Somo la 4: “Mcheni Mungu na Kumtukuza”
Somo la 4: “Mcheni Mungu na Kumtukuza”
(Ufunuo 14, Mhubiri 12, Mathayo 5 & 6)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Miaka mingi iliyopita nilinunua kofia nyeusi ya mpira wa besiboli iliyoandikwa kwa maandishi makubwa mekundu mbele, “Mcheni Mungu.” Karipio zuri kwa wapagani, si ndio! Na ukumbusho kwetu sisi tuliosalia. Hata hivyo, imekuwa nadra sana kwa mimi kuivaa. Kwa nini? Sababu mojawapo ni kwamba nina wasiwasi kuwa watu hawatayaelewa maandishi hayo. Inamaanisha nini “kumwogopa Mungu?” Wanadamu wanapojiwa na malaika wanaambiwa “Msiogope.” Angalia Luka 1:28-30. Hii inaonekana kujihusisha na uoga halisi. Kama malaika wanasababisha uoga, basi kwa hakika Mungu anatakiwa kuogopwa kiuhalisia. Lakini uoga halisi unaonekana kutoendana na uelewa wetu wa Yesu. Hebu turukie kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!
I. Mcheni Mungu
A. Soma Ufunuo 14:7. Hebu tuliweke hili kwa namna ambayo watu wengi wanaweza kulielewa. Kama umeshtakiwa kwa kosa la jinai, na jopo la wazee wa mahakama liko mbioni kutoa hukumu yake, je, utajisikia uoga halisi – aina ya uoga unaokufanya utetemeke? (Ndiyo. Hapa muktadha ni “hukumu” kwa hiyo aina ya uoga inayotetemesha kimantiki inaonekana kujengwa juu ya uelewa wetu wa maisha.)
1. Soma Luka 12:5. Hapa maneno, kwa mujibu wa Picha ya Maneno ya Robertson, yanafanana na yale yaliyopo katika Ufunuo 14:7. Je, huu ni uoga unaotetemesha? (Kama ningeambiwa kuwa nitauawa na kutupwa jehanum hayo yatakuwa matokeo mabaya kabisa yanayoweza kutokea – na nitatetemeka.)
2. Soma Ufunuo 19:5. Hii inatumia neno lile lile la Kiyunani la uoga. Je, unaweza kutafakari kwamba wale wanaomsifu Mungu mbinguni pia wanatetemeka kwa hofu?
a. Kama ungekuwa Mungu, je, ungependa kusifiwa na mtu anayeogopeshwa nawe?
B. Angalia tena Ufunuo 14:7. Je, unayo nadharia yoyote ya kwa nini neno moja la Kiyunani lina maana mbili, ya kuogopa na mtazamo wa kusifu? (Ni kawaida kwa neno moja katika lugha kuwa na maana kadhaa. Muktadha ndio unaotusaidia kuelewa kile kinachomaanishwa. Unadhani “uoga” unamaanisha nini katika muktadha wa kifungu hiki ambacho pia kinatumia maneno “kumtukuza” na “msujudieni yeye” [ambaye ni Muumbaji]? (Muktadha unatuambia kuwa kwa kiasi kikubwa linamaanisha heshima na hofu.)
1. Je, baadhi ya watu wanapaswa kutetemeka kwa hofu mbele ya Mungu? (Naam. Wale ambao ni maadui wake, wapinzani wake. Wale wanaoogopa hukumu yake.)
2. Baba yangu alikuwa mtawala katika shule ya umma kipindi kirefu cha maisha yake ya kitaaluma. Ninakumbuka alipokuwa mkuu wa shule ya kati (middle school) tulikuwa tunatembea kupita mbele ya mlango wa chumba cha darasa uliokuwa wazi na baba yangu akamwona mvulana mmoja ameshuka ghafla kutoka kwenye kiti chake. Baba yangu alimchapa kwenye vidole vyake na mara moja mvulana huyu akasimama wima. Je, unadhani mvulana yule pamoja na mimi tulikuwa na mtazamo mmoja juu ya baba yangu? (Hapana. Sote wawili tulimwogopa, lakini nilijua kuwa baba yangu alikuwa ananipenda sana.)
