Pumziko Ndani ya Kristo

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
(Mathayo 12)
Swahili
Year: 
2016
Quarter: 
2
Lesson Number: 
6

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Kama mwanasheria, ninaamini katika sheria. Kuwa na sheria sahihi husaidia kuwa na uhuru kamili, ikiwemo uhuru wa dini. Mungu anaamini katika utawala wa sheria, vinginevyo Yesu asingekuja kutimiza matakwa ya sheria kwa niaba (ajili) yetu. Kinachowafanya wanasheria wawe na kazi ni mgongano kati ya sheria na mitazamo tofauti juu ya sheria hizo. Somo letu juma hili linahusu kuzichanganua sheria za Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Mathayo ili tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu asili ya sheria za Mungu!

 

I.                   Sheria (Kanuni) ya Nira

 

A.                Soma Mathayo 11:28-30. Juma lililopita tuliyaangalia mafungu haya. Hebu tuangalie kipengele kimoja cha ziada. Yesu anatupatia “nira.” Je, hicho ni kitu kizuri au kibaya?

 

1.                  Je, nira inafanana na sheria, kwamba inatufunga? (Nira ni kikwazo, lakini jambo jema ni kwamba Yesu ndiye mtu mwingine aliyepo kwenye hiyo nira. Hii inamaanisha kuwa katika kila jambo, kila changamoto, kila tatizo, Yesu anakuinua. Hiki ni kizuizi chenye manufaa. Kinaonesha rehema.)

 

B.                 Soma Mathayo 12:1-2. Kwa nini si halali kuvunja masuke? (Tatizo halikuwa kuiba masuke (Kumbukumbu la Torati 23:25), shtaka lilikuwa ni kufanya kazi siku ya Sabato (Kutoka 20:8-11).)

 

C.                 Soma Mathayo 12:3-4. Unalichukuliaje jibu la Yesu? Je, hilo silo jibu wakujibulo wanao – kwamba watu wengine pia wanafanya vivyo hivyo? “Huyu anatenda hivyo hivyo, Yule pia anafanya hivyo hivyo!”

 

1.                  Unadhani jibu gani litakuwa zuri zaidi kuliko “watu wengine pia wanafanya jambo hilo hilo?” (Ningejibu kwamba hii sio kazi.)

 

D.                Soma 1 Samweli 21:1-6. Je, Daudi anasema ukweli kwa Mfalme Sauli kuhusu kuwa kwenye safari ya kazi ya utume? (Hapana. Ukisoma sura iliyotangulia utaona kwamba Yonathani alimwonya Daudi kuwa Mfalme Sauli anataka kumwua. Daudi anamkimbia Sauli.)

 

1.                  Jambo gani linafanana kati ya mustakabali wa Daudi na wanafunzi wa Yesu? (Wana njaa.)

 

2.                  Je, hicho ndicho tunachopaswa kujifunza kuhusu Sabato – kwamba ni sahihi kuvunja sheria ikiwa una njaa?

 

a.                   Ikiwa hicho sicho cha kujifunza, je, Yesu anafundisha juu ya jambo gani?

 

(1)               Kuwasaidia watu wengine ni muhimu zaidi kuliko sheria?

 

b.                  Vipi ikiwa kuwasaidia watu wengine ndio sheria kuu?


 

(1)               Je, hicho ndicho kipimo? Je, hiyo ndio kanuni (sheria)?

 

E.                 Soma Mathayo 12:5-8. Yesu anamaanisha nini anaposema kwamba yeye ndiye “Bwana wa Sabato?” (Yeye ndiye anayeamua kilicho sahihi kufanyika siku ya Sabato.)

 

1.                  Yesu anamaanisha nini anaposema, “Nataka rehema, wala si sadaka?” (Hosea 6:6) (Ikiwa wanafunzi wa Yesu pamoja na Daudi wangejizuia kula, hiyo ingekuwa sadaka. Hivyo, Yesu anasema kuwa katika amri ya Sabato (na kwa dhahiri, kwenye amri nyingine pia), lengo ni kuonesha rehema.)

