Somo la 1: Sehemu ya Familia ya Mungu

1 Mambo ya Nyakati 17, Mathayo 6 & 25, 1 Yohana 5
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
1
Lesson Number: 
1

Somo la 1: Sehemu ya Familia ya Mungu

(1 Mambo ya Nyakati 17, Mathayo 6 & 25, 1 Yohana 5)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Daniel Pink aliandika kitabu maarufu sana kiitwacho Drive. Katika kitabu hicho alichimbua mambo yanayotutia hamasa. Unaweza kushangaa kutambua kwamba jibu sio fedha. Fedha ni za muhimu hadi katika hatua ambayo tumeridhika – ikimaanisha kwamba tuna nyumba nzuri na tunaweza kumudu kula vyakula migahawani. Baada ya hatua hiyo, kinachomtia hamasa mwajiriwa ni uhuru, utawala, na lengo. Yesu anatuambia katika Yohana 15:15 kwamba hatuiti tena watumwa, bali marafiki. Zaidi ya hayo anatuita wanaye wa kiume na wa kike. 2 Wakorintho 6:18. Je, mwandishi Pink ametumia kanuni ya Biblia – kwamba mfumo wa Mungu wa uhamasishaji kwa familia yake ni jambo jingine zaidi ya fedha? Hetu tuzame kwenye somo letu la kwanza kwenye mada inayohusu fedha katika Biblia na tujifunze zaidi!

I.  Utawala

A.  Soma Mwanzo 1:26. Lichukulie hili kama maelekezo ya kazi. Majukumu yako ni yepi? (Unafanana na Mungu! Katika vigezo vya mahala pa kazi, wewe ni sawa na mtendaji mkuu. Una utawala dhidi ya wanyama wote.)

1.  Ina maanisha nini kuwa na “utawala?” (Wewe ndiye msimamizi! Mungu amekuweka kuwa msimamizi.)

B.  Soma Mwanzo 2:15. Mungu amekupatia majukumu gani mengine ya kazi? (Umepewa kazi ya “kuilima” na “kuitunza” bustani kamilifu.)

1.  “Uhuru” ni hamasisho la msingi katika kitabu cha Pink. Mungu ametupatia uhuru kiasi gani? (Tumepewa kiasi kikubwa sana cha uhuru!)

C.  Tunakifahamu kisa cha kitabu cha Mwanzo. Wanadamu waliingia kwenye matatizo kutokana na kutozitii sheria. Kwa kiasi gani uhuru wetu una ukomo kutokana na sheria za Mungu? (Soma Kumbukumbu la Torati 4:1-2. Tunaongozwa na sheria za Mungu. Lakini, cha kufurahisha, wanadamu hawawezi kuongezea kitu kiuhalali kwenye sheria za Mungu. Hii ina maana kubwa katika kuhifadhi uhuru na utawala wetu.)

II.  Familia

A.  Soma Waefeso 3:14-16. Inamaanisha nini “kuitwa” kwa jina la Mungu? (Je, unaifahamu familia yenye uwezo mkubwa? Je, kuwa mmojawapo wa wanafamilia hiyo kutakuwa na manufaa kwako? Je, kutakupatia uwezo? Hicho ndicho kinachomaanishwa hapa. Wewe ni sehemu ya familia ya Mungu. Roho wake hukaa ndani yako na kukupatia uwezo.)

1.  Je, hii inaongezea chochote kwenye “uhuru” na “utawala” wako? (Naam. Unaweza kufanya mambo ambayo wengine wanaogopa kuyatenda.)

B.  Soma Kutoka 5:1. Je, watu wenye nguvu kabisa duniani wanaweza kusimama dhidi ya familia yako kwa mafanikio? (Hapana! Musa na Haruni walitumia jina la baba yao “Bwana, Mungu wa Israeli,” dhidi ya mtu mwenye nguvu kubwa kabisa duniani. Tunajua jinsi makabiliano hayo yalivyoendelea.)

