Somo la 13: Kuendeleza Amani
Somo la 13: Kuendeleza Amani
(2 Wakorintho 10, 1 Timotheo 1, 1 Petro 5, Matendo 19)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Juma lililopita tulijifunza Waefeso 6:10-17 na silaha za kiroho ambazo Paulo anasema tunatakiwa “kuweza kuzipinga hila za Shetani.” Tuliona mambo mawili ya muhimu. Kwanza, pambano letu lilikuwa dhidi ya “majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho,” Waefeso 6:12, na pili, kwamba kwa asili karibia silaha zote zilikuwa ni za kujikinga. Hiyo inaweza kutufanya kufikia hitimisho kwamba kipekee “tunaendeleza amani” kwenye uhusiano wetu na watu wengine, kama kichwa cha somo hili kinavyoashiria.
Lakini baadaye Paulo alisema jambo lisiloendana kabisa na utangulizi huo. Aliomba maombi ya kumsaidia “yeye binafsi” (anatumia neno hilo mara mbili katika Waefeso 6:19-20) kutangaza injili. Huenda “kuendeleza amani,” imejikita zaidi kwenye “kuendeleza” kuliko “amani.” Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile linachokisema kwingineko kuhusu asili ya pambano letu dhidi ya uovu!
I. Maangamizi ya Amani
A. Soma 2 Wakorintho 10:1-3. Unadhani kwa nini Paulo anadai kuwa anapokuwa peke yake yeye ni mnyenyekevu, lakini anapoondoka anakuwa jasiri? Je, hii ni aina ya kale ya mitandao ya kijamii ambapo watu wanaandika mambo ambayo sio rahisi kukuambia ana kwa ana? (Nadhani Paulo anarudia tuhuma zilizotolewa dhidi yake. Wapinzani wake wanadai kuwa yeye ni jasiri pale tu anapokuwa hayupo. Ashirio ni kwamba Paulo ni mwoga.)
1. Unadhani Paulo ana maoni gani kuhusu kuwa jasiri ana kwa ana? (Anasema anaweza kutakiwa kuwa jasiri anapokuwa ana kwa ana. Hasemi kuwa hilo sio sahihi.)
2. Hebu tulihusianishe hili na Waefeso 6:19 ambapo Paulo anarejelea kutangaza injili kwa “ujasiri” katika muktadha wa pambano la kujilinda. Je, kuendeleza amani hakuendani na kuongea kwa uwazi? (Kwa dhahiri hapana.)
3. Paulo anamaanisha nini anaposema (2 Wakorintho 10:3) kwamba hatupaswi “kufanya vita kwa jinsi ya mwili?” (Kwa dhahiri wanadamu wametengenezwa kwa “nyama,” lakini Wakristo wana silaha za kiroho zilizo na nguvu zaidi.)
B. Soma 2 Wakorintho 10:4-5. Hii inatupatia jibu la aina ya vita ya kiroho tunayoiendeleza. Mkristo anaendelezaje vita ikilinganishwa na mtu wa ulimwenguni? (Tunatumia uwezo wa Mungu. Tutatumia uelewa wa Mungu. Hii inatuambia kuwa silaha zetu dhidi ya madanganyo ya ulimwengu ni udhihirisho uliofanywa kwa kuzingatia uongozi wa Roho Mtakatifu na mafundisho ya Biblia.)
1. Lengo la mwisho ni lipi? (Kuangamiza na kuteka hoja za uongo na mawazo ya uongo. “Tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka” na “tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo.”)
2. Je, hii inaonekana kama “kuendeleza amani?”
3. Nimesoma sehemu ya Qur’ani na Hadith, ambavyo ndivyo kiini cha Uislamu. Uislamu unasema kuwa ni dini ya amani. Nimesoma njia ya kutafuta amani kwa Uislamu na inahusisha kuwaongoa au kuwaangamiza wale wasioyakubali mafundisho. Baada ya wapinzani wote ama kuongolewa au kuangamizwa, amani inakuwepo. Je, hilo linaendana na kile tunachojifunza? (Paulo haonekani kuandika juu ya maangamizi halisi. Hawalazimishi watu. Bali hoja zake zilizotiwa nguvu na roho zinaangamiza hoja na mawazo kinzani.)
