Kujivunia Msalaba

(Wagalatia 6:11-18)
Swahili
Year: 
2011
Quarter: 
4
Lesson Number: 
14

Utangulizi: Kama sote tunaye Yesu mmoja, ni kwa nini basi kuna haya makanisa mengi tofauti tofauti? Katika 1 Wakorintho 3 Paulo analalamika kuhusu mgawanyiko miongoni mwa waamini. Hivi leo inaonekana kuwa kila kanisa lina upekee muhimu kwake. Kwa mfano, Wabaptisti wana ubatizo kwa njia ya kuzamishwa majini. Ingawaje mimi sio Mbaptisti, nadhani hilo ni fundisho la muhimu sana. Je, ni kwa namna gani wale tulio na mafundisho ya kipekee tunapaswa kukabiliana na dunia? Je, Wabaptisti wanapaswa kuongoza kwa ubatizo kwa njia ya kuzamiswa majini? Je, kila dhehebu linapaswa kuongoza kwa imani yake ya kipekee (na ya kweli)? Katika hitimisho la ujumbe wa Paulo kwa Wagalatia, anatoa ushauri kwenye suala hili. Hebu tuzame kwenye somo letu la mwisho la Wagalatia na tuone kile tunachoweza kukigundua!

  1. Uhalisia
    1. Soma Wagalatia 6:11 na 1 Wakorintho 16:21. Je, hii inapendekeza nini kwako? (Kwamba kwa kawaida alimtumia mwandishi katika kuandika barua zake. Hata hivyo, binafsi angeweza kuandika sehemu ya barua yake ili kuthibitisha kuwa alikuwa mwandishi.)
    2. Soma Wagalatia 4:15. Je, hii inapendekeza kuwa nini inaweza kuwa sababu ya uandishi wa maandishi makubwa wa Paulo kwa kutumia mkono? (Maoni mbalimbali yanapendekeza kuwa hii inathibitisha kwamba Paulo alikuwa na matatizo ya macho (kwamba alikuwa na uhafifu wa kuona vizuri).)
      1. Je, ni kitu gani kingine kinachopendekezwa na maandishi makubwa? (Ilikuwa tu ni njia aliyokuwa akiitumia kuandika. Ninapokuwa ninatia saini mbele ya jina langu, saini yangu huwa ni kubwa. Ninapokuwa ninaandika, kwa ujumla huwa ninaandika maandishi makubwa ingawaje sina matatizo ya macho. Ama kwa hakika, katika uandishi, hali yangu ya macho ni bora zaidi kuliko watu wengine wenye umri kama wangu.)
      2. Je, karatasi zenye ubora wa hali ya juu zilikuwepo kwa wingi? (Hatujui kile alichokuwa akikitumia kuandikia. Lakini, bila shaka kilikuwa ni cha gharama kubwa na kilipatikana kwa hali ya uchache. Huenda mwandishi kitaaluma aliandika maandishi madogo ili aweze kuwa na matumizi mazuri ya zana za kuandikia zilizokuwa na gharama kubwa.)
      3. Kwa nini tunajihusisha (tunajali) sana na suala hili? Je, kuna umuhimu gani kwetu sisi kutokana na maoni ya Paulo kuhusiana na uandishi wake wa kutumia mkono? (Suala la kwanza tulilolijadili ndilo suala la msingi – kitabu cha Wagalatia kiliandikwa na Paulo. Tunaweza kuwa na uhakika na hilo.)
      4. Hamasa ya Matendo/Wapinzani wa Sheria
    3. Soma Wagalatia 6:12. Kama niliuza nguo kwa ajili ya kuendeleza maisha yangu, nadhani mara zote nitakuwa nikiangalia thamani za nguo za mtu ambaye nilikuwa nikizungumza naye. Kwa sababu mimi ni mwanasheria, vitu vingine vinanijia mawazoni, vinakuja vyenyewe tu pasipo kuamriwa: “Je, mtazamo wa mtu huyu katika kulisema hili ni upi?” “Je, mtu huyu anasema ukweli?” Kama mtu hana mtazamo wa kudanganya, kuna uwezekano mkubwa sana kuwa anasema ukweli. Hapa Paulo anafanya hoja ya kisheria kuhusu wapinzani wake. Kwa nini anahoji kuwa wapinzani wa matendo wanadanganya? (Ni watu wa kuwafurahisha watu tu. Hii ni sehemu tu ya juhudi zao kuepusha kujiingiza kwenye matatizo kwa sababu wao ni Wakristo.)