C.  Soma Zaburi 50:10-12. Ongezea kwenye nafasi yako kwamba familia yako ni tajiri kulizo familia zote duniani! Hii ina athari gani kwenye uhuru na utawala wako?

1.  Uelewa huu wa kina wa familia yako unaathirije uelewa wako wa kutenda mambo? Kubadili mambo?

2.  Unahamasika kwa kiasi gani kufanya kazi katika shughuli ya familia?

D.  Hadi kufikia hapa unaweza kuwa unashangaa jambo gani limekutokea? Kwa nini wewe ni maskini? Kwa nini una uhitaji? Je, unajisikia kama kondoo mweusi wa familia? Jibu ni lipi kwenye mgongano mkubwa kati ya kile tulichojifunza hivi punde kwenye Biblia na mazingira yanayokukabili? (Kama unauhisi mgongano huu, ngoja nikuulize kama umewahi kuyaangalia maisha yako (familia yako) kwa namna tuliyoijadili hapa? Ikiwa sivyo, hilo linaweza kuwa jibu la mgongano huo.)

III.  Mfano wa Daudi

A.  Soma 1 Mambo ya Nyakati 17:1-2. Unadhani jambo gani limo moyoni mwa Mfalme Daudi kwa kuzingatia Sanduku la Agano? (Mungu anataka kulijengea nyumba.)

B.  Soma 1 Mambo ya Nyakati 17:4 na 1 Mambo ya Nyakati 17:11-13. Hii inatufundisha nini juu ya tamaa ya kufanya makuu katika miradi yetu kwa ajili ya Baba yetu au familia yetu? (Hata pale unapokuwa sehemu ya familia ya Mungu, hata pale unapokuwa Mfalme, bado uko chini ya mapenzi ya Mungu. Daudi alikuwa anawazia jambo kubwa, lakini haikuwa mapenzi ya Mungu kwa Daui kufanya hivyo.)

C.  Soma 1 Mambo ya Nyakati 17:16-18. Huu ni mwanzo tu wa mjibizo wa ombi la Daudi kwa Mungu. Unalizungumziaje? (Daudi ana shukrani. Ni mnyenyekevu katika kupokea uamuzi wa Mungu.)

D.  Soma 1 Mambo ya Nyakati 29:12, 1 Mambo ya Nyakati 29:14, na 1 Mambo ya Nyakati 29:16. Mfalme Daudi ana mtazamo gani juu ya mafanikio na fedha? (Anatambua kwamba yote tuliyonayo yanatoka kwa Mungu. Daudi ana hamu ya kumrejeshea Mungu. Anataka kumtukuza Mungu.)

IV.  Sheria na Upendo

A.  Soma 1 Yohana 5:1. Je, hii inatuambia juu ya kuwapenda wengine? (Kumpenda Mungu maana yake ni kwamba tunawapenda watoto wake.)

B.  Soma 1 Yohana 5:2-3. Njia ya msingi kwamba tunawapenda watoto wa Mungu ni ipi? (Tunazishika amri za Mungu.)

1.  Kwa muda mrefu nimekuwa nikijenga hoja katika masomo yangu ya kujifunza Biblia kwamba Amri za Mungu kimsingi hazilengi kuwa kipimo cha kutuhukumu, bali kama mwongozo wa kuyaboresha maisha yetu. Je, tunapaswa kuzitumia amri za Mungu tunapofanya uamuzi wa kuwapenda wengine? Kuwapenda maskini? Kuwapenda wanafamilia?

a.  Unawezaje kujumuisha kwenye jibu lako kigezo cha Yesu alivyotupenda – alitutendea mambo mengi zaidi ya haki tuliyostahili?

