Somo la 9: Chanzo cha Uzima
Somo la 9: Chanzo cha Uzima
(Yohana 1, 3, & 6, Warumi 8)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Kwa mujibu wa makala ya tarehe 11 Februari, 2022 iliyoandikwa na Anshool Deshmukh, Ukristo ndio dini kubwa duniani (31%), ikifuatiwa na Uislamu (25%), Wasio na upande wowote (15.6%), Wahindu (15.2%), Wabudha (6.6%), dini za Jadi (5.6%), na Uyahudi (0.2%). Niliangalia makadirio mengine ya takwimu na kugundua kuwa takwimu zinafanana.
Tunapaswa kuhitimisha nini kutokana na hili? Kwamba, 31% ya watu duniani watakwenda mbinguni? Kwa muda mrefu nimewasikia watu wanaounga mkono “njia nyingi” za kwenda mbinguni. Jambo linalofanana na hilo ni dhana ya kwamba dini za mrengo wa Ibrahimu, kama Uislamu na Uyahudi, zinamwabudu Mungu mmoja, kiasi kwamba wao pia, wana njia ya kwenda mbinguni. Wengine wanaweza kudhani kuwa Yesu aliufanya uzima wa milele kinadharia uwezekane kwa watu wote, ili Mungu awapembue wale walio katika dini za Mashariki watakaokingia mbinguni. Ni ukweli kwamba Mungu atapembua kuwa nani anayeokolewa, lakini somo letu juma hili linabainisha kauli mahsusi kabisa kuhusu nani ambaye atafaulu ili kuokolewa. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuchimbue vigezo vya uzima wa milele!
- Kipimo cha Uzima
-
- Soma Yohana 3:16. Ni nini nia ya Mungu ya kuufanya uzima wa milele uwepo kwa wanadamu? (Upendo wake kwetu.)
-
-
- Ni nini kigezo cha kuupata uzima wa milele? (Kumwamini Yesu.)
-
-
- Soma Yohana 6:40. Ni nini mtazamo wa Mungu kwa wanadamu kuupata uzima wa milele? (Ni mapenzi ya Mungu kwamba tuwe na uzima wa milele, lakini mapenzi hayo yamejengwa juu ya vigezo.)
-
-
- Ni nini kigezo cha kuupata uzima wa milele? (Kumtazama na kumwamini Mwana.)
-
-
- Je, umegundua kwamba vifungu vyote viwili vya awali vilisema kuwa “kumwamini” Yesu ni kipimo cha uzima wa milele? Unadhani hiyo inamaanisha nini?
-
-
- Sehemu kubwa ya watu duniani inaamini kuwa Yesu alikuwepo. Angalao baadhi ya Waislamu (Washia) wanaamini kuwa Yesu atarudi katika nyakati za mwisho akiwa na Mahdi, ambaye ni Imam wa mwisho na mwokozi wao. Je, hiyo inafuzu kama kigezo cha “kumwamini” Yesu?
-
-
-
- Kwa nini Yohana 6:40 inarejelea “kumtazama” na “kumwamini?” (Hii inaashiria kuwa kunahitajika jambo kubwa zaidi ya kumtambua Yesu kama mtu.)
-
-
- Soma Yohana 6:63-64. Hapo awali tulijifunza tukio hili ambapo Yesu alitengeneza chakula na kisha anaanzisha kinachoonekana kuwa mjadala wa ajabu kuhusu kuula mwili wake na kuinywa damu yake (Yohana 6:53). Wasikilizaji wote waliamini kuwa Yesu alikuwepo, ukizingatia kwamba alikuwa akizungumza nao! Inatakiwa imani ya namna gani katika Yohana 6:64 na mjadala wa mwili na damu? (Tiketi yako ya kwenda mbinguni ni kuamini kuwa Yesu ni Mungu, na kwamba alikufa msalabani ili kulipa adhabu kwa ajili ya dhambi zako. Yesu alipokufa, na tukalipokea hilo kwa ajili yetu, adhabu yetu ya kifo ilitoshelezwa. Linganisha Mathayo 26:26-28 na 1 Wakorintho 10:16-17.)
-
-
- Hiyo inawaacha wapi watetezi wa “njia nyingi” na dini nyingi za hapa duniani? (Neno la Mungu linatuambia kuwa hawana vigezo vya uzima wa milele. Hawaamini kuwa Yesu ni Mwokozi wao. Kimsingi Mungu ndiye Hakimu wa mwisho, lakini kile tulichojifunza ni dhahiri.)
-
-
-
- Kama unaamini kile tulichojifunza hivi punde, hilo linakuachaje? Kujisikia? Kujiona bora?
-
-
-
- Tafakari hili. Ninahisi kwamba wasomaji wangu wengi, kama ilivyo kwangu, walikuzwa na wazazi wa Kikristo, au angalao kukuzwa katika nchi ambayo watu wengi ni Wakristo. Unadhani kuna uwezekano gani wa wewe kuwa Mkristo kama ungekuzwa na wazazi wa [ingiza dini tofauti] katika nchi [ya dini tofauti]?
-
- Kipimo cha Mantiki
-
- Soma Warumi 8:1-3. Chukulia kwamba ulikuzwa kama mshiriki wa dini yoyote ile hapa duniani. Silika yako ingekuambia nini kuhusu jinsi ya kuwa na mfumo wa maisha mapya na ya hali ya juu baada ya kifo? (Mantiki ingeniambia kuwa ningetakiwa kuyafanyia kazi kwa bidi. Lingekuwa jambo ambalo, kama ilivyo kwa mambo mengine mengi duniani, ningetakiwa kulipata kwa njia ya utendaji wa hali ya juu.)
