Somo la 13: Ushindi wa Upendo wa Mungu
Somo la 13: Ushindi wa Upendo wa Mungu
(Danieli 12, Mathayo 24, Ufunuo 20)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, unakumbuka nyakati ngumu zilizopita? Binafsi nimepitia nyakati zenye changamoto kubwa. Kazi yangu inahusisha mfululizo wa mapambano. Hakuna mtu anayepigwa risasi, lakini mapambano yanayoendelea ndani ya vyumba vya mahakama ni mbadala wa kisasa wa mashtaka kwa njia ya mapigano. Kila ninapoingia kwenye chumba cha mahakama huwa ninamwomba Mungu anisaidie kuwa mahiri, au angalao aniepushe na aibu. Kwa dhahiri maombi haya mawili ni tofauti. Huwa ninalenga kuwa mahiri. Imani yangu kwenye baraka za Mungu imejengwa juu ya kile alichonitendea katika siku za nyuma. Amenisaidia mara nyingi kuwa mahiri, na kamwe sikumbuki kuwahi kuaibishwa. Tunakabiliana na wakati mgumu hapa duniani. Wakati ambao unafanya changamoto zangu ndogo ziwe kichekesho. Alichokutendea Mungu katika siku za nyuma kinapaswa kukupatia ujasiri kwenye pendo lake katika nyakati ngumu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi.
I. Wakati wa Taabu
A. Soma Danieli 12:1-2. Taabu ijayo ni mbaya kiasi gani? (Haijawahi kuwa mbaya kiasi hiki!)
1. Kifungu kinasema kuwa wenye haki wataokolewa, lakini je, kinasema kuwa wataokolewa lini? (Wakati wa uokozi unaonekana kuwa katika ujio wa Mara ya Pili. Lakini hilo linafanya ionekane kuwa wenye haki wapo katikati ya taabu.)
B. Soma Mathayo 24:21. Je, Yesu anafafanua Danieli 12:12? Ikiwa ndivyo, lazima hili litakuwa tukio lile lile. Je, unakubaliana na hili?
C. Soma Mathayo 24:22-23. Kipindi hiki cha taabu kimefupishwa kwa manufaa ya nani? (Wenye haki.)
1. Je, wenye haki wapo katikati ya taabu? (Hii inaashiria kwa uthabiti kuwa jibu ni, “ndiyo.” Kipindi cha taabu kinafupishwa kwa ujio wa Mara ya Pili ili kuwanufaisha wenye haki. Kama wasingekuwa katika taabu isingewasaidia kufupisha kipindi hicho.)
2. Baadhi ya watu wanajenga hoja kuwa hili litafanana na mapigo ya Misri. Je, mapigo yaliwakuta Wamisri pekee? (Soma Kutoka 9:4, Kutoka 9:26, Kutoka 10:23, na Kutoka 12:12-13. Kwa dhahiri vifungu hivi vinatuambia kuwa baadhi ya mapigo, likiwemo pigo la kutisha la mwisho kabisa, hayakuwadhuru watu wa Mungu. Kigezo kinajenga hoja yenye mantiki kwa kiwango fulani cha ulinzi kwa watu wa Mungu kwenye mapigo ya mwisho.
D. Soma Mathayo 28:19-20. Je, Mungu atakuwa pamoja nasi hadi mwisho kabisa? (Ndiyo. Kamwe hatuachwi kusimama peke yetu dhidi ya Shetani. Nani anaweza kufanya hivyo?
E. Soma Yohana 14:16. Je, Roho Mtakatifu anaweza kutuacha? (Hapana.)
II. Uokozi
A. Soma Ufunuo 19:11-13. Mpiganaji huyu aliyempanda farasi mweupe ni nani? (Kifungu cha 13 kinatuambia kuwa anaitwa “Neno la Mungu.”)
1. Soma Yohana 1:1-3 na Yohana 1:14. Huyu Neno ni nani? (Ni Yesu. Yesu ndiye mpiganaji.)
B. Soma Ufunuo 19:14-16 na Ufunuo 19:19-21. Nani anayeshinda hili pambano la mwisho? (Yesu na jeshi la mbinguni.)
III. Milenia
A. Hivi punde tumetoka kusoma Ufunuo 19:20 inayotuambia kuwa Mnyama na Nabii wa Uongo wametupwa katika ziwa la moto. Hii inamwacha kiongozi mkuu wa uasi akiwa amesimama. Jambo gani linamtokea? Soma Ufunuo 20:1-3. (Shetani, kiongozi wa upinzani, amefungwa kwa miaka elfu moja.)
