Somo la 2: Chimbuko na Asili ya Biblia

(Kumbukumbu la Torati 18, 2 Petro 1, Waebrania 11, Yohana 17)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
2
Lesson Number: 
2

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Jinsi tunavyojifunza Biblia ni muhimu kwa ajili ya uelewa sahihi wa Biblia. Chukulia mfano wa somo letu lililopita la Danieli. Katika Danieli 2 tulimwona akitafsiri njozi inayofunua kwa muhtasari historia yote – ikiwemo mwisho wa dunia! Wanamaoni wengi wa hivi karibuni wanadai kwamba Danieli hakuandika juu ya jambo hili katika kipindi cha utawala wa Babeli, bali katika kipindi cha utawala wa Rumi. Ingawa mimi si mtaalamu katika sababu walizozitoa, wanakiri kwamba Danieli anaelezea kwa usahihi historia hadi kufikia katika kipindi cha Antiokia IV Epifanesi, na hivyo wanajenga hoja kwamba lazima tayari kitabu kilishaandikwa. Hii inafanya uwepo wa dhana mbili. Maelezo ya Danieli ni ya kubuni, na Mungu hakufunua (au asingeweza kufunua) mustakabali wa siku zijazo. Hii imejengwa juu ya kutoiamini Biblia na kutouamini uwezo wa Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu juu ya namna nyingine ya kuiendea Biblia!

 

  1.     Chimbuko la Kimbingu

 

    1.     Soma Kumbukumbu la Torati 18:18. Wenye kushuku wanapodai kwamba lazima kitabu cha Danieli kiliandikwa baadaye, wanakabiliana na tatizo gani kwenye kifungu hiki? (Kifungu hiki kinasema kuwa nabii anazungumza maneno ya Mungu. Wale wanaoitilia shaka Biblia wanatilia shaka alichokisema Mungu.)

 

    1.     Soma 2 Timotheo 3:16. Wanamaoni wasioamini kauli ya Danieli kuhusu muda ilipoandikwa wanajihusishaje kwenye mabadiliko ya mambo? (Hii inasema kuwa Biblia “inaonya.” Wanamaoni hawa wanadhani wanaweza kuisahihisha Biblia.)

 

    1.     Soma 2 Petro 1:21. Dhana ya wanamaoni wa hivi karibuni juu ya Danieli ni kwamba upungufu wa wanadamu unapaswa kuwafahamisha uelewa wao juu ya muda kilipoandikwa. Kifungu hiki kinatuambia nini kuhusu upungufu wa wanadamu walioandika Biblia? (Kinasema kwamba mapenzi ya wanadamu hayahusiani nayo kivyovyote vile. Upungufu wa wanadamu hauna maana.)

 

  1.   Andiko

 

    1.     Nimekuwa nikifundisha darasa la Biblia la Shule ya Sabato tangu nilipokuwa mwanafunzi katika shule ya sheria. Wale waliokuja kanisani walinufaika kwa wasilisho na fundisho langu – na kisha lilipotea – likisalia tu akilini. Takriban miaka 24 iliyopita tulianza kupakia masomo kwenye tovuti – ambapo ninatarajia yataendelea kusalia hata baada ya kufariki kwangu. Tazama tofauti iliyopo katika kuandika na kuchapisha masomo kwa ajili ya matumizi ya umma!

 

    1.     Soma Kutoka 17:14. Mungu anatumia njia gani kufanya maneno yake yakumbukwe? (Kuyaandika. Hii ni muhimu sana kuliko kumbukumbu ya mtu.)

 

    1.     Soma Kutoka 24:12. Mungu alikuwa anawaza nini kwa kuzingatia kumbukumbu ya Amri Kumi? (Aliziandika kwenye jiwe!)

 

    1.     Soma Joshua 24:26-27. Kwa mara nyingine, tunaona kumbukumbu iliyoandikwa, mara hii ni kuhusu ahadi ya watu kumfuata Bwana. Ninataka kulijadili jiwe. Kwani hawakutumia mawe kutengeneza sanamu? Lengo la jiwe hili ni lipi?

 

      1.     Kwa nini Yoshua anahusianisha uwezo wa mwanadamu na jiwe hili? (Mawe yanadumu. Kuiandika ahadi, na kulichagua jiwe kama “shahidi” kunaimarisha dhana ya kwamba utiifu wetu kwa Mungu lazima uwe wa kudumu. Jiwe lenyewe halikuwa shahidi, lakini uwepo wake uliwashuhudia (uliwakumbushia) wanadamu juu ya ahadi yao kwa Mungu.)

 

  1. Imani

 

    1.     Soma Waebrania 11:1-2. Hii inatuambia kuwa wazee wa “kale” walikuwa na imani. Unapochukulia kwamba waliishi kati ya umri wa miaka 800 na takriban miaka elfu moja (Mwanzo 5), imani yao ilijengwa juu ya kile ambacho kingeweza kuwa taarifa za mashuhuda. Je, hiyo ni imani tofauti na ile tunayotakiwa kuwa nayo leo?

