“Ondoka, Uende!” Imani na Uponyaji
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Juma lililopita tulijifunza Fundisho la Yesu Mlimani. Juma hili tunaangalia mfululizo wa uponyaji na miujiza inayotupatia ufahamu mkubwa katika utume wa Yesu na kuimarisha na kuthibitisha hoja ya Mathayo anaposema kuwa Yesu ni Masihi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi kuhusu Bwana wetu aliyejaa utukufu!
I. Mtu Mwenye Ukoma
A. Soma Mathayo 7:28-8:1. Tulipojifunza kuhusu Fundisho la Yesu Mlimani, yumkini ulihitimisha kuwa Yesu alitoa changamoto halisi ya namna ya kuishi maishani. Makutano wamehitimisha nini? (Umati mkubwa unamfuata Yesu. Hawa hawakuwa wamekatishwa tamaa kwa namna yoyote ile.)
1. Kuna hitimisho gani lenye mantiki kuhusu jinsi walivyoyaelewa mafundisho yake? (Utakumbuka nilibainisha vipengele vinavyozungumzia neema katika Fundisho la Yesu Mlimani. Kwa hakika, watu hawakuelewa kuwa Yesu alikuwa anawapa wito wa kuwa na viwango visivyowezekana, vinginevyo wasingeendelea kumfuata kwa idadi kubwa. Uelewa wao katika zama zao unapaswa kuwa mwongozo katika mtazamo wetu kwenye ujumbe wa Yesu.)
2. Mathayo anatuambia kuwa Yesu alikuwa tofauti kwa maana ya kwamba aliwafundisha “kama mtu mwenye amri.” Je, kuna mashaka yoyote kuhusu mamlaka yake? (Ndiyo. Yesu alikuwa mgeni kwao.)
a. Hii inatufundisha nini kuhusu ufundishaji wa Biblia? (Kwa dhahiri, sisi si Yesu. Lakini, jambo la muhimu ni kwamba Biblia sio kitu cha kufanyia majibizano na kujengea hoja kwa ajili ya kujifurahisha, Biblia ina mwongozo kwa ajili ya maisha, mwongozo tunaotakiwa kuuelewa.)
B. Soma Mathayo 8:2-3. Je, hili ndilo ombi ambalo sote tunapaswa kuliomba tunapokuwa wagonjwa? Au, je, tuchukulie tu kwamba Yesu yu radhi kutuponya?
C. Soma Mathayo 8:4. Kwa nini Yesu anamwambia mtu huyu asimpe Mungu utukufu? Kwa nini anamwambia afiche nuru yake? Je, hii si kinyume na Mathayo 5:14-16? (Hii inabainisha kuwa kumponya mtu huyu mwenye ukoma halikuwa jambo bora kwa ajili ya utume wa Yesu. Hivyo basi, swali la, “ukitaka waweza kunitakasa,” lilikuwa sahihi kabisa. Yesu anataka kutuponya, na hata kama uponyaji huo unaweza kusababisha matatizo, bado atafanya hivyo. Lakini, tunaona kuwa lazima Yesu aweke mawazoni mwake taswira pana ya uelekeo wa ufalme wake. Hii pia inatufundisha kutumia busara katika nyakati ambazo tunashiriki (tunapeleka) injili na watu wengine.)
II. Akida
A. Soma Mathayo 8:5-9. Kwa nini akida huyu anamwambia Yesu jinsi ya kufanya uponyaji? (Soma Matendo 10:28. Katika fungu hili Petro anazungumza na Kornelio ambaye ni akida wa Kirumi. Akida alielewa matatizo ambayo Yesu angeweza kukabiliana nayo kwa kwenda nyumbani kwake, kwa hiyo anajaribu kupunguza athari kubwa zinazoweza kutokea kutokana na ombi lake.)
