Somo la 1: Utume wa Mungu Kwetu: Sehemu ya 1
Somo la 1: Utume wa Mungu Kwetu: Sehemu ya 1
(Mwanzo 3 & 27, Mathayo 1, Yohana 1, 3 & 14)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, umewahi kukutana na mtu uliyemchukulia kama mtu “Mwenye maneno mengi lakini matendo sifuri?” Au kama wasemavyo kule Texas, “All hat and no cattle?” Bila shaka sote tumekutana na watu kama hao. Changamoto katika mwenendo wetu wa Kikristo ni kutokuwa kama watu hao. Tunataka kujihusisha kwenye utamaduni wa Kristo na sio kuuzungumzia tu. Tafakari hali yako ya sasa. Natumaini u sehemu ya darasa la mjadala wa kujifunza Biblia siku ya Sabato. Unahudhuria kanisani na kusikiliza mahubiri yanayoleta changamoto ya maisha ya Kikristo mawazoni mwako. Lakini baada ya mazungumzo yote hayo je, unafanya jambo lolote ili kuutangaza Ufalme wa Mungu? Mfululizo wa masomo yetu ya Biblia katika robo hii unahusu jinsi ya kujongea kutoka kwenye kuzungumza hadi kwenye vitendo. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuanze safari yetu ya matendo!
I. Kuelewa Nia ya Mungu ya Kutukaribia
A. Soma Mwanzo 3:1-5. Shetani alikuwa na mkakati gani alipomwambia Eva, “Mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu?” (Shetani alitaka Eva aamini kuwa Mungu hakumuwazia mema. Alitakiwa kuchukulia mambo mikononi mwake ili kulinda maslahi yake.)
1. Je, kulikuwa na ukweli wowote kwenye mashtaka yale? (Historia inatuonesha kuwa maisha yaliwaendea kombo Adamu na Eva badala ya kuwaendea vizuri baada ya Eva kula tunda.)
B. Soma Mwanzo 3:8-9. Sasa Adamu na Eva wote wawili wametenda dhambi. Kama ungekuwa Mungu, je, hivyo ndivyo ambavyo ungeanzisha mazungumzao? (Ningeanza kwa kusema, “Hivi mmetambua jinsi mlivyosababisha matatizo? Mnawezaje kuwa wapumbavu kiasi hicho? Ni lini niliwahi kuwapa sababu yoyote ya kutoniamini?”)
1. Unadhani kwa nini Mungu alisema vile alivyosema? (Anaomba kukutana na Adamu na Eva. Anataka kuungana na wawili hawa ambao kwa kiasi kikubwa wameharibu mipango yake kwa ajili ya siku zijazo.)
2. Kwani Mungu hakujua mahali walipokuwepo? Kwa nini anauliza mko “wapi?” (Mungu aliwataka Adamu na Eva waelezee ukengeufu wao wa kutisha wa mpango wake.)
3. Kama ungekuwa kwenye nafasi ya Mungu, je, ungewaacha Adamu na Eva peke yao kwa muda mfupi ili wajipalie mkaa kwenye wasiwasi wao kuhusu hali yao ya sasa?
4. Hii inatufundisha nini kuhusu uhusiano wetu na Mungu? Inatufundisha nini kuhusu matunzo ya Mungu kwetu? (Msukumo wa kwanza wa Mungu sio kuadhibu au kushutumu/kushtaki. Bali, msukumo wake wa kwanza ni kuja karibu na wanadamu ili kujadili kile walichokitenda.)
II. Mungu na Uvundo Wetu wa Dhambi
A. Soma Mwanzo 27:17-19. Je, unafahamu kisa cha nyuma cha vifungu hivi? (Mungu alikuwa na uhusiano wa pekee na baba yake na babu yake Yakobo. Ahadi ya Mungu kwao ilikuwa ni kuyafanya mapenzi yake kupitia kwenye familia hiyo – na kwamba watakuwa watu wa Mungu. Babaye Yakobo alidhamiria kutoa haki ya uzaliwa wa kwanza, kama ilivyokuwa kawaida, kwa mwanaye mkubwa Esau. Lakini Yakobo, kwa msaada wa mama yake, aliamua kujichukulia haki ya uzaliwa wa kwanza kwa kumdanganya baba yake, Isaka, kwa kughushi utambulisho wake.)
B. Soma Mwanzo 27:20. Unadhani kwa nini Isaka aliuliza swali hili? (Alipata mashaka mawazoni mwake kama huyu alikuwa mwanaye mkubwa au mtu mwingine.)
1. Yakobo anasihi kwa jina la nani ili kupata mafanikio yake ya haraka haraka? (Jina la Mungu.)
a. Mungu anapaswa kuangaliaje matumizi ya jina lake kama sehemu ya udanganyifu dhidi ya Isaka?
C. Soma Mwanzo 27:21-24. Bado Isaka ana mashaka kuhusu utambulisho wa mtu aliyepo mbele yake. Je, Isaka alipaswa kumuita mtu mwingine ili kuthibitisha kwamba huyu alikuwa mwanaye mkubwa?
D. Soma Mwanzo 27:28-29. Isaka anambariki Yakobo. Udanganyifu unafanikiwa. Soma Mwanzo 27:42-44. Ni nini matokeo ya udanganyifu? (Yakobo anakimbia kutoka nyumbani kwao ili kaka yake mkubwa asimuue.)
1. Jiweke kwenye nafasi ya Mungu. Ungemchukuliaje Yakobo? Je, Mungu aenende na udanganyifu na kuendelea na kazi yake kupitia kwa Yakobo?
