Somo la 10: Kanuni za Pambano
Somo la 10: Kanuni za Pambano
(Ufunuo 12, 1 Wakorintho 10, Danieli 10)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2025, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Katika somo la 7 la mfululizo wa masomo haya tulijadili jinsi miti miwili ya bustani ya Edeni na jaribu la Ayubu yalivyokuwa ni mapambano waliyokubaliana kati ya Mungu na Shetani. Walikuwa na “masharti ya pambano.” Hilo linamaanisha nini kwetu? Je, Shetani na malaika wake wapotovu wanaruhusiwa kufungamana nasi moja kwa moja? Ikiwa ndivyo, je, tunalikana jambo hili? Mmojawapo wa marafiki wangu wakubwa katika shule ya sheria alikuwa mhubiri wa Kimethodisti. Ilikuwa ni fuhara kujadiliana naye Biblia. Miongo kadhaa baadaye alisoma jambo fulani nililoliandika kuhusu watu ambao ni maadui wa injili. Nadhani andiko lilo lilitaja neno “ya kishetani.” Alidhani kuwa nimekwenda mbali mno na kuvuka mipaka. Nisingewataja wale wasiokubaliana kama “maadui” au “wa kishetani.” Rafiki wangu huyu wa zamani ni mtu mwerevu sana, na si yeye pekee aliyenipendekezea kuwa na tahadhari. Lakini je, yupo kwenye hali ya ukanaji? Tunapaswa kuuangaliaje upinzani? Juma hili somo letu la Biblia linatupeleka nyuma ya pazia ili kufunua asili halisi ya pambano la ulimwengu mzima. Hebu tuzame kwenye somo letu na tuone kile Biblia inachokifundisha!
- Kutupwa Kutoka Mbinguni
-
- Soma Ufunuo 12:7-8. Unadhani hii ilikuwa vita halisi? (Kwa hakika inaonekana hivyo.)
-
- Soma Ufunuo 12:9. Shetani na malaika wake walioanguka pamoja naye sasa wako wapi? (Duniani pamoja nasi.)
-
- Soma Ufunuo 12:12. Habari mbaya kwetu ni ipi? (Ole! Tunaye Shetani mwenye ghadhabu ambaye anahamasishwa na muda mchache alio nao kwa ajili ya kazi yake.)
-
- Soma Ufunuo 12:17. Nani ambaye ni mlengwa wa kazi ya Shetani na mashetani wake? (Walio kanisani wanaoichukulia Biblia na uhusiano wao na Yesu kwa dhati.)
-
- Je, ni haki kuwaita wapinzani wetu “wa kishetani?”
- Kuelewa Asili Halisi ya Pambano
-
- Soma 1 Wakorintho 10:19-21. Paulo amekuwa akijadili maisha ya Mkristo, na anageukia kwenye mada ya kafara za kipagani kwa mashetani. Paulo anasema kuwa asili ya mashetani ni ipi? (Anasema kuwa mashetani si chochote wala lolote na kwamba kuyatolea kafara si lolote wala chochote.))
-
-
- Kwa nini basi hata Paulo anajadili mada hii? (Kwa sababu suala la msingi ni kushirikiana “na mashetani.”)
-
-
- Hebu tulijadili hili. Kama mpinzani wa injili anatangaza jambo ambalo unajua ni makosa au labda la kipumbavu, je, utangazaji huo ni “wa kishetani?” (Ndiyo. Mtu si shetani (hao ni malaika walioanguka), lakini msimamo wao unatangaza upande wa kishetani wa pambano la ulimwengu mzima.)
- Shindano la Mwereka/Pambano
-
- Soma Waefeso 6:10-12. Hii inatuambia kuwa Wakristo wapo kinyume na nini? (“Nguvu za ulimwengu mzima.” “Majeshi ya pepo wabaya.” Kwa mara nyingine Paulo anataka tujue asili ya hatari ya wapinzani wetu.)
