Somo la 10: Siku za Mwisho

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Marko 12 & 13
Swahili
Year: 
2024
Quarter: 
3
Lesson Number: 
10

Somo la 10: Siku za Mwisho

(Marko 12 & 13)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kama unasoma somo hili, uwezekano mkubwa ni kwamba unaamini kuwa Mungu yupo, Yesu alikuja duniani, akaishi maisha makamilifu kwa niaba yetu, akalipa deni letu kwa ajili ya dhambi kwa njia ya kifo chake, na akafufuka katika uzima wa milele ili kwamba tuweze kumfuata mbinguni. Kuna nini kingine cha kukiamini? Masuala gani mengine yanaweza kuhafifisha imani yetu kwa Mungu? Suala moja kubwa ni ujio wa Yesu Mara ya Pili. Kila kizazi kinaamini kuwa Yesu atakuja katika kipindi cha uhai wao. Lakini imani hiyo inahafifishwa na ukweli kwamba vizazi vyote vilivyotangulia havikuwa sahihi. Hebu tuzame kwenye Biblia na tuone kile ambacho Marko anatufundisha kuhusu imani na ujio wa Yesu Mara ya Pili!

  1.    Imani (Tumaini)
    1.    Soma Marko 12:41-44. Unadhani suala hili ni fundisho la jinsi tunavyopaswa kutoa kanisani? (Ikiwa hivyo ndivyo, basi haina mantiki yoyote.  Pesa ya mjane haikuleta tofauti yoyote kwenye utendaji wa hekalu. Kwa upande mwingine, angeweza kufa kwa njaa kali endapo asingetokea mtu wa kumpa chakula. Kiuhalisia, anatoa hekaluni kile ambacho mtu mwingine atampatia kwa ajili ya chakula.)
    1.    Soma Mambo ya Walawi 19:9-10. Ni nini wajibu wa mkulima kwa maskini? (Anaacha pembe za shamba lake, na chochote kile kilichoanguka chini kwenye mchakato wa uvunaji kwa ajili ya maskini kuja kuokota.)
      1.    Mkulima ana haki ya kusalia na nini? (Mavuno mengi kabisa. Kwa ujumla pembe ya shamba huwa haina uzalishaji mkubwa.)
    1.    Soma Mambo ya Walawi 27:30-32. Ni nini wajibu wa mkulima kwa Mungu kutokana na kiasi alichokivuna? (Mungu anadai 10% na mkulima anabakiwa na 90%. Wale ambao ni wataalamu katika sheria ya Kilawi wanafahamu kwamba suala hili ni gumu zaidi, lakini kinachomaanishwa kinasalia kuwa ni kwamba mkulima anasaliwa na sehemu kubwa ya kile anachokivuna.)
    1.    Angalia tena Marko 12:43-44. Je, sadaka za “matajiri” zinaendana na mafundisho ya kitabu cha Mambo ya Walawi? (Ndiyo. Matarajio ya maelekezo ya Mungu katika kitabu cha Walawi ni kwamba watu wake “wachangie zaidi ya mali iliyowazidi.”)
      1.    Hapo awali tulijifunza kauli ya Yesu kwa kijana mdogo tajiri kwamba anapaswa “akauze alivyo navyo vyote na kuwapa maskini” (Marko 10:21). Je, Yesu anatoa sheria mpya juu ya utoaji? Je, anabadili sheria ya Kilawi kwenye suala la fedha kama alivyobadili sheria za Kilawi kwenye suala la ndoa?
    1.    Soma Matendo 5:1-4. Hapa Petro alibainisha jambo gani kuwa ni dhambi? (Kudanganya. Isingekuwa vibaya kwa wao kuendelea kuwa na mali au fedha yao. Sidhani kama Yesu alibadili sheria. Wala Petro pia hakufanya hivyo.)
      1.    Kama Yesu habadili sheria kuhusiana na utoaji, Yesu anamaanisha nini? (Kinachomaanishwa kwa wote wawili, yaani, kijana mdogo tajiri na mjane ni kumtumaini Mungu. Imani ndilo suala la msingi kwa kile ambacho Marko anakielezea katika sehemu inayofuata.)
  1.   Maisha Yaliyopinduliwa Juu Chini
    1.    Soma Marko 13:1-4. Kama ungekuwa hawa wanafunzi wanne, uangamivu kamili wa hekalu ungemaanisha nini kwako? (Ingemaanisha mwisho wa taifa lao na moyo wa dini yao.)
    1.    Soma Matendo 1:6. Hekalu linahusishwaje na mipango ijayo ya wanafunzi? (Walidhani watakuwa wanaliendesha hekalu na taifa!)
    1.    Angalia tena Marko 13:3. Kwa nini wanafunzi hawa wanne walimwendea Yesu kwa faragha ili kujadili suala hili? (Hakukuwa na jambo la muhimu zaidi kuliko kupata uelewa kamili wa utabiri wa kushtusha wa Yesu.)
    1.    Soma Marko 13:5-9. Unadhani wanafunzi wanaamini kuwa Yesu anafafanua nini? (Mustakabali wao. Yesu anawaambia kwa umahsusi kile kitakachowatokea katika masinagogi. Hizi zote ni habari za kutisha.)
    1.    Soma Marko 13:10-13. Mjane na fedha zake anawafundisha nini wanafunzi? (Mtumaini Mungu katika nyakati ngumu zijazo.)
  1.      Chukizo
    1.    Soma Marko 13:14-17 na Mathayo 24:15-19. Je, Mathayo na Marko wanaandika utabiri wa Yesu unaofanana? (Ndiyo.)
