Injili Yapelekwa Thesalonike
(1 Wathesalonike 2, Matendo 16 & 17)
Swahili
Year:
2012
Quarter:
3
Lesson Number:
1
Utangulizi: Je, unachukuliaje/unafanyaje pale mtu anapokupa wazo jipya? Vipi kuhusu mtu anapokupendekezea kuwa unahitajika kufanya mabadiliko maishani mwako? Vipi kama mtu akikuonya kuhusu jambo fulani baya la siku zijazo kama usipobadilika? Tunaanza somo letu la Wathesalonike wa Kwanza na wa Pili: Barua za Paulo kwa waumini wa Thesalonike. Katika hizi barua Paulo analeta ujumbe ambao anadhani kuwa hawatauamini. Mwanasheria anapotaka kuthibitisha ukweli unaosemwa na shahidi, huwa anauliza maswali yanayohusu utambuzi na motisha. Paulo, huku akionekana kuwa kama mwanasheria, anatoa hoja kwa nini Wathesalonike wanapaswa kumwamini. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!
- Nia
- Soma 1 Wathesalonike 1:1. Nani anayeandika hii barua kwa kanisa la Wathesalonike? (Paulo, Silwano na Timotheo. Katika mfululizo wa somo hili, nitawarejea wote kwa pamoja kama “Paulo.”)
- Soma 1 Wathesalonike 2:1-4. Je, Paulo anajihusisha na jambo gani? (Kwamba washiriki wa kanisa watakuwa na mashaka naye.)
- Je, Paulo anaibua mambo gani? (Kwamba ujumbe wake ni wa uongo au nia yake ni chafu. Anasema kuwa hana nia ya kuwafanyia mambo ya ujanja ujanja (kuwadanganya).)
- Kwa nini Paulo anaandika jambo la aina hii? (Lazima iwe kwamba baadhi ya watu walikuwa wanahoji nia ya Paulo na usahihi wa teolojia yake. Utetezi wake unatuonyesha asili (aina) ya mashambulizi yaliyofanywa dhidi yake.)
- Hebu turejee kwenye maswali niliyoyauliza kwenye utangulizi: mtu anapojaribu kukushawishi ili ukubaliane naye, je, unakubaliana na nia (mtazamo) yake? (Ninakubaliana – hususan kama simfahamu mtu huyo vizuri. Lakini, hii inawezekana ni matokeo ya mafunzo yangu ya sheria.)
- Tafakari kuhusu jambo hili kidogo. Sote tunawafahamu watu ambao huwa wanakosea kwa sababu sio werevu sana, hisia zao zinazidi uwezo wao wa mantiki, au hawana elimu kuhusu masuala mbalimbali. Je, unawalinganishaje watu wa aina hiyo na wale wanaojaribu kukudanganya? (Tuna mawazo machache ya watu wenye mambo ya ujanjaujanja! Watu wengine wanakuwa wamekosea tu, lakini wadanganyaji ni waovu.)
- Je, Paulo anasema nini kuhusu nia yake? (Nia yake ni kumtii Mungu.)
- Nia Zimebainishwa
- Soma tena 1 Wathesalonike 2:2. Paulo anarejea tukio lililotokea Filipi. Kwa nini? (Hii ni sehemu ya hoja ya Paulo kuhusu nia yake. Hebu tuchimbue zaidi kilichotokea kule Filipi.)
- Soma Matendo 16:9-10. Je, hapa Paulo anafuata maelekezo ya nani? (Anaamini kuwa Mungu anawaelekeza waende Makedonia.)
- Soma Matendo 16:11-12. Je, hii inaingilianaje na maelekezo ya Mungu? (Filipi ni mji mkuu katika jimbo la Makedonia.)
- Soma Matendo 16:13-15. Kama wewe ungekuwa Paulo, je, hii ingekuthibitishia maelekezo ya Mungu kwamba uende Makedonia? (Unakutana na watu sahihi na wanajitolea kukaa na wewe kwao. Kila kitu kinakwenda barabara!)