-
-
- Tunawezaje kusimama kinyume na mashetani (malaika walioanguka?) (Soma tena Waefeso 6:10. Tunasimama hodari kwa nguvu za Mungu.)
-
-
- Soma Waefeso 6:17-18. Tunaweza kuchukua hatua gani mahsusi kupambana dhidi ya hao maadui wanaoogofya? (Biblia, Roho Mtakatifu, na maombi.)
- Safari ya Mbinguni (Celestial Travel)
-
- Soma Danieli 10:1-3. Je, Danieli amepokea ujumbe chanya kwenye maono yake? (Hapana. Aliyaelewa maono na yakamfanya aomboleze.)
-
- Soma Danieli 10:4-5. Maono haya yalianza lini? (Yalianza siku ya 24 ya mwezi. Hiyo inamaanisha kuwa kwa zaidi ya majuma matatu Danieli alikuwa anafunga na alikuwa kwenye maombolezo kwa sababu ya ujumbe wa maono. Na baada ya hayo majuma matatu Danieli liona maono mengine.)
-
- Ruka vifungu kadhaa chini hadi Danieli 10:8-11. Tutaruka maudhui ya maono ya pili kwa sababu si mazingatio yetu, lakini Danieli ana mwitiko hasi kwenye maono ya pili pia. Nini kinatokea ili kumtia moyo Danieli? (Mtu “ametumwa” kuzungumza na Danieli kwa sababu “anapendwa sana.”)
-
- Soma Danieli 10:12. Nani anayeyasikia maneno ya Danieli? (Pendekezo ni kwamba Mungu aliyasikia maneno ya Danieli na kumtuma mjumbe wake kutoka mbinguni.)
-
- Ruka vifungu kadhaa chini hadi Danieli 10:18. Hii inatuambia nini kuhusu mjumbe anayemtia nguvu Danieli? (Hakuwa mwanadamu. Lakini alikuwa na “mfano wa mwanadamu.” Mguso wake tu ulikuwa na uwezo wa kumtia nguvu Danieli.)
-
- Sasa hebu tugeukie hii safari ya mjumbe wa kimwujiza kumwona Danieli. Soma Danieli 10:13-14. Mjumbe amecheleweshwa kwa muda gani? (Majuma matatu. Mara moja mbingu zikamtuma mjumbe huyu kwenda kwa Danieli, lakini safari ilicheleweshwa kwa muda wa majuma matatu kwa sababu “mkuu wa ufalme wa Uajemi alimpinga” mjumbe.)
-
-
- Mjumbe huyu wa mbinguni ni nani? (Soma Danieli 9:20-23. Katika sura iliyopita mjumbe anatambulishwa kama malaika Gabrieli. Ingawa Danieli 10 haimtambulishi kwa umahsusi yule anayempelekea Danieli ujumbe, inaleta mantiki kuhitimisha kuwa bado huyu ni Gabrieli.)
-
-
-
- Mkuu wa ufalme wa Uajemi ni nani ambaye “amempinga” Gabrieli kwa muda wa majuma matatu? (Soma tena Danieli 10:1. Hii inatuambia kuwa Koreshi alikuwa Mfalme wa Uajemi.)
-
-
- Hebu turejee kwenye Danieli 10:13. Je, inawezekana kwamba mfalme wa kidunia anaweza kumchelewesha mjumbe wa mbinguni kwenye safari ya kutoka mbinguni ili kumwona Danieli? Je, mwanadamu anaweza kupambana na Gabrieli kwa muda wa majuma matatu? (Jibu kwa maswali yote mawili ni “Hapana.” Rasimu yangu ya awali ya somo hili ilichambua kwa kina vifungu vya Biblia juu ya nani ni mkuu wa ufalme wa Uajemi na nani ni Mikaeli. Hatuna nafasi kwa ajili ya huo mjadala mgumu, hivyo nitanukuu tu hitimisho langu kwamba mfalme wa Uajemi ama ni Shetani au mmojawapo wa maluteni wake wakuu na Mikaeli ama ni Yesu au malaika mkuu.)
