Baba Wetu Mpendwa wa Mbinguni
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mojawapo ya mbaraka mkubwa maishani mwangu ulikuwa ni kuwa na baba mwenye upendo. Baba wangu ndiye aliyenifundisha kwamba utii na upendo vinaendana. Sikuwa na shaka kwamba baba wangu alikuwa akinipenda kwa dhati. Kwa upande mwingine, nilielewa maana ya hukumu! Huu ulikuwa ni muunganiko wa mambo ulionifanya nimwelewe vizuri zaidi Baba wetu wa mbinguni. Ufahamu wetu wa Baba wetu wa Mbinguni unawekwa wazi zaidi kutokana na kile ambacho Yesu alikisema kumhusu. Hilo ndilo somo letu la juma hili. Hebu tuzame kwenye Biblia zetu ili tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu Baba wetu mpendwa wa mbinguni!
- Mtazamo Wetu Juu ya Watu Wengine
- Soma Mathayo 7:1-2. Je, kanuni inasemaje kuhusu namna ambavyo tunapaswa kutendeana? (Tunapata kile tunachokitoa. Tukiwa na huruma, basi nasi tutaonewa huruma.)
- Soma Mathayo 7:3-5. Je, kwa kawaida huwa tunatendeanaje? (Kwa ujumla, huwa tunawakosoa sana watu wengine kuliko tunavyojikosos sisi wenyewe.)
- Soma Mathayo 7:6. Je, jambo hili linaendanaje na mafungu ya Biblia yalitotangulia? Hili linaonekana kuwa jibu kwenye maelekezo yaliyotolewa. Je, ni kweli? (Katika huruma zetu na misaada yetu tunatakiwa kutoa hukumu zenye ukomavu na zenye mantiki.)
- Mtazamo wa Mungu Juu Yetu
- Soma Mathayo 7:7-8. Yesu anabadilika hapa. Amehama kutoka kwenye namna tunavyotendeana hadi kwenye mada gani nyingine mpya? (Jinsi Mungu anavyotutendea.)
- Je, unadhani mafungu yaliyopita yanayozungumzia jinsi tunavyopaswa kutendeana yanatufahamisha jinsi Mungu anavyotutendea? (Mathayo 7:1 inaonekana kusema kuwa Mungu anaangalia jinsi tunavyowatendea watu wengine pale anaposhughulika nasi, lakini kwangu mimi inaonekana kwamba Mungu ni mkarimu zaidi kwetu kuliko vile tulivyo wakarimu kwa wenzetu.)
- Je, matarajio ya Mungu ni yapi? (Tukiomba, Mungu atatupatia.)
- Je, huu ndio uzoefu wako maishani? Kuwa mwaminifu.
- Soma Mathayo 7:9-11. Je, Yesu anarejea jambo gani linaloonyesha mtazamo wa Mungu dhidi yetu? (Jinsi tunavyowatendea watoto wetu.)
- Kwa nini Yesu anamlinganisha Baba wake wa Mbinguni na sisi? (Nafahamu baba wangu alikuwa anataka kunipatia kipawa kizuri [zawadi nzuri]. Nafahamu kwamba ninataka kuwapatia wanangu vitu vizuri. Hii ni hamasa ya pekee kwangu. Kila mara huwa ninashangaa na kujiuliza, “Kile aniwaziacho Mungu,” ninatakiwa kukiomba tu, “Je, nitamtendea nini mwanangu?” “Je, baba wangu angenitendea nini?”)
- Hebu sasa tupitie tena Mathayo 7:7-8. Kama umejisemea kwamba, “Mungu hajibu maombi yangu,” je, wewe uliwapatia wanao kila walichokuomba? (Mathayo 7:11 inamrejea Mungu akitupatia “vipawa vyema.” Katika somo letu la robo iliyopita, tulijifunza kwamba kumtumaini Mungu ni kiini cha uhusiano wetu na Mungu. Mungu anafahamu kila kitu. Anatupatia vipawa vyema. Ikiwa vipawa hivyo vinaonekana kuwa ni vibaya kwetu, tunatakiwa kumtumaini tu ili kufahamu kilicho bora kwa ajili yetu.)
