamba mustakabali wetu uko mikononi mwa Yesu, ambaye sio tu kwamba anao uwezo wote, bali pia anatujali na kututunza. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!
- Maisha ya Yohana
-
- Soma Ufunuo 1:9. Maisha ya Yohana yakoje katika kipindi hiki? (Anasema kuwa anashiriki na Wakristo wengine katika mateso yao. Hii haitoi taswira ya furaha.)
-
-
- Yesu anasema jambo gani chanya? (Hajisikii upweke. Yeye ni “ndugu yetu na mshirika wetu” katika Ufalme wa Mungu.)
-
-
-
- Yohana anaandika juu ya “subira katika ustahamilivu.” Tunawezaje kuwa na subira hiyo ikiwa tunateseka kama yeye? (Anasema kuwa Yesu atatupatia uvumilivu.)
-
-
-
-
- Endapo ungekuwa unateseka, ungemwomba nini Mungu? (Ningemwomba aniondolee mateso! Tunapaswa kujifunza jambo fulani hapa. Wakati mwingine tunatakiwa kuomba uvumilivu na uwezo wa kustahamili mateso.)
-
-
-
- Angalia tena sehemu ya Mwisho ya Ufunuo 1:9. Kwa nini Yohana anapata mateso? (Si kwamba ametenda jambo lolote baya. Anasema ni kwa sababu ya “neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu.”)
-
-
- Yohana anamaanisha nini anapoandika kwamba matatizo yake yanatokana na ”neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu?” (Anapata mateso kwa sababu amekuwa akimshuhudia Yesu. Amekuwa akifuata amri ya Mungu iliyoandikwa kwenye Mathayo 28:18-20.)
-
-
-
- Unapokuwa kwenye mateso, je, huwa unauliza swali la “kwa nini?” Je, hii ni kwa sababu ya jambo fulani nililolitenda vibaya? (Ingawa nimewaona baadhi ya watu ambao wanajilaumu bila sababu, mara nyingi inaonekana kwamba wale wanaopitia mateso huwa hawaulizi swali hili. Kwa kuwa hawaulizi swali hili, hawajifunzi kuepuka mambo hayo yanayowasababishia mateso.)
-
-
- Bado hatujajadili nini hasa kilicho kiini cha tatizo la Yohana. Je, unafahamu kile anachokizungumzia? (Ukiangalia tena Ufunuo 1:9 Yohana anasema kuwa yupo katika kisiwa cha Patmo. Yohana hayuko likizo akifurahia jua na mchanga wa kisiwa hiki kilichopo kwenye eneo la kitropiki, hii ni adhabu ya kikoloni. Yupo hapo kama mfungwa wa Rumi. Kosa lake? Kupeleka injili juu ya habari za Yesu.)
- Siku ya Bwana
-
- Soma Ufunuo 1:10 na Yohana 5:9-10. Ikiwa hii ni Sabato ya siku ya saba, kwa nini Yohana haiiti hivyo?
-
-
- Soma Yohana 20:19-20. Ikiwa hii ni Jumapili, siku ya kwanza ya juma, kwa nini Yohana haiiti hivyo katika Ufunuo 1:10?
-
-
-
- Soma 1 Wakorintho 11:20. Hapa ndipo mahala pekee katika Agano Jipya ambapo neno la Kiyunani lililotumika kwenye Ufunuo 1:10 (kuriakee – likitafsiriwa kama “ya Bwana”) linapatikana. Je, hii inatoa mwanga wowote juu ya siku ambayo Yohana anaizungumzia? (Maoni ya watu kadhaa niliyoyasoma yanasema kuwa kuna uwezekano mkubwa Yohana anazungumzia siku ya Jumapili, lakini sioni msingi wowote kwenye Biblia kwa ajili ya hitimisho hilo. Ukiangalia mahali kwingineko kote ambapo Yohana anairejea Sabato, inahusiana na Yesu kufanya uponyaji siku ya Sabato. Suala la usahihi wa kufanya hivi katika siku ya Sabato linaleta mgogoro kwa viongozi wa Kiyahudi. Hivyo, itakuwa jambo la kawaida kabisa kwa Yohana kuandika “Sabato” kwa muktadha huo, pasipo kuiita Jumamosi kuwa ni Sabato katika miktadha mingine.)
-
-
- Soma Kumbukumbu la Torati 5:12-15. Sabato inaadhimisha nini hapa? (Watu wa Mungu kuwekwa huru dhidi ya serikali iliyoamuru utumwa.)
-
-
- Taswira ya Robertson katika Agano Jipya inatuambia kwamba mfumo wa hili neno la Kiyunani lililotafsiriwa kama “ya Bwana” kwa kawaida lilitumika kurejelea Rumi ya kifalme, kama vile “fedha za kifalme na hazina ya kifalme.” Mantiki iliyopo ni kwamba Mungu anamiliki siku. Ukweli kwamba Yesu alipumzika kaburini siku ya Sabato, ukweli kwamba Sabato inaakisi uhuru dhidi ya utumwa ulioamriwa na serikali, inaweza kuwa imemfanya mtu ambaye amewekwa kizuizini na serikali aizungumzie Sabato kama kipindi ambacho anaweza kuwa na Mungu – “siku ya Bwana.”)
-
- Maono
-
- Soma Ufunuo 1:10-11. Ujumbe wa kitabu hiki unaelekezwa wapi? (Kwenye makanisa saba. Haya yalikuwa makanisa ya Kikristo yaliyokuwepo katika kipindi hiki.)
-
- Soma Ufunuo 1:12-15. Hii inamwelezea nani?
