Kanisa Lililo Katika Mapambano
Utangulizi: Unakichukuliaje kitabu cha Ufunuo? Je, unawawazia akilini mwako wanyama wanaotisha? Vipi kuhusu mafumbo magumu kuhusu siku zijazo? Juma hili tunageukia sehemu tofauti ya kitabu cha Ufunuo, sehemu inayozungumzia ushauri wa Mungu kwa kanisa la Kristo. Ingawa sehemu hii ya kitabu cha Ufunuo inatoa ushauri kwa makanisa mahsusi yaliyokuwepo wakati kitabu hiki kilipoandikwa, wasomi wengi (wa Kikristo) wa Biblia wanaamini kuwa makanisa haya pia yanawakilisha maelezo ya kanisa la Kristo katika nyakati tofauti za historia. Kanisa la Laodikia linawakilisha kipindi cha mwisho cha historia kabla Yesu hajarudi tena. Ikiwa unaamini, kama ambavyo ninaamini, kwamba tunaishi katika kipindi cha mwisho, basi kanisa la Laodikia linatuelezea sisi. Hebu tuchimbue zaidi ili tuone yale tunayoweza kujifunza kutokana na ushauri wa Laodikia!
I. Utangulizi kwa Makanisa
A. Soma Ufunuo 1:1-2 na Ufunuo 1:4-5. Yohana anaandika ujumbe huu kwa niaba ya nani? (Yesu. Hata hivyo, Yesu anatoa salaam kwa niaba ya Mungu Baba na “roho saba” mbele ya kiti chake cha enzi.”)
1. Anawaandikia watu gani? (Anasema “makanisa saba” ambayo yapo “Asia.” Hii inatuambia kuwa tunashugulika na makanisa saba halisi.)
B. Soma Ufunuo 1:19-20. Makanisa yanalinganishwa na nini? (Vinara vya dhahabu.)
1. Kwa nini kanisa linalinganishwa na kinara cha dhahabu? (Unakumbuka majuma mawili yaliyopita tulijifunza kuwa tunapaswa kutenda kazi kwa “kiwango cha dhahabu” kwa ajili ya kanisa? Mungu anatafuta makanisa ya viwango vya dhahabu yatakayotoa nuru ya injili kwa ulimwengu.)
2. Je, “malaika mmoja kwa kanisa moja” inaashiria nini kuhusu kanisa lako mahalia? (Kwamba malaika mmoja amekabidhiwa ili kuliangalia!)
a. Hebu subiri kidogo. Tafakari jambo hili. Ikiwa “kinara cha dhahabu” kinaashiria kanisa, je neno “malaika” pia linaashiria mtumishi au kiongozi wa kila kanisa? (Suala hili linaibua mjadala. Inaweza kuwa inarejea kiongozi (mchungaji/kasisi/mhudumu) wa kanisa mahalia, lakini Ufunuo 11 inaanza kwa kumrejea “malaika” ambaye kwa dhahiri ni kiumbe asiye wa kawaida (ambaye si wa dunia hii).
3. Kauli ya “na yale yatakayokuwa baada ya hayo” inaashiria nini? (Kwamba huu sio tu ushauri kwa makanisa saba halisi, bali pia ni ushauri kwa kanisa la siku zijazo.)
II. Laodikia
A. Soma Ufunuo 3:14. Badala ya kuiandikia Laodikia, Yohana anaandika kuhusu malaika wa kanisa lililopo Laodikia. Kwa nini? (Lazima iwe ni kwamba malaika anapeleka ujumbe wa Mungu kwa kanisa. Unakumbuka tulipojifunza juu ya maono ya Kornelio na Petro kuhusu paa, tulijifunza kwamba malaika ndiye aliyezungumza na Kornelio. Matendo 10:3-4. Hivyo, malaika wanawapatia wanadamu ujumbe, na huu ndio ujumbe ambao malaika wa Laodikia anapaswa kulifikishia hilo kanisa. Kwa upande mwingine, ikiwa tunadhani “malaika” ni ishara inayomrejea kiongozi wa kanisa, basi hii inaonesha Mungu hufikisha ujumbe wake kwa njia ya viongozi walioteuliwa na Mungu.)