 

2.                  Je, hiyo ni sheria? (Nadhani ni sheria. Angalia mtazamo wako kwenye nusu ya pili ya Amri Kumi na kila sheria nyingine inayofanana na hizo katika Biblia. Je, sheria hizo zipo kwa ajili ya kutukwaza na kutuangusha, na kututia dhambini? Au, zipo hapo kwa kuwa Yesu anatupenda na anatutaka tuishi maisha huru dhidi ya matatizo yasiyo ya lazima? Nadhani sheria zipo ili kutuonesha rehema – na hicho ndicho anachokimaanisha Yesu. “Nira” yake ni rehema kwetu.)

 

3.                  Utagundua kwamba amri ya Sabato haipo kwenye “nusu ya pili” ya Amri Kumi. Je, amri hiyo inahusu kumwabudu Mungu au inahusu kuwa na maisha bora? (Amri ya Nne ni kiunganishi cha amri zinazomhusu Mungu na zile zinazowahusu wanadamu wenzetu. Soma Marko 2:27-28. Sabato ni siku ya pumziko kwa wanadamu, lakini pia ni muda wa pekee wa kutafakari kile ambacho Mungu amekifanya kwa ajili yetu.)

 

II.                Sheria (Kanuni) ya Mkono Uliopooza

 

A.                Soma Mathayo 12:9-10. Ungejibuje swali hili ikiwa unaelewa kwamba rehema ndilo lengo lililopo nyuma ya sheria za Mungu? (Jibu ni dhahiri kabisa, “ndiyo.”)

 

B.                 Soma Mathayo 12:11-13. Kisa hiki kinakazia vipi visa vilivyotangulia kuhusu kuvunja masuke na Daudi kula mikate ya wonyesho? (Hii inaonesha kwamba rehema ndio sheria kiongozi.)

 

1.                  Hebu tujikite kwenye kisa cha Daudi kuhusu mikate ya wonyesho. Lengo la hekalu na sherehe (taratibu) za hekalu lilikuwa ni lipi? (Kuelezea ujio wa Yesu na kufa kwa ajili yetu.)

 

a.                   Je, hiyo ilikuwa ni kutuonesha rehema? (Ndiyo! Kuzipa kipaumbele sheria zinazohusu mikate ya wonyesho dhidi ya mahitaji ya Daudi kungepuuzia maana yote ya taratibu za hekalu – kwamba Mungu alikuwa anakuja ili kutuonesha rehema!)

 

C.                 Je, unadhani Mungu ana tabaka la sheria (kanuni)? Je, baadhi ya sheria ni muhimu zaidi kuliko nyingine?

 


1.                  Katika sheria za Marekani, kuna sheria inayotawala inayosema kwamba hakuna sheria inayoizidi nyingine isipokuwa tu kama kuna ukinzani wa moja kwa moja. Kwenye visa tulivyoviangalia hadi sasa (kuvunja masuke na uponyaji siku ya Sabato/Daudi kula mikate ya wonyesho), je, palikuwepo na ukinzani wa moja kwa moja kati ya sheria ya rehema na Sabato au sheria za hekalu? (Mambo ya Walawi 24:8-9 inakinzana moja kwa moja na Daudi kula mikate ya wonyesho. Na kwa kuongezea, Yesu anakiri kuwa kuna ukinzani (Mathayo 12:4). Ingawa sioni ukinzani kwenye kuvunja masuke, Yesu alijizuia kujenga hoja kwamba wanafunzi wake hawakuwa wakifanya kazi. Nadhani anachokimaanisha Yesu ni kwamba kuna tabaka la sheria.)

 

2.                  Je, kuna maelezo ya ziada kuhusu mbadala wa tabaka la sheria mbalimbali? (Kwamba sheria zote zina maana moja – kuonesha rehema.)

 

D.                Soma Mathayo 12:14. Viongozi wa dini wanaonesha nini? (Hawadhihirishi rehema. Wanaonesha chuki. Huu ni ukiukwaji wa dhahiri wa sheria.)

 

III.             Sheria (Kanuni) ya Rehema

 

A.                Soma Mathayo 12:15-16. Baada ya Yesu kufahamu njama ya kutaka kumwua, anaondoka. Je, ilikuwa hatari kwake kufanya uponyaji? (Ndiyo, ingewachochea zaidi viongozi wa dini kutaka kumwua Yesu.)