C. Soma 2 Wakorintho 10:6. Paulo anasema kuwa “atapatiliza maasi” pale “kutii kutakapotimia.” Unaweza kuelezea anachokimaanisha? Unaweza kuelezea ni kwa jinsi gani huku ni “kuendeleza amani?” (Hii inaelezea hatua ya muhimu sana inayopaswa kufuatwa: Paulo hatawaadhibu wasio watiifu ikiwa sehemu kubwa ya kanisa haina utiifu. Ili kanisa liweze kusonga mbele, washiriki wengi wanatakiwa kuwa watiifu na mistari isiyopaswa kuvukwa ikiwa bayana.)
D. Soma 1 Timotheo 1:18-20. Je, hii inatusaidia kuelewa “kuendeleza amani?” (Nadhani. Paulo atachukua hatua madhubuti dhidi ya wale wanaofundisha mafundisho ya uongo. Matokeo yake itakuwa ni kuwepo kwa amani kanisani.)
1. Hadi kufikia hapa tunatakiwa kuangalia kama onyo la Paulo katika waefeso 6:12 kwamba tuko vitani dhidi ya “majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” linaleta mantiki. Tunaweza kupatanishaje hili na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya washiriki wenzetu wa kanisa? (Huku akiwa na mafundisho ya Biblia na kuongozwa na Roho Mtakatifu, kiongozi muhimu wa kanisa kama Paulo anaweza kurejesha amani ya kiroho kanisani kwa kuwaondosha wale wanaoyapinga mafundisho ya wazi ya Biblia na kutangaza kanuni za kiovu.)
2. Je, tunazungumzia tu kuhusu kuwapinga washiriki wa kanisa? Vipi kuhusu kuendeleza amani dhidi ya wasioamini? (Angalia tena 2 Wakorintho 10:4-5. Paulo anapigia chapuo kuangamiza hoja na mawazo “yajiinuayo juu ya elimu ya Mungu.” Nadhani sehemu kubwa ya jambo hili ipo nje ya kanisa kuliko ndani ya kanisa.)
E. Soma Matendo 19:8-9. Ni njia gani hii ya kuendeleza amani? (Unakumbuka mkakati wa Paulo kwamba watu wengi wanatakiwa kuwa watiifu kwake ili kupiga hatua dhidi ya kutokutii? Wakati mwingine tunatakiwa tu kurudi nyuma/kuondoka. Tunadai ushindi kwa wale walioongolewa na tunaanzia mahala pengine papya.)
II. Upinzani na Mateso
A. Soma 1 Petro 5:8-9. Tunampingaje Shetani? Tunatakiwa kuwa makini. Tunampinga Shetani kwa kuitegemea imani yetu.)
B. Soma 1 Petro 5:10. Petro anaangazia jambo gani la uhalisia kwenye mjadala wetu wa vita ya kiroho? (Tunaweza kupata mateso. Hakuna ahadi kwamba kila pambano la kiroho litafanyika kwa ukamilifu. Bali, tunaye adui anayetaka kutudhuru.)
1. Je, wale wanaoyafuata mapenzi ya Mungu wataishia kuwa washindi? (Ndiyo. Mungu “atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu.”)
C. Kama umekuwa Mkristo kwa kipindi fulani bila shaka umeshuhudia mgogoro kanisani. Unajuaje nani yuko upande sahihi? (Funzo la kwanza tulilojifunza ni kwamba upande sahihi utaungwa mkono na Biblia. Upande sahihi utaakisi uwezo wa Roho Mtakatifu. Pili, tunatakiwa kuwazingatia viongozi ambao Mungu amewaweka madarakani ili kuliongoza kanisa.)
