Somo la 8: Kuwafundisha Wanafunzi: Sehemu ya II
Somo la 8: Kuwafundisha Wanafunzi: Sehemu ya II
(Marko 10)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, umewahi kumsikiliza mwalimu wa Biblia na kudhani, “Hilo halina mantiki yoyote, huo ni uongo!” Mojawapo ya sehemu ya kuwa wazi kwa ajili ya kumpokea Roho Mtakatifu ni kuwa radhi kuyakubali na kuyapokea mafundisho ya Biblia. Mara nyingi tatizo ni suala la “mfano” ambalo tumelijadili katika siku za hivi karibuni. Mara nyingi Yesu anafundisha kwa namna ambazo ni ngumu kuzielewa isipokuwa tu kama utatenga muda wa kusoma na kujifunza kile ambacho hasa anakisema. Juma hili tunayaangalia mafundisho mawili ya Yesu yaliyowafanya wanafunzi wake kimsingi kusema, “Utakuwa unaleta utani. Hilo lawezaje kuwa kweli?” Hebu tuzame kwenye mafundisho haya yenye utata na tuone kile tunachoweza kujifunza!
- Ndoa
-
- Soma Marko 10:1-2. Kwa nini Mafarisayo wanauliza swali kama hilo? Mara zote walikuwa “wakimjaribu,” lakini jaribu halionekani dhahiri kwenye swali. (The IVP New Testament Commentary inabainisha kuwa Yesu yupo mahali ambapo Yohana Mbatizaji alihubiri. Yohana alimshutumu Herode Antipa kwa kumwoa mke wa ndugu yake na matokeo yake yalikuwa ni kwa Yohana kukatwa kichwa. Viongozi wa Kiyahudi walitamani hatima hiyo hiyo kwa Yesu.)
-
- Soma Marko 10:3-4. Je, hili ni jibu litakalomwacha Yesu salama? (Yesu anawauliza tu alichokisema Musa kwenye mada inayohusika.)
-
- Soma Marko 10:5-9. Je, mtego umemkamata Yesu? (Kwa dhahiri hajaribu kuepuka kumchukiza Herode antipa.)
-
-
- Hebu tuangalie kwa kina zaidi anachokisema Yesu. Rejea ya alichokisema Musa kwenye mada hii inapatikana katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 24:1-4. Je, Musa amevuviwa na Roho Mtakatifu kuyaandika haya? Je, hii ni sehemu ya Biblia? (Jibu kwa maswali yote hayo mawili ni “Ndiyo.” Musa anamnukuu “Bwana” kama mamlaka ya kile anachokisema.)
-
-
-
-
- Kifungu cha tano kinatufundisha kanuni gani kuhusu talaka? (Mungu anazingatia asili yetu ya dhambi. Jambo hili linapaswa kuwa faraja kwa watu wengi ambao wametalikiana.)
-
-
-
-
- Je, Yesu anabadili sheria? (Yesu anapofundishwa kwamba “Wawili hao watakuwa mwili mmoja” ndio kanuni ya asili na kimsingi anairejelea tu.)
-
-
- Soma Marko 10:10-12. Je, Yesu ameamua kuachana na uhuru kwa ajili ya ugumu ya mioyo ya wanadamu?
-
-
- Utaona kwamba anashughulikia mazingira ambayo mwanamke anatafuta kumtaliki mumewe, jambo ambalo Musa halitafakari. Kwa nini anafanya hivyo?
-
-
- Soma Mathayo 19:10. Marko hakuandika juu ya huu mwitiko (reaction) wa kufurahisha wa wanafunzi. Je, unakubaliana nao kwamba ikiwa ndoa ipo kwa ajili ya maisha yote ya mwanadamu, ni bora kukaa bila kuoa/kuolewa?
