Somo la 13: Bwana Mfufuka

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Marko 16
Swahili
Year: 
2024
Quarter: 
3
Lesson Number: 
13

Somo la 13: Bwana Mfufuka

(Marko 16)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Tunaelekea kujifunza habari njema kabisa! Yesu alifufuka kutoka kaburini! Yesu aliwaahidi wanafunzi wake katika Marko 14:25 kwamba hatakunywa “uzao wa mzabibu” hadi atakapokuwa katika “ufalme wa Mungu.” Maana yake ni kwamba ataunywa mzao wa uzabibu akiwa na wanafunzi wake watakapokuwa pamoja tena, lakini safari hii wakiwa mbinguni! Aliahidi atarudi tena, na sasa tunaelekea kujifunza habari za kufurahisha kwamba Yesu alifufuka kutoka kaburini! Hebu tuzame kwenye somo letu la Marko!

  1.    Hayupo Hapa
    1.    Soma Marko 16:1-2. Kwa nini walisubiri hadi “Sabato ipite?” (Waliitunza Sabato ya siku ya Jumamosi kama siku takatifu. Hawakumwelewa Yesu aliposema kuwa Sabato ilipitwa na wakati.)
      1.    Walikuwa wanapanga kufanya nini? (Walipanga “kupaka manukato” mwili wa Yesu.)
        1.    Hii inazungumzia nini kuhusu uelewa wao kwamba Yesu atafufuka kutoka katika wafu?
      1.    Walipajuaje pa kumpata Yesu? (Soma Marko 15:46-47. Walimfuata Yesu hadi mahali Yusufu wa Arimathaya alipomuweka kaburini na kuviringisha jiwe mbele ya mlango.)
    1.    Angalia tena Marko 16:1. “Mariamu mamaye Yakobo” ni nani? Tuliposoma Marko 15:47 tuliona rejea ya “Mariamu mamaye Yose.” Je, watu hawa wawili ni mtu mmoja? (Soma Marko 6:3. Mamaye Yesu pia alikuwa mama wa Yakobo na Yose.)
        1.    Kwa nini Marko asimuite “mama wa Yesu?” (Mojawapo ya maoni yanaashiria kuwa Marko anatutaka tutafakari kuwa mwanamke huyo alikuwa nani. Hilo halina ushawishi. Nadhani Marko ana wasiwasi kuwa kwa kiasi fulani ufafanuzi wake unahafifisha uungu wa Yesu.)
    1.    Soma Marko 16:3. Kwa kuwa walikuwa wanajua habari za jiwe, kwa nini hawakuwachukua wanaume kwenda nao? (Huenda wanafunzi hawakuwa tayari, kutokana na hofu. Huenda wanawake wale hawakuwa na tafakari na kujipanga kwa kina. Kwa dhahiri, hawakuyajua matatizo waliyokabiliana nayo kutokana na matukio yaliyoandikwa katika Mathayo 27:64-66.)
    1.    Soma Marko 16:4-5. Kwa nini wanawake wale walishtuka (alarmed)? (Mwanzoni, inawezekana walidhani kuwa mwili wa Yesu ulikuwa umevurugwa walipoona kaburi liko wazi. Mara nyingi wanadamu wanapokutana na malaika huwa wanapata mshtuko. Yumkini huo ndio ufafanuzi.)
    1.    Soma Marko 16:6. Malaika anatambua kuwa chanzo cha mshtuko wao ni kipi? (Kwamba Yesu ametoweka.)
      1.    Kwa nini malaika yuko pale? (Zingatia upendo mkubwa wa Yesu kwao. Baada ya yote aliyoyapitia, na ushindi wake dhidi ya dhambi, anaweka mipango ya wanawake wale kuliwazwa.)
        1.    Unadhani Yesu ana wasiwasi juu ya faraja yako?
    1.    Soma Marko 16:7. Yesu anawajali watu gani wengine? (Wanafunzi.)
      1.    Je, ungewajali kwa upekee kama ungekuwa Yesu? (Wote walikuwa wamemtelekeza.)
      1.    Unadhani kwa nini Yesu anamtaja Petro kwa jina? (Tafakari mtazamo wa Bwana wetu. Petro alidai kuwa yeye ndio mwaminifu kuliko wote, lakini (isipokuwa Yuda), ukanaji wake ulikuwa mbaya kupindukia. Yesu anamkimbilia Petro. Anataka kumfariji.)
        1.    Je, unaweza kuanguka mbali sana kiasi kwamba Yesu hatakukimbilia?
      1.    Yesu anatimiza ahadi gani nyingine? (Soma Marko 14:28. Aliahidi kukutana nao Galilaya baada ya kufufuka kwake.)
    1.    Soma Marko 16:8. Wote walikuwa na dalili ya hofu. “Walikimbia,” walikuwa “wanatetemeka,” na hawakuzungumza. Kwa nini? (Matukio yaliwazidia kipimo (overwhelming). Wanajaribu kuyaelewa.)
    1.    Soma Mathayo 28:8-10. Mathayo anaongezea kwamba wanawake walipokuwa wanaondoka mbio, Yesu anakutana nao na kuwaambia kuwa wasiogope. Kwa nini sasa wanaogopa? (Huenda sasa tumefikia kwenye chanzo halisi cha mshtuko wao. Wamezidiwa na matukio yote yanayotokea. Kumbuka kwamba walikuwa na Yesu hadi saa zake za mwisho. Walimwona akiwekwa kaburini. Matukio haya ni makubwa mno kiasi cha wao kuweza kuyachakata kiurahisi.)
      1.    Kama ungekuwa unabuni na kuandika kisa hiki, je, ungejumuisha maoni yote haya kuhusu hofu na mshtuko? (Hapana. Tunapewa hisia halisi za kibinadamu za kuupitia uzoefu huu.)
