Somo la 5: Ghadhabu ya Upendo wa Mungu

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Kumbukumbu la Torati 28, Warumi 1, Zaburi 78, Yona 4
Swahili
Year: 
2025
Quarter: 
1
Lesson Number: 
5

Somo la 5: Ghadhabu ya Upendo wa Mungu

(Kumbukumbu la Torati 28, Warumi 1, Zaburi 78, Yona 4)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2025, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, unapendelea dhana ya Mungu anayeonesha ghadhabu? Ninachokiwaza ni kwamba unaipenda dhana hiyo kwa watu fulani, lakini kamwe si kwako binafsi. Mama yangu alipozeeka, aliendelea kuwa na mwili wenye afya lakini hali ya akili yake iliporomoka vibaya. Alipoendelea kuporomoka, kampuni iliyokuwa ikiuza vitamini ilimpigia simu na kumuuzia vitamini nyingi mno ambazo kamwe asingeweza kuzitumia zote. Je, mtu anayewachukulia wazee kama fursa anapaswa kushukiwa kwa ghadhabu? Vipi kuhusu wale wanaowalenga wazee kwa ghasia za kimwili? Kama unawapenda watu wengine, basi unapenda haki. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze kuhusu ghadhabu ya Mungu iliyojengwa juu ya upendo!

  1.    Ghadhabu Inayojiendesha Yenyewe (Automated Wrath)?
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 28:1-6. Baraka hizi zimejengwa juu ya vigezo gani? (Utii kwa Mungu.)
      1.    Unadhani hili linafanyaje kazi? Je, Mungu anapima utii wako na kisha kukupatia baraka kwa kipimo hicho hicho? (Nadhani hili linatokea lenyewe. Mungu aliandaa amri kwa kiasi kikubwa ili kuyaboresha maisha yetu. Tunapofuata sheria za Mungu kwa ajili ya kuishi maisha mazuri, basi kimsingi tunaishi vizuri.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 28:15-19. Hii inaelezea kinyume cha baraka zilizoelezewa katika Kumbukumbu la Torati 28:1-6. Laana hizi zinafanyaje kazi? Je, Mungu anachungulia chini, na kuona kwamba wewe si mtiifu, na kisha anakulaani? Anakudhuru?
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 28:20. Kifungu hiki kinasema kwa umahsusi kuwa Mungu “atapeleka” “laana, mashaka, na kukemewa katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya.” Je, hii inaashiria kuwa adhabu “hazitokei zenyewe” kama nilivyopendekeza? (Zingatia sehemu ya mwisho ya kifungu cha 20, pale inaposema, “kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.” Hii inaashiria kuwa tunayakaribisha matatizo haya.)
    1.    Soma Warumi 1:18. Unadhani ni nini sababu ya ghadhabu ya Mungu “kudhihirishwa” tofauti na kutekelezwa, au neno lolote jingine la kivitendo? (Kudhihirishwa huashiria kuwa hili ni jambo ambalo tunaweza kujionea wenyewe. Ni aina ya udhihirisho wa “hivi ndivyo mambo yanavyotendeka.”)
    1.    Soma Warumi 1:19-23. Ghadhabu ya Mungu inadhihirishwa kwenye jibu gani kwa wadadamu? (Wanakuwa wapumbavu. Fikra yao inapata mkanganyiko. Hilo liliwafanya kutenda mambo ya kipumbavu kama vile kuabudu wanyama.)
      1.    Je, hii ni tafsiri ya moja kwa moja ya ghadhabu ya Mungu? (The IVP New Testament Commentary inataarifu kuwa baadhi ya watu husema, kama nilivyopendekeza, kwamba huu ni mchakato tu wa “chanzo na madhara.” Lakini pia unaukataa mtazamo wa “kujiendesha wenyewe (automatic)” kwa msingi wa kwamba ghadhabu ya Mungu ni pana sana kiasi kwamba hairuhusu tafsiri hii. Ninaamini IVP Commentary inaziangalia dhambi zilizoorodheshwa katika Warumi 1:28-31.)