- Soma Mathayo 7:12. Kwa nini Yesu anarejea nyuma na kujadili jinsi tunavyopaswa kutendeana? (Jinsi Mungu anavyotutendea inaendana na jinsi tunavyopaswa kuwatendea watu wengine. Mungu ni mkarimu kwetu. Anaangalia mambo yaliyo mema kwetu. Kwa hiyo, tunapaswa kuangalia na kutenda mambo mema kwa wengine.)
- Soma sehemu ya mwisho ya Mathayo 7:2: “Kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa.” Nani anayechukua vipimo kwa upande wako? (Mungu ndiye anayechukua vipimo. Jinsi tunavyowatendea watu wengine ndicho kipimo anachokitumia Mungu kututendea sisi.)
- Soma Mathayo 7:7-8. Yesu anabadilika hapa. Amehama kutoka kwenye namna tunavyotendeana hadi kwenye mada gani nyingine mpya? (Jinsi Mungu anavyotutendea.)
- Taswira ya Yesu Juu ya Baba
- Soma Yohana 14:1-3. Je, Mungu anatuomba tufanye nini? (Tusifadhaike hapa duniani. Tumtumaini Mungu kwa kuwa hatimaye atatuchukua na kutupeleka nyumbani ili kukaa pamoja naye.)
- Soma Yohana 14:4-5. Tomaso anahamaki kusikia kwamba anafahamu uelekeo wa hii sehemu kuu ambayo Yesu ameiandaa kwa ajili ya makao yake. Je, ana tatizo gani? (Yesu anajenga dhana za uongo. Tomaso hafahamu uelekeo huo, na hili ni jambo la muhimu sana analopaswa kufahamishwa! Tomaso anataka kwenda huko.)
- Soma Yohana 14:6-7. Je, Yesu anazungumzia uelekeo? Je, anairejea ramani? (Yesu anazungumzia wokovu. Njia pekee ya kwenda mbinguni ni kupitia kwa Yesu.)
- Soma Yohana 14:8. Unadhani Filipo anasema juu ya jambo gani? (Swali kuu la karne zote ni, “Yesu ni nani?” Filipo anasema tunaweza kuwa na uhakika kwamba wewe ni nani, Yesu, ikiwa tu utatuonyeshau Baba wa mbinguni.)
- Soma Yohana 14:9. Je, Yesu amefadhaishwa na Filipo? (Ndiyo.)
- Je, Yesu na Filipo wana fikra moja? (Filipo yupo nyuma sana ya Yesu. Filipo anataka kuthibitisha kwamba Yesu ni Mungu. Yesu anamwambia Filipo kwamba ikiwa anataka kumfahamu Mungu, anachotakiwa kukifanya ni kumwangalia Yesu tu.)
- Soma Yohana 14:10-11. Tuchukulie kwamba wewe uko mbele zaidi ya Filipo. Je, unajifunza habari gani za Mungu kupitia kwa Yesu? (Yesu alitenda miujiza ili kuondoa mateso ya wanadamu. Taswira anayotupatia Yesu ni ya Baba anayetupenda kwa kiwango cha juu kabisa.)
- Taswira ya Uumbaji Juu ya Mungu
- Soma Mathayo 6:25-26. Je, Yesu anashauri nini kuhusu kuwa na vipaumbele sahihi? (Anasema kuwa maisha yetu na afya zetu ni muhimu zaidi kuliko chakula au mavazi.)
- Unadhani kwa nini Yesu alisema jambo hili katika muktadha wa Mungu kututafuta? (Tunatakiwa kuwa na shukrani kwa mambo ya msingi. Watu wanaokula vyakula vya bei ghali na kuvaa mavazi mazuri, lakini hawana afya nzuri, wanaelewa vipaumbele hivi.)
- Je, ndege wanatufundisha nini kuhusu upendo wa Baba wa Mbinguni? (Mungu anahakikisha kuwa wanapata chakula. Atahakikisha kuwa tuna chakula cha kutosha.)
- Soma Mathayo 6:27. Je, Yesu anaongezea jambo gani halisi? (Wasiwasi haukuongezei kimo, haukufanyi uonekane mzuri au kurefusha maisha yako. Je, kuna uzuri gani?)