      1.    Vipi kama wanawake wale wangekuwa wamezipokea kauli za Yesu kikamilifu kuhusu kuuawa kwake na kufufuka kutoka katika wafu? Je, wangeyapokea mambo yote haya kwa ujasiri na furaha?
      1.    Kama ungekuwa Marko, je, ungeachana na injili yako hadi kufikia hapa?
  1.   Anajitokeza
    1.    Kabla hatujajadili vifungu vinavyofuata, ni muhimu kuzingatia suala ambalo linaibuliwa mara kwa mara. Tafsiri za Biblia zilizojengwa juu ya nakala zisizokamilika (partial) na nakala kamili za awali za vitabu kwa kiasi kikubwa ni za kuaminika. Hakuna vitabu halisi (original) vya Agano Jipya ambavyo vipo. Hakuna kitu chochote halisi kilichoandikwa wakati, au miaka mia moja baada ya maisha ya Yesu ambacho kipo. Badala yake, kilichosalia ni nakala za nakala za vitu halisi. Kutokana na kasoro za kibinadamu, isipokuwa kama kuna sababu ya kutilia shaka nakala fulani, kanuni yenye mantiki ni kwamba kadiri nakala inavyozidi kuwa ya zamani zaidi, uwezekano mkubwa ni kwamba itakuwa sahihi. Miaka 200 iliyopita imeleta uvumbuzi wa nakala nyingi za ziada na za kale sana – jambo linalotupatia ushahidi bora kabisa wa kile ambacho kwa asili Biblia ilikisema. Marko 16:9-20 haipatikani kwenye miswada miwili ya mwanzo kabisa. Hata hivyo, tutasoma vifungu hivyo kwa sababu mbili. Kwanza, injili nyingine zinaandika taarifa inayofanana. Pili, kiongozi wa kanisa la awali, Irenaeus, alinukuu kutoka Marko 16:19. Irenaeus aliishi kuanzia mwaka 120-205 Baada ya Kristo. Miswada ya awali inayoacha (isiyojumuisha) Marko 16:9-20 haikunakiliwa hadi mamia ya miaka baadaye. Hiyo inamaanisha kuwa sehemu hii ya Marko 16 ilikuwa inatumiwa na Wakristo muda mfupi sana baada ya andiko la asili kuandikwa.
    1.    Soma Marko 16:9-11. Kama ungekuwa mwanafunzi, ungependa kuamini nini? Kwa nini usiamini habari njema?
    1.    Soma Marko 16:12-13. Je, haya ni maelezo mengine tu ya kutokuamini? Au, hili ni jambo la muhimu linalojitegemea? (Hii inaakisi maelezo ya “Njiani Kuelekea Emau” katika Luka 24 ambapo Yesu anawatokea wanafunzi wa kiume wawili. Njia ya jumla ya marabi ilikuwa ni kutowajumuisha wanawake kama mashuhuda. Hivyo, ukataaji huu wa pili wa ukweli kutoka kwa mashuhuda wa kiume unaonesha ugumu wa upinzani wa kuzipokea na kuzikubali habari hizi njema.)
    1.    Soma Marko 16:14. Yesu anafanya nini kuhusu kutokuamini? (Kwanza, anajitokeza mwenyewe ili kuthibitisha kuwa amefufuka. Pili, Yesu anawakemea kwa “kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao.”)
      1.    Kama wanafunzi waliuiba mwili wa Yesu na walikuwa wanatengeneza uongo juu ya kufufuka kwake kutoka katika wafu, je, Marko angeandika jambo kama hili?
      1.    Wanafunzi wanawezaje kuwa na “moyo mgumu” kuhusu Yesu kufufuka? Je, wameamua kuwa miaka yao mitatu wakiwa na Yesu ilikuwa ni kupoteza muda? (Sidhani. Karipio ni kwa ajili ya kutokuamini taarifa za awali. Kwa kuwa sasa Yesu yupo pamoja nao mashaka yote yametoweka.)
  1.      Anaamuru
    1.    Soma Marko 16:15-16. Je, hii pia ni amri kwetu?
      1.    Suala gani la “kuamini” linahusika hapa? (Kiini ni imani kwamba Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu na akafufuka. Hiyo ni imani ambayo imekuwa ikipingwa na wale ambao Yesu alikuwa anazungumza nao.)
    1.    Soma Marko 16:17-18. Uthibitisho wa imani ni upi? (Uwezo wa Mungu na ulinzi wa Mungu.)
      1.    Utasema nini kama washiriki wa kanisa lako wataanza kuonesha ishara hizi za imani? Je, Yesu atakuwa na haja ya kukukemea kwa “kutokuamini na ugumu wa moyo” (Marko 16:14)?
    1.    Soma Marko 16:19-20. Je, kisa chako kina mwisho wenye furaha? (Ndiyo! Yesu alikwenda mbinguni na kukaa mkono wa kuume wa Mungu. Lakini hakuwaacha wanafunzi wake wajitafutie wenyewe. Aliendelea tu kufanya kazi pamoja nao.)
    1.    Rafiki, je, unaamini? Lengo la Marko limekuwa ni kutushawishi kuwa Yesu ni Mungu. Kutushawishi kuwa Yesu alikuja ili afe. Na kutushawishi kuwa alifufuka ili kwamba sisi, ambao tunaamini na kubatizwa, tuweze kumfuata mbinguni. Kama huamini, kwa nini usichukue uamuzi wa kuamini sasa hivi?
  1.   Juma lijalo: Tunaanza kujifunza injili ya Yohana.