-
-
- Ni nani “afananaye na mwanadamu?” (Soma Mathayo 9:4-6 na Danieli 7:9. Yesu anajizungumzia mwenyewe kama “Mwana wa Adamu.” Mwitiko wetu wa kwanza ni kwamba taswira hii inaonekana kama ni Mungu (“Mzee wa Siku” wa Danieli), lakini huyu ni Mungu ambaye anaonekana kama mwanadamu, hivyo hiyo inatuambia kuwa lazima huyu anayeongea na Yohana atakuwa ni Yesu.)
-
-
- Soma Ufunuo 1:16. Umewahi kumsikia mtu katika Biblia aliye na upanga utokao kinywani mwake? (Soma Ufunuo 19:13-15, ambapo tunaona rejea yenye kufanana na hiyo. Katika Yohana 1:1 hapo awali Yohana alimrejea Yesu kama “Neno.” Hii inathibitisha kwamba Yohana anamwelezea Yesu.)
-
-
- Je, si jambo zito kueleweka kuwa na upanga utokao kinywani mwako? (Upanga unapaswa kuwa mikononi mwako, na si mdomoni mwako. Hapa ishara ni kwamba Yesu hana haja ya kupambana kwa mikono yake. Anahitajika kutamka tu na anaweza kuwashinda maadui wake.)
-
-
-
- Badala ya kushikilia upanga mkononi mwake, Yesu anashikilia “nyota saba.” Vinara hivyo ni vitu gani, na kuvishikilia inamaanisha nini? (Soma Ufunuo 1:20. Nyota saba ni malaika au wajumbe wa makanisa saba. Taswira ya Yesu kuzishikilia inamaanisha kwamba ana shughuli nazo maalumu. Hivyo, Yesu amewekeza binafsi kwa malaika wanaotenda kazi na haya makanisa saba.)
-
-
-
-
- Je, unadhani kuwa malaika amepewa jukumu la kuliangalia kanisa lako?
-
-
-
- Soma tena Ufunuo 1:12. Kwa kuwa sasa tumeshasoma juu ya habari hii, inaashiriwa nini kwa Yesu kuwa “kati ya vinara saba?” (Ufunuo 1:20 inavibainisha vinara saba kama makanisa saba. Hivyo, tunaona mwelekeo kamili wa Yesu na kazi yake kwa ajili ya kanisa lake. Sio tu kwamba anawamiliki wajumbe wa mbinguni kwa makanisa hayo yaliyo mkononi mwake, bali yupo yeye binafsi.)
-
- Soma Ufunuo 1:17. Kwa nini Yohana alizimia alipomwona Yesu? (Hii inaonesha mwonekano wa Yesu wa kupendeza na wa kutisha. Yohana anaanguka chini.)
-
-
- Yesu anafanya nini Yohana anapozimia? (Anamliwaza.)
-
-
- Soma Ufunuo 1:18. Je, hii ni sehemu ya ujumbe wa faraja wa Yesu kwa Yohana? (Yesu anayo mamlaka yote, na hili linapaswa kutufariji, kwa kuwa anatupenda.)
- Kanisa la Efeso
-
- Soma Ufunuo 2:1. Chanzo cha ujumbe huu ni nani? (Kutokana na kile tulichojifunza hivi punde, ni Yesu!)
-
- Soma Ufunuo 2:2-3 na Ufunuo 2:6. Kanisa hili limetenda mambo gani? (Limestahamili, limetenda kazi kwa bidii, na limechukua hatua kujaribisha ujumbe wa wale wanaodai kuwa viongozi sahihi. Limekataa matendo ya Wanikolai.)
-
- Soma Ufunuo 2:4-5. Kanisa hili limeshindwa kufanya nini? (Limeuacha “upendo [wake] wa kwanza.”)
-
-
- Hili ni tatizo kubwa kiasi gani? (Yesu anatishia kuondoa kinara chake.)
-
-
-
-
- Hii inazungumzia nini kuhusu bidii ya kazi, ustahamilivu na fundisho safi? (Haya hayatoshi.)
-
-
-
-
-
-
- Fikiria kinyume chake: Yesu anasema ninashukuru kwamba unashikilia upendo wako wa kwanza, lakini unapungukiwa bidii ya kazi, ustahamilivu na fundisho safi. Je, Yesu atatishia kuchukua kinara chao katika hali kama hiyo?
-
-
-
-
- Soma Ufunuo 2:7. Je, inaonekana ajabu kwako kwamba Yesu ana ujumbe kwa ajili ya makanisa ya Kikristo saba pekee? (Hii inasema kwamba ujumbe ni kwa mtu yeyote mwenye masikio. Kumbuka kwamba Ufunuo ni kitabu cha ishara. Tunapozidi kuingia ndani zaidi kwenye somo letu la ujumbe kwa makanisa saba, tutaona kwamba huu ni ujumbe wa ulimwengu wote. Wasomi wa Biblia wanaamini kwamba haya makanisa saba yanawakilisha maelekezo ya hatua za historia ya kanisa la Kikristo – ambapo Waefeso inaelezea historia ya mwanzo kabisa ya kanisa.)
-
- Rafiki, unapokuwa chini ya shinikizo na kutafakari sana juu ya mustakabali wako, kumbuka kwamba Yesu sio tu kwamba anakukumbatia kwa upendo, bali pia anao ufunguo wa mustakabali wako! Kwa nini usifanye uamuzi, sasa hivi, kumpokea na kumtumaini kwa ajili ya mustakabali wako?
- Juma lijalo: Ujumbe wa Yesu kwa Makanisa Saba.