Somo la 3: Mkataba wa Zaka

Mwanzo 14, Waebrania 7, 1 Wakorintho 9
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
1
Lesson Number: 
3

Somo la 3: Mkataba wa Zaka

(Mwanzo 14, Waebrania 7, 1 Wakorintho 9)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Juma lililopita tulijadili kwamba wokovu hupatikana bure, lakini Mungu anatupatia changamoto ili kupokea baraka za pekee. Juma hili tunaingia kwa kina zaidi kwenye somo la utoaji zaka. Mungu anatutarajia tufanye nini? Kitendo hiki kinawasilisha fursa gani zilizopo? Je, suala la zaka ni suala la nadharia tu? Bibilia inafundisha nini hasa juu ya zaka kwa Wakristo? Hebu tuzame kwenye somo letu na Biblia na tujifunze zaidi! 

I.  Muda wa Zaka

A.  Mwanzo sura ya 14 inaandika juu ya pambano kubwa miongoni mwa wafalme tisa katika eneo ambalo Lutu, mpwa wa Ibrahimu, aliishi. Lutu alichukuliwa mateka, pamoja na mali yake yote. Ibrahimu alipata habari juu ya janga hili na kwa kutumia jeshi lake (ndiyo, alikuwa na jeshi dogo), akawashinda wafalme waliomteka Lutu, na kurejesha sio tu mali za Lutu, bali pia mali nyingi za watu wengine. Hebu tusome Waebrania 7:1-2. Ibrahimu alikutana na nani alipokuwa anarejea kutoka katika ushindi wake vitani? (Melkizedeki, Mfalme wa Salemu na Kuhani wa Mungu aliye juu.)

1.  Kuna jambo gani lisilo la kawaida juu ya maelekezo ya kazi ya Melkizedeki? (Alikuwa kuhani na mfalme. Kamwe Mungu hakuunganisha nafasi ya mfalme na nafasi ya kuhani katika Agano la Kale.)

B.  Soma Waebrania 7:3. Mwandishi wa Waebrania anaelezeaje hali hii isiyo ya kawaida? (Anasema kuwa Melkizedeki anafanana na Yesu. Yesu ni Mfalme na Kuhani wetu Mkuu.)

C.  Soma Waebrania 7:4-6. Msisitizo wetu hauhusu mtazamo wa Mungu juu ya uhusiano kati ya kanisa na taifa, bali ni juu ya zaka. Kwa nini Ibrahimu alimtolea zaka Melkizedeki? (Melkizedeki alikuwa “kuhani wa Mungu aliye juu” (Waebrania 7:1), na alimbariki Ibrahimu. Waebrania 7:6.)

1.  Je, kuna kiashiria chochote kwamba Melkizedeki, kwenye nafasi yake kama Mfalme wa Salemu, alimsaidia Ibrahimu kushinda pambano? (Hapana. Ukipitia Mwanzo 14 Mfalme wa Salemu hakuwa mpiganaji. Badala yake, alijitokeza akiwa na divai na mkate kumpokea Ibrahimu baada ya pambano. Mwanzo 14:17-18. Inaonekana kama vile aliandaa mandari!)

a.  Je, hii inakukumbusha juu ya Ushirika Mtakatifu?

D.  Angalia tena Waebrania 7:6. Hii inatufundisha nini kuhusu kutoa zaka nje ya mfumo wa Kilawi uliowekwa na Musa? (Kifungu hiki na muktadha wake kinaonesha kwamba utoaji zaka ulikuwepo pasipo kutegemea mfumo wa kikabila wa watu wa Mungu katika Agano la Kale.)

1.  Hii inazungumzia juu ya ukosoaji mkubwa wa utoaji zaka katika zama za leo. Juma lililopita nilizungumzia kwenye mjadala wetu wa Malaki 3 kwamba mfumo wa hekalu na “ghala” (Malaki 3:10), viliangamizwa, na ukuhani wa Kilawi haukuwepo tena. Je, utoaji zaka unajitegemea tofauti na mfumo wa Agano la Kale wa hekalu na ukuhani? (Ndiyo.)