      1. Nadhani ni busara kuendana na watu wanaotuzunguka. Kwangu mimi hiyo haionekani kuwa hoja kubwa. Je, kwa undani zaidi ni hoja gani unayoweza kuiona kwenye maneno ya Paulo? (Maoni kuhusu “msalaba” yanapendekeza kwamba wangeikana injili ili waweze kuwafurahisha/kuwapendeza wale wanaowazunguka. Tohara ni sehemu tu ya taswira kubwa ya kuikana injili.)
        1. Je, unadhani kuwa hawa watu wanaowafurahisha watu watakubali “hatia” ya hili shtaka? Au, je, inawezekana kwamba hawakulifikiria hili kwa kina?
      2. Juma hili nilikuwa ninasikiliza hubiri la mtu ambaye ni mwanafunzi wa dhati kabisa (makini) wa Biblia. Alikuwa anazungumza kuhusu unabii na jinsi ambavyo washiriki wa dini nyingine kubwa wataijia imani ya Yesu, hata kama wanaweza wasiwe na uelewa sahihi wa Utatu Mtakatifu. Hakujali sana kuhusiana na tatizo hili kwa sababu alisema, “Hakuna mtu hata mmoja aliye mkamilifu kwenye fundisho, lakini fundisho hili ni muhimu kiasi gani? (Kama huamini kuwa Yesu ni Mungu, huelewi sehemu ya msingi kabisa ya injili!)
    4. Soma Wagalatia 6:13. Miaka nenda miaka rudi tunasoma kuhusu mashujaa wanaopokea vikombe kutoka kwa waathirika wao: ngozi za vichwa na nywele zake, masikio, nk. Je, Paulo anapendekeza kuwa kundi la waliotahiriwa linakusanya kitu gani? (Magovi!)
      1. Je, kwa nini Paulo anakuwa mtu wa ishara sana? (Lazima atakuwa alikuwa anataka kuweka taswira nzuri kwa Wagalatia kwamba wapinzani wake kwa hakika kabisa hawakuwa wakiwajali.)
  2. Mitazamo Sahihi
    1. Soma Wagalatia 6:14. Je, Paulo anatofautianaje na watu wanaowafurahisha watu? (Wanaepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba, anajivunia msalaba.)
      1. Hebu tuliangalie hili kwa undani zaidi. Kwa nini wafurahisha watu wanajivunia kuhusu tohara na sio msalaba? (Wanajivunia vitu vitakavyowafanya waonekane wema mbele za macho ya watu wengine.)
      2. Je, kanisa lako limetangaza? Washiriki wa kanisa la Mormon walikuwa na matangazo mazuri sana ya televisheni yanayohusu familia (kaya). Nimeona matangazo kama hayo ama kwa Walutheri au kwa Wamethodisti. Kanisa langu linajivunia kuhusu masuala ya afya na kuishi kwa muda mrefu kwa washiriki wake. Je, matangazo haya yanatangazwa ili kulifanya kanisa likubalike kwa jamii na kuepusha kuteswa?
        1. Kanisa linapotangaza aina hii ya matangazo (nina uhakika makanisa mengi yanatangaza matangazo kama haya), je, tunajivunia kitu kingine kabisa tofauti na msalaba?
        2. Je, Paulo anafanya ukosoaji wenye haki? Kwa mfano, je, Biblia inazungumzia kuhusu msalaba tu?
        3. Kama nikikuuliza kuhusu shirika linaloitwa “Samaritan’s Purse,” je, utalielezeaje? (Makasha ya Krismasi kwa ajili ya watoto. Msaada wa majanga. Juma lililopita Franklin Graham, mkuu wa “Samaritan’s Purse,” alitembelea chuo kikuu ninachofundisha. Alisema kila walichokifanya kilikuwa ni kwa ajili ya kuiendeleza injili. Kujivunia kuhusu familia (kaya), afya, nk ni vema kama lengo lake ni kuiendeleza injili. Tatizo linakuja pale ambapo kujivuna kwetu kunaikana injili.)
        4. Kabla hatujajisikia hatia kidogo, je, Paulo anamaanisha nini anaposema kuwa amesulibishwa kwa ulimwengu? (Hajali kile ambacho ulimwengu unakifikiria.)
