Somo la 6: Shuhuda Zaidi Kuhusu Yesu
Somo la 6: Shuhuda Zaidi Kuhusu Yesu
(Yohana 1, 6, & 7, na Mambo ya Walawi 17)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, umewahi kutafakari mantiki ya mfumo wa kafara wa Agano la Kale? Ukitenda dhambi kwa kukiuka sheria, kwa nini mnyama asiye na hatia auawe? Hilo halina mantiki. Kwa hakika kafara za wanyama au mwanadamu kwa miungu ya kipagani zipo katika baadhi ya jamii, lakini zinaonekana kuwa ni kwa ajili ya kuishukuru miungu badala ya adhabu kutokana na kikuika sheria. Baadhi ya tamaduni za Kikristo zilijitahidi kurejesha mantiki kwenye mfumo kwa kumhamasisha mfuasi kujipiga au kulipa adhabu kutokana na tabia mbaya ya dhambi. Hilo linaleta mantiki! Kutokuleta mantiki (illogic) kwa mfumo wa kafara wa Agano la Kale ni mojawapo ya ushuhuda mkubwa kwenye ukweli kwamba Yesu ni Masihi, Yeye ni Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu la kutokuwa na mantiki kunakothibitisha kuwa Bwana wetu ni Mungu!
- Mwana-kondoo
-
- Soma Yohana 1:32-34. Yohana Mbatizaji alijuaje kuwa mtu fulani ni Yesu, Mwana wa Mungu? (Yohana anakiri kuwa hakumjua Yesu, lakini Mungu aliyeanzisha utume wa Yohana alimwelekeza Yohana kwamba Roho Mtakatifu atashuka kama hua na kukaa juu ya “Mwana wa Mungu.”)
-
- Soma Yohana 1:29. Yohana anasema kuwa sifa mbili za Yesu ni zipi? (Sifa ya kwanza ni kwamba Yeye ni “Mwana-kondoo wa Mungu,” na ya pili ni kwamba “anachukua dhambi ya ulimwengu.”)
-
- Soma Mambo ya Walawi 1:3-4 na Mambo ya Walawi 5:5-6. Utaona kwamba vifungu hivi vinatumia maneno “upatanisho,” “hatia,” “dhambi,” na “upatanisho kwa ajili ya dhambi.” Ni nini lengo la vifungu hivi mahsusi, na zaidi sana Mambo ya Walawi kuanzia sura ya 1-7? (Haya ni maelekezo ya Mungu ya jinsi watu wake wanavyoweza kujikinga na adhabu na hatia kwa ajili ya dhambi zao.)
-
- Hebu tujadili anachokisema Yohana Mbatizaji kumhusu Yesu na kile tunachokiona katika Mambo ya Walawi kuhusu jinsi ya kukabiliana na dhambi.
-
-
- Weka kando yote unayoyafahamu kama Mkristo, na ujiulize kama mungu mwenye nguvu angependa kujitambulisha kama mwana-kondoo, mnyama wa kufugwa, au angependa kuondoa dhambi? (Haya yanaonekana kutoelekea kutokea (unlikely).)
-
-
-
- Sasa yachukue yote unayoyafahamu kuhusiana na mfumo wa kafara wa Agano la Kale, na ujiulize kama kumuita Yesu “Mwana-kondoo” na kuzungumzia juu ya kukabiliana na dhambi kunaleta mantiki? (Bado hili lina matatizo mengi ya kimantiki kwa mungu, lakini linaendana moja kwa moja na mfumo wa kafara wa Agano la Kale.)
-
- Chakula
-
- Utakumbuka kwamba katika Somo la 2 la mfululizo wa masomo haya tulijifunza muujiza wa kushangaza wa Yesu kuwalisha maelfu ya watu kwa kutengeneza mkate na samaki. Soma Yohana 6:14-15. Watu walijifunza nini kutokana na muujiza huu? (Kwamba Yesu alikuwa “nabii” ajaye aliyetabiriwa na Musa aliyesema kuwa kiongozi huyu atafanana naye. Kimsingi, Musa aliwatoa watu kutoka utumwani Misri, akaishinda Misri, na akawalisha watu katika safari yao kuelekea nchi ya ahadi.)
-
-
- Je, inaleta mantiki kuhitimisha kwamba Yesu ni Masihi Mfalme atakayewashinda Warumi wenye nguvu? (Naam. Maelezo haya yanaendana kikamilifu.)
-
-
- Kisa hiki kinaendelea siku inayofuata. Soma Yohana 6:26-27. Yesu anawaambia nini watu kuhusu uelewa wao wa utume wake? (Anawahamasisha kutafakari kuwa Yeye ni Masihi, lakini anawataka wayaangalie mambo katika mwanga wa kiroho.)
-
- Soma Yohana 6:31-33. Yesu anasema nini kinachoonekana kuwa cha ajabu kidogo kwa wasikilizaji wake? (Anajiita “chakula cha Mungu.”)
-
- Soma Yohana 6:47-52. Je, Wayahudi wanauliza swali lenye mantiki katika kifungu cha 52? (Ndiyo. Anachokisema Yesu ni kigumu kukielewa kwa kuzingatia uzoefu wa kila siku.)
-
- Soma Yohana 6:53-57. Ninapoyaandika haya, sikukuu ya Kimarekani inayojulikana kwa jina la “Halloween” imekaribia. Kula mwili wa mwanadamu na kunywa damu kunaendana vizuri sana na sikukuu hii ya kusikitisha. Ungekuwa unawaza nini kama ungekuwa unamsikiliza Yesu?