2. Je, ungefanya kazi na Yakobo? Je, ungemfanya kuwa mshirika wako wa kibiashara?
E. Soma Mwanzo 28:10-13. Mungu anakuwa na mwitiko gani kwenye udanganyifu wa Yakobo? (Anaamua kuendela kufanya kazi kupitia kwa Yakobo.)
1. Kwa nini? Hii inatuambia nini kuhusu Mungu wetu? (Tumeruka taarifa zinazotuambia kuwa kijana mkubwa hataendana vizuri sana na kazi ya Mungu. Lakini hiyo haibadili ukweli kwamba Yakobo na mama yake walifanya udanganyifu. Habari njema kuhusu Mungu wetu ni kwamba alikuwa radhi kufuatilia ahadi yake kwa kufanya kazi na Yakobo mwenye upungufu/dosari. Hiyo inatuambia kuwa Mungu anatenda kazi na watu wenye upungufu kama sisi.)
III. Mungu na Kazi ya Uokozi
A. Soma Mathayo 1:18-21. Je, umewahi kuwa na rafiki “mhitaji” (ambaye anahitaji msaada mara kwa mara)?
1. Unakuwa na mwitiko gani kwa marafiki kama hao? Je, unakatisha urafiki nao?
B. Soma Yohana 1:14. Fikiria juu ya kile ambacho rafiki yako aliye mhitaji zaidi alikihitaji kutoka kwako, na kisha ulinganishe hitaji hilo na kile ambacho Yesu alitutendea. Fikiria sio tu kuhusu kuwa masikini, bali pia kuhusu kifo chake kilichotokana na mateso.
1. Hiyo inatufundisha nini kuhusu mtazamo wa Mungu kwetu?
C. Soma Yohana 1:16-18. Kifungu cha 17 kinapotuambia kuwa “kweli” zilikuja kwa njia ya Yesu Kristo, ni kweli gani huo?
1. “Kweli” zinaonekana kulinganishwa na sheria. Ikiwa niko sahihi, ni ukweli gani unaokosekana kutoka kwenye sheria? (Neema ya Mungu. Upendo wa Mungu. Namna ambayo Mungu atachangamana nasi.)
2. Kifungu cha 18 kinafafanua kuwa Yesu alimfanya Mungu Baba ajulikane. Je, umedhani kuwa Agano la Kale linawasilisha taswira tofauti kabisa ya Mungu tofauti na Agano Jipya? Kama umejibu, “Ndiyo,” hii inatuambia kuwa tunapaswa kupatanishaje hizi taswira tofauti? (Tunatakiwa kuendana na taswira ya Yesu. Yesu ndiye aliyemfanya Mungu “ajulikane.”)
3. Unadhani kwa nini hata tuna taswira ya Mungu ya Agano la Kale? (Neema. Vipimo vitakatifu vya Mungu vinatusukuma kwenye kuhesabiwa haki kwa imani na kufunua, ikiwa tu wakweli, kwamba matendo yetu yako mbali sana na kipimo cha Mungu.)
D. Soma Yohana 3:16. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu taswira sahihi ya Mungu Baba? (Hii inajikita kwenye upendo wa Baba. Anatupenda sana kiasi kwamba alimtoa Mwanawe adhalilishwe na kuteswa ili tuweze kuishi.)
1. Je, ungefanya hivyo kama ungekuwa kwenye nafasi ya Mungu?
2. Hiyo inatufundisha nini kuhusu kipimo cha upendo wa Mungu kwetu?
E. Soma Yohana 14:16-17. Mungu ametupatia kipawa gani kingine? (Nadhani tunashindwa kuelewa kikamilifu juhudi za Mungu zisizo za kawaida anazozichukua kwa ajili yetu. Yesu alikuja ili aishi, kufa, na kufufuka kwa ajili yetu. Baada ya hapo, Mungu alitoa kazi ya kudumu kwa Roho Mtakatifu ambaye “anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.”)
1. Uwepo wa Roho Mtakatifu ni wa muhimu kiasi gani maishani mwako? (Asubuhi ya leo nimesoma makala nyingine inayohusu kuongezeka kwa wasiwasi kwa watu nchini Marekani. Nipo katika mwaka wangu wa 48 katika kazi yangu ya uwakili. Mara kwa mara huwa ninajikuta nikijenga hoja kwenye mahakama ambazo sijazizoea zenye mazingira ya chuki. Hii sio tu suala la kuzungumza mbele ya watu, ongezea pia kuuliza maswali magumu, na kujibu hoja mbalimbali. Roho Mtakatifu amekuwa msingi wa kukabiliana na nyakati zangu za msongo na mashinikizo.)
F. Soma Yohana 14:1-3. Ni nini hatma ya lengo la Mungu kwetu? (Kukaa pamoja nasi katika ulimwengu utakaofanywa mkamilifu tena! Tutakuwa na nyumba ya majumui (condominium) katika ule jengo kubwa/mji mkubwa (angalia Ufunuo 21:16) uitwao Yerusalemu Mpya.)
G. Rafiki, hatua ya kwanza ya kuchukua hatua ni ushawishi wa upendo usio wa kawaida wa Mungu kwetu. Kwa kuwa Mungu anatupenda kiasi hicho, je, utachukua hatua ya kwanza kumpenda mtu mwingine kwa kumwomba Roho Mtakatifu akuletee mawazoni mwako mtu wa kumwombea?
IV. Juma lijalo: Utume wa Mungu Kwetu: Sehemu ya 2