Somo la 2: Siku Moja Katika Huduma ya Yesu
Somo la 2: Siku Moja Katika Huduma ya Yesu
(Marko 1:16-45)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Nchini Marekani tuna siku ambazo tunawatia moyo wazazi kuwapeleka watoto wao (kila mtoto kwa wakati wake) kufanya kazi ili watoto wajifunze kile ambacho wazazi wao wanakifanya kazini. Hivyo ndivyo ambavyo ninaona somo letu linafanana. Marko alianza injili yake kwa kutangaza kwamba Yesu alikuwa Mwana wa Mungu, na kisha akatupatia ushahidi kutoka kwenye Biblia. Halafu Marko akaongezea idhinisho kutoka kwa Yohana Mbatizaji, Mungu Baba, na Roho Mtakatifu! Baada ya hapo Marko anatupeleka kushuhudia anachokitenda Yesu anapoanza utume wake. “Huyu ni Mungu na angalia jinsi anavyoutumia muda wake.” Linaonekana jambo bora sana kwangu, hivyo hebu tuzame kwenye Injili ya Marko na tutumie siku yetu tukiwa na Yesu!
I. Kuwachagua Wasaidizi
A. Soma Marko 1:16-18. Kwanza, jiweke kwenye nafasi ya Yesu. Kwa nini awachague wawili hawa kuwa wanafunzi? Je, alikuwa na wasiwasi wa kutokuwa na chakula cha kutosha? Marko hazungumzii chochote kuhusu kuwachagua kwa sababu ya umahiri wao wa kiteolojia.
1. Sasa badilisha majukumu. Kwa nini wavuvi hawa wawili wanaamua kuacha zana zao za uvuvi ili “kuwa wavuvi wa watu?”
a. Na “wavuvi wa watu” inamaanisha nini?
B Soma Yohana 1:35. Yohana ni nani na kwa nini ana wanafunzi? (Huyu ni Yohana Mbatizaji, mhubiri mashuhuri sana katika kipindi hicho. Kimsingi alikuwa na wanafunzi.)
C. Soma Yohana 1:36-37. Ghafla, Yohana anapungukiwa wanafunzi wawili. Kwa nini? (Yohana amembainisha Yesu kama Masihi. Wanafunzi wawili wa Yohana wanaondoka mara moja ili kumfuata Yesu.)
D. Soma Yohana 1:38. Wanafunzi hawa wawili wanapaswa kumjibuje Yesu? (Hivi punde tumetoka kusikia kwamba wewe ni Masihi, na tunataka kuwa sehemu ya kazi yako.)
1. Wanatoa jibu gani tofauti? (Unakaa wapi?)
a. Kwa nini wanatoa jibu kama hilo? Linaonekana kama jibu la kipumbavu. Jiweke kwenye nafasi yao na uone kama hili ni jibu ambalo ungeweza kulitoa? (Wameambiwa kuwa Yesu ni mtu wa muhimu sana katika historia ya ulimwengu. Itakuwa ni suala la kujiamini mno kusema, “Tunadhani tunapaswa kuwa wanafunzi wako.” Kwa sababu hiyo wanatoa jibu lenye uthabiti mdogo.)
E. Soma Yohana 1:39. Kama ungekuwa kwenye kundi hili la wanafunzi wawili, ungelichukuliaje jibu la Yesu? (Hamasisho kubwa kiasi gani! Yesu anawakaribisha kuambatana naye.)
F. Soma Yohana 1:40-42. Watu hawa wawili ni akina nani wanaotaka kuwa wanafunzi wa Yesu? (Andrea na Simoni.)
1. Rejea nyuma na uangalie Marko 1:16-17. Je, Marko anaacha kujumuisha taarifa za muhimu sana? Au hili ni kutaniko la pili kati ya Yesu, Andrea na Simoni? (Ukiendelea na kisa katika Yohana 1, hakiendi zaidi ya Andrea na Simoni kumfuata Yesu hadi pale alipokuwa akikaa, na kisha kuwa naye. Katika kitabu cha Marko inaonekana tunaona kutaniko la pili ambapo Yesu anawapa mwaliko rasmi wa kuwa wanafunzi. Kimsingi wanakubali mara moja.)
G. Soma Marko 1:19-20. Je, wanafunzi hawa wawili wanaonekana kuwa tofauti na Simoni na Andrea? (Simoni na Andrea walikuwa na nyavu. Yakobo na Yohana wanamiliki boti. Wao ni sehemu ya biashara ya familia ambayo ina waajiriwa. Hawa ni wavuvi wenye mafanikio!)
1. Swali linabakia, kwa nini Yesu anawaajiri kuwa wanafunzi wake? Bila kujali kama Yesu anawaajiri wavuvi masikini au wavuvi wenye mafanikio, bado hawana vigezo vya kufanya kazi iliyokusudiwa, sawa?
2. Yesu anaposema katika Marko 1:17 kwamba atawafanya kuwa “wavuvi wa watu,” je, Yesu anasema kuwa ujuzi wao wa kazi unaweza kuhamishika? Wavuvi wazuri? Mnaweza kuwa wainjilisti wazuri!
H. Hebu tusome nje ya injili ya Marko ili tuweze kunyoosha kweli zetu. Soma Luka 5:10. Je, Yakobo na Yohana wana ushirika wa kibiashara na Simoni? (Ndiyo. Hili sio suala la wavuvi masikini dhidi ya wavuvi matajiri. Wote kwa pamoja wapo kwenye biashara moja.)
