Somo la 2: Upendo wa Kiagano
Somo la 2: Upendo wa Kiagano
(Kumbukumbu la Torati 7, 1 Yohana 4, Mathayo 18)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2025, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: “Agano” ni makubaliano. Katika zama za leo tunaweza kuuita “mkataba.” Kwa watu wengi, upendo ni wa “kiagano,” ikimaanisha kwamba tunawapenda wale wanaotupenda. Na hatuwapendi wale wasiotupenda. Lakini je, huo ndio ukweli kwa Mungu? Katika Mathayo 5:44-46 Yesu anafundisha kuwa lengo si kuwapenda wale wanaotupenda tu. Tunasoma katika Yohana 3:16 kwamba Mungu aliupenda ulimwengu, hivyo akamtoa “Mwanawe pekee” ili kutuokoa. Yesu alikuja kuwaokoa watu wengi ambao kamwe alikuwa hawajasikia habari zake. Kwa dhahiri, walikuwa hawajakubali kumpenda. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi kuhusu uhusiano kati ya upendo wa Mungu na upendo wetu kwake!
- Kuwachagua Wapenzi?
-
- Soma Kumbukumbu la Torati 7:6-8. Mungu anafafanua kwa nini aliichagua na kutoichagua Israeli kuwa watu wake maalumu. Ni sababu gani za kukataliwa? Mungu hakuwachagua kwa kuwa walikuwa wengi.)
-
-
- Kwa nini basi aliwachagua? (Mungu anawapenda. Na kwa kuongezea, Mungu alitoa ahadi kwa mababu wao.)
-
-
- Soma Kumbukumbu la Torati 7:9-11. Je, Mungu anampenda kila mtu? (Si kwa mujibu wa vifungu hivi. Mungu anawapenda wale “wampendao na kuzishika amri zake.” Atawaangamiza wale wanaomchukia.)
-
- Kabla ya vifungu katika Kumbukumbu la Torati 7 vinavyozungumzia juu ya upendo wa Mungu kwa Wayahudi, tunaona vifungu vinavyohusu watu watakaoangamizwa. Soma Kumbukumbu la Torati 7:1-2. Makundi haya maalumu ya watu yanapaswa kutendewaje? (Lengo kwa ajili yao ni “kuangamizwa kabisa.”)
-
-
- Ninauliza tena, “je, Mungu anampenda kila mtu?” (Vifungu hivi vinaashiria kuwa Mungu hawapendi watu wote.)
-
-
- Hebu tulichunguze hili kwa kina zaidi kwa kusoma Kumbukumbu la Torati 7:3-5. Tunaona sababu gani za Mungu kuwaangamiza watu hawa? (Wanaitumikia miungu mingine. Wamemkataa Mungu wa kweli.)
-
-
- Je, tunaweza kuunda kanuni ya upendo wa Mungu? Kanuni ambayo ni ya “kiagano” – ukimchagua Mungu anakupenda? Usipofanya hivyo, unatakiwa kutimka mbio.
-
-
- Soma 2 Petro 3:9 na 1 Timotheo 2:3-4. Hili linaongezea kitu gani kwenye taswira ya upendo wa Mungu? (Mungu anampenda kila mtu kwa mantiki ya kwamba anataka watu wote wamjie. Lakini kama humwendei utaangamizwa.)
-
-
- Je, hili linaendana kikamilifu na Mathayo 5:44-45?
-
- Upendo Mdogo? (Limited Love?)
-
- Soma Yuda 20-21. Inamaanisha nini “kujilinda” katika upendo wa Mungu? Je, inamaanisha kuwa suala la Mungu kutupenda linategemeana na kama tunaendelea kuchagua nafasi ndani ya upendo wake?
-
- Soma Hosea 9:15 na Yeremia 16:5. Vifungu hivi vinatufundisha nini kuhusu upendo wa Mungu endelevu? (Vinatufundisha kuwa Mungu anafikia hatua ambayo hawapendi watu walio na matendo maovu.)
