Somo la 9: Pambano la Ulimwengu Mzima

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Matayo 4 & 13, Isaya 14
Swahili
Year: 
2025
Quarter: 
1
Lesson Number: 
9

Somo la 9: Pambano la Ulimwengu Mzima

 

(Matayo 4 & 13, Isaya 14)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2025, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Fikiria mchezo ambao ulishindwa kabisa kujua timu gani zinashiriki au wachezaji gani walikuwa uwanjani. Sehemu kubwa ya kutomwelewa Mungu inatokana na huu ujinga wa kawaida. Kama Mungu hayupo, basi uovu hauwezi kuinuka kuzidi wanadamu wanaotenda uovu. Kama Mungu yupo, na timu ya Mungu pekee ndio ipo uwanjani, basi uovu unatoka kwa Mungu. Mungu angalao kwa kiasi fulani ni mwovu. Lakini kama kuna timu mbili uwanjani, na timu moja ni Mungu na wachezaji wake, na nyingine ni timu pinzani dhidi ya Mungu, basi tunaweza kuanza kutenganisha nani anawajibika kwa Mungu, na nani anawajibika kwa uovu. Tunaweza kuchukua uamuzi wa kimantiki kwamba timu ipi tuishangilie. Biblia inatibu ujinga wetu kuhusu wachezaji hawa. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuliangalie suala hili!