- Soma Matendo 16:16-18. Unawezaje kuelezea kuwa pepo liliweza kutoa ujumbe huu? Je, hatukujifunza robo iliyopita kwamba tunaweza kutambua pepo kwa ujumbe wao?
- Je, unadhani ni kwa nini alisumbuliwa? Je, kelele zile zilikuwa za kila siku? Je, inawezekana kwamba pepo lilikuwa linashughulikia/linatawala hadhara/habari zao?
- Soma Matendo 16:19-23. Je, ni haki gani waliyotendewa kule Filipi?
- Kama wewe ungekuwa Paulo, je, ungeanza kutilia mashaka maono yako?
- Je, Paulo amefanya jambo lolote baya?
- Soma Matendo 16:24-28. Chukulia kwamba wewe ni Paulo, hiki ni kisa chako na unaandika kwenye ukurasa wako wa Facebook kilichokutokea siku mbili zilizopita. Je, aina yako ya sauti (ya kiandishi) itakuwaje? (Janga moja baada ya jingine! Kwanza manyanyaso, kisha kupingwa kusiko kuwa kwa haki, halafu kutupwa jela, na kisha tetemeko la nchi. Kama rafiki yeyote atabofya kitufe cha “like,” utajisikia kumfutilia mbali.)
- Soma Matendo 16:29-34. Je, sasa unasemaje kuhusu maono? Je, hii inabadilishaje andiko lako kwenye ukurasa wako wa Facebook?
- Soma Matendo 16:37-40. Taarifa ya ziada kwa ufupi tu hapa. Je, Paulo aliamini nini kuhusu Wakristo kudai/kutetea haki zao za kisheria?
- Nani anayemtia moyo mtu mwingine? Nani aliyepigwa? (Paulo alipigwa na anafanya utiaji moyo.)
- Soma Matendo 17:1. Fungu hili linaturejesha Thesalonike. Unadhani Paulo alijisikiaje? (Yumkini bado alikuwa anateseka kutokana na yale mapigo!)
- Kama ulikuwa unafahamu maelezo haya, je, ungesema nini kuhusu nia ya Paulo? Je, yeye ni mjanja mjanja (mtu mwenye kona koza za kudanganya watu)? Je, kuna sababu yoyote tunayoweza kusema kwamba anahamasishwa na kitu zaidi ya mapenzi ya Mungu? (Paulo alifahamu kuwa kushiriki injili na watu wengine lilikuwa ni jambo la hatari. Angeweza kudhoofika afya yake au kupoteza uhuru wake.)
- Soma 1 Wathesalonike 2:2. Je, upokeaji wa injili Thesalonike ukoje? (“Upinzani mkali.” Katika huu mji mpya, Paulo alifahamu kuwa alikuwa anakabiliana na hatari.)
- . Ujumbe
- Kwa kuwa tumeona kuwa ana nia safi tu, hebu tuangalie ujumbe wake. Soma Matendo 17:2-3. Je, ujumbe wa Paulo kwa wale waliopo Thesalonike ni upi? (Injili!)
- Kwa nini unadhani Paulo alikwenda kwa Wayahudi kwanza? (Agano la Kale linamtabiri Yesu. Kama waliyaamini maandiko ya kale, basi wanapaswa kumwamini Yesu.)
- Je, Paulo alikuwa anakwenda kanisani siku ya Sabato kwa sababu tu ndipo walipokuwa wakikutana kwenye sinagogi? (Hapana. Fungu linasema kuwa kuabudu siku ya Sabato ilikuwa ni “kawaida” ya Paulo. Ilikuwa ni jambo analolifanya mara kwa mara.)
- Utabaini kuwa Matendo 17:3 inasema kuwa Paulo aliwaelezea kwamba ni kwa nini Yesu atateswa. Soma Yeremia 23:5-8 na Isaya 9:4-7. Je, mafungu haya yanamrejea Yesu? (Ndiyo.)