-
- Soma Mathayo 19:11-12. Kwa nini sasa Yesu anawazungumzia matowashi? Je, hii ni mada mpya? (Hapana. Mitazamo yetu ya kisasa inatufanya tusielewe kikamilifu kile kinachosemwa. Wanafunzi na Yesu wanazungumzia juu ya kuwa waseja. Hawazungumzii juu ya kulala na watu wengine tofauti na kwenye ndoa)
-
-
- Angalia kauli ya mwisho ya kifungu cha 12. Inamaanisha nini? Kama sitaki “kupokea” maelekezo haya, je, nina uchaguzi huo? (Maoni yote ambayo nimeyapitia yanamwelewa Yesu akisema kuwa si kila mtu ana uwezo wa kuwa mseja. Hao wanapaswa kuoa/kuolewa.)
-
-
-
- Tukiangalia nyuma katika Marko 10:5 tunamwona Mungu akiweka uhuru kwenye sheria. Je, hicho ndicho tunachokiona katika sehemu ya mwisho ya Mathayo 19:12?
-
- Mali
-
- Soma Marko 10:17-18. Kwa nini Yesu anamtia changamoto mtu anayemuita “mwema?” (Yesu anataka kijana huyu mdogo atafakari kama Yesu ni Mungu.)
-
- Soma Marko 10:19. Kama unaamini kuhesabiwa haki kwa imani pekee, Yesu anatoa jibu la kutisha kwenye swali la jinsi ya kwenda mbinguni. Je, unaweza kufafanua jibu la Yesu?
-
- Soma Marko 10:20-21. Hebu subiri kidogo! Hili ni kosa. Hakuna hata amri moja kati ya Amri Kumi inayotutaka kuuza “ulivyo navyo vyote” na kuwapa maskini. Je, kuna mtu ambaye angependa kutetea nyongeza ya Yesu kwenye Amri Kumi? (Maoni ya E.W. Bullinger yanasema kuwa hii ni Amri ya Kumi, lakini kwa dhahiri hilo si kweli. Kijana huyu alikuwa tajiri. Hakuwa, kwa mujibu wa taarifa tulizopewa, akitamani chochote alichokuwa nacho mtu mwingine.)
-
- Hebu turukie mbele na tusome Marko 12:30-31 ili tuone anachokisema Yesu kuhusu kushiriki vitu vyetu na wengine. Yesu anafundisha nini kuhusu Amri Kumi na kuwasaidia wengine? (Anafundisha kuwa tunapaswa kuwapenda majirani wetu kama tunavyojipenda wenyewe. Kumpatia jirani yangu mali yangu yote kunanifanya nimpende kuliko ninavyojipenda mwenyewe. Fundisho jingine la Biblia juu ya mali ni utoaji wa zaka – ambapo ninapata fursa ya kusalia na 90%. Angalia Malaki 3:10.)
-
- Soma Marko 10:22-26. Kwa mara nyingine tunaona kuwa wanafunzi wanastaajabishwa na kushangazwa. Je wanapaswa kushangaa? (Sababu ya kustaajabu kwao sio ngumu kuijua. Kwenye vifungu kama vile Kumbukumbu la Torati 28 Biblia inafundisha kuwa utii kwa Mungu huleta utajiri na kutokutii huleta umaskini. Kuwa tajiri ni ishara ya Kibiblia ya utiifu.)
-
- Soma Marko 10:27. Matajiri wanaokolewaje? (Kwa njia ile ile ambayo kila mmoja anaokolewa kwayo – Mungu anafanya yasiyowezekana yawezekane kwa njia ya maisha, kifo, na kufufuka kwa Yesu kwa ajili yetu.)
-
-
- Je, unakumbuka mjadala wetu katika majuma machache yaliyopita kuhusu mifano na kufuatilia kwa kina fundisho la Yesu? Unaona jinsi ambavyo pale tunapochunguza kwa kina kile kinachoonekana kuwa ni ushauri wa kutisha kutoka kwa Yesu tunaupata ukweli?
-
-
- Hebu tupitie tena Marko 10:25. Je, unaweza kulifafanua hili kutokana na kile ambacho tumekibaini hivi punde? (Tatizo la kuwa tajiri ni kutumaini mali yako badala ya kumtumaini Mungu. Hili ndilo tatizo lile lile kama la kutumaini katika kuzishika Amri Kumi kwa ajili ya wokovu wako. Mungu pekee ndiye mkamilifu, sisi sio wakamilifu. Hatuwezi kuyatumainia matendo yetu, mafanikio yetu, au utajiri wetu, ili kuingia mbinguni. Tunaweza tu kutumaini kile ambacho Yesu ametutendea.)
