Miungu ya Roho
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Jeffrey Brauch, aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Regent, ni mmojawapo wa watu wa pekee sana niliowahi kukutana nao. Mara zote alionekana kuyaelekeza mawazo yake yote kwangu tulipokuwa tukizungumza. Ninapokuwa ninazungumza na watu wengine, ninasikitika kwamba kwa ujumla huwa ninawaza mambo yangu. Nina uhakika anaenenda vivyo hivyo kwa kila mtu – kwamba anayaelekeza mawazo yake yote kwa watu anaozungumza nao. Jeff anayaishi yale ambayo Mathayo anayafundisha juma hili: kuishi maisha ya kuwajali watu wengine. Hebu tuchimbue somo letu ili tujifunze zaidi!
1) Watoto
a) Soma Mathayo 18:1-4. Nani aliye na mawazo yenye msimamo thabiti kuhusu malezi ya watoto: wazazi wenye watoto kadhaa au watu wasio na watoto?
i) Je, watoto unaowafahamu ni wabinafsi kwa asili? Je, huwa wanajipendelea wao wenyewe kuliko watu wengine? (Kutokana na kile nilichokiona, watoto wanafanana nasi tu – wamezaliwa dhambini.)
ii) ikiwa hilo ni kweli, je, Yesu anazungumzia jambo gani?
b) Soma tena Mathayo 18:1. Kwa nini mtu atake kuwa mkuu katika ufalme wa mbinguni? (Ili aweze kuwatawala watu wengine.)
i) Je, watoto hawako hivyo? (Watoto wadogo ni tegemezi kwa kiwango cha juu sana. Hata kama wana tabia nyingine mbaya, kwa mfano kuwa wachoyo/wabinafsi, bado wanahitaji msaada na wanalitambua hilo.)
c) Angalia tena Mathayo 18:4. Yesu anatuambia nini basi kuhusu tabia njema? (Kwamba tunatakiwa kujinyenyekeza kwake na kumtegemea yeye – kama mtoto anavyowategemea wazazi wake.)
d) Soma Mathayo 18:5-6. Hili linahusianaje na alichokimaanisha Yesu kuhusu watoto kuwa tegemezi? (Kwa kuwa watoto ni tegemezi, watu wazima wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wanawafundisha vizuri na kuwatendea watoto vyema kwa mujibu wa ushawishi wetu mzuri.)
2) Dhambi
a) Soma Mathayo 18:7. Je, umewahi kumsikia mtu anayenufaika kutokana na msemo wa kiovu kwamba, “Nisingefanya hivyo mtu mwingine angefanya. Nami pia naweza kuwa mmojawapo wa watu wanaopata fedha kutokana na kitendo hicho.”
i) Jibu la Yesu kwa swali hilo ni lipi? (“Ole wako!” uovu utakuja, lakini ingekuwa heri uovu huo usitokane nawe (usipitie kwako).)
b) Soma Mathayo 18:8-9. Je, dhambi inaanzia mkononi mwako, mguuni mwako au kwenye jicho lako? (Hapana. Dhambi inaanzia akilini (mawazoni).)
i) Unakielewa kile anachokisema Yesu? (Yesu anabainisha madhara ya dhambi. Watu wanatenda dhambi kutokana na wanachodhani ni manufaa yatokanayo na vitendo hivyo vya dhambi. Yesu anasema ni heri kupoteza kitu cha muhimu kuliko kutenda dhambi.)
c) Soma Mathayo 18:10. Je, Yesu anazuga kwa kuyazungukazunguka maoni yake, na amerukia tena kuwazungumzia watoto? (Yesu yupo kwenye mada ile ile. Hatimaye watoto watakabiliana na dhambi, lakini ni heri dhambi hiyo isipitie kwako.)
d) Soma Mathayo 18:12-14. Yumkini umewahi kusikia kisa cha kondoo tisini na kenda na kondoo mmoja aliyepotea. Yesu anamaanisha nini kwenye huo mfano wa watoto? (Katika tamaduni nyingi watoto hawathaminiwi. Katika baadhi ya tamaduni watoto wanatumikishwa. Yesu anatufundisha kuwa watoto wana thamani kubwa sana – kila mmoja wao.)
e) Soma Mathayo 18:15-17. Lengo la kushugulikia tofauti zetu na matatizo kwa kutumia njia hii ni lipi? (Lengo ni kumfanya mtu huyo asikilize na kutafakari.)
i) Inamaanisha nini kumchukulia mtu kama “mpagani au mtoza ushuru?”
(1) Je, ni sahihi kuwatendea wapagani tofauti?
3) Kanisa
a) Soma Mathayo 18:18. Tumejadili suala la kupeleka mashauri ya watu kanisani. Uamuzi wa kanisa ni wa muhimu kwa kiasi gani?
b) Hebu turejee nyuma na tusome Mathayo 16:18-19. Tulipojifunza suala hilo kitambo kifupi kilichopita nililifanya kuwa jambo la kiroho kwa kusema kuwa wale wanaoelewa kwamba Yesu ni Mungu na kumpokea “wanafunguliwa” na wale wanaomkataa “wanazuiliwa” mbingui. Je, sikuwa sahihi? (Huu muktadha mpya unaonesha kuwa sikuingia kwa kina zaidi kwenye suala la matumizi ya dhana hiyo kivitendo. Yesu anatuambia kuwa kanisa limepewa mamlaka ya kiroho hapa duniani.)
i) Mamlaka haya yana ukomo gani? Je, kanisa linaweza kubadili siku ya ibada? Je, kanisa linaweza kumbadilisha Yesu na kutupatia mwombezi/mpatanishi mbadala? (Muktadha uliopo katika Mathayo 18 unazungumzia mfarakano kati ya washiriki wa kanisa.)
