Somo la 5: Imani Pale Ionekanapo Kutowezekana
Somo la 5: Imani Pale Ionekanapo Kutowezekana
(2 Timotheo 3, 2 Petro 1, 2 Wakorintho 4, Waefeso 2)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Unakielewaje kichwa cha habari, “Imani pale ionekanapo kutowezekana?” Je, imani ni suala la kubahatisha? Mtu anapotafakari kama amwamini Mungu au la, je, imani ni suala lisiloyamkinika (unlikely)? Kama umekielewa kichwa cha habari cha somo letu kwa namna hiyo, hilo si somo letu la juma hili. Badala yake ninaamini kile alichokiandika Paulo kwenye Warumi 1, kama humwamini Mungu basi haufikirii vizuri. Isivyo bahati, kihistoria watu wenye kutafakari kwa kina wamekabiliana na magumu walipokuwa wakiishi na kushiriki fikra zao na jamii ya kilimwengu (secular society). Juma lililopita tulijadili jinsi ya kusambaza injili kwa wengine. Juma hili tunageukia kikamilifu kwenye mada ya kile tunachopaswa kukiamini na kukisambaza. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia!
I. Baraka za Somo
A. Soma 2 Timotheo 3:16-17. Biblia ilitengenezwaje? (Iliandikwa kwa pumzi ya Mungu.”)
1. Kama hukuwa na msingi wa Kikristo, kwa dhahiri hiyo ni kauli isiyo ya kawaida. Unadhani inamaanisha nini? (Soma Yeremia 1:9. Hii inatuambia kuwa Mungu anaweka maneno yake kinywani mwa mwandishi wa Biblia.)
2. Wakati bado tukiendelea kuangalia 2 Timotheo 3:16-17, kuna uzuri gani katika kusoma na kujifunza Biblia? (Inatuweka tayari kwa ajili ya kila kazi njema. Inatukamilisha.)
a. Je, una wasiwasi juu ya uhodari (competence) wako? Je, hii inatuahidi kwamba kujifunza Biblia kutaboresha uhodari wetu?
B. Soma 2 Petro 1:20-21. Tumejifunza kuwa maneno ya Mungu kinywani mwa mwandishi wa Biblia yamehusianishwa na pumzi ya Mungu. Hii inafafanuaje zaidi mchakato? (Roho Mtakatifu anawatia moyo wanadamu kutoa maneno ya Mungu. Roho Mtakatifu anafananishwa na upepo katika Yohana 3:8 na Matendo 2:1-4.)
1. Unadhani Mungu anasema kwa sauti (anatoa imla) maneno ya Biblia kwa mwandishi wa Biblia? (Maneno “wakiongozwa” yanaashiria kuwa hii sio imla. Unaposoma injili na kuwaona waandishi wakifafanua suala moja kwa namna tofauti, unapoangalia kwa makini mtindo wao wa kipekee wa uandishi, hilo linakinzana na dhana ya imla.)
C. Soma 2 Petro 1:3-4. Tumejadili jinsi kujifunza Biblia kunavyotufanya kuwa na ustadi/uwezo zaidi. Kunatufanyia nini kingine? (Tunafanana zaidi na Yesu. Kusoma Biblia kunatufanya “kuwa washirika wa tabia ya Uungu.” Hii ni ahadi kutoka kwa Mungu.)
D. Soma 1 Wakorintho 2:6-7. Je, ungependa kumiliki ramani halisi ya hazina? Je, Biblia ni sawa na ramani ya hazina? (Ndiyo! Inatupatia “hekima ya Mungu ya siri iliyofichwa.”)
E. Soma 1 Wakorintho 2:8-10. Sio tu kwamba kusoma Biblia kunatufanya kuwa na hekima kuliko viongozi wa dunia, bali pia inadhihirisha nini kwa njia ya Roho Mtakatifu? (Mwisho wa safari (destination) yetu: Mbinguni!)