1. Mwandishi wa ujumbe wa malaika wa Laodikia ni yupi? Tulijifunza mwanzo wa somo hili kwamba Yesu ndiye mwandishi wa ujumbe mbalimbali kwa makanisa. Je, mwandishi wa ujumbe kwa Laodikia amebadilika? (Badala ya kutoa jina, ujumbe unatoa maelezo, “yeye aliye Amina. Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.”)
a. Maelezo hayo yanamwelezea nani? (Soma tena Ufunuo 1:5 na usome Wakolosai 1:18. Bado haya ni maneno ya Yesu.)
b. Kwa nini jambo hili linahusika sana kivitendo? (Yesu alipitia uzoefu wa maisha yetu! Huu ni ushauri kutoka kwa Mtu anayefahamu maana ya kuishi maisha ya kibinadamu.)\
B. Soma Ufunuo 3:15-16. Kwa nini Yesu anatutaka tuwe moto au baridi? Kuna ubaya gani kuwa “katikati ya barabara,” “watu wa wastani?” (Yesu anatulinganisha na kinywaji, jambo ambalo linatufanya tukumbuke kuwa tunapendelea vinywaji vya baridi au vya moto. Vinywaji vya vuguvugu sio chaguo letu.)
1. Kinywaji ni analojia. Yesu anazungumzia matendo. Matendo vuguvugu ni yapi?
C. Soma Ufunuo 3:17. Hii ndio tafsiri yetu ya neno “vuguvugu.” Washiriki wa kanisa hili wanafikiria mambo gani? (Ni matajiri na maisha ni mazuri.)
1. Kwa uhalisia wakoje? (Wanyonge, wenye mashaka, maskini, vipofu na wako uchi.)
a. Sijui unachofikiria, lakini jambo hilo linaonekana kuwa zuri sana kwangu. Vipi kama kila uliyemfahamu ambaye alikuwa “mnyonge, maskini na kipofu” alidhani kuwa maisha ni mazuri? Ingemaanisha kuwa usingekuwa na haja ya kuwa na wasiwasi juu yao, sawa? (Hiyo ingekuwa tiba nzuri sana ya umasikini na magonjwa duniani kote!)
b. Je, hii inamaanisha kuwa ikiwa kweli wewe ni masikini, na unadhani kuwa wewe ni maskini, basi “uvuguvugu” hauhusiki kwako? Na kwamba unahusika tu kwa matajiri?
2. Unadhani hasa Yesu anamwambia nini malaika wa Laodikia? (Kuwa “tajiri” na “masikini” ni mambo mawili makubwa, na sio vuguvugu, na katikati ya barabara. Hivyo, sidhani kama tunazungumzia wale wanaodhani kuwa kiuhalisia ni matajiri, lakini kiuhalisia ni maskini na vipofu.)
a. Jambo gani litaleta mantiki kwenye rejea ya kuwa “vuguvugu?” (Utajiri, umasikini na upofu lazima virejee hali yetu ya kiroho. Tunadhani kuwa tuko kwenye njia sahihi kiroho. Tunafahamu sana habari za Mungu. Lakini, kimsingi, sisi ni ombaomba wa kiroho.)
b. Watu wengi si matajiri, kwa hiyo manufaa ya kudhani kuwa jambo hili linawarejea watu ambao kiuhalisia ni matajiri ni kwamba unaweza kusema, “Jambo hilo halinihusu!” Ikiwa Yesu anazungumzia utajiri halisi, je, ujumbe ni upi? (Kwamba unajitegemea wewe mwenyewe. Unajisikia vizuri kabisa. Wewe ni Mkristo, lakini Ukristo huo unaweza kuwa ni utambulisho zaidi kuliko matendo.)