    1.    Soma Warumi 1:24-25. Je, hii inaonekana kama Mungu anatekeleza ghadhabu kwa wadhambi hawa? (Kitabu cha Warumi kinasema kuwa Mungu “aliwaacha.” Waliiendea ghadhabu ya Mungu wenyewe.)
    1.    Zaburi 78 ni simulizi ya uzoefu wa watu wa Mungu katika safari ya wana wa Israeli kutoka Misri kuelekea Nchi ya Ahadi. Soma Zaburi 78:18-22. Jambo gani limeamsha ghadhabu ya Mungu? (Watu walikuwa na mashaka kama Mungu angeweza kuwalisha, na walitoa madai kwamba Mungu awape chakula.)
    1.    Soma Zaburi 78:23-31. Je, hii inaonekana kama adhabu ya moja kwa moja (automated)? Je, wangeweza kuteseka kutokana na kutokuwa na mazoea ya kula nyama?
    1.    Soma Hesabu 21:5-6. Watu wana malalamiko yale yale kuhusu chakula, na safari hii nyoka wanawashambulia. Je, hili linaonekana kuwa jibu la moja kwa moja? (Hapana. Ingawa kufa kutokana na kula nyama linaweza kuwa jambo lenye kuzua mjadala, vifungu hivi vinatuambia kuwa Mungu “akatuma” nyoka. Kung’atwa na nyoka si matokeo yenye mantiki ya malalamiko kuhusu chakula chako.)
      1.    Vifungu hivi vinatufundisha nini kuhusu ghadhabu ya Mungu? (Sehemu ya ghadhabu hiyo ni matokeo ya asili ya kutotii kanuni za maisha. Hata hivyo, Mungu anaweza na amechukua hatua kutokana na ghadhabu yake na kuwaadhibu waasi.)
    1.    Hebu tutafakari ujumbe wa jumla wa vifungu tulivyojifunza. Je, Mungu anawapenda watu wake? (Ndiyo! Alitoa amri zake ili maisha yetu yawe mazuri. Anataka tuwe na afya nyema.)
  1.   Ghadhabu ya Yona
    1.    Soma 2 Wafalme 14:23-25. Huu ndio utangulizi wetu kwa nabii Yona. Unadhani Yona alikuwa na umaarufu kiasi gani miongoni mwa watu? (Yona alitabiri ushindi uliorejesha mpaka wa Israeli! Lazima itakuwa alikuwa shujaa wa taifa.)
      1.    Je, mfalme ambaye Yona alifanya naye kazi alikuwa mtu mwema?  (Hapana. Alitenda maovu machoni pa Mungu.)
    1.    Soma Yona 1:1-2. Unadhani kwamba Yona atalifurahia jukumu hili? (Yona alikuwa shujaa kwa kutabiri ushindi wa watu wake. Hakuwa na mazoea ya kuwa nabii kwa wapagani, na inawezekana aliogopa kwenda Ninawi.)
    1.    Soma Yona 1:3. Yona alijaribu kuikimbia amri ya Mungu ya kufanya kazi na Mungu kuhusiana na watu wa Ninawi. Je, unafahamu ni watu wa namna gani walioishi Ninawi? (Ninawi ulikuwa mji mkuu wa Ashuru. Walikuwa watu wabaya sana. Waliwaua maadui wao kwa namna za kutisha.)
    1.    Tutaelezea kwa ufupi sehemu kuu ya kisa hiki. Mungu anamrejesha Yona kwenye msitari, Yona anawaonya watu wa Ninawi juu ya maangamizi yanayokuja, na wanatubu. Soma Yona 3:10. Je, hapa utasema kuwa haya ni matokeo makubwa ya utume wa Yona?
    1.    Soma Yona 4:1-2. Kwa nini Yona anakasirika kwa sababu Mungu ameghairi ghadhabu yake kwa watu walioishi Ninawi? (Watu wa Ninawi walikuwa maadui wa Israeli na Yona alitaka waangamizwe. Yona anafanana na sisi. Anafurahia pale “haki” inapotendeka ili kuwashinda maadui wa watu wake, lakini hafurahii pale Mungu anapoonesha rehema kwa watu wabaya.)