c) Soma Mathayo 18:19-20. Kanisa linatakiwa kuwa kubwa kiasi gani ili liweze kuwa na aina ya mamlaka ambayo tumekuwa tukiyajadili? Je, kanisa la watu wawili linatosha?
i) Unapokaa na kuyatafakari mafungu haya, unadhani ni jambo gani la msingi analolimaanisha Yesu? (Mbingu zinafanya kazi kupitia kwetu. Mungu anatupatia mamlaka.)
ii) Je, hili linahusiana kwa vyovyote vile na mjadala wa Yesu uliopita kuhusu watoto? (Yesu anatufundisha kuwa wanyenyekevu na kumtegemea. Hiyo inabainisha kiwango cha “mamlaka” yetu hapa. Mamlaka yetu yanatakiwa kuendana na mapenzi ya Yesu yaliyobainishwa. Hii inamaanisha kwamba kanisa halipaswi kuweka sheria zinazokinzana na mafundisho makuu ya Mungu. Kwa kuwa tunayo haya mamlaka, tunatakiwa kuwa makini sana jinsi tunavyoyatumia.)
4) Msamaha
a) Soma Mathayo 18:21-22. Namna pekee ya kuwa na uhakika kwamba tunazo mara sabini na saba ni kwa kuandika. Je, haya ndio maelekezo ya Yesu kwetu?
b) Soma Mathayo 18:23-30. Unamchukuliaje mtu ambaye alikuwa anadaiwa mamilioni kutomsamehe mdeni wake aliyekuwa akimdai kiasi kidogo?
c) Soma Mathayo 18:31. Mashuhuda walisikitika, kama jinsi ulivyosikitika! Je, ni kwa sababu mtu aliyewiwa deni dogo hakusamehewa mara saba, achilia mbali mara sabini na saba?
d) Soma Mathayo 18:32-33. Bwana anasema kuwa tatizo ni lipi? (Rehema. Sio kuendeleza kile anachokiamrisha Yesu, bali ni kuwa na rehema kwa wale wanaoomba msamaha.)
i) Kipimo cha msahama maishani mwako ni kipi? (Yesu alikufia kwa ajili ya dhambi zako. Dhambi yako i kinyume na Mungu. Tunaathiriwa na dhambi, lakini kuvunja sheria ya Mungu ni dhambi dhidi yake. Sisi ndio yule mtumwa aliyesamehewa “mamilioni.”)
e) Soma Mathayo 18:34-35. Yesu anatoa onyo gani?
i) Inamaanisha nini “kusamehe … kutoka moyoni?”
5) Ndoa
a) Soma Mathayo 19:3-6. Je, Yesu anaamini maelezo ya uumbaji? (Anayaamini kwa uthabiti mkubwa kiasi kwamba anajenga hitimisho la kiroho kutokana na maelezo ya uumbaji.)
b) Soma Mathayo 19:7-9. Je, unadhani ni kama ajali tu kwamba huu mjadala wa ndoa mara moja unaufuatia mjadala kuhusu msamaha?
i) Je, mjadala wa ndoa unaboreshaje uelewa wetu wa suala la msamaha? (Ikiwa mara zote mwenzi anatakiwa kumsamehe mwenzi wake, basi hatupaswi kuwa na talaka. Hii inatuonesha kuwa rehema inatokana na mpango wa Mungu kwa ajili ya ndoa na maisha.)
ii) Je, mwenzi anaweza kusamehe “kutoka moyoni” kitendo cha mwenzi wake kutokuwa mwaminifu, na bado akataliki kutokana na kutokuwepo kwa uaminifu? (Ndiyo. Msamaha haumaanishi kutelekeza (kutotumia) akili ya kawaida.)
c) Soma Mathayo 19:10. Baadaye katika sura hii ya kitabu cha Mathayo Yesu anasema kuwa ni vigumu kwa tajiri kuokolewa. Soma Mathayo 19:25. Wanafunzi wa Yesu wanayachukuliaje mafundisho yake? (Wanashangaa. Kwao kitendo hicho hakionekani kuwa sahihi. Haiwaingii akilini kutokana na uelewa wao juu ya mapenzi ya Mungu.)
d) Soma Mathayo 19:11-12 (ndoa) na Mathayo 19:26 (utajiri). Yesu anatoa maoni gani kuhusu mafundisho ambayo ni magumu kuyaelewa na kuyafuata? (Kwamba Mungu atatenda kazi pamoja nasi ili kuyafanya mambo yanayoonekana kuwa hayawezekani yawezekane.)
6) Ujira
a) Soma Mathayo 20:1-12. Je, unakubaliana na wale wanaonung’unika? Jiweke kwenye nafasi ya wale waliofanya kazi kutwa nzima!
b) Soma Mathayo 20:13-16. Ikiwa Yesu anatufundisha somo kuhusu Ufalme wa Mbinguni, na sio ujira, je, kuna kipi cha kujifunza? (Mungu haangalii usawa tu. Yeye ndiye usawa. Lakini, yeye ni zaidi ya usawa. Anatupatia kile tunachostahili, na anatupatia zaidi ya tunachostahili. Anafanya mambo yasiyowezekana yawezekane.
c) Rafiki, Mungu anakujali. Anawajali watoto tegemezi. Anatutaka tuwe mbaraka kwa watu wengine, badala ya kutafuta tu kile tunachodhani kuwa ni usawa.
7)Juma lijalo: Yesu Akiwa Yerusalemu.