Somo la 3: Mapambano
Somo la 3: Mapambano
(Marko 2 & 3)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Huwa unakuwa na mjibizo (reaction) gani kwenye ukosoaji? Biblia inatuambia kuwa kuzingatia ukosoaji hutufanya kuwa na busara zaidi. Mithali 15:31-32. Katika siku za hivi karibuni, nimekuwa nikipokea ukosoaji usiotarajiwa kutoka kwa wageni kwenye darasa langu la ufundishaji wa masomo haya. Niamini pale ninapokuambia kuwa ukosoaji huu umekuwa wa ajabu sana na wa kufedhehesha. Na ukosoaji mwingi haukuwa na uhusiano wowote na kile nilichokuwa ninakifundisha. Somo letu juma hili linahusu mfululizo wa visa vinavyoanza kwa ukosoaji na matusi yaliyoelekezwa kwa Yesu. Hii inanifanya kutabasamu kwa kuzingatia uzoefu wangu wa hivi karibuni. Hebu tuzame kwenye Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu kubadili ukosoaji kuwa fundisho maridhawa!
I. Mtu Aliyepooza Msumbufu
A. Soma Marko 2:2-4. Huwa unafanyaje pale unapowasili kwenye tukio ukiwa umechelewa na hakuna nafasi iliyosalia? Je, utadhamiria kuwahi mapema wakati mwingine? Au unatoboa tundu kwenye jengo?
1. Jiweke kwenye nafasi ya Yesu. Unahubiri halafu kuna mtu anatoboa tundu darini juu ya mahali uliposimama. Utakuwa na mwitiko gani kwenye vurugu hizi za kutisha?
a. Je, hawa watoboa tundu darini wanavuruga mahubiri kwa kila aliyewasili pale kwa wakati?
2. Jiweke kwenye nafasi ya watoboa tundu darini. Hawa ni watu wa namna gani? Wana mtazamo gani juu ya rafiki wao aliyepooza?
B. Soma Marko 2:5. Kwa nini Yesu anasema hivi? Kwa sababu wanatakiwa kutubu kutokana na kuvuruga mahubiri yake? (Utaona kuwa kifungu kinasema Yesu “alipoiona imani yao,” na sio kwamba Yesu “aliona kutokuwa kwao na adabu.”)
1. Je, hiki ndicho ambacho mwenye kupooza na marafiki wake wanataka kukisikia?
C. Soma Yohana 9:1-2. Kulikuwa na mtazamo gani wa jumla juu ya ugonjwa na dhambi? (Dhambi ilisababisha ugonjwa.)
1. Je, dhambi inasababisha ugonjwa? (Ndiyo. Lakini soma Yohana 9:3. Jibu la Yesu halihusianishi ugonjwa na dhambi. Kitabu cha Ayubu na Waebrania 11 ni mafundisho mengine makuu kuhusu kutokuwepo kwa uhusiano kati ya dhambi na ugonjwa.)
2. Je, unadhani mwenye kupooza aliamini kuwa kupooza kwake kulitokana na dhambi yake?
D. Soma Marko 2:6-7. Je, huu ni ukosoaji wenye mantiki kwa Yesu?
1. Kwa nini Marko anaandika kisa hiki?
E. Soma Marko 2:8-12. Je, kitendo hiki kitakushawishi kwamba Yesu ni Mungu?
II. Kula na Wadhambi, Kufunga Mbele ya Uwapo wa Yesu
A. Soma Marko 2:15-17. Je, una haja ya kula na wenye dhambi ili uweze kuwaongoa?
1. Kiini cha swali kinaonekana kuwa tatizo la kuidhinisha vitendo vya watoza ushuru. Unapata fundisho gani kutoka kwenye jibu la Yesu? (Viongozi wa Kiyahudi walikuwa wakosoaji mno. Yesu ana njia nyingi sahihi za kuwaongoa wadhambi, na hii ni njia mojawapo.)
B. Soma Marko 2:18 na Luka 18:11-12. Kwa nini wanafunzi wa viongozi wa Kiyahudi na wanafunzi wa Yohana walifunga? (Walidhani kuwa kufunga huwafanya kuwa watu wa kidini zaidi.)
C. Soma Marko 2:19-20. Una maoni gani juu ya jibu la Yesu? Je, lisingekuwa jambo la msaada kwa wanafunzi wake kuwa wa kidini zaidi hata wakati wa uwapo wake? (Jambo la muhimu sana linabainishwa kwenye majibu ya Yesu kuhusu kula na watoza ushuru na kufunga. Isipokuwa kama Biblia inakuambia kuwa unapaswa kufanya au usifanye jambo fulani, unaweza kutumia akili yako mwenyewe kuamua. Angalia Kumbukumbu la Torati 4:2.)
III. Ukweli wa Sabato
A. Soma Marko 2:23-24. Yesu analetewa malalamiko gani? Je, ni kwamba wanafunzi wanaiba chakula au kwamba wanafanya kazi siku ya Sabato
B. Soma Marko 2:25-26. Tafakari jibu la Yesu. Je, anakiri kwamba wanafunzi wake wanatenda jambo lisilo halali? (Ikiwa suala la ufananisho ni jambo jingine unalokiri kuwa si halali, jibu ni “ndiyo.”)
