Somo la 2: Kipindi cha Majaliwa

Ufunuo 14, Mathayo 24, Marko 4
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
2
Lesson Number: 
2

Somo la 2: Kipindi cha Majaliwa

(Ufunuo 14, Mathayo 24, Marko 4)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Juma hili nilisoma matokeo ya utafiti wa zaidi ya wanafunzi 37,000 wa vyuo uliofanywa na Mfuko wa Haki ya Elimu kwa Mtu Binafsi. Utafiti huo ulihusiana na suala la uhuru wa kutoa maoni na fujo. Karibia 25% ya wanafunzi waliamini kwamba ni haki kutumia vurugu kumzuia mnenaji mbishani (controversial). Katika vyuo kadhaa maarufu vya wanawake idadi hiyo ilikaribia 50%. Wewe, rafiki, ni mnenaji mbishani. Yesu anafundisha katika Yohana 15:19 kwamba ikiwa sisi “si wa ulimwengu” basi ulimwengu utatuchukia. Mabadiliko haya makubwa ya maoni (nchini kwangu) yananiambia kuwa tunaelekea kwenye kipindi cha majaliwa kwa ajili ya chaguzi za kidini tunazozifanya. Yumkini kipindi hiki kinakuja mapema zaidi kuliko tunavyodhani. Hebu tuzame kwenye Biblia zetu na tujifunze zaidi!

I.  Wavunaji

A.  Soma Ufunuo 14:14-15. Nani aliyeshikilia mundu? (Ni Yesu.)

1.  Nani anayempa Yesu amri ya kuanza kuvuna? (Taswira ya mjumbe kutoka ndani ya hekalu inaashiria kwamba Mungu Baba anampa malaika ujumbe kwa ajili ya Yesu: muda wa ujio wa Mara ya Pili ni sasa.)

2.  Kwa nini Yesu asijue saa ya kurudi kwake? (Soma Mathayo 24:36. Kifungu kinatuambia kuwa Mungu Baba pekee ndiye anayejua.)

B.  Soma Marko 4:26-29. Je, mavuno tunayoyajadili katika Ufunuo 14 ni kwa ajili ya watu wema au wabaya? (Pendekezo kutoka kwenye vifungu vingine, kama hiki hapa kwenye kitabu cha Marko, ni kwamba ni watu wema. Dhana hii inaungwa mkono na ukweli kwamba Yesu mwenyewe ndiye anayefanya uvunaji.)

1.  Je, mavuno ni jambo jema? (Ndiyo! Yesu anaingilia kati kuwachukua watu wake nyumbani pamoja naye.)

C.  Soma Ufunuo 14:17-19. Je, haya ni mavuno ya watu wema au wabaya? (Wabaya. Wanatupwa “katika shinikizo la ghadhabu ya Mungu.” Hiyo inatuambia kuwa hao ni waliopotea. Malaika “mwenye mamlaka juu ya moto” anamwamuru malaika mwingine kuzivuna zabibu hizi. Tofautisha hili na Yesu akifanya uvunaji.)

D.  Soma Ufunuo 14:20. Hii inaashiria nini kuhusu idadi ya wapotevu? (Hii ni damu nyingi sana.)

E.  Tunapaswa kuhitimisha nini kutokana na vifungu hivi tulivyojifunza? (Muda unakuja ambapo hukumu ya mwisho itatolewa.)

1.  Unadhani kwa nini Biblia inatoa taswira ya jambo hili kama mavuno?

II.  Ishara ya Wavunaji

A,  Soma Mathayo 24:3. Wanafunzi wanauliza swali lisilo sahihi, bali linahusiana na “mwisho wa nyakati.” Kwa nini wanafunzi wanamwendea Yesu “faraghani?” (Wanaamini kuwa hii ni taarifa ya muhimu kwa ajili ya watu wa ndani.)

B.  Katika Mathayo 24:5-7 Yesu ananukuu matukio yatakayoashiria ujio wake wa Mara ya Pili. Soma Mathayo 24:8-9. Sasa tunao mpito wa matukio. Unaelezeaje mpito huu? (Yesu anatuambia kuwa mambo mabaya yatafuatia.)

C.  Soma Mathayo 24:10-12. Ni mambo gani haya mabaya sana yanayoendelea Yesu anapokuja? (Watu watakuwa na chuki. Upendo wa wengine “utapoa.”)

1.  Marekani imeandika kwenye Katiba na sheria zake dhana ya kwamba kila mtu anapaswa kuwa na uhuru wa kutoa maoni hata kama wananchi hawataki kusikia kile kinachosemwa. Mjibizo halali kwa mambo usiyotaka kuyasikia ni kuondoka zako katika eneo mambo hayo yanaposemwa. Tiba ya taarifa isiyo sahihi ni taarifa nyingi zaidi. Mjibizo unaotaarifiwa katika Mathayo 24 ni upi? (Kifungu cha 9 kinataarifu juu ya chuki ambayo matokeo yake ni kifo chako.)

2.  Utafiti niliourejelea kwenye sehemu ya utangulizi inatuambia nini kuhusu kizazi kijacho? (Vijana wengi wadogo hawajafundishwa kuupenda uhuru, bali wamefundishwa kuchukia. Ikiwa vurugu dhidi ya maoni usiyoyapenda ni jambo sahihi, basi huoneshi upendo. Watu wengi wanapokuwa na mtazamo kama huo basi hakuna tena jamii iliyo huru.)