-
- Soma Yohana 6:58-60. Je, wanafunzi wa Yesu wanaelewa kile anachokisema? (Hapana. Wanasema kuwa hilo ni “neno gumu” na kulalamika kuwa ni vigumu kusikiliza mazungumzo ya aina hii.)
-
- Soma Yohana 6:61-63. Yesu anapofafanua “neno lake gumu,” je, anaashiria kuwa kiuhalisia anazungumzia kuhusu kula nyama ya binadamu na kunywa damu ya mwanadamu? (Hapana! Anasema kuwa anazungumzia kuhusu “roho na uzima.” Anasema kuwa kama wangeweza kumwona katika utukufu wake mbinguni, wangeelewa kwamba hazungumzii juu ya mambo ya kidunia.)
-
- Soma Yohana 6:64-69. Kitu gani ni cha muhimu ili kuyaelewa maneno ya Yesu kuhusu kula mwili na kunywa damu? (Lazima tuwe na uelewa “uliojaliwa” na Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Petro anaelewa na kusema kuwa Yesu “ndiye Mtakatifu wa Mungu.”
-
- Hebu twende kwenye kitabu cha Walawi na tusome kuhusu kafara. Soma Mambo ya Walawi 17:10-11, Kumbukumbu la Torati 18:3, na Kumbukumbu la Torati 12:17-18. Nani aliyekula kafara ya Agano la Kale? (Makuhani na watu. Walizuiwa kula damu kwa sababu ilifanya “upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu,” lakini wanaweza kula nyama.)
-
-
- Sasa hebu tafakari tulipoanzia kwa Yohana Mbatizaji kumuita Yesu Mwana-kondoo aichukuaye dhambi. Je, mjadala wa Yesu juu ya kula mwili wake ni jambo linaloleta mantiki kwa mtazamo wa kiroho? (Naam, kwa hakika kabisa! Yesu anawafundisha watu kwamba wakiliangalia hili kwa mtazamo wa kiroho wataona kwamba yeye ndiye anayetimiza lengo la mfumo wa kafara.)
-
-
- Hebu tuwazungumzie mashuhuda. Unapowatafakari mashuhuda ambao tuliwajadili katika masomo yaliyotangulia na sasa hivi, unadhani shuhuda gani ana ushawishi mkubwa zaidi? (Mungu ndiye shuhuda mwenye ushawishi mkubwa kuliko wote, lakini tatizo ni kwamba tunaye Yohana ambaye anasema kuwa Mungu alimwambia (Yohana 1:33-34) kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. Hatuna haja ya kuutegemea mtazamo wowote wa kibinadamu ili kuuelewa mfumo wa kafara wa Agano la Kale na jinsi kuja kwa Yesu duniani na kufa kwa ajili yetu kunavyoendana na mfumo huo.)
- Roho
-
- Soma Yohana 7:37-39. Unaielewaje kauli ya “Roho alikuwa hajaja?” (Hii ni rejea ya Matendo 2, ambapo wakati wa Pentekoste Roho Mtakativu aliwajaza nguvu wanafunzi wa Yesu.)
-
-
- Je, uzoefu wa maisha yako ni ushuhuda kwamba Yesu ni Mungu? (Juma hili nilikuwa katika kampasi ya Chuo Kikuu cha Andrews. Nilisimama mahali pale pale ambapo zaidi ya miaka hamsini iliyopita nilijiambia kuwa, “simwamini Mungu.” Kitendo hicho kilichukua takriban dakika kumi kwa sababu nilianza kufikiria maisha yangu yangekuwaje bila kuwa na Mungu. Baada ya kipindi hicho kifupi, kamwe sijawahi kuacha kumwamini Mungu kwa sababu ninamwona akifanya kazi maishani mwangu. Sasa, zaidi ya miaka hamsini baadaye, Mungu amekuwa nguvu itendayo kazi maishani mwangu. Hiyo imekuwa baraka ya namna gani kwangu!)
-
-
- Soma Yohana 7:46-49. Mafarisayo wanadhani ushuhuda gani ni wa muhimu sana? (Mafarisayo wanasema kuwa “mamlaka,” yaani wao, lazima zikubali kwamba Yesu ni Masihi.)
-
- Soma Yohana 7:50-51. Nikodemo ni mmojawapo wa “mamlaka,” je, anasema kuwa ushuhuda bora ni upi? (Kuusikiliza ushahidi na kujielimisha kuhusu habari za Yesu.)
-
-
- Je, hicho ndio ambacho tumekuwa tukikifanya?
-
-
- Rafiki, mfumo wa kisheria wa Marekani haumruhusu mwanasheria kuliambia baraza la wazee wa mahakama kile ambacho anaamini kuwa ndio ukweli. Wewe si mzee wa baraza, hivyo nitakuambia kuwa ninaamini kutokana na ushuhuda kwamba Yesu ni Masihi ambaye alishuka kutoka mbinguni, akaishi maisha makamilifu, akawa kafara yetu kamilifu ili kundoa dhambi zetu, na kisha akarejea mbinguni kwa ushindi mkuu ili tuweze kuwa na uzima wa milele. Je, utamwamini na kumkiri Yesu kama Bwana wako sasa hivi?
- Juma lijalo: Wamebarikiwa Wale Waaminio.