Yesu Akichangamana na Watu
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Yesu na Mafarisayo walikuwa na njia tofauti za kuwaongoa wadhambi. Yesu alikula na wadhambi. Mafarisayo walidhani kuwa wadhambi wanapaswa kutamani kuwa kama wao. Tunafahamu kwamba kuwaongoa wadhambi ni jambo la muhimu kwa sababu uongofu huleta furaha mbinguni tunapaswa kuhusianaje na wadhambi bila ya kuwaruhusu wao kutuongoa (kutubadilisha) na kuwa kama wao? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza kwenye hizi mada za muhimu!
1) Mungu Pamoja na Wadhambi
a) Soma Luka 15:1-2. Kuna tatizo gani hapa? Kwa nini Mafarisayo “wananung’unika” juu ya Yesu kuwakaribisha wadhambi na kula pamoja nao?
i) Unaufahamu msemo “Mtu anajulikana kutokana na aina ya watu anaohusiana nao?” Je, hilo ndilo tatizo lililopo hapa? (Nadhani. Huenda Mafarisayo walidhani Yesu alikuwa anawahamasisha wadhambi kuendelea kuwa wadhambi.)
ii) Soma Luka 7:36. Tunaona taswira gani pana kutokana na washirika wa Yesu chakulani? (Yesu alikula na kila mtu. Haangalii wala kujaribu tabia za watu.)
iii) Nilipokuwa mdogo, nilifundishwa (au angalao nilielewa) kwamba endapo ningetenda dhambi, Mungu angeniacha. Mafungu haya yanaashiria nini kuhusu wazo hilo? (Mungu hawakimbii wadhambi.)
b) Soma Luka 15:3-6. Hii inatufundisha nini kuhusu uhusiano wa Mungu na wadhambi? (Sio tu kwamba anawakimbilia, bali pia anawabeba na kuwapeleka nyumbani!)
i) Katika kisa hiki, ni nani aliyekuwa na uhusiano wa karibu na Yesu, kondoo aliyeokolewa au kondoo aliyepotea? (Yesu alitumia muda mwingi kumtafuta kondoo aliyepotea. Aliyaweka mawazo yake yote kwa kondoo aliyepotea. Hata hivyo, lengo lilikuwa ni kumfanya kondoo aliyepotea afanane na mmojawapo wa kondoo wenye haki.)
ii) Hebu turejee mjadala tuliokuwa nao juma lililopita kuhusu uinjilisti. Utakumbuka kwamba katika Mathayo 10:14-15 Yesu anawaambia wanafunzi wake kuwa ikiwa mtu hatausikiliza ujumbe wa injili, “kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu” kisha msonge mbele. Hakuna kuwafukuzia wala kuwang’ang’aniza wale wanaoukataa ukweli. Unayalinganishaje maelekezo yale na kitendo cha Yesu kumfukuzia kondoo aliyepotea? (Sidhani kama mfano wa Yesu juu ya kondoo unahusu uinjilisti. Nadhani unahusu kuudhihirisha mtazamo wa Mungu dhidi ya wadhambi.)
c) Soma Luka 15:7. Tunapaswa kuwa na mtazamo gani dhidi ya wadhambi wanaotubu? (Tunapaswa kuwa na furaha kuu.)
d) Turejee kwenye suala la uinjilisti, soma tena Luka 15:1. Je, Yesu anawafukuza wadhambi? (Hapana, wao ndio wanaomfukuza. Tatizo la Mafarisayo ni juu ya kitakachofuata mara wadhambi watakaposhikamana na Yesu.)
e) Soma Luka 15:8-10. Mwanamke huyu amejikita kufanya nini? (Kutafuta shilingi yake iliyopotea.)
i) Kama unavyofahamu kutokana na masomo ya hivi karibuni yaliyopita, ninashadadia mtazamo wa kuboresha zaidi huduma ya ibada kwa kuifanya kuwa ya pekee. Mfano huu unaashiria kuwa mtazamo wa kanisa unapaswa kuwa upi? (Mfano huu pamoja na ule wa kondoo aliyepotea unajikita katika kutafuta kilichopotea.)
ii) Tulihitimisha (au angalao nilihitimisha) kwamba kisa cha kondoo aliyepotea hakikuhusu uinjilisti, bali kilihusu mtazamo wa Mungu dhidi ya wadhambi. Je, unadhani dhana hiyo pia ni ya kweli katika kisa cha shilingi iliyopotea?
iii) Hata kama kilichopo katika hivi visa viwili ni kuonesha mtazamo wa Mungu dhidi ya wadhambi, je, visa hivi havisemi jambo lolote kuhusu uinjilisti?
2) Kuviacha Vyote
a) Kama unavyofahamu, ninaamini kuwa muktadha katika Biblia ni jambo la muhimu sana. Hebu tuchunguze mafundisho ya Yesu yaliyotangulia mara baada ya mjadala wake kuhusu mtazamo wa Mungu dhidi ya wadhambi. Soma Luka 14:28-30. Kuna fundisho gani kutoka kwenye hiki kisa?
b) Soma Luka 14:31-32. Kuna fundisho gani kwenye hiki kisa? (Visa vyote viwili vinatufundisha kuwa na mipango mizuri. Hatupaswi kuanza mradi isipokuwa tu kama tumeshaangalia namna bora ya kuutekeleza na pia kama tuna rasilimali za kuumalizia.)
c) Soma Luka 14:33. Jambo hili linaleta mshtuko kidogo? Je, hitimisho hili kimsingi sio tu kinyume cha hivi visa viwili? Mnara na vita vinamhitaji mjenzi na mfalme kuwa na rasilimali za kutosha ili kumaliza kazi. Sasa Yesu anasema unapaswa kuwa tayari kutokuwa na rasilimali! Au je, hamaanishi hivyo?