B. Soma Mathayo 8:13. Soma tena Mathayo 8:3 na usome Mambo ya Walawi 13:45-46. Kwenye kisa cha akida tunaona kuwa Yesu anaweza kuponya kwa mbali. Kwa nini anamgusa mtu mwenye ukoma – mtu aliyepaswa kukaa mbali na watu wengine? (Wote wawili, yaani mwenye ukoma na akida wa Kirumi hawakuwa watu wa maana kwa Wayahudi. Yesu anaonesha kuwa yu radhi kuwakumbatia watu wasio na maana (wasio maarufu).)
C. Hebu turejee nyuma na kusoma Mathayo 8:10-12. Tunapata tumaini gani kwa wale ambao miongoni mwetu ni watu wa mataifa? (Kwa imani tunaweza kuwa sehemu ya ufalme wa Mungu wa milele!)
III. Mama Mkwe
A. Soma Mathayo 8:14-15. Tunaona kwamba Yesu amemponya mtu mwenye ukoma, mtumishi wa akida na jinsi anavyomponya mama mkwe. Je, kuna mtu yeyote ambaye Yesu hatamponya? (Ninatania tu.)
1. Utaona kwamba Yesu alimgusa, na kwamba alimgusa mkononi. Ikiwa unamponya mtu mwenye homa, je, utamgusa mtu huyo mkononi au kichwani? (Nadhani sababu iliyosababisha mkono wake ukatajwa ni kutuonesha jinsi Yesu alivyomponya kikawaida kabisa.)
2. Je, hili lilikuwa jambo la kawaida kwa Petro? (Sidhani. Hivyo, imani ya Petro kwa Yesu inaimarishwa.)
B. Soma Mathayo 8:16-17. Mathayo anatuonesha (kwa mara nyingine tena) kuwa Yesu anatimiza unabii kuhusu Masihi. Jambo gani linakufurahisha kutokana na jinsi Yesu anavyofanya uponyaji? (Yesu anaondoa pepo kwa kutumia neno lake tu. Hakuna ugonjwa ulio mgumu kwake wa kumshinda kuuponya. Anamponya kila mtu. Mathayo anatuonesha kwamba Yesu anatimiza unabii kwa uwezo mkubwa.)
IV. Wanafunzi
A. Soma Mathayo 8:18-27. Vigezo vya kuwa mfuasi wa Yesu ni vipi? (Inaonekana tunatakiwa kuwa radhi kumpa Yesu kipaumbele dhidi ya raha, familia na usalama.)
1. Unadhani Mathayo anamaanisha nini kwa kuzungumzia suala la uanafunzi katikati ya hii miujiza? (Utaona kwamba hawa wanafunzi wawili wapya wanaoonekana kuwa na uwezo mkubwa walikuja kwa Yesu baada ya Yesu kutenda miujiza mikubwa. Mathayo anaweza kuwa anatuambia kuwa uwezo wa Yesu ni kwa ajili ya kusukuma nyuma madhara ya dhambi, badala ya kukufanya kujisikia faraja zaidi.)
V. Nguruwe
A. Soma Mathayo 8:28-29. Je, ungependa kuwa mwanafunzi wa Yesu wakati watu hawa wawili wanapomjia? (Watu waliwaogopa kutokana na vurugu zao.)
1. Pepo wenye vurugu wana mtazamo gani dhidi ya Yesu? (Wanamwogopa. Watu wanamtii Yesu na pepo wanamwogopa!)
2. Tafakari maneno ya pepo. Unajifunza nini kutoka kwa adui? (Wanafahamu watapoteza mpambano kati ya wema na uovu. Wanafahamu muda umetengwa wakati mtafaruku/mgogoro utakapohitimishwa. Wanaamini kuwa hitimisho litakuwa chungu sana kwao.)
3. Kwa nini wanapiga kelele?
B. Soma Mathayo 8:30-32. Jiweke kwenye nafasi ya pepo. Walikuwa wanafikiria nini? Kuna haja gani ya kuwaingia nguruwe ikiwa utaishia kuwaua? (Hii inaonesha kuwa lengo kuu la pepo ni kuangamiza. Kuangamiza bila kujali. Unaweza kufikiria kile ambacho pepo wanakuwazia?
