Somo la 8: Tumaini la Agano Jipya
Somo la 8: Tumaini la Agano Jipya
(1 Yohana 5, Yohana 3 & 16, Yakobo 1)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Somo la mantiki lilikuwa la muhimu sana darasani. Somo hilo lilinifundisha kuwa hoja za aina fulani ni za uwongo – njia za fikra zilizo na kasoro. Mantiki za uwongo zinaweza kutambuliwa kutokana na mpangilio wa hoja. Juma hili tunaangalia mojawapo ya uwongo mkuu wa kidini: kwamba kutofautisha (discrimination) ni jambo baya. Tunajua kwamba huu ni uwongo kwa sababu mara zote tunatofautisha juu ya mambo ya muhimu na yasiyo ya muhimu. Ulipomchagua mwenzi wako je, ulimtofautisha? Vipi wakati ulipotuma maombi ya kazi? Vipi kuhusu asubuhi ya leo ulipochagua nguo gani ya kuvaa? Kutokana na muktadha wa Biblia jambo kuu ni kutofautisha na kiini cha injili ni kwamba Mungu anatofautisha linapokuja suala la uzima wa milele. Lakini je, Mungu anatofautisha ili kuwatenga wanadamu dhidi ya fursa ya wokovu? Tunawezaje kuwa na uhakika? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili kuuchimbua ukweli!
I. Njia Moja Pekee
A. Soma 1 Yohana 5:9. Chanzo cha muhimu kabisa cha ukweli ni kipi? (Ushuhuda wa Mungu. Ni “mkuu” kuliko mawazo ya wanadamu.)
B. Soma 1 Yohana 5:10. Je, ushuhuda wa Mungu unaweza kutolewa na wanadamu? (Ndiyo! Hili sio suala la Mungu dhidi ya wanadamu, hili ni suala la “je, unaliamini neno la Mungu.”)
1. Hapa tunazungumzia ushuhuda gani wa Mungu? (Kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.)
C. Soma 1 Yohana 5:11-12. Mungu anatuambia nini kumhusu Mwana na uzima wa milele? (Kwamba tunaupokea uzima wa milele katika Yesu. Kama hatuna Yesu, hatuna uzima wa milele.)
1. Je, suala hili ni jozi? Yaani, tuna machaguo mawili pekee? (Ndiyo, ni jozi. Kama tunaye Yesu tunao uzima, kama hatunaye Yesu, hatunao uzima.)
D. Soma 1 Yohana 5:13. Tunampokeaje Yesu? (Tunao uzima wa milele kwa kuamini “katika jina la Mwana wa Mungu.”)
E. Soma Mwanzo 3:2-4. Uongo huu wa kwamba Yesu sio wa muhimu kwenye uzima wa milele una umri gani? (Huu ndio udanganyifu wa kwanza.)
F. Soma Yohana 6:40. Kama wewe ni mtu unayedhani kuwa hakupaswi kuwepo kwa utofauti, yumkini hujali kama watu wanatofautisha kwenye suala la rangi ya viatu wanavyovivaa. Kwa nini? Kwa sababu sio jambo la muhimu. Uzima wa milele ni suala la muhimu kiasi gani? (Masuala mengine sio ya muhimu kuliko uzima wa milele.)
1. Maneno ya “kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye” yanamaanisha nini? (Yanamaanisha kumtafakari Yesu na kufanya uamuzi kwamba yeye ni Mungu anayetuokoa. Huu unaonekana kama mchakato wenye hatua mbili.)
G. Soma Yakobo 1:22-24. Yakobo anauelezeaje mchakato huu wenye hatua mbili? Na je, ni kweli kwamba una hatua mbili? (Kama kweli “umeangalia” na kuamini huthibitishwa na kama umetenda jambo fulani kama matokeo ya huko kuangalia. Kimsingi sio hatua mbili. Ni uthibitisho wa imani.)
H. Soma Yakobo 1:25. Je, una tatizo la usahaulifu? Tunaliepukaje tatizo hilo? (Sote tunafahamu kwamba kwa kuendeleza “kumbukumbu ya msuli” (kwa kurudiarudia) tunaweza kujikinga dhidi ya usahaulifu. Kuifanyia kazi imani yetu huonesha kwamba kweli tunaiamini.)
I. Soma Yohana 14:6. Tomaso alipotaka kujifunza juu ya maelekezo ya kwenda mbinguni, Yesu alimjibuje? (Yesu ndiye njia pekee ya kwenda mbinguni. Yeye ndiye “njia, kweli, na uzima.”)
J. Soma Matendo 4:12. Kifungu hiki kinazungumzia nini juu ya njia ya wokovu? (Kuna jina moja pekee linalotuokoa.)
1. Hadi kufikia hapa tumejifunza nini kuhusu uzima wa milele na utofautishaji? (Kuna njia moja tu ya kuufikia uzima wa milele. Njia hiyo ni kumwamini Yesu. Hiyo ndio tofauti inayohusu suala la muhimu kabisa maishani!)
II. Kutofautisha na Tumaini
A. Watu wengi wanaamini kwamba kama ukiishi maisha mema basi unapaswa kwenda mbinguni. Kuwatofautisha watu wema ni ubaguzi mbaya sana! Soma Yohana 3:16-18. Hali yetu ya asili linapokuja suala la kifo ni ipi? (Tulihukumiwa tangu mwanzo kabisa wa uhai wetu. Eva alipouamini uongo wa Shetani kuhusu Mungu na uzima wa milele, Adamu na Eva walipomkataa Mungu, sote tulihukumiwa mauti ya milele.)