i) Sura inayofuata inaanza na mafundisho juu ya mtazamo wetu dhidi ya wadhambi. Kwa nini? (Ikiwa tumetingwa na kuwa “juu” ya wadhambi ili tuweze kuwaepuka, basi hatuachani na majivuno yetu.)
d) Hebu turejee nyuma zaidi ili tuangalie muktadha. Soma Luka 14:25-27. Je, Yesu anatufundisha kumpenda kila mtu isipokuwa familia yetu? (Hapana. Dhana ya kuchukia familia inakinzana na Biblia yote, ikiwemo Amri ya Tano (Kutoka 20:12). Sidhani kama Yesu anatuambia kuacha kuipenda familia na kuanza kuichukia. Na, sidhani kama Yesu anatuambia kuuza kila kitu na kubaki bila ya kitu chochote.)
e) Hebu turejee nyuma zaidi ili kuuangalia muktadha. Soma Luka 14:16-20. Unaufahamu mfano huu kwa kuwa unajitokeza kwenye zaidi ya kitabu kimoja kati ya vitabu vinne vya injili. Kitu gani kinawazuia kwenda kwenye karamu ya harusi? (Wanayajali zaidi masuala ya maisha yao.)
i) Sasa, hebu niambie, unadhani Yesu anamaanisha nini kuhusu “kuichukia” familia yako, kuviacha “vyote” na kula na wadhambi? Yesu anajaribu kutufunza fundisho gani? (Hatuwezi kuruhusu kazi zetu, mambo tunayoyapenda, familia zetu au hadhi zetu kuzuia kuuendeleza Ufalme wa Mungu. Mafarisayo hawakutaka kuweka kando hadhi yao ili kula na wadhambi.)
f) Soma Luka 14:34-35. Unayo masikio, je unasikia nini? (Wakristo wanatakiwa kuchangamana na ulimwengu. Hatuwezi kuruhusu hadhi yetu, hali ya ukubwa/ukuu kuliko wengine, kazi zetu, mambo tunayoyapenda au familia zetu kuingilia suala la kushirikiana na wadhambi wanaotaka kuchangamana nasi.)
3) Lutu
a) Soma Mwanzo 13:8-13. Je, huu ndio uchaguzi ambao Yesu anatufundisha tuuchague? Kuhamia kwenye miji miovu na kuanzisha vituo vya uinjilisti?
i) Unadhani Lutu alichukua uamuzi huu ili kupeleka injili?
b) Soma Mwazo 14:11-12. Lutu anatekwa na wadhambi! Je, hatari inapaswa kutusababisha tuachane na uinjilisti mijini?
c) Soma Mwanzo 14:15-16. Tukio hili linayazungumziaje mapigano halisi dhidi ya watu wabaya? Linasema nini kuhusu ulinzi wa Mungu kwa Lutu?
i) Je, umeona jambo la tofauti kuhusu makazi ya Lutu? (Katika Mwanzo 13:12 Lutu anajenga mahema yake “karibu” na Sodoma. Katika Mwanzo 14:12, Lutu anaishi “Sodoma.”)
d) Soma Mwanzo 19:12-16. Kuna hatari gani halisi kwa mtu mwenye haki (au wanandoa) kuhamia mahali palipojaa wadhambi? (Hatari ni kushirikishwa kwenye mazingira na ushawishi wa kiovu.)
e) Soma Mwanzo 19:17 na Mwanzo 19:26. Kwa nini mke wa Lutu alitazama nyuma? (Nilipoegesha gari langu jipya na kuondoka, niligeuka nyuma na kuliangalia. Moyo wake, maisha yake, na vitu vyake vilikuwa Sodoma. Hakuweza kujizuia kugeuka kuyaangalia maisha yake ya kale kwa mara ya mwisho.)
4) Yohana Mbatizaji
a) Soma Mathayo 3:1-3. Kutokana na utangulizi wa somo letu, unamwelezeaje Yohana Mbatizaji? Je, ni mtu wa kujichanganya na watu wengine?
b) Soma Mathayo 3:5. Je, kulikuwa na tatizo, kwamba Yohana aliishi nje kabisa nyikani? (Hapana. Watu walimwendea!)
c) Fikiria tofauti zilizopo kati ya Yesu, Mafarisayo, Yohana Mbatizaji na Lutu. Je, unaweza, kuanza kutunga kanuni (sheria) zinazohusu kuwafikia wadhambi? (Mafarisayo wanatufundisha tusiwaangalie wadhambi. Yohana anatufundisha kuwa ikiwa tuna ujumbe sahihi, wadhambi watatujia. Lutu anatufundisha kuwa ni hatari kwa mali na wokovu wetu kushikamana na wadhambi. Yesu anatufundisha kuwa tujitoe kwa wadhambi na tuwe tayari kuchangamana nao.)
i) Je, unapaswa kufanya jambo gani tofauti na lile unalolifanya sasa hivi ili kuwafikia wadhambi?
ii) Je, unafanya jambo gani sasa hivi kuwafikia wadhambi linaloonekana kuhalalishwa na Biblia?
d) Rafiki, kushiriki neno la Mungu na wadhambi ni kazi ya muhimu sana. Wadhambi wanapopata ufahamu na kumgeukia Mungu, mbingu zinashangilia. Je, utakubali, sasa hivi, kufikiria njia inayopendekezwa na Biblia kupeleka injili na kisha kuanza kuitekeleza?
Juma lijalo: Yesu Atamani Wema Wao.