- Je, unadhani ni Masihi wa aina gani ambaye watu wangempendelea – je, Yule aliyeteswa au Yule aliyeshinda?
- Je, unaweza kuona vizingiti ambavyo Paulo alipaswa kuvishinda? Alikuwa anamhubiri Masihi aliyeuawa na Rumi!
- Pitia Isaya 53 halafu soma Isaya 53:5. Je, Paulo anapaswa kuhoji vipi hoja yake? Je, unadhani alielezeaje taswira hizi za Yesu zenye ukweli unaochanganya akili?
- Soma Matendo 17:4. Je, hawa “Wayunani wenye kumcha Mungu” ni akina nani? (Soma 1 Wathesalonike 1:9. Hawa ni Mataifa “waliomgeukia Mungu kwa kuachana na sanamu.” Baadhi ya maoni yanapendekeza kwamba waliyakubali mafundisho ya Agano la Kale, wakakutana siku ya Sabato na Wayahudi, lakini hawakuwa wamebadilika kikamilifu kwenye dini ya Kiyahudi.)
- Soma Matendo 17:5. Hii inapaswa kuwa inafahamika kwa Paulo. Kwa nini Wayahudi wanaona wivu? (Mambo mawili. Kwanza, Wayahudi yumkini wana matumaini kwamba hawa Wayunani watabadilishwa kikamilifu kuingia kwenye dini ya Kiyahudi. Sasa, Paulo amewashawishi kuhusu jambo jingine. Pili, Paulo anatoa hoja kwamba Agano la Kale lilimtabiri Yesu. Yesu ndio ukamilifu wa huduma ya patakatifu na unabii mwingineo. Wayahudi hawa wanakataa hilo na wanadhani kuwa Paulo anaanzisha dini nyingine inayojiondoa kutoka kwenye dini yao. Tunaweza kuona kwamba ni kwa nini Paulo anajihusisha sana kujua kama watu wanaamini ujumbe wake.)
- Soma Matendo 17:6-8. Wapinzani wa Paulo wanakusanya kundi la watu wabaya (wahuni) na kuanzisha vurugu, na kisha wanaifanya serikali kuwa kwenye upande wao. Je, hii inatufundisha nini kuhusu nguvu ya hoja zao za kidini? (Kukimbilia matumizi ya fujo na mkono mrefu (na imara) wa serikali kunaonyesha kwamba jaribio lako la kutumia ushawishi kupitia mantiki na sababu za msingi kumeshindwa. Wanatumia vitisho na nguvu kulinda maoni/mawazo yao ya kidini.)
- Angalia tena Matendo 17:7. Je, unadhani hawa Wayahudi waliamini nini kuhusu Masihi – mateso au ushindi? (Bila shaka kabisa waliamini kuwa Masihi atakuwa mshindi.)
- Je, hiyo inasema nini kuhusu hoja yao hapa? (Ni yenye hila/ulaghai/udanganyifu kabisa. Walikuwa wanamtuhumu Paulo kwa mambo waliokuwa na matumaini kuwa yangetokea!)
- Rafiki, vipi kuhusu wewe? Je, unaviamini vitabu alivyoviandika Paulo katika Agano Jipya kwa sababu vitabu hivyo ni “sehemu ya Biblia,” au una imani binafsi inayojitegemea kwenye vitabu hivyo kutokana na vile Paulo alivyoteseka kufikisha ujumbe wake kutoka kwa Mungu? Kama huna uhakika kuhusu kweli ya injili, je, utaikubali hivi sasa?
- Kwa kuwa tumeona kuwa ana nia safi tu, hebu tuangalie ujumbe wake. Soma Matendo 17:2-3. Je, ujumbe wa Paulo kwa wale waliopo Thesalonike ni upi? (Injili!)
- Juma Lijalo: Kuyatunza Mahusiano.