 

    1.     Soma Waebrania 11:3-4. Je, hapa tunazungumzia ushuhuda wa watu walioshuhudia? (Hapana. Hivi vifungu viwili vinazungumzia kuamini kile alichokisema Mungu.)

 

      1.     Hebu tuchunguze kwa kina Waebrania 11:3. Hii inatuambia nini kuhusu chimbuko la ulimwengu? (Ulitokana kwa kutamkwa (“Mungu anaamuru”).)

 

      1.     Tunapoambiwa kwamba kile tunachokiona hakikutengenezwa kutokana na kitu kinachoonekana, hiyo inasema nini kuhusu nadharia ya uibukaji inayohusu mianzo? (Uibukaji unafundisha kwamba tunatokana na kitu tunachofanana nacho. Tulibadilika kutokana na mabadiliko na mambo ya asili.)

 

      1.     Kama hatuamini kile tunachokisoma kwenye Biblia, kwa mfano katika Mwanzo 1, hiyo inazungumzia nini kuhusu imani yetu kwa Mungu? (Inasema kwamba hatuna imani kwa kile ambacho Mungu amekifunua kwenye Biblia.)

 

      1.     Je, inawezekana kuwa Mkristo na usiamini kwenye “amri” ya siku sita halisi za uumbaji? (Tunatakiwa kuwa makini kutofautisha kati ya Wakristo wasioiamini Biblia na wale walio na tafsiri tofauti wa kile Biblia inachokisema. Kwa mfano, wale Wakristo wanaojenga hoja juu ya uumbaji wa “siku ndefu” wanaigeukia Mwanzo 2:4. Ukisoma kifungu hicho kwenye tafsiri ya KJV au ESV, kinasema kuwa “siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi.” Matumizi ya neno “siku” (kwa Kiebrania, “yom”) hayaashirii kipindi cha saa 24. Sitaki kuingia ndani katika jambo hili, ninachomaanisha tu ni kwamba tunatakiwa kutofautisha kati ya wale Wakristo wanaoyakataa maneno ya Mungu na wale wanaohoji tafsiri tofauti ya maneno ya Mungu.)

 

    1.     Soma Waebrania 11:6. Vipengele viwili vya msingi vya imani ni vipi? (Kwamba Mungu yupo na kwamba anachangamana nasi ili kuwapa thawabu wale “wamtafutao.”)

 

      1.     Je, “wamtafutao” inatutaka tufanye nini tunaposoma Biblia? (Tunatakiwa kujifunza Biblia. Tunatakiwa kumkaribisha Roho Mtakatifu kuyaongoza mawazo yetu.)

 

  1.   Kuitafakari Biblia

 

    1.     Soma Yohana 17:17. Inamaanisha nini kwa sisi “kutakaswa” kwa maneno ya Mungu?

 

    1.     Soma Yohana 17:19. Yesu anasema kwamba anajiweka wakfu mwenyewe. Anaweza kuwa anamaanisha nini kwa kusema hivyo? Yeye ni mkamilifu. (Yesu alizichukua dhambi zetu na kufa kwa ajili yetu msalabani. Nadhani kuielewa kweli juu ya Yesu ni nani na kile alichotutendea hututakasa.)

 

    1.     Soma Yohana 17:15. Tukiweka kivitendo kile ambacho Mungu anatufundisha kwenye Biblia, basi tutakingwa dhidi ya uovu mwingi. Sidai kwamba Wakristo hawatateseka. Ninachokisema ni kwamba hatutateseka kutokana na matatizo ya kujitakia ikiwa tutatii maelekezo ya Mungu maishani mwetu.)

 

    1.     Soma Yohana 8:32. Kweli ya Biblia inatuweka huru dhidi ya nini? (Dhidi ya mauti ya milele. Dhidi ya maisha yasiyo na Mungu. Fikiria kuishi bila mwongozo wa neno la Mungu na kutiwa moyo na mwongozo wa Roho Mtakatifu.)

 

    1.     Soma Yohana 8:34. Yesu anajibuje swali kuhusu uhuru? (Anasema kwamba sisi ni watumwa wa dhambi. Tunahitaji uhuru dhidi ya dhambi.)

 

    1.     Soma Yohana 8:35-36. Yesu anaelezea nini juu ya kipengele kingine cha uhuru wetu? (Tunakuwa wana na binti wa Mungu. Tunaungana na familia ya Mungu.)

 

    1.     Rafiki, je, utasoma na kujifunza Biblia kwa macho ya imani? Kwa kufanya hivyo unaingia kwenye ulimwengu mpya wa uhuru. Kwa nini usichukue uamuzi huo sasa hivi?

 

  1.     Juma Lijalo: Mtazamo wa Yesu na Mitume Kwa Biblia.