Somo la 11: Kusimamia Nyakati Ngumu

2 Mambo ya Nyakati 20, Ufunuo 13
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
1
Lesson Number: 
11

Somo la 11: Kusimamia Nyakati Ngumu

(2 Mambo ya Nyakati 20, Ufunuo 13)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Takriban miaka kumi na sita iliyopita nilipoanza kufundisha katika shule ya sheria, niliwataka wanafunzi wangu wa somo la “Labor Law” wasome makala inayohusu mgomo uliotokea nchini Ufaransa. Nilichokitaka kwao ni kulinganisha hali ya migomo nchini Ufaransa na Marekani. Mgogoro uliokuwepo nchini Ufaransa ulihusu ukubwa wa deni la taifa la Ufaransa na uwezo wake wa kufikia vigezo vya kuingia katika Umoja wa Ulaya. Uwiano wa deni na pato la nchi ya Ufaransa ulikuwa chini, lakini wachumi wa Ulaya walisema kuwa uwiano huo ulitakiwa kuwa chini zaidi. Hii leo, nchi hizi hizi za Umoja wa Ulaya zina madeni ya taifa yanayokaribiana kabisa na pato lao. Hali iko vivyo hivyo nchini Marekani. Deni la taifa la Japan ni kubwa sana kuzidi pato lake. Mimi sio mtaalamu wa deni la taifa, lakini mabadiliko haya makubwa yananifanya niamini kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kutokea anguko kubwa la kiuchumi duniani sasa kuliko ilivyokuwa huko miaka ya nyuma. Wakristo wanapaswa kujiandaaje kwa tukio kama hilo? Tunapaswa tutumie njia gani kushughulika na nyakati ngumu? Hebu tuchunguze kile Biblia inachotufundisha kuhusu namna ya kushughulika na migogoro!

I.  Mgogoro wa Yehoshafati

A.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:1-2. Majeshi mangapi yameishambulia Yuda? (Matatu! Maoni ya kwamba wapo En-gedi inamaanisha kuwa wapo umbali wa saa kumi na tano!)

B.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:3. Mfalme Yehoshafati anakuwa na mwitiko (reaction) gani kutokana na habari hizi? (Anaogopa.)

1.  Kama majeshi yanaishambulia nchi yako na wewe ndiye Mfalme, mambo yatakuwaje endapo watashinda?

2.  Somo letu linahusu kushughulikia migogoro. Je, ni sahihi kuogopa pale unapokabiliana na matatizo? (Tatizo sio uoga wa awali, bali ni kile unachokifanya kuhusiana na uoga huo.)

3.  Yehoshafati anachukua hatua gani ya kwanza? (Anamtafuta Bwana na kutangaza kufunga. Huku ni kufunga na kuomba.)

a.  Jiweke kwenye nafasi ya Yehoshafati. Ana chaguzi gani nyingine? (Kulikusanya jeshi. Kuimarisha ulinzi wa mji. Angeweza pia kutoroka.)

C.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:4-5. Yehoshafati alifanya jambo gani jingine kwa kuzingatia maombi? (Anawakaribisha wengine waungane naye katika maombi kuhusu mgogoro huu.)

1.  Je, inaonekana kuwa jambo la ajabu kwako kwamba unapokabiliana na jeshi la uvamizi unawakusanya mashujaa wa maombi na sio mashujaa wako wa kijeshi?

2.  Unapata mafunzo gani katika hili kwa ajili ya mgogoro wowote unaoupitia sasa maishani mwako?

3.  Tafakari matatizo ya nyuma maishani mwako. Je, kwanza ulizikimbilia rasilimali zako mwenyewe? Au, je, kwanza ulimkimbilia Mungu?

II.  Ombi la Yehoshafati

A.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:6. Unaweza kuelezeaje mwanzo wa sala ya Yehoshafati? (Ni kusifu. Inathibitisha uwezo wa Mungu.)

B.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:7-9. Unaelezeaje sehemu hii ya ombi la Yehoshafati? (Anadai ahadi ya Mungu. Anaelezea jinsi ahadi hii ilivyofanya kazi siku za nyuma.)

C.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:10-11. Je, Yehoshafati anamlaumu Mungu kutokana na jinsi mambo yalivyo sasa? (Inaweza kusomeka hivyo. Badala yake, tunaweza kuliangalia hili kama sehemu ya ahadi: “Mungu, ulitupatia nchi hii ulipowaruhusu washambulizi wetu wa sasa kuishi. Kuishi tukiwa pamoja nao wakituzunguka ilikuwa sehemu ya mpango wako wa awali. Tunakuhitaji ili kuulinda mpango wa awali.”)

D.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:12. Je, Yehoshafati anapendekeza suluhisho kwa Mungu kabla hajasema “Hatujui nini cha kufanya?” (Ndiyo. Anamwomba Mungu atoe hukumu kwa washambuliaji.)

1.  Ninadhani kipengele cha muhimu kwenye ombi hili kinapatikana katika kifungu cha 12. Unadhani ni kipi hicho? (Mungu, hatuwezi kupambana nao, tunakutegemea ili kutuokoa na janga hili. Tuna pendekezo la suluhisho, lakini tunahitaji suluhisho lako.)

E.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:13. Je, kuna mambo mengi ya kufanya ili kujiandaa kuuzuia uvamizi? Wanafanya nini? (Wanamsubiria Mungu.) 

III.  Jibu la Mungu

A.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:14. Jibu halitolewi moja kwa moja kwa Mfalme Yehoshafati, bali kupitia kwa nabii wa Kilawi aitwaye Yahazieli. Je, kuna fundisho kwa ajili yetu katika hilo? (Wakati mwingine Mungu atanena nasi na kutupatia jibu kupitia kwa watu wengine ambao amewachagua.)