F. Soma 1 Wakorintho 2:11-12. Je, Roho Mtakatifu atatudhihirishia fikra ya Mungu? (Kifungu hiki kinasema, “ndiyo,” lakini pia kinarejelea kuyaelewa mambo ambayo Mungu ametupatia “bure.”) hiyo inaashiria kuwa uelewa wetu una ukomo.)
1. Je, kile tulichojifunza kinafafanua kwa nini Biblia ni kitabu bora cha wakati wote?
II. Sola Scriptura (Biblia Pekee)
A. Soma Kumbukumbu la Torati 4:2 na Ufunuo 22:18-19. Utakumbuka kwamba hivi karibuni tuliangalia vifungu hivi. Unavielewaje vifungu hivi viwili kwa kuzingatia “Biblia Pekee?”
1. Soma Yoeli 2:28-29. Manabii hawa wana Roho Mtakatifu, chanzo kile kile kama walichokuwa nacho waandishi wa Biblia. Je, wanapaswa kuwekewa ukomo na Kumbukumbu la Torati 4:2 na Ufunuo 22:18-19?
a. Je, amri za Mungu zilizoandikwa na vifungu vya Biblia vina ubora/viko juu ya maneno ya manabii? (Kura yangu ni, “ndiyo.” Manabii wa ziada (walio nje ya Biblia) wanazuiwa na Biblia na hawatakiwi kuchukuliwa kama nyongeza kwenye Biblia.)
B. Soma 1 Wathesalonike 5:19-21. Kwa nini tunaambiwa kuujaribu unabii? (Biblia haikuanguka kutoka mbinguni kama kitabu kilichokamilika. Badala yake, viongozi wa Mungu waliamua maandiko yepi yanapaswa kujumuishwa kwenye Biblia. Huu ni mchakato wa kujaribu, na mchakato huo (kwa kiwango cha chini zaidi) pia unapaswa kutumika kwa wale wanaodai kuwa na neno kutoka kwa Mungu.)
1. Unazijaribuje kauli za nabii? (Kipimo kimojawapo salama ni kuzilinganisha na Biblia. Hiyo inaifanya Biblia kuwa kipimo cha nabii, na sio kinyume chake.)
III. Kusambaza Injili kwa Uadilifu
A. Soma 2 Wakorintho 4:1. Kifungu hiki kinazungumzia utume gani? (Soma 2 Wakorintho 3:18. Paulo amekuwa akielezea ugumu kwa watu wa “mkataba wa zamani” kuielewa injili – mioyo yao imetiwa utando. Mioyo yetu haijatiwa utando na tunabadilishwa na Roho Mtakatifu.)
1. Utume wetu ni upi basi? (Kuwafundisha wengine kufanana na Yesu zaidi.)
B. Soma 2 Wakorintho 4:2. Tunapaswa kusambazaje injili? (Kwanza, tuenende kwa unyofu kabisa. Pili, tutoe “kauli ya wazi” kuhusu ukweli hadharani.)
1. Unadhani inamaanisha nini “kuichezea” Biblia? (Hii inaakisi Kumbukumbu la Torati 4:2 – usibatilishe kitu chochote kwenye Biblia na usiongezee “mawazo yako mazuri” kwenye kile kinachotakiwa na Biblia.)
2. Je, umekutana na watu wanaosema kuwa ushuhuda wao wa injili ni jinsi wanavyoishi? Una maoni gani juu ya hilo? (Ninadhani huo ni ushahidi dhaifu. Ni sawa na kumtarajia mtu ayasome mawazo yako. Kifungu cha pili kinasifia maisha mazuri, lakini kinaongezea kauli halisi ya ukweli.)
C. Soma 2 Wakorintho 4:3-4. Tutakuwa na mafanikio kwa kiasi gani kwa kusambaza injili? (Tunakabiliana na tatizo la Shetani “kupofusha fikira” za watu.)
