Somo la 1: Ishara Zinazoonesha Njia
Somo la 1: Ishara Zinazoonesha Njia
(Yohana 2, 4 & 5)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Tunaanza mfululizo mpya wa masomo juu ya Injili ya Yohana! Tovuti ya GoBible.org ina somo juu ya Injili ya Yohana nililoliandika miaka ishirini iliyopita. Somo letu katika robo hii liko tofauti. Badala ya kwenda na sura kwa sura, tutajifunza mada zilizopo katika injili ya Yohana. Kwa nini tufanye hivyo? Katika Yohana 20:30-31 Yohana anaelezea kwa nini alijumuisha katika kitabu chake baadhi ya mambo tu. Lengo lake ni kumtia moyo msomaji kuamini kwamba Yesu ni “Mwana wa Mungu,” Masihi, ili kwamba kwa kuamini haya msomaji aweze “kuwa na uzima kwa jina lake.” Katika somo hili la kwanza tunazingatia “ishara,” miujiza inayotuelekeza kwenye hitimisho kwamba Yesu ni Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu!
- Muujiza Harusini
-
- Soma Yohana 2:1-3. Je, mamaye Yesu anateta na Yesu? Je, anamwambia kuwa wazazi wa watoto wanaooana hawajajiandaa vizuri au ni maskini sana?
-
- Soma Yohana 2:4. Mazungumzo haya baina ya Yesu na mamaye yanaashiria kuwa ni ipi sababu ya mama kumwambia Yesu kuhusu tatizo la divai? (Anaamini kuwa Yesu anaweza kutatua tatizo. Yesu anaelewa kwa uhakika kile ambacho mamaye anakitaka. Jibu lake ni kwamba kazi yake haijafikia hatua ambapo anapaswa kutenda miujiza.)
-
- Soma Yohana 2:5-7. Nani anayeongoza mambo hapa? (Kwa dhahiri mamaye Yesu yuko juu ya anachokifikiria Yesu kuhusu suala la muda wa matukio.)
-
-
- Je, kuna lolote la kujifunza kwetu katika hili? (Wazazi wako wa kimungu wanapaswa kuheshimiwa. Hii pia inaonesha kuwa Yesu anayasikiliza mahitaji ya wanadamu.)
-
-
-
- Kwa nini mamaye Yesu ajali? Yeye si mzazi wa maharusi.
-
-
- Soma Yohana 2:7-9. Yesu amebadili kati ya galoni 120 na 180 za maji kuwa divai. Mada iliyopo hapa ni ipi? Tunajifunza ishara gani kuhusu Yesu kama Mungu? (Muujiza huu hauna maana kabisa isipokuwa tu kama upendo kwa wazazi wako, upendo kwa wengine, na kuwasaidia wengine kuepuka fedheha ndio mambo ya muhimu maishani.)
-
- Huu ni muujiza wa kwanza wa Yesu. Soma kuhusu mwingine wa kwanza katika kitabu cha Kutoka 7:14-17. Hili ni pigo la kwanza juu ya Misri. Jambo gani linadhihirishwa kwa Farao kwa kugeuza maji kuwa damu? (Kifungu cha 17 kinabainisha kwamba atajua Mungu ni nani.)
-
-
- Je, Yesu anatudhihirishia kwamba yeye ni Mungu kwa muujiza harusini?
-
-
- Soma Yohana 2:10. Kwa nini Yohana anajumuisha tathmini hii ya divai? (Mungu anafanya kila kitu kwa ubora, nasi tunapaswa kufanya vivyo hivyo.)
-
-
- Mara ngapi umeona wasilisho la Sabato linaloonekana kama limetupwa katika dakika za mwisho?
-
-
- Soma Yohana 2:11-12. Yohana anatuambia kuwa athari halisi ya muujiza wa kwanza wa Yesu ni ipi? (Wanafunzi wa Yesu “wakamwamini.” Yesu alidhihirisha “utukufu wake.”)
- Muujiza wa Uponyaji
-
- Soma Yohana 4:46-47. Habari za muujiza harusini zilisambaa. Je, hili ni gumu zaidi kuliko kubadili maji kuwa divai?
