Matukio ya Siku za Mwisho

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
(Mathayo 23 & 24)
Swahili
Year: 
2016
Quarter: 
2
Lesson Number: 
11

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Mojawapo ya faida maridhawa ya kuandika masomo haya ni kwamba yananilazimisha kujifunza Biblia. Malengo makuu ya kuandika masomo haya ni kuiboresha Shule ya Sabato na kuwasaidia wanafunzi kuyaelewa mapenzi ya Mungu vizuri zaidi. Hata hivyo, ninapojifunza Biblia mara zote huwa ninafikiria juu ya athari za neno la Mungu maishani mwangu. Juma hili baadhi ya kauli za Mathayo zinaingiliana sana na maisha yangu binafsi kiasi kwamba natangulia kuomba radhi kwa kujihusisha sana katika somo hili. Hebu tuchimbue zaidi na tuone kama wewe pia unajisikia kujihusisha na somo letu la Biblia!

 

I.                    Walafi wa Sifa

 

A.                Soma Mathayo 23:1-4. Unapotambua kwamba mtu fulani ni mnafiki, je, unayachukuliaje mafundisho ya mtu huyo? (Wazo la jumla ni kuyakataa mafundisho ya mtu mnafiki.)

 

1.                  Kwa nini Yesu anasema kuwa wanafiki hawa waheshimiwe? (Kwa sababu “wanaketi katika kiti cha Musa.”)

 

a.                   Hiyo inamaanisha nini, na kwa nini jambo hilo ni muhimu sana? (Nadhani inamaanisha kwamba wanafundisha torati iliyotolewa na Mungu kupitia kwa Musa.)

 

2.                  Nawakumbuka viongozi wa dini kadhaa maarufu waliokuwa na dhambi maarufu. Mwitiko wangu ulikuwa ni kwamba waliikumbatia na kuikubali dhambi – jambo ambalo ni kweli kwetu sote. Tunawezaje kuwatofautisha wale viongozi wa dini “walioketi katika kiti cha Musa” na wale wanaotupotosha? (Sababu kuu ya kuanza na maswali yanayotokana na fungu la Biblia katika mfululizo wa masomo haya ni kwamba hatuwezi (natumaini hivyo) kupotoka sana ikiwa tutajikita kwenye neno la Mungu. Suala la muhimu zaidi ni endapo kiongozi anafundisha Biblia au anafundisha kitu kingine kabisa.)

 

B.                 Soma Mathayo 23:5-7. Kuwa mwaminifu. Je, unapenda kutukuzwa, pamoja na kupewa kiti bora kabisa? Je, unapenda kusalimiwa na watu wanaokuheshimu? (Ikiwa umesema “hapana,” nadhani tu kwamba umevunja Amri ya Tisa. Sote tunapenda kutukuzwa/kuheshimiwa.)

 

1.                  Tunawezaje kuepuka kuwa kama hawa viongozi wa dini? (Angalia tena fungu la 5, “matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu.” Ikiwa kila jambo unalolitenda linahamasishwa na kujitukuza kwako, tofauti na kumpa Mungu utukufu au kumpenda mtu mwingine, basi una tatizo kubwa.)

 

 

C.                 Soma Mathayo 6:2. Nini maana ya “wamekwisha kupata thawabu yao?” Je, inamaanisha kwamba “thawabu kamili” ni kujitukuza binafsi – itakayokukosesha mbingu? (Napenda kuhubiri, ninapenda kufundisha, na hakuna shaka yoyote kwamba sehemu ya sababu yangu ni kwamba ninataka watu wamjue Mungu vizuri zaidi. Lakini, sehemu nyingine ya sababu zangu ni kwamba ninapenda watu waseme kuwa, “anafanya kazi nzuri.” Ninaposoma habari za hawa viongozi wa dini ambao thawabu yao pekee ipo hapa, ninasikitika. Dkt. William H. Shea ni mmojawapo wa Wakristo wa pekee kabisa niliowahi kuwafahamu. Ni mwerevu sana na mnyenyekevu kupindukia. Nilimuuliza, “Je, unafurahia heshima/sifa unayopewa kwa kuhubiri na kufundisha?” Alijibu, “ndiyo,” hiyo ni sehemu mojawapo. Hiyo iliufanya moyo wangu utulie katika suala hili.)