1. Umewahi kujiuliza kwa nini, baada ya kuiweka injili bayana na kwa namna yenye kuleta mantiki, wale wanaosoma au kusikiliza hawakumpokea Yesu?
D. Hebu turejee nyuma na tusome tena 2 Wakorintho 3:18. Nani ambaye ni nguvu iliyo nyuma ya mabadiliko kwa mtu? (Roho Mtakatifu. Hii inasaidia kuthibitisha kuwa ni kazi ya Roho Mtakatifu kubadili mioyo. Kazi yetu ni kuishi maisha makamilifu na kushiriki na wengine kile tunachokiamini.)
E. Soma Yohana 14:26. Je, Roho Mtakatifu ni wa muhimu tu kwa roho ya mtu unayejaribu kumwongoa? (Hapana. Roho Mtakatifu anatusaidia sisi ambao tunasambaza injili kuelewa na kukumbuka mafundisho ya Yesu.)
F. Soma Yohana 16:13-14. Tumekuwa tukipigilia msumari mada ya kutoongezea neno lolote kwenye Biblia. Hii inazungumzia nini kuhusu Roho Mtakatifu kuongezea neno?
1. Kwa nini hii iwe tatizo kwa Mungu? (Kinachomaanishwa kinaonekana kuwa tofauti kidogo. Tunaposikia habari kutoka kwa Roho Mtakatifu tunajua kuwa ni neno la Mungu. Hiyo ni njia ya kutofautisha kile ambacho roho yetu inataka tukifanye na kile ambacho Roho Mtakatifu anatutaka tukifanye.)
G. Soma Yohana 7:18. Kitu gani kitamhamasisha mtu kuongezea neno kwenye kile kinachoelekezwa kufanywa na Biblia? (Majivuno.)
1. Unakumbuka hapo awali tulijadili kwa muktadha wa 2 Wakorintho 4:2 hitaji ya uaminifu kamili? Je, mtu anayeongeza “mawazo mazuri” na kuyapitisha kama matakwa ya Mungu anakuwa si mwaminifu? (Mwitikio wangu wa awali kwa wale wanaoongezea mawazo mazuri ilikuwa ni kwamba walikuwa wanajaribu kutenda jambo jema. Hii inaashiria kutokuwa na uaminifu kutokana na kigezo cha majivuno.)
IV. Sola Fide (Imani Pekee) na Sola Gratia (Neema Pekee)
A. Unaweza kujiuliza kwa nini ninajumuisha maneno ya Kilatini kwenye somo hili wakati lengo langu la kawaida ni kuandika kwa namna inayoeleweka. Kinachotenganisha mafundisho ya waleta mabadiliko (reformers) dhidi ya fundisho la kihistoria la Kikatoliki ni “solas” tano zinazomaanisha “Pekee.” Maneno hayo ni Biblia pekee, Kristo pekee, imani pekee, neema pekee, na utukufu kwa Mungu pekee. Angalao maneno matatu kati ya hayo yanaendana na somo letu juma hili.)
B. Soma Waefeso 2:1-3. Hali ya asili ya wanadamu ikoje? (Tumepotea – “watoto wa hasira.”)
C. Soma Waefeso 2:4-6. Kitu gani kilituokoa? (Rehema kuu na upendo wa Mungu kama ilivyofafanuliwa katika kile ambacho Yesu alitutendea.)
1. Hali yetu ilikuwaje Yesu alipotukomboa? (Wafu katika makosa yetu. Hii inaonesha kuwa matendo yetu hayawezi kutuokoa. Yesu aliwakomboa wadhambi.)
D. Soma Waefeso 2:7. Nini kipo kwa ajili yetu katika zama zijazo? (Mbingu. Furaha iliyoje!)
E. Rafiki, je, utauamini ujumbe huu na kuwashirikisha wengine? Kwa nini usijitoe kufanya hivyo sasa hivi?
V. Juma lijalo: Mashahidi Wawili.