D. Soma Isaya 59:14-15. Je, mara zote viongozi wetu watakuwa na haki? Je, mara zote watakuwa wakweli? (Isaya anatuambia kuwa wakati mwingine kilicho sahihi kinakufanya kuwa “mawindo” (muathirika) ya viongozi walio waovu.)
E. Soma Isaya 59:16-18. Katika mazingira kama hayo, waaminifu wanapaswa kuomba ili jambo gani litokee? (Mungu ataingilia kati. “Atalipa” uovu kwa kisasi.)
F. Soma Warumi 8:36-39. Hii inazungumzia mambo ya kutisha yanayowatokea watu wa Mungu. Wanawezaje kuitwa washindi “zaidi ya kushinda?” (Ujasiri wetu katika nyakati ngumu ni kwamba Mungu anatupenda. Hakuna atakayeweza kututenganisha na upendo wake. Hatimaye atatuokoa.)
III. Vizingiti vya Ushindi
A. Soma 2 Wakorintho 4:3-4. Ni jambo gani lililo gumu katika kupeleka injili? (Shetani anapofusha akili za wale wasiomwamini Yesu.)
B. Soma Warumi 1:20-22. Hii inaashiriaje kwamba Shetani anaathiri akili za wale wanaompinga Mungu? (Wale wenye akili zilizoathirika wamekubaliana na hili kwa kukataa kumheshimu Mungu.)
1. “Unapoendeleza amani” ili kuitangaza injili, tunaona mambo gani ya kutia moyo kwenye vifungu viwili tulivyojifunza hivi punde? (Hatupaswi kujisikia kwamba sisi ni washindwa ikiwa wapinzani wetu au wasio waamini hawajaongolewa na hoja zetu zinazoongozwa na Roho. Misingi ya kutoamini inakwenda mbali zaidi.)
C. Soma Matendo 19:11-12. Angalia jinsi Paulo anavyoonekana kumshinda mwovu bila kutumia nguvu! Kama nguo itagusa tu ngozi yake, nguo hiyo itaweza kutoa pepo wachafu. Hilo linawezekanaje?
D. Soma Matendo 19:13-16. Ni akina nani hawa? Tunapata onyo gani katika mapambano yetu ya kiroho? Je, ni kuepuka kujiamini kupita kiasi? Je, ni onyo la kuelewa “wajibu” wetu? (Inaonekana, kwa sababu wanaitwa “Wayahudi wenye kutanga-tanga,” kwamba huko nyuma waliweza kuondoa pepo wachafu. Lakini, kifungu hakisemi kuwa watu hawa ni wafuasi wa Yesu.)
E. Soma Matendo 19:17. Kwani sio mtu aliyepagawa pepo ndiye aliyewapiga wale wana? Kwa nini jina la Yesu linatukuzwa na kuogopwa?
F. Soma Matendo 19:18-20. Ni nini lililo tatizo miongoni mwa waamini ambalo sasa linatatuliwa? Hiyo inatuambia nini kuhusu wana wa Skewa? (Kitabu cha Matendo kamwe hakisemi kuwa wana wa Skewa walikuwa Wakristo. Hata kama walikuwa Wakristo, baadhi ya Wakristo wapya walikuwa hawajaachana na “sanaa zao za kimaajabu.” Fundisho hapa ni kwamba sio lazima kuwa waumini pekee ili kudai mamlaka ya kuwashinda pepo wachafu, bali pia tunapaswa kuyachunguza maisha yetu ili kuona kama tuko tayari. Ndio maana Paulo aliweza kuondoa pepo wachafu bila kutumia nguvu, lakini wana wa Skewa (hata pale walipotumia jina la Yesu) walipigwa kwa kulitumia jina hilo.)
G. Rafiki, kuendeleza amani kwa ajili ya injili haimaanishi kuwa tunatakiwa kuwa wapole na waoga. Tunaweza kuwa imara. Uimara wetu unatokana na silaha zetu za kiroho. Je, utadhamiria leo kumwomba Roho Mtakatifu aongoze juhudi zako zote katika kuitangaza injili?
IV. Juma lijalo: Waefeso Moyoni.