      1.    Mathayo anaandika jambo gani ambalo ni tofauti na analoandika Marko? (Mathayo ananukuu utabiri wa Danieli.)
    1.    Soma Danieli 9:26-27. Danieli anafafanua nini? (Jambo lile lile – kuangamizwa kwa hekalu.)
      1.    Utaona kuwa Marko 13, Mathayo 24 na Danieli 9 zote zinatabiri kuangamizwa kwa hekalu kutokana na chukizo la uharibifu. Unadhani hiki ni nini? (Yesu anatabiri mustakabali wa hekalu. Danieli 9 inahusisha hili na “masihi” ambaye “anakatiliwa mbali.” Hiyo inaunga mkono hitimisho pekee lenye mantiki kwamba Yesu anazungumzia kuhusu Rumi kuiangamiza Yerusalemu na hekalu lililojengwa baada ya kifo cha Yesu.)
      1.    Baadhi ya watoa maoni, kama vile John MacArthur, wanaviangalia vifungu hivi katika Mathayo 24 vikijumuisha uangamivu ujao wa hekalu mwaka 70 B.K., lakini pia uvamizi wa Antiochus Epiphanes, mwaka 168 K.K. Je, inaonekana kuwa na mantiki kwamba Yesu anazungumzia jambo lililotokea miaka 200 kabla? (Hilo halileti mantiki. Yesu anajibu maswali ya wanafunzi kuhusu kauli yake kwamba hekalu litaangamizwa.)
  1.   Ujio wa Mara ya Pili
    1.    Soma Marko 13:19-23, Ufunuo 7:14, na Danieli 12:1-2. Utaona kwamba vifungu vyote hivi vitatu vinazungumzia taabu au wakati wa dhiki, usio na mfano. Je, unadhani vifungu hivyo vinarejelea tukio la aina moja? (Nadhani.)
      1.    Je, hii dhiki kubwa ni anguko la Yerusalemu baada ya kifo cha Yesu? (Kwa ujumla haionekani kuwa hivyo, na Danieli 12 inaifungamanisha na kipindi kabla ya ujio wa Yesu Mara ya Pili.)
    1.    Soma Marko 13:24-27. Sasa Yesu anafafanua tukio gani? (Kwa wazi kabisa anazungumzia juu ya ujio wake wa Mara ya Pili.)
      1.    Tunapotafakari kauli ya wazi ya Yesu kwamba “baada ya dhiki” (Marko 13:24) atakuja, na kauli ya Yesu kuhusu watu wa Mungu kuokolewa kwa ujio wa Mara ya Pili, inaleta mantiki kuhitimisha kwamba kipindi hiki cha dhiki kuu kipo katika siku zijazo na kinafungamanishwa na ujio wa Yesu Mara ya Pili.)
    1.    Soma Marko 13:28-31. Yesu anatoa hakikisho kwamba kauli yake kuhusu mustakabali wa siku zijazo ni wa kuaminika zaidi kuliko uwapo wa mbingu na nchi. Kama utabiri wa Yesu hautatokea, je, tunapaswa kuamini chochote anachokisema? (Yesu anaweka rehani hadhi yake kwenye utabiri huo. Lazima uwe wa kweli au vinginevyo hataaminika.)
      1.    Jikite kwenye Marko 13:30. Unalielezeaje hili? Yesu hakurejea katika kipindi cha uhai wa wanafunzi. (Tunafahamu kwamba Yesu anajadili matukio mawili. Kuangamizwa kwa hekalu na ujio wake Mara ya Pili. Kuangamizwa kwa hekalu kulitokea katika kizazi cha wanafunzi.)
    1.    Angalia tena Marko 13:30. Utaona kwamba Yesu anarejelea “hayo yote,” na sio tu nusu ya mambo ambayo amekuwa akiyajadili. Unalielezeaje hilo? Kuangamizwa kwa hekalu pekee ndiko kulikotokea katika kizazi chao. (Hebu tuendelee kusoma.)
    1.    Soma Marko 13:32-37. Ni tukio gani la “siku au saa ile” ambalo Yesu analijadili hapa? (Ujio wake Mara ya Pili.)
      1.    Angalia tena Marko 13:32. Yesu anaelezea nini kuhusu uelewa wake wa kipindi cha ujio wake Mara ya Pili? (Anasema hajui muda huo utatokea lini.)
      1.    Hebu tuunganishe kauli za Yesu kuhusu muda wa kutukia kwa matukio tuliyoyajadili. Anatoa hakikisho kamili kuhusu muda wa kuangamizwa kwa hekalu, lakini anasema kuwa hajui muda wa ujio wake Mara ya Pili. Unapoangalia kauli kamili ya Yesu, je, anaaminika? (Ndiyo! Anaeleza kile anachokijua na kile asichokijua.)
      1.    Unajua kwa nini Yesu alianzisha mjadala huu na uchunguzi wake (His observations) kuhusu mjane aliyetoa senti mbili? (Tunakuja kikamilifu. Yesu anatutaka tuamini mustakabali wetu ujao kwake kama ambavyo mjane alitumaini na kuamini mustakabali wake kwa Mungu.)
    1.    Rafiki, je, utamwamini Mungu? Kuelewa alichokisema Mungu kuhusu mustakabali wa siku zijazo katika kitabu cha Danieli, Ufunuo, Marko, na Mathayo sio sayansi kamili. Tunaweza kuelewa isivyo (misunderstand). Kumtumaini Mungu kwa ajili ya mustakabali wa siku zijazo ni sayansi kamili. Je, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, utadhamiria kumtumaini Mungu kwa kumkabidhi mustakabali wako wa siku zijazo?
  1.    Juma lijalo: Kuchukuliwa na Kushtakiwa.