Somo la 7: Wamebarikiwa Wale Waaminio

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Yohana 8, 12, 18, 19 & 20
Swahili
Year: 
2024
Quarter: 
4
Lesson Number: 
7

Somo la 7: Wamebarikiwa Wale Waaminio

(Yohana 8, 12, 18, 19 & 20)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Nilikuwa na mjadala na mshiriki wa kanisa, mjadala ambao hatukukubaliana. Ghafla akaniambia, “Baba wangu alikuwa rais wa konferensi.” Ni hadi hapo baadaye ndipo nilitambua kuwa mjadala wetu ulikuwa nje ya mada kabisa. Alikuwa ananiambia kuwa mawazo yake yalikuwa ya muhimu (na kwamba huenda alikuwa sahihi) kwa sababu alikuwa binti wa mtu muhimu kanisani. Je, tunadhani kuwa tuko sahihi kwenye maoni yetu ya kidini kwa sababu ya wazazi au washirika wetu? Katika somo la hivi karibuni, mwamamke Msamaria pale kisimani alimwuliza Yesu kama yeye ni wa muhimu kuliko Yakobo. Juma hili viongozi wa Kiyahudi wanamwuliza Yesu kama yeye ni wa muhimu kuliko Ibrahimu. Umuhimu wa uhusiano huu ni upi? Je, mawazo ya watangulizi wetu yana thamani? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuangalie ushuhuda wa watu muhimu katika Biblia!

  1.    Ibrahimu
    1.    Soma Yohana 8:48. Chukulia kwamba uko kwenye mjadala na mtu kisha mtu huyo akadai kuwa wewe ni chanzo cha uovu na una jeni (genes) mbaya. Utamjibuje?
    1.    Soma Yohana 8:49-50. Yesu anajibuje mashtaka haya dhidi yake? (Anakana kwamba hana pepo, kisha anatetea kwamba matendo yake yanadhihirisha hivyo. Hatimaye, Yesu anatoa jibu la mtu mwenye mantiki. Kuniita majina mabaya ni shambulizi tu dhidi yangu, si hoja yenye mantiki. Mungu atahukumu.)
    1.    Soma Yohana 8:51-53. Tafakari shambulio hili jipya kwa Yesu. Je, lina mantiki? (Sehemu ya jibu ina mantiki. Yesu anawezaje kusema kuwa kama mtu atamfuata hatakufa, wakati Ibrahimu na manabii wote walioishi kabla wameshakufa? Lazima Yesu atakuwa anadai kuwa mkuu kuliko Ibrahimu na manabii.)
      1.    Kama ungekuwa Yesu, ungejibuje mashtaka haya?
    1.    Soma Yohana 8:54-56. Unalielewaje jibu la Yesu? (Anasema kuwa yeye ni mkuu. Anamjua Mungu binafsi. Ibrahimu aliitazamia siku ambayo Yesu atakuja!)
      1.    Inamaanisha nini kusema kuwa Ibrahimu “akamwona” Yesu akija duniani? (Soma Mwanzo 12:3. Mungu alimfunulia Ibrahimu kwamba Yesu atakuja. Haya ni madai ya kuwa Masihi, aliyeidhinishwa na Ibrahimu!)
    1.    Soma Yohana 8:57. Je, hii inaashiria kuwa kwa umri wake Yesu anaonekana kama mzee?
      1.    Ungekuwa na mtazamo gani juu ya jibu la Yesu kuhusu uhusiano wake na Mungu kama ungekuwa mmojawapo wa Wayahudi wanaozungumza naye?
    1.    Soma Yohana 8:58-59. Unapowaambia watu kwamba wewe una umri mkubwa kuwazidi, je, wanakutupia mawe? Nini kinaendelea hapa? (Kauli ya Yesu kwamba yeye ndiye “Mimi niko” iliwakumbusha kitabu cha Kutoka 3:14. Yesu anadai kwa uwazi kabisa kwamba yeye ni Mungu.)