 

D.                Soma Mathayo 23:8-12. Mmojawapo wa wanafunzi wangu wa zamani alikuwa akiniita “rabi” na mara kwa mara mke wangu huniita “profesa.” Wanangu wananiita “Baba.” Wanafunzi katika shule ya sheria huniita “Profesa Cameron.” Je, ninapaswa kuwaambia wote hawa waache kuniita hivyo?

 

1.                  Soma Kutoka 20:12. Suala mojawapo ni kuwaheshimu viongozi wa dini. Fungu hili linatuambia tuwaheshimu wazazi wetu – na hiyo inajumuisha kumuita baba yangu kuwa “Baba.” Unawezaje kuelewa mkanganyiko wa dhahiri uliopo kwenye Biblia?

 

2.                  Kumbuka muktadha. Je, viongozi wa dini wananyakua heshima gani isivyostahili? (Wanadai heshima inayomstahili Mungu. Wanafanya kila jambo kwa ajili ya utukufu wao, na sio utukufu wa Mungu au upendo kwa watu wengine. Utagundua kwamba katika Mathayo 23:8-10 anayepaswa kurelejewa ni Mungu. Wanangu, mke wangu, wanafunzi wangu hawadhani kwamba mimi ni Mungu na sijaribu kuwachanganya akili katika jambo hilo.)

 

E.                 Hebu turuke mafungu kadhaa hadi Mathayo 23:37-39. Tatizo la msingi la viongozi wa dini Yerusalemu lilikuwa ni lipi? (Walimkataa Yesu. Utaona kwamba mjadala wa “mada” ni sehemu ya kumkataa Yesu. Sasa Yesu anasema kuwa mwisho wao umefika. Hawako radhi kumkubali au kumpa utukufu.)

 

II.                 Kubomolewa

 

A.                Soma Mathayo 24:1. Unadhani kwa nini wanafunzi walimwambia Yesu aangalie majengo ya hekalu? (Pasi na shaka majengo hayo yalikuwa mazuri. Nimesoma maelezo ya Josephus kuhusu hekalu na maelezo hayo yalikuwa mazuri ajabu.)

 

B.                 Soma Mathayo 24:2-3. Bila shaka habari hii ni ya kutisha. Kwa nini wanafunzi walimwendea Yesu kwa “faragha” ili kutaka kufahamu habari kwa kina zaidi?

 

1.                  Unaona maswali mangapi katika mafungu haya? Unadhani wanafunzi walidhani walikuwa wanamuuliza Yesu maswali mangapi? (Nadhani walikuwa wanauliza angalao maswali mawili, lakini nadhani walidhani kwamba walikuwa wanauliza swali moja tu. Bila shaka walidhani kuwa hekalu halitabomoshwa hadi Yesu atakaporejea “mwisho wa dahari.”)

 

III.              Mwisho

 

A.                Soma Mathayo 24:4. Yesu anajali jambo gani kwanza? (Kwamba tuepuke kudanganywa/kulaghaiwa.)

 

B.                 Soma Mathayo 24:5-14. Mara tatu Yesu anarejea “nyakati za mwisho” katika hivi vifungu. Anajadili mwisho gani, mwisho wa hekalu au mwisho wa dunia?

 

 

C.                 Soma Mathayo 24:15-20. Unadhani jambo gani linajadiliwa hapa? (Ni kawaida kwamba unabii unaweza kutimizwa zaidi ya mara moja. Lakini hii inaonekana kuendana na kubomolewa kwa Israeli. Wakristo wengi waliukimbia mji na waliokolewa kabla ya hekalu kuangamizwa na Warumi.)