D. Soma Ufunuo 3:18. Je, hii inaonesha kuwa Yesu anataka tuwe matajiri? Je, unadhani Yesu anamaanisha kuwa katika hali ya uhalisia tunapaswa kununua dhahabu? (Ni vigumu kufikiria kwamba Yesu ana “ghala la dhahabu” mahali fulani. Ukweli kwamba injili sio biashara unakazia dhana ya kwamba Yesu anazungumzia masuala ya kiroho.)
1. Tiba ya umasikini wetu wa kiroho ni ipi? (Kwanza, kutambua kuwa sisi sio matajiri. Tunahitaji dhahabu zaidi.)
2. Dhahabu ambayo lazima “tuinunue” ni ipi? (Soma Wafilipi 3:7-9. Paulo anaandika kuhusu uhusiano uliopo kati ya fedha halisi na thamani ya kumjua Mungu na kuielewa neema. Hii inamaanisha kuwa kumjua Mungu ni dhahabu.)
a. Je, unatambua kuwa kwa kusoma somo hili unachimba dhahabu?
3. Mavazi meupe ya kuvaa ni yapi? (Mfano uliopo kwenye Mathayo 22:1-14 unaonesha kuwa hii ni rejea kuhusu vazi la Yesu la haki ambayo anatupatia.)
4. Marhamu ya macho ni ipi? (Kuelewa kile tunachokijadili. “Utajiri” wetu wa kiroho ni umaskini wa kupindukia machoni pa Mungu. Badala yake, tunatakiwa “kununua” dhahabu ya kumwelewa Yesu kutoka kwake, ambayo itafunua macho yetu ili kuelewa kuhesabiwa haki kwa imani – haki ya Yesu ambayo tunapewa kama zawadi ya bure.)
E. Soma Ufunuo 3:19. Tutarajie nini ikiwa hatuielewi neema barabara? (Yesu anasema kuwa atatuonya. Ikiwa tunagundua kwamba mitazamo yetu juu ya neema inabadilika, hii inaweza kuakisi maonyo. Huenda maisha hayaendi vizuri na hii inaakisi “kuturudi” ili kuyaelekeza mawazo yetu kwake. Lengo ni kuielewa neema kwa usahihi. Tunatakiwa kuwa na bidii na kutubu.)
1. Utaona kwamba fungu halizungumzii chochote kuhusu “neema,” bali linasema kuwa ikiwa anatupenda basi tunaweza kutarajia karipio na kuturudi. Je, upendo ni kichocheo cha karipio, na si kushindwa kuielewa neema? (Huwakemei watoto wako kwa kuwa tu unawapenda. Unawakemea wanapotenda jambo hatarishi. Upendo sio kichocheo, kufuata njia isiyo sahihi ndio kichocheo.)
F. Soma Ufunuo 3:20. Tunapata hamasa gani kutoka kwenye hili fungu? (Yesu anatufuatilia (anaandamana nasi) katika jambo hili, na wala si vinginevyo. Hatuna haja ya kusumbuka (kuteseka) kuhusu kama tunaielewa neema kwa usahihi, ikiwa tunabidii na “kuufungua mlango” Yesu ataingia ndani na kutuletea nuru.)
1. Angalia vipengele vya kuipata neema: 1) Yesu anamjia kila mmoja wetu. Hatatulazimisha, bali atabisha mlango. 2) Tunaitwa tu kusikiliza na kufungua mioyo yetu na akili zetu kwake. 3) Atakuwa sehemu ya maisha yetu. Atajifunua kwetu nasi tutamjua.
G. Soma Ufunuo 3:21-22. “Faida” za kumruhusu Yesu kuingia maishani mwetu ni zipi? (Tutakuwa na uwezo wa kukaa na Yesu katika kiti chake cha enzi!)
H. Rafiki, je, umeridhika na hali yako ya kiroho ya sasa? Je, uko makini na Yesu “kubisha” mlangoni pako? Kama sivyo, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu sasa hivi, ili akusaidie umfungulie Yesu mlango ili uweze “kununua” “dhahabu yake,” “mavazi yake meupe,” na “marhamu yake ya macho?”
III. Juma Lijalo: Ukombozi.