-
- Utambulisho wa tabia mbalimbali unatuambia nini kuhusu “kanuni za pambano” linapokuja suala la kumsaidia Danieli mzee? (Unatuambia kuwa mwujiza unahusika sana katika mapambano ya kibinadamu. Kama ilivyo kwetu Danieli alihitaji msaada. Maelezo haya yanaonesha kuwa Shetani ana uwezo wa kuchelewesha msaada unaokwenda kwa wafuasi wa Mungu.)
- Ukomo wa Wanadamu
-
- Soma Ayubu 1:9-12. Katika somo la 7 tulijifunza sehemu hii ya kisa cha Ayubu. Ni nini matokeo ya nguvu ya kimwujiza kwenye maisha ya Ayubu? (Inasikitisha. Na sehemu ya kutisha kabisa ni kwamba Ayubu hafahamu lolote kwamba Shetani ndiye adui wake namba moja. Ayubu anasimama kama shujaa wa Mungu, Shetani anajaribu kumwangusha Ayubu, na Ayubu haelewi “kanuni za pambano.”
-
-
- Mwitiko wa Ayubu ungekuwa na utofauti gani kama angeelewa kuwa Shetani alikuwa akimshambulia kwa sababu ya haki yake? Vipi kama Ayubu angefahamu kuwa alikuwa shujaa wa Mungu katika pambano hili? (Ungebadili kabisa mtazamo wa Ayubu. Angetambua kwamba Shetani ni adui wake, si Mungu. Angekuwa na ujasiri kwenye umuhimu wa dhahiri wa imani ya Mungu kwake.)
-
-
- Soma Marko 6:1-3. Ni nini mtazamo wa watu walioishi katika mji wa nyumbani kwao Yesu? (Si tu kwamba wana mashaka, bali pia wanaona hatia kwa sababu wanaamini kuwa Yesu anadai isivyostahili kuwa na uwezo wa Mungu.)
-
- Soma Marko 6:4-6. Ni kwa kiwango gani mtazamo wa watu wa nyumbani kwao Yesu ulifungamanisha mikono ya Yesu katika kutenda miujiza isiyo ya kawaida?
-
- Kutokuelewa kwa Ayubu na kutokuwa na imani kwa watu wa nyumbani kwao Yesu kunatufundisha nini? (Ni muhimu kuelewa asili ya wachezaji na kanuni za pambano. Kama tunadhani kuwa upinzani ni wa kijinga tu, wapagani ving’ang’anizi, basi hatuelewi kabisa kanuni za pambano.)
-
- Soma Mathayo 5:43-45. Ni kwa jinsi gani basi tunapaswa kuwatendea wale ambao ni mawakala wa mashetani? (Hii ni kanuni nyingine ya msingi ya pambano. Hatuwezi kuyashinda mashetani kwa uwezo wetu. Mungu pekee ndiye ana uwezo huo. Tunapaswa kuonesha upendo wa “neema ya kawaida” (mvua na jua kwa wema na wabaya) kwa maadui wetu, lakini hatupaswi kuamini hata kwa dakika moja kwamba upinzani, sawa na kutoa sadaka, hauna lolote wala chochote. Upinzani si mwepesi.)
-
- Rafiki, je, utaamini kwamba uwezo wa mbinguni unakutegemeza na kwamba mpinzani wako ni Shetani anayetisha na mwenye hasira pamoja na malaika walioanguka pamoja naye? Ukiwa na imani hiyo, basi utalichukulia kwa umakini mkubwa pambano la ulimwengu mzima ambalo sisi ni sehemu yake. Fanya uchaguzi kwa busara!
- Juma lijalo: Ningeweza Kufanya Nini Zaidi?