II. Mhubiri
A. Soma Mhubiri 12:9-10. Mhubiri anafanya nini ambalo ni la kusifika? (Anajifunza kwa umakini na kimantiki. Anawakilisha mithali nyingi.)
1. Lengo la Mhubiri huyu ni nini? (Kuleta furaha na ukweli kwa wasikilizaji wake.)
2. Je, unadhani Mhubiri anatenda jambo sahihi? (Huwa ninapenda somo lililoandaliwa na kupangiliwa vizuri ambalo linanipa furaha.))
B. Soma Mhubiri 12:11. Je, “vichocheo” au “unyofu” vinafanana na maneno ya furaha? Je, hii inahusiana na maneno ya Mhubiri? (Nadhani hii inamaanisha kuwa ina ujumbe unaofanya tuyatafakari maisha yetu kwa umakini. Vinatuchochea” kwenye uelekeo sahihi.
1. Zingatia rejea ya “maneno yaliyoandikwa kwa unyofu.” “Unyofu” ni kitu gani kwenye hubiri? Baada ya chakula cha mchana, je, unakuwa umesahau kabisa hubiri?
2. Sio muda mrefu uliopita nilikuwa ninazungumza na kijana mmoja ambaye tulikuwa hatujaonana kwa miaka mingi. Aliniambia kuwa alikuwa anakumbuka visa kutoka kwenye mahubiri niliyoyafanya si chini ya miaka kumi iliyopita. Alikuwa kijana barobaro alipovisikia visa vile na nilishangaa kwamba alivikumbuka. Nilimuuliza kama alikumbuka ujumbe wa kiroho uliobebwa na visa hivyo. Hakukumbuka. Visa vyangu vilikazia habari za kisa, lakini sio ujumbe. Je, tunawezaje “kukazia” ujumbe?
C. Soma Mhubiri 12:12-13. Je, kazi ya Mhubiri inaelekea kwenye uelekeo sahihi? (Ndiyo. Kuna vitabu vinavyotuchosha kwa taarifa za kina. Lakini hubiri la kupendeza linalochoma dhamiri zetu na ni la kukumbukwa litatuelekeza katika “kumcha Mungu na kuzishika amri zake.” Hii inatupatia mtazamo mwingine wa maana ya kumcha Mungu.)
1. Tunajifunza nini kutoka kwenye rejea ya “kusoma sana” na “uchoshi?” (Mahubiri sio tu kwamba yanapaswa kuwa ya kufurahisha, hayatakiwi kutuchosha. Kulirahisisha hubiri, kuyafanya mambo magumu kuwa mepesi na ya kuvutia, husaidia kukazia ujumbe.)
D. Soma Mhubiri 12:14. Unaona mfanano gani katika Ufunuo 14:7? (Yote mawili yameelezewa katika muktadha wa hukumu inayokuja.)
III. Kuzishika Amri na Kumtukuza
A. Soma Waefeso 2:8-9. Kuna uhusiano gani kati ya kuishika sheria na kuokolewa? (Hatuokolewi kwa matendo yetu ya kuishika sheria.)
B. Soma Waefeso 2:10. Sisi tu “kazi ya Mungu” tulioumbwa “tutende matendo mema.” Hiyo inaashiria kuwa ni nini sababu ya sisi kutenda matendo mema? (Mtengenezaji [Muumbaji] anajivunia kazi yake. Yesu anatutaka tuwe mfano hai wa kinachomaanishwa kuwa Mkristo. Tunataka kumfanya Yesu atujivunie.)