2.  Tafakari juu ya uhalisia kivitendo. Ibrahimu alikuwa na umri wa kati ya miaka 75 na 100 alipokutana na Melkizedeki. Hakuna kumbukumbu yoyote huko nyuma ya Ibrahimu kutoa zaka, na huu utoaji zaka hautokani na mapato ya Ibrahimu (angalia Kumbukumbu la Torati 14:22), bali unatokana na nyara zilizotokana na kushinda pambano. Angalia Waebrania 7:4. Tunapaswa kuhitimisha nini kutokana na hili? (Kwa dhahiri huu ni mfumo tofauti wa zaka. Melkizedeki ni aina ya Yesu, hivyo kwa kiasi kikubwa hii inaashiria kuwa nje ya mfumo wa Agano la Kale Wakristo wana wajibu fulani hivi wa kutoa zaka kwa Yesu.)

E.  Katika Mwanzo sura ya 28 tunamwona Yakobo (mjukuu wa Ibrahimu) akimkimbia ndugu yake Esau kutokana na udanganyifu wake. Anaelekea kwenye nyumba ya mjomba wake Labani wakati anapokea ndoto kutoka kwa Mungu akimpa ahadi ile ile kama iliyotolewa kwa Ibrahimu. Soma Mwanzo 28:16-18. Je, Yakobo analichukulia tukio hili kama tukio kubwa maishani mwake? (Ndiyo, kwa sababu analiwekea alama kwa kutumia nguzo ya jiwe.)

F.  Soma Mwanzo 28:20-22. Je, zaka hii inafanana na mazingira ya Ibrahimu au zaka ya Kilawi? (Hapana.)

1.  Kuna tofauti gani? (Anaweka vigezo vya utoaji zaka wake. Mungu anatakiwa kutekeleza mambo fulani kabla Yakobo hajarejesha “sehemu ya kumi” “katika kila utakalonipa.”)

2.  Je, inaonekana kama Yakobo alitoa zaka kabla ya tukio hili? (Kwenye kipindi kati ya Ibrahimu na Melkizedeki na kisa hiki cha Yakobo hakuna popote palipotajwa kuhusu utoaji zaka. Hoja juu ya kutokuwepo kwa zaka ni dhaifu. Lakini, maneno ya Yakobo yanaashiria kuwa hakuwa akitoa zaka, lakini kwamba anafahamu juu ya dhana ya utoaji zaka.)

3.  Yakobo atakuwa anamtolea nani zaka ukizingatia Mlawi ndiye kijana wake ajaye? (Mwanzo 28:22 inasema tu kuwa anamtolea Mungu.)

4.  Yakobo alikuwa na umri gani wakati anatoa ahadi hii yenye masharti? (Nilisoma ufafanuzi wa kina unaoashiria kwamba inawezekana alikuwa na umri wa zaidi ya miaka 63.)

5.  Unadhani jambo gani liliamsha ari yake ya utoaji zaka? (Alitoa zawadi kwenye uhusiano wake na Mungu. Aliizungumzia zaka katika muktadha wa kubarikiwa.)

G.  Mifano ya Ibrahimu na Yakobo inatuonesha kuwa utoaji zaka ulikuwepo nje ya mfumo uliowekwa na Musa kwa ajili ya kulitegemeza kabila la kikuhani. Hata hivyo, zaka hiyo ilikuwa na tofauti kubwa. Kuna mfanano gani mkubwa kati ya hii mifumo ya utoaji zaka? (Kwanza ni kiasi. Zote zinahusisha utoaji wa 10%. La pili ni kwamba zote zinafungamanishwa na baraka za Mungu. Utoaji zaka unahusiana na kubarikiwa!)