    1.    Hebu tuangalie madai ya uhusiano yaliyobainishwa. Wayahudi katika Yohana 8:53 wanamuita Ibrahimu “baba” yao, na wanamwuliza Yesu juu ya madai yake kwamba yeye ni nani. Anajibu kuwa yeye ni Mungu, ambaye aliahidiwa kwa Ibrahimu. Wayahudi walipaswa kuwa na mwitiko (reaction) gani? Tunapaswa kuwa na jibu gani? (Tuna chaguzi mbili. Ama tuyaamini madai ya Yesu, au tujue kwamba Yesu ana wazimu. Sioni chaguzi nyingine zozote zile.)
  1.   Tomaso
    1.    Soma Yohana 20:24-25. Kwa nini Tomaso ana huu mtazamo? Je, alidhani kuwa wanafunzi wenzake wote ni waongo? Je, alidhani kuwa ahadi ya Yesu kwamba atafufuka kutoka katika wafu ilikuwa ya uongo? (Sidhani kama Tomaso aliamini kuwa wote walikuwa waongo. Badala yake, ninadhani Tomaso, kama ilivyo kwetu sote, alijaa majivuno. Majivuno yake yalikuwa yamejeruhiwa na alikuwa amesikitika sana kwamba Yesu aliwatokea wengine, lakini hakumtokea yeye.)
    1.    Soma Yohana 20:26-28. Chukulia kwamba majivuno ndilo tatizo la Tomaso, una maoni gani juu ya jibu la Yesu? (Faraja kuu namna gani! Yesu anakwenda mbali zaidi ili kumshawishi Tomaso. Hasemi kwamba, “Achana na majivuno yako.”)
    1.    Soma Yohana 20:29. Je, hili ni karipio?
    1.    Sasa tunapaswa kutafakari nini pale Yesu anaposema kuwa yeye ndiye “Mimi niko?” Je, tuna sababu za kutosha kuamini, badala ya kuhitimisha kuwa Yesu alikuwa na wazimu? (Tomaso anatupatia uthibitisho maalumu. Si tu kwamba Yesu yu hai, bali pia huu ni uthibitisho kwamba Yesu alisulubiwa. Kwa kuongezea tunaona kuwa Tomaso ni muumini mwenye kusitasita.)
  1.      Mariamu
    1.    Soma Yohana 12:1-3. Kuna umuhimu gani juu ya Lazaro kula pamoja na kundi hili? (Ni mtu aliyewahi kufa. Yesu alimfufua.)
    1.    Soma Yohana 11:20-21. Utakumbuka kwamba hapo kabla tulijadili kisa hiki katika mfululizo wa masomo haya. Kwa nini Mariamu hakutoka nje kumwona Yesu? Kwa nini Martha peke yake? (Mariamu amemkasirikia Yesu. Alimwacha Lazaro afariki.)
    1.    Soma Yohana 11:32-33. Unadhani Mariamu alidhani Yesu anapaswa kusema nini katika kujibu mashtaka yake? (Mariamu analia. Sidhani kama analitafakari hili kwa kina. Anafahamu tu kwamba Yesu amemwangusha.)
    1.    Soma tena Yohana 12:3. Hii inatuambia nini kuhusu badiliko la mtazamo wa Mariamu? (Lazaro amefufuliwa na Yesu na maisha ya Mariamu yamerejeshwa katika hali yake ya awali.)
      1.    Tulianza kwa kuzungumzia uhusiano. Uhusiano wa Mariamu kwa Lazaro ni wa muhimu kiasi gani tunapotafakari ushuhuda wake kumhusu Yesu? (Kama ufufuo wa Lazaro ulikuwa ni udanganyifu, kama kamwe haukuwahi kufanyika, Mariamu angeendelea kuwa na mtazamo wake wa awali wa hasira dhidi ya Yesu. Huu ni ushuhuda mkubwa kwamba ufufuo wa Lazaro ni jambo halisi. Sasa Mariamu amejawa na upendo kwa Yesu kwa kipimo cha kumwagika.)