          1. Je, tunapaswa kujali kile ambacho ulimwengu unakifikiria kuhusiana na kanisa letu?
    2. Soma Wagalatia 6:15. Je, itakuwa vyema kusema kuwa “afya na urefu wa maisha” havina maana yoyote, kinachojalisha ni kuwa kiumbe kipya katika Kristo? (Afya na urefu wa maisha vina umuhimu wa kivitendo zaidi kuliko tohara, lakini kipindi kifupi cha maisha yetu hapa duniani hakina maana yoyote ikilinganishwa na umilele.)
      1. Pale ambapo wafurahisha watu walipokuwa wakihoji wakiegemea upande wa tohara, je, walikuwa wakifanya hivyo kwa lengo la kuboresha maisha ya kila siku? (Hapana. Walikuwa wanahoji suala hilo kwa sababu za kiteolojia. Katika kitabu cha Mwanzo 17 Mungu alimwambia Ibrahimu kuwa tohara ilikuwa ni ishara kwamba palikuwepo na uhusiano kati ya Mungu na uzao wa Ibrahimu. Hiyo inaonekana kuwa na umuhimu mkubwa sana kwangu!)
      2. Je, kuna kitu ambacho kanisa lako linahoji kuwa ni ishara maalum ya uhusiano kati yako na Mungu na ni cha muhimu sana kuliko msalaba?
    3. Hebu turejee kwenye utangulizi wetu. Je, ubatizo kwa njia ya kuzamishwa majini ni muhimu sana kuliko msalaba? (Hapana.)
      1. Je, tohara na ubatizo wa kuzamishwa majini vipo kwenye dhana moja? Je, Paulo hakuwa akihoji kwamba tohara ni kosa, wakati ambapo tunafahamu kuwa ubatizo ni kitu sahihi? (Tohara ni mbaya (makosa) tu kwa sababu ni sehemu ya njia ya matendo ya “tii na uishi,” badala ya njia ya neema ya “amini na uishi.”)
    4. Hebu tuchunguze tena sehemu ya mwisho ya Wagalatia 6:15. Je, Paulo anamaanisha nini anaposema, “Kinachojalisha ni uumbwaji upya (yaani bali kimbe kipya)? (Soma 2 Wakorintho 5:17. Kinachojalisha ni kuwa kwa imani katika Yesu, tunaokolewa – tunakuwa kiumbe kipya.)
    5. Hebu tusome 1 Wakorintho 7:19. Je, hii inafuta (inabatilisha) kila kitu tulichokijadili hivi punde? (Hapana! Tohara ilikuwa ni ishara ya uhusiano maalum na Mungu. Uhalisia wa uhusiano maalum na Mungu ni utii kwa amri zake. Tohara ilikuwa ni ishara. Utii ndio uhalisia.)
    6. Je, kuna mtu anayeweza kuelezea kwa ufupi kile tulichojifunza? Au je, nimewachanganya ninyi nyote? Je, Wabaptisti wanapaswa kuongoza kwa ubatizo wa kuzamishwa majini? Je, kila kanisa linapaswa kuongoza kwa fundisho lake la kipekee? (Hapana. Tunapaswa kuongoza kwa msalaba – injili ya kuhesabiwa haki kwa neema pekee. Wakati huo huo, Wabaptisti (na wengine wote tuliosalia) tunapaswa kuendelea kutii amri za Mungu – huku tukitambua kuwa hatuokolewi kwa kuzitunza/kuzishika amri.)
    7. Soma Wagalatia 6:16. Tukiuelewa vizuri uhusiano kati ya neema na matendo, je, nini kinachofuatia? (Amani na rehema!)
      1. Je, mambo hayo mawili yanahusiana? (Rehema ya Mungu inanipatia amani. Inanipatia ujasiri kwenye wokovu wangu.)
    8. Soma Wagalatia 6:17. Kwa nini tunaweza kuwa na uhakika na mafundisho ya Paulo? (Ameyasumbukia/ameyatesekea. Kwa wazi kabisa anayaamini.)
    9. Soma Wagalatia 6:18. Tunamalizia kwa suala zuri ajabu linalozungumziwa kwenye Wagalatia – neema! Tunaokolewa kwa neema pekee.
    10. Rafiki, kama haujaukubali wokovu kwa njia ya neema pekee hapo kabla, je, utaukubali sasa hivi? Je, utairuhusu rehema na amani viyaingie maisha yako?
  3. Juma lijalo: Juma lijalo tutajifunza Utatu Mtakatifu tunapoanza mfululizo mpya wa masomo unaoitwa “Mwonekano wa Mungu Wetu.”