I. Kama ukisoma kitabu cha Marko pekee, inaonekana kwamba Simoni, Andrea, Yakobo, na Yohana wote walimfuata Yesu mara moja – na hiyo inaweza kuwa sifa yao bora kwa ajili ya kazi inayohusika. Luka anaandika maelezo tofauti. Pitia kwa haraka haraka Luka 5:1-3 na usome Luka 5:4-5. Simoni anafahamiana na Yesu kwa kiasi gani? (Anamfahamu. Anamwita “Bwana mkubwa,” na kukubali kutenda jambo linalokinzana na maoni ya utaalamu wa Simoni.)
J. Soma Luka 5:6-11. Simoni Petro (pamoja na wale wengine watatu) wanadhihirisha sifa gani ili kuwa wanafunzi wa Yesu? (Sasa wanaamini kutokana na uzoefu binafsi kwamba Yesu ni Mungu. Yeye ni Masihi!)
II. Ushuhuda wa Pepo Mchafu
A. Soma Marko 1:21-24. Unadhani kwa nini Marko anajumuisha hili idhinisho la pepo mchafu la utambulisho wa Yesu? (Pepo wachafu ni wadanganyifu, lakini hili linaonekana kama ukweli. Pepo mchafu anamwogopa Yesu na anakiri mustakabali wake.)
B. Soma Marko 1:25. Kwa nini Yesu anakataa idhinisho la kishetani? (Yesu hataki kujihusisha na pepo wachafu. Hataki msaada wao. Na, kikubwa anachokijali ni kwa mtu ambaye amepagawa pepo.)
C. Soma Marko 1:26-28. Hii inaashiria kuwa Yesu ana uhusiano gani na pepo wachafu? (Angalia kinyume chake. Yesu hatafuti idhinisho la pepo mchafu ili kuinua msimamo wake. Anawaamuru pepo wachafu na wanatii. Yesu ni mtu wa vitendo na uwezo!)
D. Angalia tena Marko 1:23. Kwa nini pepo huyu mchafu alikuwa kanisani? Kama alidhani kuwa Yesu anaweza kumwangamiza au kuliweka huru windo lake, kwa nini afanye bahati nasibu?
III. Kuibariki Familia
A. Soma Marko 1:29-31. Hapa ilikuwa Sabato. Je, ni sahihi kuponya na kutumikia siku ya Sabato? (Yesu anaponya na mwanamke anatumikia. Hakuna maoni mabaya kuhusiana na hili.)
B. Soma Marko 1:32-33. Kwa nini kundi la watu liliibuka baada ya “kuchwa kwa jua?” (Watu walidhani kuwa ama safari au uponyaji uliotarajiwa usingekuwa sahihi wakati wa Sabato.)
C. Soma Marko 1:34. Marko anatupatia uthibitisho gani kwamba Yesu ni Masihi? (Uponyaji, uwezo dhidi ya pepo wachafu, na kwamba pepo wachafu wengi (wote?) walimjua kwamba Yeye ni nani.)
IV. Mwenye Ukoma Mzungumzaji Kupita Kiasi
A. Soma Marko 1:40. Je, mwenye ukoma anaamini kuwa Yesu ni Masihi? (Anampigia magoti na kusema kuwa uponyaji wake ni suala la endapo Yesu yuko radhi na sio kama Yesu ana uwezo.)
B. Soma Marko 1:41. Je, Yesu anajali matatizo yetu? (Ndiyo.)
C. Soma Mambo ya Walawi 5:3. Kwa nini Yesu anamgusa mwenye ukoma? (Kifungu hiki kinasema kuwa kumgusa mtu asiye safi husababisha “hatia.” Mambo ya Walawi 5:5 inasema kuwa lazima dhambi hii itubiwe. Yesu hakuhitaji kumgusa ili kumponya, mguso unaonesha huruma na upendo wa Yesu.)
D. Soma Marko 1:42. Je, Yesu alikuwa akitenda dhambi kwa kumgusa mwenye ukoma? (Yesu alipomgusa hakuwa tena najisi.)
E. Soma Marko 1:43-45. Kwa nini mwenye ukoma hamtii Yesu wakati Yesu aliweka bayana (“usimwambie mtu neno lolote”) kuwa mwenye ukoma anapaswa kufunga mdomo wake kuhusiana na muujiza wake?
F. Soma tena Marko 1:38 na Marko 1:45. Mwenye ukoma amemsababishia Yesu tatizo kubwa kiasi gani?
1. Vipi kuhusu wagonjwa wengine na wengine waliopagawa na pepo ambao sasa wataendelea kuwa wagonjwa na kupagawa pepo?
2. Je, Yesu alipaswa kuacha kumponya mwenye ukoma?
a. Ukweli kwamba Yesu alimponya mwenye ukoma inatuambia nini kuhusu asili ya mtazamo wa Mungu dhidi ya matatizo yetu?
3. Je, mwenye ukoma alidhani alikuwa anatenda jambo sahihi kwa kuwaambia wengine habari za Yesu? (Ninaamini kabisa kuwa alidhani hivyo. Hili ni onyo kuhusu kufuata kile tunachodhani kuwa ni sahihi tofauti na kile ambacho Mungu anatuambia tukitende.)
4. Je, kazi ya Yesu inasimamishwa na mwenye ukoma? (Hapana. Iliifanya tu kuwa ngumu zaidi kwa watu kumwona Yesu.)
G. Rafiki, umejifunza nini kumhusu Yesu baada ya kukaa naye kwa hii siku moja? Nimejifunza kwamba Yesu ni Mungu, na Yesu ana huruma kubwa na upendo kwetu. Je, huyu ni mtu, kama ilivyokuwa kwa mvuvi, ambaye ungependa kumfuata? Kwa nini usiamue kuwa mfuasi wa Yesu sasa hivi?
V. Juma lijalo: Mabishano.