1. Je, huo ndio mwisho wa Shetani? (Hapana. Kifungu cha tatu kinatuambia kuwa atafunguliwa “kwa muda mchache.”)
B. Soma Ufunuo 20:4. Jambo gani linaendelea wakati Shetani akiwa amefungwa kwa miaka elfu moja? (Hukumu inaendelea.)
C. Soma Ufunuo 20:5-6. Unauelewaje ufufuo wa kwanza na wa pili? (Ufufuo wa kwanza ni wa wenye haki. Huu unahusianishwa na ujio wa Yesu Mara ya Pili katika Ufunuo 19. Waliookolewa wapo mbinguni wakihusishwa kwenye aina fulani hivi ya hukumu wakati Shetani akiwa amefungwa duniani na waovu wakiwa wamekufa. Waovu wanafufuliwa baada ya miaka elfu moja. Huu ndio ufufuo wa pili.)
1. Kwa kuwa hatima ya wote imeshaamuliwa, ni jambo gani, ambalo kimantiki wenye haki watakuwa wakikihukumu katika kipindi hiki cha miaka elfu moja? (Watakuwa na marafiki, familia, na wapendwa wao waliopotea. Kimantiki, hii inawapatia muda wa kutosha kubaini kwamba Mungu amekuwa mwenye haki katika hukumu yake kwa waliopotea.)
2. Mteja wangu wa zamani amenitumia nyaraka zenye dhamira ya kunishawishi kwamba waliopotea wanaungua jehanum milele. Bila kuchunguza vifungu vya dhahiri vinavyoleta ukinzani kwenye suala la kuungua milele, wazazi wanapopitia kumbukumbu ya watoto wao waliopotea na kukubaliana kwamba mbingu hazitakuwa mahala sahihi kwao, je, unadhani kuwa pia watakubaliana kuwa wanapaswa kuteswa milele?
D. Soma Ufunuo 20:7-8. Sasa tunaelewa kuhusu kufunguliwa kwa Shetani na ufufuo wa pili. Wanapambana na nani? (Yesu na watakatifu.)
E. Soma Ufunuo 20:9. Shambulio hili linaendanaje na hukumu ya wenye haki? (Kama walikuwa na mashaka yoyote kuhusu hukumu ya Mungu, hii inathibitisha kuwa kuendelea kuwapo kwa waliopotea hakuendani na ufalme wa Mungu.)
F. Soma Ufunuo 20:10. Hukumu ya mwisho ya Shetani ni ipi? (Anatupwa katika ziwa la moto.)
IV. Mada ya Hukumu
A. Soma Ufunuo 20:11-13. Wafu hawa ni akina nani? (Hii ni rejea kwa waliopotea. Wafu wamefufuliwa katika ufufuo wa pili.)
1. Wanahukumiwa kwa msingi gani? (Kwa msingi wa kazi zao kama zilivyoandikwa kwenye vitabu.)
B. Soma tena Ufunuo 20:12 na usome Ufunuo 20:15. Kitabu gani kingine ni sehemu ya hukumu? (Kitabu cha uzima.)
1. Kitu gani kimeandikwa katika kitabu cha uzima? (Majina, sio matendo.)
2. Ni nini matokeo ya jina lako kuandikwa katika kitabu cha uzima? (Hauangamizwi. Umeokolewa!)
3. Hiyo inatuambia nini kuhusu kipimo cha hukumu? (Waliookolewa hawahukumiwi kutokana na matendo yao. Waovu wanahukumiwa kwa matendo yao.)
C. Soma Ufunuo 3:5 na Warumi 10:9-11. Ni nini kipimo cha hukumu kwa wenye haki? (Sio matendo yao, bali kumkiri kwao Yesu kama Mwokozi wao. Wanavaa mavazi meupe ya haki ya Yesu.)
1. Katika majuma ya hivi karibuni tumekuwa tukijadili suala la ibada. Ni nini nafasi ya ibada kwa wale ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima? (Soma Ufunuo 13:6-8. Kama jina lako limeandikwa katika kitabu cha uzima, unamwabudu Mungu wa kweli pekee.)
V. Furaha!
A. Soma Ufunuo 7:9-10. Wangapi majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima? (“Mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu.”)
1. Wamevaa nini? (“mavazi meupe.”)
2. Wanamshukuru nani kwa wokovu wao? (Mungu na Mwana-Kondoo.)
B. Soma Ufunuo 7:11-12. Kuna mtazamo gani katika mazingira yanayozunguka kiti cha enzi cha Mungu? (Kusifu! Furaha! Shukurani!)
C. Rafiki, je, unapenda kuwapo mbinguni ukimsifu Mungu? Je, unapenda jina lako liwepo katika kitabu cha uzima? Je, unapenda kupata uzoefu wa ushindi wa upendo wa Mungu? Mpokee sasa hivi. Mwabudu yeye peke yake!
VI. Juma lijalo: Tunaanza kujifunza Injili ya Marko.