1. Unaposoma Yohana 3:17-18, je, unaweza kujenga hoja ya kwamba Mungu habagui? (Ndiyo. Sote kwa usawa tulitumbukizwa kwenye mauti ya milele. Sote tunayo fursa ya kumchagua Yesu. Kwa sababu gani? Kwa sababu alikuja kuokoa na sio kuhukumu. Sote tunayo fursa sawa ya kuokolewa. Sote tunalo tumaini.)
B. Soma Warumi 3:20. Hii inazungumzia nini juu ya kuwaokoa watu wazuri wasiompokea Yesu? (Kuishika sheria ya Mungu na kuwa mtu mwema ni jambo zuri! Lakini, hiyo haikufanyi uepuke adhabu ya mauti ya milele.)
1. Kauli ya kwamba sheria hutufundisha juu ya dhambi inaongezea jambo gani kwenye haki ya kuwaruhusu watu wema kufa milele? (Maana yake ni kwamba kama kweli una nia ya kuishi maisha mema, sheria itakufunulia jinsi ulivyo mtu mbaya na hiyo itakusukuma kwenye safari ya kumtafuta Yesu.)
2. Hebu tuangalie jinsi jambo hili linavyohusika maishani mwetu kama Wakristo. Tunapaswa kutenganisha kati ya wema na ubaya. Tunapaswa kuikataa teolojia ya kisasa ya kutotofautisha. Lakini, kitu gani kinachotokea pale mdhambi anapoingia kanisani na kukaa miongoni mwa wadhambi wengine? Tunapaswa kusema nini kuhusu dhambi? (Tunapaswa kuhakikisha kuwa tunaitenga dhambi. Kanuni za “sheria” zinapaswa kubainishwa wazi.)
a. Jambo gani linafuatia? (Fursa ya kumchagua Yesu kwa uhuru – fursa inayotolewa bila ubaguzi – pia inapaswa kuwekwa bayana.)
b. Ukiinyamazia dhambi, matokeo ya asili ni yapi? (Ni kwa njia ya uelewa wa sheria pekee ndipo tunapotambua hitaji letu la Yesu. Kushindwa kuitenganisha dhambi kwa uwazi huwanyima wengine msaada wa muhimu wa wokovu.)
C. Soma Yohana 16:7-10. Taarifa za kina ni za muhimu. Tunapoitambua dhambi kwa uwazi, je, hiyo inamaanisha tunapaswa kuwashutumu watu wengine kanisani juu ya dhambi zao binafsi?
1. Nani anayehakikishwa dhambi? (Ulimwengu. Hii haiashirii kwamba unapaswa kuwazonga washiriki wenzako juu ya dhambi zao.)
2. Ni nini asili ya dhambi inayojadiliwa? (Ulimwengu haumwamini Yesu, hauamini kwamba yeye ni Masihi. Hii haihusiani na jinsi tunavyoenenda, hii inahusu swali la msingi kabisa maishani – Yesu ni nani?
3. Inamaanisha nini kuhakikishwa “kwa habari ya haki?” je, ni haki yetu? (Utaona kwamba kifunghu cha 10 kinatoa muktadha – Yesu anakwenda kwa Baba ambapo hatutamwona tena. Watu wasio wa haki pekee ndio watakaosulubishwa. Yesu anasema kuwa Roho Mtakatifu atalithibitisha jina lake na kumwonesha Yesu kuwa Mwenye Haki.)
4. “Hukumu” gani inarejelewa hapa? (Soma Yohana 12:31. Shetani alikuwa “mkuu” wa ulimwengu hadi Yesu alipomtupa nje (alipomhukumu) pale msalabani.)
5. Unapoyatafakari matendo haya ya Roho Mtakatifu, je, hii inazungumzia chochote kuhusu utofautishaji? (Ndiyo. Tunampokea Yesu na kumkataa Shetani. Yesu alishinda, Shetani alishindwa.)
a. Kama unaliamini hili, je, hii inaleta tofauti kwa namna unavyoishi?
III. Uthibitisho wa Ushindi
A. Soma Yohana 6:56-57. Je, Yesu anatutaka tuwe wala nyama? (Soma Yohana 6:58. Ukiangalia sura hii utaona kwamba Yesu ametenda muujiza na kuwalisha maelfu ya watu kwa mkate na samaki. Yesu anauelezea muujiza kwa kusema kuwa yeye ni mkate wa kiroho, alishuka kutoka mbinguni na kuwapa watu mkate wa uzima wa milele.)
B. Soma Yohana 6:60-62. Wasikilizaji wa Yesu walipata ugumu kwenye suala la “kumla” Yesu kama mkate. Hawakuwa wala nyama! Kwa nini Yesu anadokeza juu ya kumwona akipaa kwenda mbinguni? (Yesu anajenga hoja kwamba ufufuo wake ndio uthibitisho wa mwisho wa kile anachokisema.)
C. Soma Yohana 6:63-65. Ni kwa jinsi gani Yesu kupaa mbinguni ni uthibitisho juu ya kumla yeye? (Yesu anafafanua kwamba anazungumzia masuala ya kiroho. Yesu ni Masihi aliyekuja, akaishi, akafa, na atafufuka ili kuwawezesha kuwa na uzima wa milele.)
D. Soma Yohana 6:66-69. Petro aliamini nini, na hilo linahusianaje na Yesu kuwa mkate? (Yesu ndiye ufunguo wa uzima wa milele. Ufufuo wa Yesu unathibitisha kwamba tunaweza kufufuliwa.)
E. Rafiki, je, utaikubali ofa ya Yesu ya uzima wa milele? Je, utatofautisha mambo ili kumpendelea Yesu na kuwa kinyume na Shetani?
IV. Juma lijalo: Vifungu Vinavyokinzana?