  1.    Shamba/Konde
    1.    Soma Mathayo 13:24-27. Swali la msingi kwenye mfano huu ni lipi? (Inakuwaje magugu yapo kondeni/shambani kwetu?)
      1.    Ni nini msingi wa kushangaa jambo hili? Ninayaona magugu nyakati zote katika mimea ninayoipanda. (Mmiliki alipanda mbegu njema pekee. Haikuwa na magugu.)
      1.    Huu ni mfano. Mfano huu unaakisi jambo gani maishani? (Ni kwa jinsi gani tunao uovu hapa duniani? Ni kwa jinsi gani tunao uovu kanisani? Mungu aliumba vitu vikamilifu pekee.)
    1.    Soma Mathayo 13:28. Taarifa gani muhimu inakosekana kwa wale wanaouliza swali la msingi? (Hawajui kuwa kuna zaidi ya mchezaji mmoja uwanjani. Si tu kwamba mwenye nyumba ndiye apandaye, bali mtu mwingine, adui, pia anapanda shambani/kondeni.)
      1.    Wafanyakazi (watumwa) wanataka kutatua tatizo mara moja. Je, huo ni mtazamo sahihi?
    1.    Soma Mathayo 13:29. Je, tatizo linapaswa kutatuliwa mara moja? (Hapana.)
      1.    Kwa nini isiwe hivyo? (Kutatua tatizo mara moja kutasababisha madhara kwenye mimea mizuri.)
      1.    Unadhani kwa nini hili ni kweli?
    1.    Bila kujali kama unaishi au hauishi nchini Marekani, kuna uwezekano mkubwa umesikia kazi ya haraka haraka tena ya hasira iliyofanywa na Rais Trump kung’oa kile anachoona kuwa ni rushwa na utapanyaji. Hivi karibuni nimekuwa mjumbe wa bodi mbili zenye nguvu kubwa kanisani kwangu. Kwa asili huwa nina tabia ya kuingia kwenye jambo na kutafuta ufumbuzi. Lakini baadhi ya wajumbe wenye uzoefu zaidi huwa wananionya dhidi ya kitendo hicho. Utatumiaje tahadhari ya Mathayo 13:29 kwenye kazi ya mageuzi? Tujikite mjadala wetu kanisani, na kuachana na siasa. (Kwa kuzingatia kanisa, kukatisha tamaa mbegu njema ni tatizo.)
    1.    Soma Mathayo 13:30. Niambie unachokifikiria kuhusu suluhisho la mwenye nyumba? Je, lina ufanisi kama kung’oa magugu mara moja?
      1.    Je, inaendana na hatari kwamba kutokana na ucheleweshwaji mbegu bora inaweza kuharibiwa na mbegu mbaya?
        1.    Kwa kuwa mwenye nyumba ana wasiwasi wa kuharibu mbegu njema kwa kuchukua hatua ya haraka, je, hatari kwa mbegu njema haizuiliki?
      1.    Mfano huu unatufundisha nini kuhusu uovu kanisani?
        1.    Je, unatufundisha kuwa mara zote tunapaswa kuyaacha magugu bila kuyabughudhi?
    1.    Soma Ufunuo 2:18-20. Hii inaashiria nini kuhusu kuwavumilia washiriki wa kanisa wanaofundisha kwa kuunga mkono uzinzi? (Yesu anaanza kwa kusema kuwa huu ni mfano wa ufalme wa mbinguni. Anaweza tu kuwa anafafanua kwa nini hauondoi uovu mara moja. Hata hivyo, kisa cha onyo kipo hapo ili watu wote waone na kujifunza.)
      1.    Mfano huu unatufundisha nini kuhusu idadi ya wachezaji katika uwanja wa dunia?
  1.   Majaribu
    1.    Soma Mathayo 4:1. Tunaona wachezaji wangapi kwenye kisa hiki? (Tunaye Yesu na Ibilisi.)
      1.    Je, hii inaashiria kuwa wawili hawa ni wapinzani? (Ndiyo, endapo Ibilisi yupo ili kumjaribu Yesu atende dhambi.)
      1.    Kifungu hiki pia kinamtaja Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu yuko upande wa nani? Kama moja kwa moja umejibu kuwa, “Yesu,” kwa nini amwongoze Ibilisi kumjaribu Yesu? (Kwa haraka haraka hili linaibua udadisi. Hitimisho langu ni kwamba Roho Mtakatifu anaamini kuwa Ibilisi bado hajajiandaa kwa pambano. Kukurupuka kuingia katika uwanja wa mapambano kutamnufaisha Yesu.)
    1.    Soma Mathayo 4:2-3. Je, hii inaashiria kuwa kuharakisha kumnufaisha Yesu kwa dhahiri si jambo sahihi? Yesu ni mnyonge na ana njaa!
      1.    Jiweke kwenye nafasi ya Ibilisi. Haya ni makabiliano ya muhimu sana. Je, utajiandaa kwa umakini mkubwa? Je, utakuja na jaribu lako kubwa kabisa? (Ibilisi anajenga jaribu lake juu ya kile ambacho kimemtokea Yesu hivi punde. Mhubiri akiweka jambo lililomtokea jana kuwa kiini cha hubiri lake, ninajua kuwa hubiri hilo halikuandaliwa kwa umakini. Hicho ndicho kinachoonekana hapa.)