    1.    Soma Yona 4:3. Kwa nini Yona akasirike kiasi hicho? (Yona alizoea kuwa nabii wa kweli. Wakati maadui wa watu wa Mungu walipotabiriwa kwa usahihi na Yona kwamba wataangamizwa alishangiliwa. Sasa anaonekana kuwa na kile ambacho ni unabii uliofeli dhidi ya watu wabaya.)
    1.    Soma Yona 4:4. Je, Mungu anashangazwa na mwitiko (reaction) wa Yona?
    1.    Soma Yona 4:5-6. Je, bado Yona anatarajia kuangamizwa kwa watu wa Ninawi?
      1.    Je, unadhani mti huu wa kustaajabisha uliotoa kivuli ulikuwa na athari kwenye fikra ya Yona kuhusu watu wa Ninawi? (Ninatarajia Yona alidhani huu ulikuwa ni upendeleo mdogo kutoka kwa Mungu kuonesha kwamba Mungu bado alikuwa anamfanya kuwa nabii wa kweli. Katika zama za leo tutaliita hili “kupepesa kwa Mungu.”)
    1.    Soma Yona 4:7-9. Jambo gani sasa limemkasirisha Yona? (Mti wake wa kivuli umekufa.)
      1.    Je, afya ya akili ya Yona inaonekana kuwa na mushkeli?
    1.    Soma Yona 4:10-11. Hii inatufundisha nini kuhusu upendo na haki ya Mungu tofauti na upendo na haki ya mwanadamu?
      1.    Kasoro mahsusi ya tabia ya Yona ni ipi? (Ni mbinafsi. Anataka Mungu amwoneshe upendo yeye pamoja na mti wake. Anataka Mungu aoneshe ghadhabu, si upendo, kwa watu wa Ninawi.)
      1.    Je, Mungu anawapenda wanyama?
      1.    Mungu anamaanisha nini pale anapowarejelea wale “wasioweza kupambanua katika mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto?” (Nadhani hii inawarejelea watoto wadogo. Inaweza kumaanisha wale wasioelewa kanuni za kimaadili.)
    1.    Hebu tutafakari kidogo kuhusu kisa cha Yona. Je, Mungu alikuwa radhi kuiangamiza Ninawi?
      1.    Je, hiyo ingekuwa adhabu ya “moja kwa moja (automatic)”? (Hapana. Mungu angetekeleza adhabu. Tuna uhakika na hili kwa sababu Mungu alitoa uamuzi dhidi ya uangamivu.)
        1.    Je, hiyo ingekuwa haki? (Ndiyo, walikuwa watu wabaya kiasi cha kutisha.)
        1.    Je, kuangamizwa kwa mji mkuu wa Ashuru kungeonesha upendo kwa wengine? (Mungu angepunguza hofu waliyoileta kwa wengine.)
      1.    Je, Mungu angekuwa tayari kuwaangamiza watoto endapo Ninawi isingetubu? (Matendo yetu maovu yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa watu wengine, wakiwemo watoto wetu.)
  1.      Jambo la Kushangaza
    1.    Soma Maombolezo 3:31-33. Ni nini mtazamo wa Mungu dhidi ya uangamivu? (“Hautoki moyoni mwake.” Haufurahii. Ezekieli 33:11.)
    1.    Soma Isaya 28:21-22. Kazi ya “ajabu” ya Mungu ni ipi? (Uangamivu. Mungu anaangamiza pale tu watu wasipotubu. Ni tamaa yake kwamba watu wote wamgeukie yeye.)
    1.    Rafiki, tunafahamu kwamba dhambi na wadhambi lazima vifikie ukomo. Haitakuwa upendo kuuruhusu ulimwengu kuendelea jinsi ulivyo. Tunatakiwa kukubali kwamba uangamivu utatujia endapo hatutaipokea karama ya bure ya Yesu ya uzima wa milele. Je, utamgeukia Yesu na kuipokea karama yake sasa hivi?
  1.   Juma lijalo: Upendo wa Mungu wa Haki.