-
- Soma Yohana 4:48. Kwa nini Yesu aseme jambo kama hili? Kwani baba hakumwendea Yesu kwa ajili ya uponyaji? (Yesu anazungumzia juu ya mojawapo ya mada za kitabu cha Yohana. Imani inayoongelewa ni endapo Yesu ni Masihi. Baba huyu anamjia Yesu kwa ajili ya uponyaji, si kama mfuasi wa Yesu.)
-
-
- Je, kuna mtu aliyekuomba utende jambo si kwa sababu wewe ni rafiki yake, bali kwa sababu una kitu anachokitaka? (Miongo kadhaa iliyopita, ilikuwa ghali sana kupiga simu umbali mrefu. “Marafiki” ambao kamwe hawakupiga simu ili kuzungumza tu, waliniachia ujumbe wa sauti wakiniomba niwapigie simu wakiwa mbali sana ili niwapatie ushauri wa kisheria bure. Nadhani hili ni suala la motisha ambalo Yesu analiibua.)
-
-
- Soma Yohana 4:49-50. Je, Yesu ametenda zaidi ya alichokiomba yule baba? (Yesu anaonesha kuwa hana haja ya kumwona kijana ili kumponya. Yesu ananena tu neno la uponyaji.)
-
- Soma Yohana 4:51-53. Yohana anataka tuhitimishe nini?
-
-
- Jambo gani lilimhamasisha Yesu kutenda muujiza huu? (Kwa mara nyingine, Yesu anaonesha huruma kwa mtu ambaye bado si muumini. Muujiza uliiongoa nyumba yote ya baba yule)
-
-
- Soma Yohana 4:54. Yohana anaporejelea hii “ishara ya pili,” hii ni ishara ya nini? (Kimantiki kauli hii inahusiana na mjadala wetu wa uponyaji wa kijana. “Ishara” si kwamba Yesu ni mponyaji, bali kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.)
- Muujiza Birikani (Kisimani)
-
- Soma Yohana 5:1-3. Jaribu kutafakari kuwa mahala hapa. Kwa mujibu wa Maoni ya Matumizi Maishani (the Life Application Commentary) uchunguzi unabainisha kuwa palikuwepo na mabirika mawili na matao matano. Hapa panaonekana kama mahali pazuri, lakini taswira niliyo nayo ni kama bustani ya kisasa yenye watu wasio na makaazi waliotapakaa mahali kote bustanini. Wewe unapaonaje? (Yohana 5:4 haipo katika nakala halisi (original). Mtu aliyenakili kitabu cha Yohana alitaka msomaji ajue kwa nini wagonjwa wote hawa walikusanyika hapa – palikuwepo na imani kwamba wangeweza kuponywa maji yalipotibuka.)
-
- Soma Yohana 5:5-6. Kwa nini Yesu aliuliza swali hili? Kwani hapa jibu si la dhahiri? (Yesu hajilazimishi kwetu.)
-
- Soma Yohana 5:7. Je, hili ni jibu kwa swali la Yesu? (Hapana. Yesu hakumuuliza kitu gani kilimzuia kuingia kwenye maji wa kwanza. Mgonjwa alimpa Yesu jibu la kiuhalisia. Ilichukuliwa kwamba alitaka kuponywa, lakini akaelezea vikwazo vya kuupata uponyaji huo.)
-
- Soma Yohana 5:8-9. Je, mtu huyu alikuwa na imani yoyote kwa Yesu kabla Yesu hajamwambia “Simama?” (Hakujua chochote kumhusu Yesu vinginevyo asingezungumzia matatizo halisi kivitendo.)
-
-
- Je, mtu yule alionesha imani? (Ndiyo. Alijaribu kusimama – na akaweza.)
-
-
-
- Je, Yesu angeweza kumponya kila mtu kwenye mabirika haya? (Jibu ni “ndiyo.”)
-
-
-
-
- Kwa nini Yesu hakuwaponya wote?
-
-
-
- Soma Isaya 35:4-6. Kwa nini Yesu amemponya mtu huyu? (Kuonesha kwamba anatimiza angalao unabii mmoja wa Kimasihi. Yeye ni Mwana wa Mungu.)
