Somo la 10: Utume kwa Wasiofikika: Sehemu ya 1

Matendo 17, Wagalatia 3, 1 Wakorintho 2
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
4
Lesson Number: 
10

Somo la 10: Utume kwa Wasiofikika: Sehemu ya 1

(Matendo 17, Wagalatia 3, 1 Wakorintho 2)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, huwa “unachukizwa” (provoked) na mitazamo ya dhambi ya watu wengine? Matendo 17:16 inatuambia kuwa roho ya Paulo “ilichukizwa” kwa jinsi “mji ule ulivyojaa sanamu.” Kihistoria, sanamu ni kitu ambacho unakitegemea ili kikupatie upendeleo wa pekee, kikusaidie kutatua matatizo yako, au kikulinde dhidi ya maadui wako. Kitu hicho ni kipi katika dunia ya sasa? Vipi kuhusu serikali? Vipi kuhusu imani za kidini ambazo hazijajengwa juu ya Yesu? Vipi kuhusu falsafa za maisha ambazo baadhi ya watu wanazitegemea ili kuweza kuishi? Kama tuna moyo wa huruma kwa wale wanaokosa furaha kwa kutomwamini Yesu, ni njia gani bora ya kuwapelekea habari njema ya injili? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!

I. Miungu ya Athene

A. Soma Matendo 17:16-17. Paulo aligundua kuwa Athene ilikuwa imejaa miungu. Alikuwa na mwitikio gani? (Alipeleka injili kwa Wayahudi katika sinagogi na alipeleka injili sokoni.)

1. Kama ungetaka kufuata mfano wa Paulo, katika zama za leo ni kitu gani kingefananishwa na sinagogi? (Kupeleka injili kwa wafuasi wa dini wanaoamini baadhi ya kweli za Biblia, lakini hawaamini ukweli kumhusu Yesu.)

a. Je, Wayahudi walikuwa sehemu ya ibada ya sanamu? (Soma Kutoka 20:1-5. Wayahudi walikatazwa kabisa kuabudu sanamu. Ilikuwa sehemu ya Amri Kumi.)

b. Je, hii inatusaidia kuelewa jambo linalofanana na Paulo kupeleka injili katika sinagogi katika zama za sasa? (Ndiyo.  Kwa kuwa tu kanisa linapaswa kumwamini Yesu haimaanishi kuwa washiriki wana uelewa sahihi.)

B. Soma Wagalatia 3:10-11. Hebu tuliangalie kanisa lako. Wangapi wanasema kuwa wokovu wao unatokana na imani yao kwa Yesu pekee na sio utii wao wa sheria? (Huenda wote watasema hivyo.)

1. Ni wangapi ambao kimsingi wanaamini hivyo?

2. Wangapi wanaamini kuwa utii wao wa sheria unawafanya wawe na uwezekano mkubwa wa kuokolewa kuliko washiriki wengine?

3. Wangapi kati yao wanajenga hoja dhidi ya “neema ya bure” na kudai kuwa utii wa sheria ni muhimu ili kuweza kuokolewa?

4. Ikiwa kwa kiwango chochote wokovu wako unategemea utii kwa Mungu (utii wa sheria yake), je, wewe ni mwabudu sanamu? (Ndiyo! Hivi ndivyo ambavyo tuna waabudu sanamu katika mikusanyiko yetu ambao hawana habari yoyote na hatari iliyo mbele yao. Kinyume chake ni kwamba, wanaamini kuwa wao ni Wakristo wazuri kuliko wengine.)

C. Hebu turejee kwa Paulo, Athene, na Areopago. Soma Matendo 17:21. Je, unamfahamu mtu kama huyu? Mtu anayetumia muda wake wote kusikiliza au kuelezea jambo jipya?

1. Unatumia kiasi gani cha muda kuangalia simu janja yako ili kusoma (au kuelezea) jambo jipya?

II. Uinjilisti Katika Athene

A. Soma Matendo 17:22-23. Paulo anachukua hatua gani mbili muhimu kuanza kuzungumza na wapagani kuhusu injili? (Kwanza, anajitokeza pale ambapo watu wanatafuta jambo jipya. Pili, anatumia mfumo wao wa miungu ili kumwelezea Mungu wa kweli.)

1. Linganisha hili na jinsi ambavyo kidesturi umekuwa ukifanya uinjilisti. Je, hii inafanana na kwenda nyumba kwa nyumba ukifundisha Biblia? (Haifanani. Kwanza, watu katika makazi yao hawajaonesha nia ya kusikiliza kile unachotaka kukisema. Pili, upo nyumbani kwao, hapa si mahali ambapo wangetaka kukutana na wageni.)

2. Anachokifanya Paulo kinafananaje na kuwatumia kadi za mialiko ya kuhudhuria kwenye mkutano? (Barua ni desturi ambayo watu hupokea taarifa kuhusu mambo ambayo wanaweza kujihusisha nayo. Wakija kwenye mkutano wako, basi wamekubali kusikiliza jambo jipya.)

a. Mtuma barua zinazohusu mkutano wako ana tofauti gani? (Watu wangapi wanaangalia mawazo mapya kwenye masanduku yao ya barua? Waathene pale Areopago walikuwa wanatafuta mawazo mapya. Hiyo ndio sababu ya kuwepo mahali pale.)