 

D.                Soma Mathayo 24:23-27. Jambo gani linaelezewa hapa? (Ujio wa Yesu Mara ya Pili.)

 

1.                  Kuna jambo gani mahsusi kuhusu Wakristo kudanganywa? (Watatokea makristo wa uongo – na ishara zao na miujiza yao ina ushawishi mkubwa sana.)

 

2.                  Tunawezaje kuepuka kudanganywa? (Hakuna mtu atakayetakiwa kutuambia kuhusu ujio wa Yesu Mara ya Pili. Watu wote watauona kwa mara moja. Nimeepuka baadhi ya masuala magumu zaidi kwenye ujumbe wa Yesu kwa sababu ninaweza kukosea. Hata hivyo, sehemu rahisi ya ujumbe huo iko dhahiri kabisa – utafahamu tu Yesu atakapokuja!)

 

a.                   Kwa nini basi Yesu anatuonya kwamba tunatakiwa kuepuka kudanganywa, na kwamba uongo ujao utakuwa na nguvu kubwa sana? (Tuna nafasi kubwa sana ya kudanganywa na hao walaghai. Ikiwa unajihusisha kwenye mjadala unaomhusisha mtu fulani kwamba ni Yesu, basi huo ni uthibitisho madhubuti kwamba mtu ni mlaghai na si Yesu!)

 

E.                 Soma Mathayo 24:30-31 na Mathayo 24:40-41. Je, tutakuwa na uthibitisho gani mwingine kamili kuhusu ujio wa Yesu Mara ya Pili? (Watakaookolewa watachukuliwa mbinguni!)

 

1.                  Je, “sauti ya parapanda” inahusu nini? (Soma 1 Wakorintho 15:51-52. Wale waliokufa wakimtumaini Yesu watafufuliwa kwa dakika moja, kufumba na kufumbua wakati wa mlio wa parapanda.)

 

F.                  Hebu tupitie mambo yote haya ili usiweze kudanganywa. Jambo gani litatokea Yesu atakapokuja tena? (Mwanga kama wa radi utatokea duniani kote – kila mtu atauona kwa wakati mmoja. Waliokufa katika Kristo watafufuliwa kutoka makaburini. Watakaookolewa wakiwa hai watakuchukuliwa mbinguni. Hautachanganyikiwa kuhusiana na hili tukio. Ikiwa hutachukuliwa mbinguni, hiyo ni habari mbaya sana.)

 

G.                Soma Mathayo 24:42-44. Hebu subiri kidogo, hivi punde tu tumejifunza kwamba ujio wa Yesu Mara ya Pili utakuwa dhahiri kwa kila mtu. Kwa nini tunaonywa “kukesha” na kuhusu matatizo ya ujio wa ghafula? Ninaweza kuwa kwenye usingizi mzito lakini sitaweza kuukosa ujio wa Yesu Mara ya Pili! (Mwizi havunji na kuingia nyumbani kwa Yesu katika huu mfano. Mwizi anavunja na kuingia nyumbani kwako. Onyo halihusu utata juu ya ujio wa Yesu, bali endapo u tayari!)

 

H.                Soma Mathayo 24:45-46. Unapaswa kuwa unafanya nini wakati ukiutarajia ujio wa Yesu Mara ya Pili? (Kazi yako – “kuwalisha” watumishi wa Yesu. Tunatakiwa kuendelea kufanya kazi ili kuuendeleza Ufalme wa Mungu!)

 

 

I.                    Rafiki, viongozi wa dini walikuwa na tatizo gani tulilolijadili mwanzoni mwa somo hili? Tatizo ni kwamba walikuwa wanafanya kazi ya kuuendeleza utukufu wao wenyewe. Yesu anatupatia wito wa kufanya nini wakati tunasubiria kurudi kwake? Kuuendeleza Ufalme wa Mungu. Je, unafanya nini siku hizi? Je, unauendeleza utukufu wako au Ufalme wa Mungu? Ikiwa hulipendi jibu lako, kwa nini usitubu sasa hivi na umwombe Roho Mtakatifu akuoneshe njia bora zaidi?

 

IV.              Juma lijalo: Siku za Mwisho za Yesu.