1. Kama una watoto, je, umewahi kusikia utetezi huu hapo kabla? (Mtoto mmoja anakamatwa, na anajitetea kwa kusema kuwa mtoto mwingine ametenda jambo ambalo pia linakiuka sheria za nyumbani.)
a. Je, huo ndio utetezi wa Yesu? Au, anajenga hoja juu ya jambo jingine? (Anajenga hoja juu ya umuhimu. Daudi alikuwa na njaa na mhitaji. Hilo lilifanya tabia isio halali ikubalike.)
b. Kama ungekuwa mtawala wa Kiyahudi, ungetoa jibu gani? (Waambie wanafunzi wako wapate kifungua kinywa! Walipaswa kujiandaa siku ya Ijumaa kwa ajili ya Sabato kwa kufungasha chakula cha mchana. Hata hivyo, kufunga ni jambo jema kwao!)
2. Ungetoa jibu gani kama ungekuwa Yesu? (Jibu rahisi ni kusema kwamba wanachokifanya wanafunzi ni halali. Angalia Kumbukumbu la Torati 23:25.)
C. Soma Marko 2:27. Sote tunakubaliana kwamba Yesu ni mwerevu kutushinda. Kama tunaweza kuona kwamba uelewa wa namna fulani wa majibu yake hauna mantiki yoyote, ni nini uelewa sahihi wa majibu yake? “Uhitaji” unaendanaje kikamilifu kwenye jibu lililotolewa? (Yesu anasema kuwa kuridhisha mahitaji ya kibinadamu kwa ajili ya mtu kujisikia vizuri (comfortable) kunaendana na Sabato. Hoja juu ya jinsi ambavyo wanafunzi wangeweza kuepuka kutotulia kimawazo (uncomfortable) haina msingi.)
D. Soma Marko 2:28. Hii inamaanisha nini? (Yesu anatuambia kuwa Yeye ni “Bwana” wa Sabato, hivyo anabainisha kanuni zipi zitumike.)
1. Je, kuna kiashiria chochote kwenye kisa hiki kwamba utunzaji wa Sabato unakaribia kukoma? (Hapana, bali ni kinyume chake. Kwa nini Yesu atumie muda wake kufafanua jinsi inavyopaswa kutunzwa kama ilikuwa inakaribia kukomeshwa kwa ufufuo wake.)
E. Hebu turejee nyuma na tusome Marko 1:21-22. Je, tunaona ukweli wa kauli ile kwenye kisa tulichojifunza hivi punde? (Hii ni sehemu ya uthibitisho wa Marko kwamba Yesu ni Masihi. Ana mamlaka ya kusema kanuni zinamaanisha nini.)
1. Je, Yesu anatoka nje ya msitari ili kufafanua kuwa Sabato ni kwa ajili ya utulivu (comfort) wetu? Kwa kuwa ni ukweli kwamba walichokuwa wanakifanya wanafunzi kilikuwa halali, kwa nini asitoe hilo jibu jepesi?
F. Soma Marko 3:1-4. Kama viongozi wa Kiyahudi walidhani haikuwa sahihi kuponya siku ya Sabato, kwa nini wanyamaze?
G. Soma Marko 3:5-6. Kifungu kinasema kuwa hali hii ilimfanya Yesu akasirike. Kwa nini? (Kifungu kinasema, “ugumu wa mioyo yao.”)
1. Jambo gani kuhusiana na hili lilifanya mioyo yao kuwa migumu? (Walipendelea sheria zao za Sabato kuliko kumponya mlemavu.)
2. Ukiangalia nyuma katika Marko 3:4 Yesu anarejelea, inaonekana pasipo na umuhimu wowote, kuua siku ya Sabato. Tunaona nini katika Marko 3:6 kinachoonesha kuwa Yesu yuko kwenye msitari sahihi? (Kimsingi, viongozi wa Kiyahudi walikuwa wanapanga kumwua Yesu siku ya Sabato. Tofauti kubwa ajabu kati ya mamlaka mbili za kidini.)
IV. Roho Mtakatifu na Ukanda wa Hatari
A. Soma Marko 3:22. Yesu na baadhi ya viongozi wa dini wa Kiyahudi ni wapinzani wa dhahiri. Wangeweza kusema jambo gani jingine ili kufafanua miujiza ya Yesu?
B. Soma Marko 3:23-27. Yesu anajenga hoja gani ya kimantiki dhidi ya ufafanuzi huu kwenye miujiza yake? (Kwa nini Shetani ajishambulie mwenyewe?)
C. Soma 2 Wathesalonike 2:9-10. Je, Shetani anaweza kutenda miujiza?
1. “Ishara na ajabu za uongo” na “madanganyo ya udhalimu” vinamaanisha nini? (Shetani hawezi kutenda miujiza. Anafanya ionekane tu kwamba anaweza.)
2. Zingatia Ayubu 1:12. Je, Shetani anazuiwa na Mungu? (Ndiyo. Alitakiwa kuomba ruhusa.)
D. Soma Marko 3:28-30. Kuna hatari gani ya kuhusianisha maajabu na miujiza na Shetani? (Unaweza kuwa unamkufuru Roho Mtakatifu. Hili ni suala tunalotakiwa kulichukulia kwa umakini na tusiwe na papara ya kusema kuwa uponyaji umetoka kwa Shetani. Mungu pekee ndiye anayeweza kuponya.)
E. Rafiki, je, Yesu ni Mungu? Marko anaendeleza uthibitisho wake kwamba Yesu ni Mungu. Yesu anabadili ukosoaji wa uongo kuwa fundisho maridhawa linaloimarisha madai ya kwamba Yeye ni Mungu. Je, utamkiri Yesu kama Bwana wako? Kwa nini usifanye hivyo sasa hivi?
V. Juma lijalo: Mifano.