-
-
- Sasa swali gumu. Je, hii ndio sababu Yesu hakumponya kila mtu? (Yesu anaponya kwa ajili ya utukufu wake. Angalia Yohana 9:1-3.)
-
-
-
- Je, hii ndio sababu pekee ya Yesu kuponya? (Kubadili maji kuwa divai hakuendani na taswira hiyo. Yesu anawahurumia watu.)
-
-
- Soma Yohana 5:10-11. Je, mgonjwa huyu wa zamani ni mtu asiye na shukrani? Sasa anamlaumu Yesu? (Haiyumkiniki. Kama aliweza kumponya mtu yule baada ya miaka 38 ya kuugua, basi mtu huyo alikuwa na mamlaka.)
-
-
- Yesu alijua kuwa kumwambia mtu yule kubeba godoro lake siku ya Sabato kungesababisha tatizo. Kwa nini alifanya hivyo? (Siku za mtu yule kuwa mgonjwa zilikuwa zimekwisha. Amri ya Yesu ilifutilia mbali historia yake ya ugonjwa.)
-
-
- Soma Yohana 5:12-15. Je, mgonjwa huyu wa zamani sasa anajaribu kumwingiza Yesu kwenye matatizo? (Mgonjwa huyu wa zamani alidhani kuwa walipaswa kujua habari za Yesu. Na kwa kuongezea, hii inaonesha kuwa mgonjwa huyu wa zamani alikuwa mwaminifu kabisa. Alipoweza kuwaambia viongozi ni nani aliyemponya, alifanya hivyo.)
-
- Angalia tena Yohana 5:14. Hebu subiri kidogo! Kwani Yesu hakumfanya atende dhambi kwa kubeba godoro lake siku ya Sabato? (Kwa dhahiri Yesu hakukichukulia kitendo hicho kuwa ni dhambi.)
-
-
- Je, Yesu anatufundisha kuwa dhambi husababisha ugonjwa? (Hebu tupitie tena Yohana 9:1-3. Kwenye suala la kipofu Yesu hahusianishi ugonjwa na dhambi. Tena ikizingatiwa kwamba, alikuwa kipofu tangu kuzaliwa. Lakini tunatakiwa kuwa wakweli kwamba watu wengi ni wagonjwa kutokana na dhambi zao.)
-
-
- Soma Yohana 5:16-18. Jiweke kwenye nafasi ya viongozi wa Kiyahudi. Je, ungetaka kumwua mtu kwa kuivunja Sabato ambaye alikuwa na uwezo wa kuponya?
- Miujiza na Ishara za Uungu
-
- Soma Yohana 5:19-21. Yesu anatoa madai gani? (Anasema kuwa yeye ni Mwana wa Mungu na kwamba ana uwezo wa kuwafufua wafu.)
-
-
- Kwa mara nyingine, hebu jiweke kwenye nafasi ya viongozi wa Kiyahudi. Je, kauli hii ingekusababisha utafakari upya kutaka kumwua Yesu? (Kwa hakika, kuna jambo la pekee sana linaendelea hapa. Mtu mwenye akili ya kawaida angezichukulia kauli za Yesu kwa umakini mkubwa.)
-
-
- Soma Yohana 5:22-23. Je, hili ni onyo kwa viongozi wa Kiyahudi? (Wanamhukumu Yesu. Hukumu yao ni kwamba Yesu anastahili kifo. Yesu anaonya kwamba yeye ndiye atakayetekeleza hukumu.)
-
- Soma Yohana 5:24. Yesu anatupatia ahadi gani katika muktadha wa kumponya mtu aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka 38? (Ana nguvu ya uzima. Tukiamini kwamba Mungu alimtuma Yesu hatutateseka na hukumu. Badala yake, tutavuka kutoka mautini na kuingia uzimani.)
-
- Rafiki, je, ungependa, sasa hivi, kuvuka kutoka katika mauti ya milele na kuingia katika uzima wa milele? Unaweza kufanya hivyo kwa kuamini kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu aliyetumwa na Mungu kuja kutuokoa kutoka kwenye mauti ya milele.
- Juma lijalo: Ishara za Uungu.