3. Tuna nini leo kinachokaribiana kabisa na alichokuwa anakifanya Paulo pale Areopago? (Intaneti! Watu wanaperuzi kwenye mitandao kwa njia ya intaneti ili kujifunza mambo mapya. Hawahisi kuwa faragha yao imeingiliwa na hawashinikizwi kutenda jambo fulani.)

a. Inawezekana unasoma somo hili kwenye mtandao wa intaneti. Unaweza kufanya nini au kanisa lako linaweza kufanya nini ili kurudufu (replicate) anachokifanya Paulo? (Angalia kama kuna mtandao (website) wenye mawazo mapya ya kidini?)

b. Mtandao wa intaneti unashindwaje kurudufu kile anachokifanya Paulo? (Paulo alikuwepo ana kwa ana na wasikilizaji wake.)

(1) Je, vikao kwa njia ya Zoom vingetatua tatizo hilo?

(2) Je, umewahi kusikia mkutano wa injili ukifanyika kwa njia ya Zoom (au kwa njia inayokaribiana na hiyo) ambapo watu waliokuwepo kwenye mkutano waliweza kuuliza maswali au kujenga hoja mbadala (challenge) kwenye kauli zako?

B. Katika Matendo 17:24-31 Paulo anawasilisha injili kwa Waathene. Tutarejea kwenye ujumbe wake baadaye. Soma Matendo 17:32-34. Mwitikio wa watu ulikuwaje? (Wengine walidhihaki, wengine waliutafakari, na wengine waliamini.)

1. Je, utakuwa tayari kwa mwitikio kama huo endapo ungekuwa unafanya mkutano wa injili kwa njia ya Zoom?

III. Athene Inajutia?

A. Soma 1 Wakorintho 2:1-4. Baadhi ya watu wanajenga hoja kwamba Paulo anakiri kuwa njia yake ya kupeleka injili kule Athene haikuwa bora. Msingi wa hoja yao ni kwenye kauli yake kwamba aliamua kwenda kinyume na “maneno ya hekima yenye kushawishi,” na badala yake akadhamiria kutojua neno lolote “isipokuwa Yesu Kristo naye msulubiwa.” Una maoni gani?

B. Hetu tufanye kile nilichokiahidi kwa kurejea nyuma na kuangalia hoja za Paulo kule Athene. Soma Matendo 17:22. Paulo anaanza kwa kuwasifia wasikilizaji wake wapagani. Je, nasi pia tunapaswa kufanya hivyo?

C. Soma Matendo 17:23. Hapa mkakati wa Paulo ni upi? (Anaiingiza injili kwenye mfumo wao wa sasa wa imani za kidini.)

1. Utafanyaje hivyo hii leo na wapagani – hususani wapagani wachanga? (Imani ya kidini ya vijana wadogo ni kuachana na ubaguzi kwa msingi wowote. Au angalao hayo ndio madai yao. Mtazamo wa Biblia juu ya uhuru wa mtu binafsi huunda msingi wa utamaduni wa Magharibi. Tunaweza kuangia hapo.)

D. Soma Matendo 17:24-25. Paulo amebadilije gia katika wasilisho lake? (Sasa anajenga hoja kuwa Mungu wake ni mkuu kuliko mtazamo wao juu ya miungu.)

E. Soma Matendo 17:26-29. Je, sasa Paulo analaani mitazamo ya wasikilizaji wake? (Ananukuu washairi wao, lakini anasema sanamu zote hizi haziwezi kutusaidia ili kumtazama kwa usahihi Mungu mkuu wa mbinguni.)

1. Angalia tena vifungu vya 26-29 na uniambie msingi gani wa ukweli unabishiwa sana na wapagani wa leo? (Uumbaji. Paulo anasema Mungu aliwaumba wanadamu. Tuliumbwa kwa mfano wake. Tunawezaje kuamini kimantiki kwamba tulitokana na miamba, dhahabu, au fedha? 

F. Soma Matendo 17:30-31. Jembo gani limetokea kwenye sifa za awali wakati wa ufunguzi? (Sasa Paulo anawaambia kuwa kwa sababu ya mtazamo wao mfinyu kwa Mungu wanatakiwa kutubu. Wanatakiwa kubadili mitazamo yao.)

1. Ni nini nia ya kuipokea hoja ya Paulo?  (Hukumu inakuja. Kuna sababu ya kulichukulia hili kwa dhati.)

G. Angalia tena Matendo 17:31. Paulo anawataka wasikilizaji wake waamini nini? (Wamwamini Yesu, na kwamba alifufuka kutoka katika wafu.)

1. Je, hii inaonekana kana kwamba Paulo anajenga hoja juu ya Yesu Kristo na kusulubiwa kwake? (Nadhani hivyo. Ndio maana nadhani wasomi wa Biblia wanaojenga hoja kuwa Paulo alitafakari upya njia aliyoitumia Athene hawako sahihi.)

2. Ikiwa Paulo alijenga hoja juu ya Yesu “naye msulubiwa” katika Athene, lakini akarekebisha ujumbe wake kwa wasikilizaji wake, hiyo inatufundisha nini kuhusu juhudi zetu za kufanya uinjilisti? (Ujumbe wetu wa injili haupaswi kubadilika. Kinachopaswa kubadilika ni njia za kupeleka injili kwa wale wanaotuzunguka.)

H. Rafiki, je, utaichukulia kwa dhati njia ya Paulo ya kuwafikia watu wa nje? Je, utajitahidi kwa kadiri ya uwezo wako kupeleka injili kwa kutumia njia yenye ufanisi zaidi? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu ayaongoze mawazo yako ili kufikia lengo hilo?

IV. Juma lijalo: Utume kwa Wasiofikika: Sehemu ya 2.