-
- Hebu tupitie tena Marko 12:30-31. Nilielekeza usikivu wako kwenye kifungu cha 31. Je, kifungu cha 30 kina jambo la kuzungumzia kuhusu wokovu na kijana mdogo tajiri? (Ndiyo. Aliruhusu utajiri wake usimame kati yake na kile ambacho Yesu alimwambia akifanye. Yesu hajapanua matakwa ya Amri Kumi kwa muktadha wake. Kwa mara nyingine kinachomanishwa hapa ni kwamba unatumaini na kuamini nini?)
-
- Soma Marko 10:28. Hili linaendanaje na mjadala wetu? Je, kauli ya petro haifanani na ya kijana mdogo tajiri, “Angalia nilichokifanya ili kuingia mbinguni. Je, hilo linatosha?”
-
- Soma Marko 10:29-30. Hebu subiri kidogo! Yesu anamaanisha nini anaposema “sasa wakati huu?” Je, Yesu anatilia mkazo Kumbukumbu la Torati 28? (Jibu la Yesu halina kifani. Anasema kuwa kumfuata hutupatia matokeo “mara mia” sasa hivi, na uzima wa milele. Hii inatuambia nini kuhusu kuwa matajiri? (Tukimtanguliza Mungu, tukimtumaini na kumwamini, tunapaswa kutarajia matokeo mara mia. Fedha zitakuwa salama mikononi mwa wale wanaomtumaini Mungu na si kuzitumaini fedha zao.)
-
-
- Je, umegundua habari mbaya, kauli ya “udhia?”
-
-
-
- Tunaufahamu mustakabali wa wanafunzi. Je, walikuwa matajiri, au walipata udhia? (Waliteswa.)
-
-
-
-
- Unaweza kuelezeaje matokeo ya mara mia kwao? (Wanafunzi ni baadhi ya watu maarufu sana katika historia ya dunia. Na kwa kuongezea, walipokea furaha ya kutembea katika hatua za Yesu.)
-
-
-
- Soma Marko 10:31. Kwa nini Yesu anatumia neno “wengi” tofauti na “wote” ambao ni wa kwanza watakuwa wa mwisho? (Ni kwa sababu ambazo tumezijadili hivi punde. Matokeo ya kumtumaini Mungu ni kupata baraka.)
- Mwanzo na Mwisho
-
- Soma Marko 10:35-37. Unadhani Yakobo na Yohana walikuwa wamelala nyuma ya chombo (mtumbwi) wakati wa mazungumzo tuliyojifunza hivi punde? (Nadhani kinachomaanishwa ni kwamba kukipokea na kukikubali kile tulichokijadili ni jambo gumu.)
-
- Soma Marko 10:38-40. Nani anayeaminiwa kufanya uamuzi wa nafasi katika Ufalme wa Mbingu?
-
- Soma Marko 10:41. Je, wanafunzi wote walikuwa wamelala wakati wa mazungumzo yetu ya awali? (Wote wanadhani kuwa wanapaswa kuwa wa kwanza.)
-
- Soma Marko 10:42-45. Hivi punde tumejadili juu ya ndoa, utajiri, kumtumaini Mungu, na sasa nafasi za kimamlaka. Je, kuna msitari wa ukweli unaopita kwenye mada hizi? (Kumtanguliza Mungu ndio siri ya mafanikio. Wajibu wetu wa kwanza ni kumtumikia Mungu.)
-
- Rafiki, je, utafanya uamuzi sasa hivi kutoa huduma kwa Mungu kuwa kipaumbele chako cha kwanza? Kwa nini usichukue msimamo huo sasa hivi? Ukifanya hivyo, utapata baraka nyingi sasa hivi, ikiambatana na mateso, ikifuatiwa na uzima wa milele hapo baadaye.
- Juma lijalo: Mitafaruku Yerusalemu.