C. Soma Mathayo 5:14-15. Tunapaswa kuifanyia nini nuru? (Kuiweka mahala inapoweza kuonekana.)
1. Kifungu hiki kinasema kuwa sisi ni “nuru ya ulimwengu.” Kwa nini vifungu hivi vinajihusisha zaidi kuhusu mahali pa kuweka nuru badala ya asili [chanzo cha] ya nuru? (Ili kuwa mfuasi wa kweli wa Mungu inamaanisha kuwa sisi ni “nuru” ya asili. Hata hivyo, hiyo haitatui swali la mahali nuru inapowekwa.)
D. Soma Mathayo 5:16. Hii inaielezea nuru vizuri zaidi. Nuru ya Mkristo ni ipi? (“Matendo mema.”)
1. Malengo ya wewe kutenda mambo mema ni yepi? (Unamtukuza Mungu.)
2. Kama matendo yako mema ndio nuru inayomtukuza Mungu, tunayawekaje matendo yetu mema mahali ambapo ulimwengu unaweza kuyaona? Tunajibuje changamoto ya mahali pa kuiweka nuru?
E. Soma Mathayo 6:1-2. Unapatanishaje kifungu hiki na dhana ya kwamba matendo yetu mema yanatakiwa kuonekana ili tuweze kumtukuza Mungu?
1. Inamaanisha nini kusema kwamba watu hawa wanaoyatangaza matendo yao mema “wamekwisha kupata thawabu yao?”(Sifa zinazotoka kwa wengine ndio kipimo cha thawabu yao.)
F. Soma Mathayo 6:3-4. Je, unaweza kuja na mpango wa kubadilisha utakaokusaidia kuyatenganisha haya matendo mema katika Mathayo 6 na matendo mema yaliyopo katika Mathayo 5? (Ukiangalia Mathayo 6:4 inaonekana kuwa lengo la matendo katika Mathayo 6 ni thawabu kwa mtu anayetenda matendo mema. Katika Mathayo 5 lengo la matendo ni kumtukuza Mungu.)
1. Je, hiyo inamaanisha kuwa jibu la utenganisho ni kuuliza “Lengo langu ni lipi kwenye haya matendo?”
a. Mara baada ya kuyatenganisha je, hiyo itasaidia katika fumbo linaloendelea kuhusu namna tunavyopaswa kuziweka ili ulimwengu uyaone matendo yetu mema?
2. Je, hili ni rahisi kutenganisha? (Sio kwa upande wangu. Lengo langu katika kuandika masomo haya ni kuwahamasisha watu kusoma Biblia na kuyatafakari mapenzi ya Mungu. Hii humtukuza Mungu. Juma lililopita mtu wa muhimu mwenye ushawishi mkubwa aliniambia kuwa anasoma masomo haya mara kwa mara. Nilichukulia hilo kama taadhimu njema na ilinitukuza.)
3. Kama siko peke yangu ninayehangaika kutofautisha suala la kumtukuza Mungu na kujitukuza, jibu ni lipi? Je, tunapaswa kujiuliza kuwa ni nini lengo letu la msingi kwa ajili ya matendo mema?
G. Soma Zaburi 75:4-7. Je, hili ndilo jibu la jinsi tunavyopaswa kuyaendea matendo mema? (Ndiyo. Hatupaswi kuwa watu wa kujiinua kwa ajili ya kujitukuza. Hilo ndilo lililokuwa tatizo katika Mathayo 6. Badala yake, tunapaswa kumsubiria Mungu kutuinua (au kutotuinua). Tunapaswa kumwachia Mungu suala la ubadilishaji (huku tukiruhusu nuru yetu iangaze.)
H. Rafiki, lengo la maisha yako ni kumcha Mungu na kumtukuza. Malengo haya yanaungana katika mtazamo wa kumpendeza Mungu kwa kuyatenda mapenzi yake. Je, utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie kumcha Mungu kwa usahihi na kumtukuza?
IV. Juma lijalo: Habari Njema za Hukumu.