 

1.                  Pamoja na hayo kwa nini Yesu anafanya hivi? (Rehema!)

 

B.                 Soma Mathayo 12:17-21. Tunaambiwa kuwa Yesu atafanya nini? (Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu atatangaza hukumu, na ataiongoza “hukumu kushinda.” Ataleta tumaini.)

 

1.                  Yesu hatafanya nini? (Hatazua wala kushiriki kwenye ugomvi au kulia. Hatainua sauti yake. Hatawajeruhi zaidi wale ambao tayari wameshajeruhiwa.)

 

C.                 Soma tena Mathayo 12:20. “Utambi utokao moshi” umezimika. “Mwanzi wenye mchubuko” uko hatarini kuvunjika kwa sababu tayari una mchubuko. Vitu hivi vinawaelezea watu wa aina gani? Wagonjwa? Waliokata tamaa? Waliopoteza moto wa imani?

 

1.                  Je, watu wanaohamasisha mtindo wa maisha uliojaa dhambi, na wana uhasama na dini, pia wanastahili kuwa kwenye kundi la mianzi (matete) yenye mchubuko na tambi zitokazo moshi?

 

IV.             Sheria ya Hatari

 

A.                Soma Mathayo 12:22-23. Watu hawa wanaonekana kufikiri juu ya jambo gani? (Wanaashiria kwamba Yesu ni Masihi.)

 

B.                 Soma Mathayo 12:24. Viongozi wa dini wanatoa madai gani? (Kwamba Yesu anapewa uwezo na Shetani.)

 

C.                 Katika Mathayo 12:25-29 Yesu anajenga mfululizo wa hoja zenye mantiki akibainisha kwamba hatumii uwezo wa Shetani. Soma Mathayo 12:30-32. Kwa nini Yesu anazungumzia kunena “dhidi ya Roho Mtakatifu” na kusema kwamba hiyo ni dhambi isiyoweza kusamehewa? (Kuihusisha kazi ya Roho Mtakatifu na Shetani ndio dhambi isiyoweza kusamehewa.)

 


1.                  Asubuhi hii nilibadilishana mawazo na mtu aliyekuwa anajenga hoja kwamba muziki wa kisasa wa kumsifu Mungu wenye mdundo ni wa kishetani. Ninaamini kwamba muziki wa kisasa wenye kusifu unahusisha, kwa kiasi fulani, Roho Mtakatifu kuyaelekeza mawazo yangu kwa Mungu moja kwa moja. Angalia 1 Wakorintho 14:14-17. Hata hivyo, suala ninalotaka ulitafakari sio muziki, bali shtaka la uwezo (nguvu) wa kishetani. Hatari ni ipi? (Hatari iliyopo ni dhambi isiyosamehewa! Wakristo wanaowatuhumu Wakristo wengine kwamba wanatumia uwezo wa Shetani wako kwenye hatari hiyo hiyo ya dhambi isiyosamehewa. Wanatakiwa kuwa na uhakika na mashtaka haya, vinginevyo wasiwatuhumu.)

 

2.                  Je, yule mtu ambaye hakukubaliana nami ametenda dhambi isiyosamehewa? (Hii si sawa na mtego wa waya. Tatizo ni kwamba Roho Mtakatifu anatugusa na kutufanya tutambue dhambi zetu. Yohana 16:8-9. Tunapoanza kuupinga uwezo wa Roho Mtakatifu kwa kudai kwamba uwezo huo ni wa kishetani, tunaufukuzilia mbali uwezo huo wenye mguso maishani mwetu. Ni mchakato, sio shtaka moja.)

 

D.                Rafiki, je, unaamini kwamba rehema iko nyuma ya sheria za Mungu kwa ajili ya maisha yetu? Je, utafanya uamuzi leo, kuwaonesha watu wengine rehema ya Mungu? Kupata pumziko kwenye rehema ya Mungu kwako?

 

V.                Juma lijalo: Bwana wa Wayahudi na Mataifa.