II.  Ghala

A.  Soma Kumbukumbu la Torati 12:5-6. Je, ghala la Hekalu lilikuwepo katika kipindi hiki? (Hapana. Maelekezo haya yalikuwepo kabla Hekalu halijajengwa. Kimsingi, watu walikuwa bado hawajavuka mto Yordani kuingia nchi ya ahadi. Angalia Kumbukumbu la Torati 12:10.)

1.  Watu wanapaswa kupeleka zaka na sadaka zao wapi? (Mahali ambapo Mungu “atapachagua ... apaweke jina lake maana ni makao yake.”)

2.  Mimi ni mshiriki wa kanisa ambalo lina mfumo wa aina moja wa malipo kwa wachungaji na walimu. Kila mmoja analipwa kwa mujibu wa ngazi ya mshahara, na malipo yao hayategemei utajiri wa kanisa lake mahalia. Je, kutoa zaka na sadaka kwenye hilo “ghala” ni tafsiri yenye mantiki ya maelekezo ya kutoa pale ambapo Mungu “ameweka jina lake?”

B.  Soma Hesabu 18:21. Zaka ilitolewa kwa ajili ya kazi gani? (Kuwalipa Walawi waliotumikia “katika hema ya kukutania.” Malipo kwa Walawi yalitangulia uwepo wa Hekalu.)

C.  Soma Kumbukumbu la Torati 12:8-9. Watu walikuwa wanafanyia nini zaka zao kabla hawajaingia katika nchi ya ahadi? (Walikuwa wanafanyia chochote walichodhani kuwa ni sahihi.)

1.  Je, kifungu hiki kinaashiria kuwa hili ni jambo jema au baya?

III.  Zaka Katika Zama za Leo

A.  Soma 1 Wakorintho 9:6-7. Paulo anazungumzia jambo gani kuhusu watendakazi wa injili? (Kama unafanya kazi ili kuutangaza Ufalme wa Mungu, unapaswa kulipwa kwa kazi hiyo.)

B.  Soma 1 Wakorintho 9:8-10. Paulo anatoa wito juu ya jambo gani kwenye hoja yake kwamba watumishi wa Kikristo wanapaswa kutegemezwa na makanisa yao? (Anarejelea “Torati ya Musa.”)

1.  Torati ipi ya Musa? (Kumbukumbu la Torati 25:4, inayorejelea kuwaacha ng’ombe wale.)

2.  Kwa nini, kati ya mambo yote, Paulo anarejelea torati inayohusu kuwategemeza ng’ombe na sio torati juu ya utoaji zaka?

C.  Soma 1 Wakorintho 9:11-13. Torati gani ya Musa inarejelewa hapa? (Hii ni rejea ya mfumo wa utoaji zaka wa Kilawi.)

D.  Soma 1 Wakorintho 9:14. Hii inatuambia nini juu ya mfumo wa Mungu wa kuwategemeza watendakazi wake wa injili? (Paulo anaaiita “amri,” kwamba tuwategemeze viongozi wetu wa kiroho.)

1.  Hebu tuiangalie amri hiyo ambayo tunaweza kuisoma katika Luka 10:7. Nani anayeweka kiwango cha ujira? (Mmiliki wa nyumba.)

E.  Soma 2 Wakorintho 9:6-7. Kifungu hiki kinasema kuwa kiasi gani kitolewe? (Chochote “alichokusudia moyoni mwake.”)

1.  Je, hiki ni kiasi cha kutegemeza huduma ya utume? (Ukiiangalia sura yote, 2 Wakorintho 9, utaona kuwa huu ni msaada kwa Wakristo wengine, na sio kuwategemeza watenda kazi. Ni sawa na sadaka ya hiari, badala ya zaka.)

F.  Rafiki, tafakari juu ya wajibu wako wa kuitegemeza kazi ya Mungu. Kama wewe u mkarimu kwa Mungu, naye atakuwa mkarimu kwako!

IV.  Juma lijalo: Sadaka kwa Ajili ya Yesu.