-
- Soma Warumi 11:22. Ninauliza tena, je, wanadamu wanaudhibiti upendo wa Mungu? Kuiweka kwa namna nyingine, je, lazima “tuendelee katika wema wa Mungu” ili kuendelea kufurahia wema wake?
-
- Mwanamaoni mmoja alijenga hoja kwamba, kifungu cha “sitawapenda tena” katika kitabu cha Hosea hakimaanishi kuwa Mungu anaweza kuacha kumpenda mtu kwa sababu katika Hosea 14:4 tunamwona Mungu akisema “anapenda bila masharti.” Unadhani kifungu cha “kupenda bila masharti” kina maana sawa na “kupenda siku zote?” (Kwa uaminifu mtu anaweza kusema kuwa anampenda kila mtu “bila masharti” bila kusema kuwa ataendelea kumpenda mtu aliyejiingiza kwenye matendo maovu.)
-
-
- Hebu subiri kidogo. Je, watu “wanaopendwa bila masharti” katika Hosea 14:4 ni watu wema? (Hapana. Wapo kwenye “uasi” kwamba Mungu anasema atawaponya. Hii inaashiria kwamba Mungu yuko tayari kuwapokea tena.)
-
- Neema ya Jumla (Common Grace)
-
- Kwa kuwa kifungu kinachoonekana kutoendana na dhana ya upendo wa Mungu (na wetu) ni Mathayo 5, hebu tukiangalie kwa kina zaidi. Soma Mathayo 5:43-45. Upendo wa namna gani unafafanuliwa hapa? (Mimi nitauita “upendo wa fursa sawa.” Neno la kiteolojia ni “common grace” (neema ya jumla). Mungu anasema anafanya mambo ya msingi kwa wema na wabaya – huwaangazia jua na kuwanyeshea mvua wote.)
-
-
- Je, “neema ya jumla” ndio namna unavyowapenda wanafamilia wako? (Hapana! Unawatendea kwa namna ya pekee, na ya kupendeza.)
-
-
- Soma 1 Yohana 4:7-10. Ni “neema ipi ya jumla” iliyo ya msingi sana ambayo Yesu aliwapatia watu wote? (Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi za watu wote.)
-
- Angalia kwa ukaribu zaidi 1 Yohana 4:9. Utaona kuwa kifungu kinasema kwamba ili “tupate” uzima kupitia kwa Yesu. Je, hii inamaanisha kuwa upendo wa Mungu una ukomo ikiwa hatuishi kwa njia ya Yesu? (Tusipomkiri Yesu kama Mwokozi wetu, kifo chake kwa ajili yetu hakitufai kitu.)
-
- Soma 1 Yohana 4:15-17. Unadhani inamaanisha nini kwa upendo wa Mungu “kukamilishwa” kwetu? (Upendo wa fursa sawa, neema ya jumla, hutolewa kwa watu wote. Upendo huo hautatuepusha kuangamizwa katika hukumu. Kinachotupatia ujasiri wa kukabiliana na hukumu ya mwisho ni kwamba tumempokea Mungu maishani mwetu na kwa hilo upendo wa Mungu hufikia kiwango kipya cha upendo kamili.)
-
- Unakumbuka kutoka juma lililopota (Somo la 1 katika mfululizo wa masomo haya) mfano wa Mathayo 22 wa karamu ya harusi? Soma Mathayo 22:8-10. Sehemu ipi inaonesha neema ya jumla katika mfano huu? (Hatimaye kila mtu alialikwa kwenye karamu ya harusi. Hata “waovu” walialikwa.)
-
- Soma Mathayo 22:11-13. Ni wakati gani ambapo upendo wa Mungu “unakamilishwa” kwetu, kwa mujibu wa mfano huu? (Tunapovaa vazi la haki lililotolewa na Mungu. Tunapaswa kuwa makini tusichanganye Mungu anapobadilika kutoka kwenye neema ya jumla hadi kwenye upendo mkamilifu kwa utii wetu. Tunapaswa kumchagua Mungu, lakini kasoro kwa mgeni asiye na vazi la harusi ni kwamba alidhani mavazi yake yalikuwa yanakubalika kikamilifu kabisa. Matendo yetu mema hayatupatii wokovu.)