-
- Angalia tena Warumi 8:3. Je, hitimisho langu lenye mantiki linaendana na Ukristo? (Hapana. Mungu alifanya kile ambacho wanadamu dhaifu hawakuweza kukifanya, kwa kumpeleka Yesu.)
-
- Soma Warumi 8:4. Yesu anatutendea nini kuhusiana na kuishika sheria? (Aliitimiza kwa ajili yetu. Alitimiza “maagizo ya torati” ndani yetu.)
-
-
- Kama bado hujafanya hivyo, fanya utafiti mdogo wa dini zote hapa duniani na ujiulize kama zote zinaendana na hitimisho langu lenye mantiki? (Jibu ni, “ndiyo,” zote zimejengwa juu ya matendo. Hata dini mpya ya kipagani ya “matendo ya chini,” Wicca, inafuata jambo linaloitwa the Wiccan Rede. Kimsingi dini hiyo inasema kuwa unaweza kufanya chochote utakacho alimradi tu haumdhuru mtu yeyote. Inahitaji matendo ya “kutokudhuru.”)
-
-
-
- Tunapaswa kufikia hitimisho gani kuhusiana na hili? Ukweli ni kwamba Ukristo uko tofauti, Mungu ndiye mtendaji. Lakini, je, hilo ni jambo jema? Je, hiyo inatushawishi kwamba Ukristo ndio dini pekee inayotupatia uzima wa milele? (Kimantiki, ndio dini pekee inayomwinua Mungu kuwa juu ya wanadamu. Matendo ya wanadamu, na hivyo majisifu ya wanadamu, ndio msingi wa dini nyingine zote za dunia. Kwa masikitiko, baadhi ya Wakristo wameangukia kwenye fikra hiyo hiyo.)
-
- Jambo Lisiloeleweka (The Incomprehensible)
-
- Soma Yohana 1:9-11. Kwa nini ulimwengu ulipaswa kumpokea Yesu? (Aliufanya ulimwengu.)
-
- Soma Yohana 1:12-13. Hii inazungumza nini kuhusu njia ya kuwa mtoto wa Mungu? (Si kwa njia ya uwezo binafsi, si kwa njia ya uwezo wa mwanadamu mwingine, inatoka kwa Mungu.)
-
-
- Kwa nini hili ni gumu sana kuliamini? (Yesu aliufanya ulimwengu! Je, unashindwa kuelewa kwamba anaweza kukupatia maisha mapya?)
-
-
- Soma Yohana 1:16-17. Musa na Yesu wanalinganishwaje? (Torati ilitolewa kupitia kwa Musa, neema ilitolewa kupitia kwa Yesu. Yesu ni Mungu na anaweza kuwapa neema wale wanaomwamini.)
- Mwendo (The Walk)
-
- Soma Warumi 8:5-8. Hebu subiri kidogo! Kuna mtu ambaye mara zote anakuja na kuharibu sherehe. Je, kitabu cha Warumi sasa kinatuambia kuwa Ukristo unafanana na dini nyingine yoyote ile kwa maana ya kwamba tunahitaji “kumpendeza Mungu,” kwa kuitii “sheria ya Mungu?”
-
- Soma Warumi 8:9-10. Nani anayefanya kazi hapa? (Roho Mtakatifu na Kristo.)
-
- Soma Warumi 8:11. Je, ni sehemu ya “matendo” yako kuwa na Roho Mtakatifu kukaa ndani yako?
-
- Hebu turejee nyuma na tusome tena Warumi 8:6. Utaelezeaje kinachomaanishwa kwako “kuyaweka mawazo yako” kwenye jambo fulani? (Mtazamo wangu ni kwamba haya si matendo, bali ukaribisho wa kuingia kwenye mtazamo. Kama kweli ninaamini kuwa mapichi (peaches) ni mazuri kuliko mapea (pears), basi nitanunua mapichi na si mapea. Kama unaamini kuwa Yesu alikufa kifo cha kutisha badala ya wewe kufa kifo hicho, na alifanya hivyo ili kutimiza adhabu kwa ajili ya dhambi zako, basi utaiepuka dhambi. Hutaikumbatia dhambi.)
-
-
- Ni rahisi kiasi gani kuyadhibiti mawazo yako? Je, unaweza kufanya uamuzi wa kuwa na mtazamo fulani na kisha kwa umadhubuti kuukubali (adopt) mtazamo huo? (Hii inafafanua dhana ya “kuyaweka mawazo yako.” Unaamua kwamba Kristo ni Bwana wako na unataka kuutangaza ufalme wake. Kisha Roho Mtakatifu anachukua suala la “kuyaweka” na kwa maombi yako, anabadili mtazamo wako katika uelekeo unaotakiwa.)
-
-
- Ruka vifungu kadhaa na usome Warumi 8:14-15. Kuna tatizo kubwa la hofu na wasiwasi kwa watu wa Marekani leo. Je, unadhani hilo linahusiana na dhambi? (Ninadhani hivyo. Ninachodhani kuwa kinamaanishwa na kitabu cha Warumi ni kwamba tunapofanya uamuzi kwa ajili ya Yesu, tunapomwomba Roho Mtakatifu kubadili mtazamo wetu, basi mabadiliko mengi chanya hutokea, ikiwemo kupungua kwa kiwango chetu cha hofu. Kwa nini? Kwa sababu tunamtumaini Mungu, hatujitumainii wenyewe.)
-
- Rafiki, je, “umemwamini” Yesu kwa namna tuliyojadiliana? Ikiwa ndivyo, unao uzima wa milele. Ikiwa hujamwamini, kwa nini usifanye uamuzi wa kumwamini na kuyaweka mawazo yako kwenye imani hiyo sasa hivi?
- Juma lijalo: Njia, Kweli na Uzima.