C. Soma Mathayo 8:33-34. Watu wanamtaka Yesu aondoke mjini. Hii inakuambia nini kuhusu vitu ambavyo wanavithamini? (Wanawajali zaidi nguruwe wao zaidi kuliko wanavyojali wokovu wa hawa watu wawili.)
VI. Mtu Aliyepooza
A. Soma Mathayo 9:1-2. Ikiwa wewe ndiye mwenye kupooza, je, hili ndilo jibu unalotaka kulisikia kutoka kwa Yesu? Katika sura iliyopita tuliona kuwa Yesu alikuwa akimponya kila mtu aliyemjia. Kwa nini isiwe kwa mtu huyu?
1. Je, unakumbuka kipindi fulani maishani mwako ulipoomba kwamba Mungu akutendee jambo fulani na badala yake Mungu akatenda jambo jingine?
2. Soma Yohana 9:1-2 na Zaburi 103:2-3. Watu walidhani kuwa dhambi ilisababisha magonjwa. Hivyo, tatizo kuu ni dhambi. Katika kitabu cha Zaburi, msamaha wa dhambi unaorodheshwa kabla ya uponyaji. Yesu alishughulikia kile ambacho bila shaka mtu huyu alidhani kuwa ndilo tatizo kubwa la msingi.)
B. Soma Mathayo 9:3. Je, haya ni mashtaka yenye mantiki? (Naam! Madai ya Yesu yanaweza tu kumaanisha kuwa yeye ni Mungu!)
C. Soma Mathayo 9:4-5. Ungejibuje swali la Yesu? (Ni rahisi kusema kuliko kutenda jambo fulani.)
1. Kwa nini ni sawa sawa kuyaita haya mashataka ya kukufuru kuwa ni “uovu?” (Nadhani yanahusiana na ukweli kwamba viongozi hawa wa dini hawakuwa wanakubali hitimisho la kwamba Yesu ni Masihi.)
D. Soma Mathayo 9:6-7. Je, hoja hii ina ushawishi? Tuchukulie kwamba mtu ambaye una uhakika kuwa sio Mungu anamponya mtu fulani. Je, huo utakuwa ni uthibitisho wa uungu? (Haitathibitisha jambo lililomo akilini mwangu.)
1. Kwa nini basi, Yesu anatumia aina hii ya uthibitisho? Kwa nini Mathayo anatumia hii kama sehemu ya uthibitisho wake kwamba Yesu ni Mungu? (Ni vigumu kwangu kutafakari njia ya dhahiri kuthibitisha kuwa Yesu ni Mungu. Hivyo, Yesu anatenda kile awezacho kwa uzuri zaidi katika mazingira yaliyopo.)
2. UtagunduaYesu anadai kuwa na mamlaka ya kimbingu ya kusamehe dhambi. Je, hiyo ni sehemu ya uthibitisho wa Mathayo? (Ndiyo. Tafakari jambo hili kidogo. Ikiwa Yesu si Mungu, je, yeye ni nani? Ana wazimu. Ametenda ulaghai wa kupindukia. Je, mtu kama huyo anaweza kutenda muujiza? Madai ya Yesu pamoja na uponyaji halisi alioufanya ndivyo vinavyothibitisha dhana ya uungu wake.)
E. Rafiki, tunaona kwamba Yesu anawaendea watu wa aina zote ili kuwaponya na kuwasaidia. Kwa upande mwingine, Pepo wanajihusisha na uangamivu usio na maana kabisa. Je, utachagua upande gani kwenye pambano kati ya wema na uovu? Kwa nini usifanye uamuzi thabiti sasa hivi?
VII. Juma lijalo: Vita Vinavyoonekana na Visivyoonekana.