B.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:15. Mungu anajibu juu ya wasiwasi gani kwanza? (Anawatuliza watu wake. Anawaambia wawe watulivu kwa sababu atalishughulikia tatizo.)

C.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:16. Tafakari asili ya mwelekeo wa Mungu. Kuna jambo gani zuri ajabu juu ya mwelekeo huo? (Mungu anawapa taarifa kuhusu kile kitakachotokea. Anawaambia watu wake juu ya mwenendo wa maadui wao unaofuata.)

D.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:17. Je, watu wa Mungu watatakiwa kupigana? (Hapana.)

1.  Watatakiwa kufanya nini? (Wajitokeze. “Simameni imara, jipangeni.”)

a.  Tumia maelekezo haya kwenye mapambano yako maishani mwako. Mungu anatutaka tufanye nini? (Tusihafifishe mambo ambayo maelekezo yake yako dhahiri. Tunaweza tusihitajike kupigana sisi binafsi, lakini tunatakiwa kusimama imara katika nafasi yetu.)

E.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:18-19. Mungu anapojibu maombi yetu, mtazamo wetu unatakiwa kuwaje? (Tumtukuze Mungu.)

F.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:20. Je, watu wanatakiwa kutiwa moyo ili kuuamini ujumbe wa Mungu? Je, unahitaji kutiwa moyo ili kuziamini ahadi zilizopo kwenye Biblia na ujumbe wa aina mbalimbali kutoka kwa Roho Mtakatifu?

G.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:21. Je, watu wameamini kwamba wanapaswa kumtumaini Mungu? (Wao ni sehemu ya uamuzi wa kuongoza kwa kwaya!)

1.  Tafakari jambo hili. Mungu anasema, “Niamini Mimi, nitalishughulikia hili. Wewe jitokeze tu na kusimama imara.” Watu wa Mungu wanajibu kwa kuweka kwaya mbele ya jeshi ili kumwimbia Mungu nyimbo za sifa na utkufu. Mungu hakusema chochote kuhusu kwaya. Alisema tu kwamba, “simameni imara.” Tunaweza kufanya nini katika kushughulikia matatizo maishani yanayoakisi udhihirisho huu wa imani?

H.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:22. Uvamizi ulianza wakati gani? (Watu walipoanza kuimba.)

I.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:23-24. Nini kimetokea? (Majeshi matatu yaliyoungana yamegeukiana. Wameshambuliana wao kwa wao hadi wote kabisa walipokufa!)

1.  Je, unaweza kuona suluhisho kama hili likiwatokea wale wanaokusababishia matatizo maishani mwako? (Maadui wako wanashindana wao kwa wao. Shambulizi lao kwako linawageukia wenyewe. Uwezo na nguvu zao vinawageukia dhidi yao.)

J.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:25. Mgogoro huu unageuka na kuwaje kwa watu wa Mungu? Matokeo ya kumtumaini kwao Mungu kikamilifu ni yepi? (Adui ameshindwa kabisa. Sasa watu wa Mungu wanamiliki mali za adui. Watu wa Mungu wanasitawishwa kutokana na kipimo hiki cha imani na kumtumaini kwao Mungu.)

K.  Hebu tupitie tena ombi la Mfalme Yehoshafati katika 2 Mambo ya Nyakati 20:10. Anamkumbusha Mungu kwamba kuyaruhusu mataifa haya matatu kuendelea kuwepo inaweza kuwa ni uchaguzi mbaya. Je, ni kweli? (Watu wa Mungu sio tu kwamba imani yao inaimarishwa, bali utajiri wao pia unaongezeka. Matokeo yake ni kwamba huu unaonekana kuwa uamuzi sahihi.)

L.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:26-27. Tunaona jambo gani mwishoni mwa mgogoro huu? (Furaha! Hisia za ushindi kwa njia ya uwezo wa Mungu.)

M.  Soma 2 Mambo ya Nyakati 20:29. Je, hii inaweza kuwa wewe? Ukimruhusu Mungu apigane mapambano yako, je, wapinzani wako watajifunza kuogopa kujaribu kukudhuru?

IV.  Mustakabali

A.  Ufunuo 13 inatabiri mustakabali wa mgogoro ujao kwa watu wa Mungu unaowataka wachague kati ya kusimama imara na kumtumaini na kumwabudu Mungu au kuwa hafifu na kuwaabudu maadui wa Mungu. Soma Ufunuo 13:16-17. Je, teknolojia imetufikisha mahali ambapo serikali ina uwezo na mamlaka ya kufanya hivi? (Nimeona kipande cha video ambapo wale wanaoishi nchini China hawawezi kupanda treni bila uthibitisho wa kompyuta juu ya hali yao (status) kwa serikali. Nchini Canada, akaunti za benki za madereva wa magari makubwa (trucks) zilisitishwa na serikali bila amri ya mahakama. Nina saa ambayo inafanya malipo kidigiti. Hili linaweza kutokea kufumba na kufumbua!)

B.  Rafiki, inawezekana kwa sasa uko kwenye mgogoro. Biblia inatuambia kuwa watu wa Mungu watakuwa katika mgogoro katika kipindi cha mwisho wa nyakati. Je, utamwomba Roho Mtakatifu akupatie ujasiri kama wa Mfalme Yehoshafati ili kumgeukia Mungu mara moja pale unapokuwa kwenye mgogoro na kuutegemea uwezo wake na wala sio kuzitegemea nguvu zako mwenyewe?

V.  Juma lijalo: Thawabu za Uaminifu.