    1.    Soma Mathayo 4:4. Kwa kuzingatia jibu analolitoa Yesu, je, wawili hawa wanapingana? (Yesu ananukuu Biblia (Kumbukumbu la Torati 8:3) kukataa pendekezo la Ibilisi.)
    1.    Soma Mathayo 4:5-7. Katika majaribu mawili ya kwanza Ibilisi anatumia maneno, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu.” Hiyo inatuambia nini kuhusu asili ya pambano? (Shetani anaamua ubishani wa endapo Yesu ni Mungu.)
      1.    Yesu anajibuje? (Kwa mara nyingine, Yesu ananukuu Biblia (Kumbukumbu la Torati 6:16) kukataa jaribu la Ibilisi. Kwa mara nyingine hii inatuambia kuwa Ibilisi ni mpinzani.)
    1.    Soma Mathayo 4:8-9. Je, kuna shaka yoyote sasa kwamba Yesu na Ibilisi wapo kwenye ugomvi? (Shetani alipomwambia Yesu kuwa amwabudu, hii iliwaonesha kuwa wapinzani.)
    1.    Soma Mathayo 4:10. Je, hili ni swali kwa wanadamu wote: unamwabudu nani? (Ndiyo. Hii inaonesha kuwa Yesu na Shetani (Ibilisi) ni washindani. Wapo kwenye ugomvi wa juu ya nani anatakiwa kuabudiwa. Tunamwabudu ama Mungu au Shetani.)
      1.    Soma Warumi 10:9. Ufunguo wa wokovu ni upi?
  1.      Jinsi Uovu Ulivyoanza
    1.    Hadi kufikia hapa tumejifunza kwamba timu mbili zipo uwanjani. Timu ya Yesu inamuunga mkono Mungu na Biblia, na timu ya Shetani inatafuta madai ya kuabudiwa anayoyastahili Mungu kwa kutumia njia zinazokinzana na Biblia. Soma Ezekieli 28:12-15. Je, kauli hizi zinaweza kuwa zinamrejelea mwanadamu? (Mtu anayeelezewa hapa alikuwapo sehemu zote mbili, yaani, mbinguni na katika bustani ya Edeni. Lazima jibu ni, “Hapana.”)
    1.    Soma Ezekieli 28:17 na Isaya 14:12-14. Je, vifungu hivi vinaonekana kumwelezea mtu yule yule?
      1.    Angalia rejea ya kutupwa chini kutoka mbinguni. Soma Luka 10:18, Isaya 14:12, na Ufunuo 12:8-9. Nani aliyetupwa kutoka mbinguni hadi duniani? (Shetani. Ukivilinganisha vifungu vyote hivi, ni wazi kwamba mtu anayeelezewa hapa ni Shetani.)
    1.    Majuma mawili yaliyopita tulijifunza asili ya uovu duniani. Nilisema kuwa hatutaangalia jinsi uovu ulivyoibuka ulimwenguni. Sasa tunaigeukia mada hiyo. Je, Isaya 14:13-14 na Ezekieli 28:17 zinatuambia nini kuhusu jinsi uovu ulivyoibuka kutoka kwenye ukamilifu? (Ilikuwa ni majivuno kutokana na uzuri na fahari yake. Lakini utaona kwamba ni zaidi ya hayo. Shetani alitaka “kufanana na Aliye Juu.” Alitaka kutawala.)
    1.    Soma 1 Timotheo 3:6. Kiburi cha nafasi kilifanya jambo gani limtokee Shetani? (Alijivuna.)
    1.    Hebu turejee kwenye Mathayo 4:8-9. Je, hili ni jaribu kwa Yesu, au jambo hili linaakisi dosari ya kitabia ya Shetani?
    1.    Nilipokuwa nikiendelea kukua kanisani, palikuwepo na mambo kadhaa ambayo yangeweza kukufanya ufukuzwe kanisani. Mojawapo ni uvutaji wa sigara. Je, kuna mtu ambaye amewahi kufukuzwa kanisani kwako kwa sababu ya kiburi, majivuno, au kutamani kutawala?
      1.    Ikiwa sivyo, kwa nini? (Kwanza, kumbuka mfano wa magugu tuliojifunza hivi punde. Pili, mitazamo hii ni ya ulimwenguni kote miongoni mwa wale wanaotamaniwa ndani na nje ya kanisa.)
    1.    Unakumbuka sehemu ya utangulizi ambapo niliuliza kuhusu nani aliye uwanjani na timu ngapi zipo uwanjani? Utajibuje swali hilo sasa hivi? (Kwa dhahiri tuna timu za Yesu na Shetani. Lakini pia tunao wale waliopo katika Timu ya Yesu wanaoenenda kana kwamba wapo upande mwingine.)
    1.    Rafiki, je, pambano la ulimwengu mzima linaendelea maishani mwako? Ninafahamu kwamba majivuno, kupenda makuu, na tamaa ya mamlaka ndizo changamoto zilizopo maishani mwangu. Kwa nini usiombe pamoja nami sasa hivi kwamba Roho Mtakatifu achepushe talanta zako kwa ajili ya wema na si kwa ajili ya kujitukuza?
  1.   Juma lijalo: Kanuni za Mafungamano (Rules of Engagement).