- Soma Mathayo 6:28-30. Fungu lililotangulia limetuambia tuwe na vipaumbele sahihi. Hapa Yesu anasema jambo tofauti. Je, Mungu atatupatia mambo ya msingi tu? (Hapana! Unahitaji wanao wawe na vitu vizuri. Mungu ana matamanio hayo hayo kwa ajili yako.)
- Soma Mathayo 6:31-33. Badala ya kuwa na wasiwasi, je, tunapaswa kufanya nini? (Mweke Mungu kuwa wa kwanza [kuwa kipaumbele]. Uendeleze na kuutangaza Ufalme wa Mungu. Tenda haki.)
- Soma Mathayo 6:25-26. Je, Yesu anashauri nini kuhusu kuwa na vipaumbele sahihi? (Anasema kuwa maisha yetu na afya zetu ni muhimu zaidi kuliko chakula au mavazi.)
- Mwana Mpotevu na Taswira ya Mungu
- Soma Luka 15:11-12. Je, ungesema nini mwanao angekuambia jambo hili? (Bado sijafariki!)
- Je, jambo hili linasema nini kumhusu baba?
- Soma tena Mathayo 7:6. Je, baba alikuwa anatenda kosa?
- Ikiwa umesema, “ndiyo,” tutajifunza kwamba katika kisa hiki baba anamwakilisha Mungu Baba. Je, Mungu anaweza kutenda kosa kama hili?
- Soma Luka 15:13-16. Je, mambo yanamwendeaje huyu mwana? Je, ndoto zake zimetimizwa?
- Soma Luka 15:17-19. Jambo gani linamhamasisha mwana huyu kurejea? (Chakula.)
- Soma Luka 15:20. Jiweke kwenye nafasi ya baba. Je, ungeitikia vivyo hivyo? Vipi kama ungetambua kwamba kilichomhamasisha mwanao kurudi ni chakula?
- Soma Luka 15:21-24. Baba wangu alinifundisha mpatano wa pekee wa upendo na hukumu. Je, kuna hukumu yoyote hapa? (Hapana. Hakuna hukumu hata moja.)
- Tunawatendeaje wale wanaomgeukia Mungu?
- Soma Luka 15:25-28. Je, kijana mkubwa anamwakilisha nani? (Sisi – wale wanaomtii Mungu kwa uaminifu.)
- Soma Luka 15:29-30. Unaufikiriaje mtazamo wa kijana mkubwa dhidi ya babaye?
- Umewahi kufikiria, “Ningependa kuwa kama mwizi pale msalabani: nifanye lolote nitakalo na katika dakika ya mwisho kabisa nitubu na kuokolewa?”
- Je, kuna tatizo gani na mtazamo wa aina hii? (Robo iliyopita tulijifunza kwamba Mungu anatupatia sheria yake kwa sababu anatupenda na anataka kutuepusha na matatizo. Tunatakiwa kumtumaini Mungu. Kijana mkubwa alimwonea wivu kijana mdogo. Alifikiria kwamba maisha yake na babaye hayakuwa na chochote bali “utumwa.”)
- Je, kijana mdogo na mkubwa wanafananaje? (Wote walionekana kuhamasishwa na kile wanachoweza kukipata kutoka kwa baba wao.)
- Je, hili linatufundisha nini kuhusu Baba wetu wa mbinguni? (Anatupenda hata kama mitazamo yetu bado sio sahihi!)
- Soma Luka 15:11-12. Je, ungesema nini mwanao angekuambia jambo hili? (Bado sijafariki!)
- Rafiki, je, umewahi kuuona upendo mkubwa kiasi hicho? Sisi tu mbali sana na ukamilifu. Kama ilivyokuwa kwa Filipo, nasi pia hatuelewi. Kama ilivyo kwa wanandugu, nasi pia tunayo mitazamo mibaya. Yesu anasema kuwa upendo wetu kwa watoto wetu ni mwanzo tu wa kuuelewa upendo wa Mungu Baba kwetu. Je, utauitikia upendo huo leo? Je, utaipokea kafara ya Yesu kwa ajili yako, na kumtumaini Mungu katika maisha yako?
- Juma lijalo: Mwana.