2.  Leo nilisoma mapitio ya kitabu juu ya kinachodaiwa kutokuwepo kwa usawa nchini Marekani. Mapitio hayo yalinukuu kitabu kikisema kuwa wale wasiofanya kazi wana kipato kinachokaribiana na wengi wa wale wanaofanya kazi. Hilo linawezekanaje? Wasiofanya kazi wanapokea fedha na marupurupu kutoka serikalini. Fedha zinachukuliwa na serikali kutoka kwa wale wanaofanya kazi na kuwapa wale wasiofanya kazi. Je, hii inaendana na amri za Mungu? (Haiendani. Mpango wa Mungu kwa ajili ya maskini ni kuwataka wafanye kazi. Angalia, kwa mfano, Mambo ya Walawi 19:9-10. Kwa kuwahamasisha maskini wasifanye kazi, kamwe hawawezi kuboresha hali yao ya kiuchumi.)

C.  Mathayo 25:14-18 inaelezea mfano wa bwana aliyewapa watumwa wake mali kuzitunza wakati aliposafiri. Mtumwa mmoja alipokea talanta tano, mwingine talanta mbili, na wa mwisho talanta moja. Je, ukweli kwamba mtumwa mmoja alipokea mara tano zaidi kuliko mwingine haipaswi kutufundisha jambo?

D.  Soma Mathayo 25:19. Vifungu vinavyofuata vinanukuu kwamba wote walizalisha talanta mara mbili zaidi ya walizozipokea isipokuwa mtumwa aliyepokea talanta moja. Soma Mathayo 25:25-28. Je, “walegevu” pia ni “waovu?” Kwa nini talanta apewe mtumwa tajiri? Kuna fundisho gani linapatikana katika hili?

1.  Je, mfano huu unahusu fedha au wokovu? (Sura yote inahusu hukumu inayokuja, na hivyo ninadhani fundisho linahusu zaidi tofauti iliyopo kati ya wale wanaompokea Yesu kama Bwana na wale wanaomwogopa. Lakini, ninadhani ina mafundisho madogo ya jinsi tunavyopaswa kuwatendea watu walegevu.)

V.  Shambulio la Nondo

A.  Soma Mathayo 6:19-20. Je, hili ni katazo la kutengeneza mfuko wa kustaafu?

1.  Ujumbe gani mahsusi unatolewa hapa? (Utajiri wa hapa duniani hauaminiki. Utajiri wa mbinguni ni wa kuaminika.)

2.  Unaweza kunionesha mahala ninapoweza kufungua akaunti kwenye benki ya mbinguni? Benki hiyo inalipa kiwango gani cha riba? (Maswali haya mepesi yanabainisha kuwa vitu hivi viwili havilingani.)

B.  Soma Mathayo 6:24. Hii inaakisi vipi kwenye maswali mawili ya benki? Tunawekaje fedha mbinguni badala ya hapa duniani? (Suala ni kama unajikita katika kuuendeleza ufalme wa Mungu au kama unajikita katika kuendeleza ustawi wako wa kifedha.)

1.  Angalia sehemu ya ajabu kabisa ya kifungu hiki. Inatuambia kuwa tukizitumikia fedha zetu tutamchukia Mungu. Tukimtumikia Mungu, tutazichukia fedha. Je, unamjua mtu yeyote anayeendana na mojawapo ya ufafanuzi huu?

C.  Soma Mwanzo 29:30-31. Je, Yakobo alimchukia Lea? (Hapana. Kifungu cha 30 kinabainisha kuwa alimpenda kidogo zaidi kuliko Raheli. Hiki ndicho kinachomaanishwa katika Mathayo 6:24. Tunatakiwa tupende fedha kidogo kuliko kumtumikia Mungu. Kwa nini? Kupenda fedha sio uwekezaji wa kiuerevu wa muda mrefu.)

D.  Rafiki, Mungu amekupatia uhuru, utawala, na lengo. Ukivibadilisha hivyo kwenye msukumo wa kutafuta fedha zaidi, utakuwa umechukua uamuzi wa kipumbavu. Sio tu kwamba fedha ni za muda mfupi, bali utakuwa umekosa mambo ya kufurahisha zaidi maishani. Kwa nini usimchague Mungu dhidi ya fedha sasa hivi?

VI.  Juma lijalo: Maagano ya Mungu na Sisi.