D.  Soma Mathayo 24:13. Wajibu wako ni upi? (Kuvumilia uhasama.)

1.  Unadhani hiyo inamaanisha nini hasa? Moyo wangu (wa kisheria) wa asili ni kupambana. Kuwapinga wale wanaoukataa uhuru.

E.  Soma Mathayo 24:14. Hii inaendanaje na dhana ya kwamba haki za uhuru wa maoni zimepungua? Hii inaashiria kuwa tunapaswa kupingaje? (Tuna mapambano mawili yanayofanana. Kwanza, tunafanya kazi ya kubadili mioyo kwa njia ya injili. Watu wanaoongolewa hawana chuki. Pili, kuulinda uhuru wa kutoa maoni ili tuweze kupeleka injili ya Yesu inatupasa kupambana dhidi ya ukandamizaji kwa njia za kisheria. Hebu tuliangalie hili kwa kina zaidi katika sehemu inayofuata.)

III.  Tunachopaswa Kukifanya

A.  Hebu tuangalie tena Marko 4:26-29 lakini kwa upande tofauti. Soma Marko 4:26. Hii inatuambia kuwa wajibu wa mkulima ni upi? (Kutawanya mbegu.)

B.  Soma Marko 4:27. Jambo gani linazungumziwa kifungu kinaposema mkulima “asivyojua yeye” jinsi mbegu inavyomea na kukua? (Hawajibiki na hatua za ukuaji.)

1.  Hebu tutumie hili kwenye onyo la kwamba tutachukiwa katika siku zijazo kutokana na ujumbe wetu wa injili. Hii inaashiria mkakati gani ili kupunguza chuki? (Wajibu wetu ni kupeleka injili. Wajibu huo unafafanuliwa kwa ufinyu sana. Haionekani kujumuisha mabishano na maadui wa injili.)

C.  Soma Mathayo 28:19-20. Wajibu wetu unaoendelea hadi “mwisho wa nyakati” ni upi? (Wafanye kuwa wanafunzi. Wabatize. Wafundishe.)

1.  Ikiwa ubishani una nafasi kwenye mfululizo huu, utakuwa sehemu gani? (Kwenye sehemu ya ufundishaji. Sehemu ya ufundishaji inahusiana na wale waliobatizwa.)

D.  Soma Mathayo 10:14-15. Hii inatufundisha nini kuhusu kubishana na wapinzani wa injili? (Hatupaswi kubishana nao, badala yake tunapaswa kuwaacha wapinzani hawa wakabiliane na hukumu yao ya mwisho.)

1.  Jambo gani litakufanya utake kubishana na wapinzani wa injili? (Majivuno.)

2.  Je, hii inamaanisha kuwa kamwe hatutakiwi kuwa na majadiliano na wasioamini? (Hapana. Walengwa wa ujumbe wetu ni watu, sio wapinzani tunaofanya nao mdahalo.)

E.  Soma Mathayo 10:16. Hii inatuambia nini kuhusu kutumia akili ya kawaida (mantiki)?

F.  Soma Mathayo 10:21-23. Usaliti utakuwa jambo la binafsi kwa kiasi gani? (Wanafamilia watakusaliti na watoto wako watafanya uuawe.)

1.  Angalia tena utafiti uliobainishwa kwenye sehemu ya utangulizi ambapo karibia 25% ya wanafunzi wa vyuo wanaamini kuwa vurugu ndilo jibu la mambo wasiyotaka kuyasikia. Je, hiyo inafanya Mathayo 20:21 ieleweke vizuri zaidi?

2.  Tunapata ushauri gani katika Mathayo 10:23 kuhusu kuwa na msimamo, kupambana, au kujadiliana (mdahalo)? (Tunapokabiliana na mateso halisi tunapaswa kukimbia.)

G.  Soma Mathayo 10:26. Kama wenye chuki hawa wanataka kutuua, kama tunaambiwa tukimbie, tunawezaje kutokuwa na hofu?

1.  Nini kinamaanishwa kwa waliofichwa kujulikana? (Ukweli wa nani yuko sahihi na asiye sahihi hatimaye utajulikana.)

H.  Soma Mathayo 10:27. Tunapaswa kuwa na mtazamo wa namna gani tunapopeleka injili? (Huu ni mtazamo wa uthabiti. Kutokuwa na hofu maana yake ni kwamba tupeleke injili, lakini pia tunapaswa kuwa tayari kurudi nyuma itakapohitajika kufanya hivyo.)

I.  Soma Mathayo 10:28. Nadhani hili ni jibu la msingi kwenye swali la awali kuhusu namna ambayo tunaweza tusiwe na hofu. Ni namna gani hiyo? (Tunaweza kuuawa duniani, lakini hatuwezi kuzuiliwa uzima wa milele. Uzima wa milele ndio majaliwa yetu.)

J.  Rafiki, kipindi kizuri na cha kutisha kinakuja. Je, utamkiri Yesu kama Mwokozi wako sasa hivi ili uwe miongoni mwa mavuno yatakayochukuliwa mbinguni? Je, hutaogopa kushiriki hizi habari njema na wengine hata kama unachukiwa kwa habari hizo? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu akusaidie kuwa na ujasiri kwa ajili ya kipindi hiki cha majaliwa?

IV.  Juma lijalo: Injili ya Milele.