- Kuwapenda Wengine
-
- Soma 1 Yohana 4:19-21. Neema ya jumla inaendanaje na kuwachukia wengine? Unadhani Yohana alitumia neno “chuki” kwa makusudi? (Upendo wa neema ya jumla huwatendea wengine kwa haki, ikiwemo wale tusiowapenda. Hatuwatengi kwa ajili ya kuwatendea kivingine na isivyo sawa. Hicho ni kiwango cha chini cha upendo, na si kiwango tunachokitumia kwa marafiki na wanafamilia.)
-
- Soma Yohana 15:12-14. Je, Yesu anapandisha kiwango? Alikufa kwa ajili ya watu wote na hivyo tunapaswa kuyaacha yote kwa ajili ya maadui wetu? (Angalia ukomo unaopatikana katika kifungu cha 14. Sisi ni marafiki wa Mungu ikiwa tunamtii. Sidhani, baada ya uchunguzi wa kina, kama kiwango kimebadilika.)
-
- Soma 1 Yohana 3:16-17. Je, hii inapandisha kiwango upendo wa neema ya jumla ulio wa kiwango cha chini? Je, “ndugu” ni kitu kingine tofauti na kila mtu mwingine duniani? (Soma 1 Yohana 3:13. Yohana anatofautisha kati ya wale waliompokea Yesu na wale ambao ni “ulimwengu.”)
-
- Soma Mathayo 18:23-28. Kanuni ya neema ya jumla ni ipi? (Kutenda kwa usawa. Wote wanapaswa kulipa madeni yao.)
-
-
- Unaitumiaje kanuni ya neema ya jumla kwa mtu aliyesamehewa kiasi kikubwa cha fedha? (Hii inapandisha kiwango. Neema ya jumla ya Mungu kwetu ilimaanisha kuwa alikufa ili kutupatia fursa ya uzima wa milele. Tunapaswa kuwasamehe wengine.)
-
-
- Soma Mathayo 18:29-34. Je, msamaha wa Mungu ni wa “kiagano?” Ikimaanisha kuwa bado kanuni zinahusika?
-
-
- Chukulia kwamba mhalifu amemuua mtu wa familia yako. Je, unatakiwa kumsamehe mhalifu? Je, unatakiwa kuiomba serikali isimuue mhalifu? (Ninapendekeza kwamba tunatakiwa kusamehe – hiyo inaakisi msamaha wa Yesu kwetu. Lakini hatutakiwi kwenda zaidi ya neema ya jumla kwa suala la serikali. Hatutakiwi kuiomba serikali kuacha kanuni za jumla za adhabu.)
-
-
- Hebu tuangalie alichokisema Yesu kuhusu wale waliomshtaki isivyo haki, wakamtesa, sasa walikuwa wanamwua. Soma Luka 23:34. Je, Yesu anavuka mipaka ya neema ya jumla? Je, kimsingi anaiomba serikali isimuue mhalifu?
-
-
- Unadhani Mungu alijibu ombi la Yesu kwa jibu chanya? (Yesu anasema watu hawakujua walitendalo. Kwa hakika, baadhi yao walijua walilokuwa wakilitenda. Ninaamini Mungu anatupatia taarifa za kutosha kabla hajatekeleza hukumu pale tunapomkataa. Utakumbuka kuwa baada ya hapo Yerusalemu iliangamizwa na viongozi wa Kiyahudi walichinjwa.)
-
-
- Rafiki, je, uelewa wako juu ya upendo wa Mungu na wajibu wako kwa wengine vimeongezeka kupitia mjadala huu? Je, utadhihirisha neema ya jumla kwa watu wote huku ukikumbuka kile alichokutendea Yesu?
- Juma lijalo: Kumpendeza Mungu.