  1.   Pilato
    1.    Pilato alikuwa Gavana, mwakilishi wa Rumi.  Sehemu ya kazi yake ilikuwa ni, kama ilivyo kwa hakimu wa zama za sasa, kusikiliza kesi. Hapo kabla Baraza la Sanhedrin la Kiyahudi lilikuwa limepitisha hukumu ya kifo kwa Yesu. Hata hivyo, Baraza la Sanhedrin halikuwa na mamlaka ya kutekeleza hukumu yake. Hivyo, Yesu alipelekwa kwa Pilato. Soma Yohana 18:28-29. Ungekuwa katika hali gani kiakili kama ungekuwa Pilato? (Tunaambiwa hii ilikuwa “mapema asubuhi,” na viongozi wa Kiyahudi wasingeweza kwenda katika makao makuu ya Pilato, hivyo ikampasa awaendee. Kama mtu muhimu, ningeudhika.)
    1.    Soma Yohana 18:30. Je, hali ya kiakili ya Pilato inaimarika? (Ningekasirika. Viongozi wa Kiyahudi wanamwambia Pilato asifanye kazi yake.)
    1.    Soma Yohana 18:33-34. Pilato anawapuuzia viongozi wa Kiyahudi na anaanza kumuuliza Yesu maswali katika makao makuu yake. Je, mambo yanamwendea vizuri Pilato? Je, anaheshimiwa na Yesu? (Mambo yanazidi kuwa mabaya. Sasa Yesu anamuuliza Pilato maswali.)
    1.    Hatutapitia mchakato wote wa kesi mbele ya Pilato. Soma Yohana 19:4-6 na Yohana 19:11-12 ili kuona mtazamo wa Pilato kwenye mashtaka dhidi ya Yesu. Unadhani Pilato aliufikiaje mtazamo huu? (Kama ungekuwa hakimu ambaye umezoea kuwaona watu wenye hatia, na umedhihakiwa kwa kile kinachoendelea, ungekuwa na mwitiko gani? (Kwani ninajali nini? Muueni mtu huyu asiye na heshima. Lakini hivyo sivyo ambayo Pilato aliliangalia jambo hili. Kuna jambo limetokea katika mazungumzo yake na Yesu lililosababisha Pilato atafute “namna ya kumfungua.”)
      1.    Kwa nini maoni ya Pilato ni ya muhimu sana? (Pilato hana ubaguzi kwenye mtafaruku huu. Anagundua kwamba Yesu hatafuti ufalme wa kidunia, huu ni mgogoro wa kidini – na Yesu hana hatia.)
    1.    Soma Yohana 19:19-22. Je, unadhani Pilato aliamini kuwa Yesu ni “Mfalme” wa dini ya Kiyahudi? (Asingeweza kudhani kuwa Yesu alikuwa “Mfalme” ambaye angeweza kuitia Rumi changamoto, vinginevyo Pilato angeshindwa kufanya kazi yake. Pilato kusisitiza kuandika kwamba Yesu ni “Mfalme wa Wayahudi” inamaanisha kuwa alidhani kwamba madai ya kidini ya Yesu yaliaminika.)
  1.    Yohana
    1.    Soma Yohana 21:24. Je, Yohana anaamini kuwa Yesu ni Mungu? (Ndiyo. Yohana anatuambia kuwa tunapaswa kumwamini kwa sababu ana sifa njema ya kuwa mkweli.)
    1.    Soma Yohana 20:30-31. Ni nini lengo la Yohana kuandika kitabu chake? (Kutushawishi kuamini kuwa “Yesu ndiye Kristo” ili “tuwe na uzima kwa jina lake.”)
    1.    Rafiki, je, unaamini? Uzima wa milele uko mbele yako. Kwa nini usikubali sasa hivi kwamba Yesu ni Mungu aliyekuja duniani? Hutakuwa na uamuzi wa muhimu zaidi kuliko huu.
  1.   Juma lijalo: Kutimiza Unabii wa Agano la Kale.