Somo la 12: Mataukio ya Kufunga Historia ya Dunia
Somo la 12: Mataukio ya Kufunga Historia ya Dunia
(Waefeso 4, Yoeli 2, Matendo 2, Ufunuo 18)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Juma lililopita tulijifunza kile ambacho watu wabaya wanakifanya kama sehemu ya matukio ya mwisho wa dunia. Wanaufanya ujio wa Yesu Mara ya Pili kuwa wa bandia na kudai ibada inayomstahili Yesu. Kilichomaanishwa katika somo la juma lililopita ni “Usifanye hivyo moja kwa moja au kwa kuzunguka.” Juma hili tunageukia kwenye kile ambacho watu wema wanakifanya kama sehemu ya matukio ya mwisho. Tunatarajiwa kufanya nini? Yakobo 5:7 inaulinganisha ujio wa Yesu Mara ya Pili na kilimo. Anasema kuwa mkulima “hungoja” “mvua za kwanza na za mwisho.” Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachongoja kukiona na kile ambacho sisi, watu wema, tutakuwa kukifanya!
I. Roho Mtakatifu na Muhuri
A. Soma Waefeso 4:30. Sura ya 4 ya Waefeso kwanza inawaelezea watu wabaya na jinsi walivyo. Kisha sura hiyo inawageukia watu wema na kimsingi inaorodhesha mambo wanayopaswa kuacha kuyatenda. Mojawapo ya mambo ya “kuacha kuyatenda” ni kumhuzunisha Roho Mtakatifu wa Mungu. Unadhani inamaanisha nini kumhuzunisha Roho Mtakatifu?
B. Soma Isaya 63:10. Hii inafafanuaje suala la kumhuzunisha Roho Mtakatifu? (Uasi. Kutokutii.)
C. Soma Zaburi 78:40-41. Hii inatuambia kuwa kumhuzunisha Mungu maana yake ni nini? (Uasi. Kuchokoza. Kumjaribu Mungu.)
1. Tafakari jinsi kumhuzunisha Mungu kunavyoelezewa. Tatizo la msingi ni lipi? (Ni mtazamo. Mtazamo unaoukataa mpango wa Mungu kwa ajili ya maisha. Mtazamo wa uasi.)
D. Hebu turejee kwenye Waefeso 4:30. Kwa kuzingatia kile kinachomaanishwa kwenye suala la kumhuzunisha Roho Mtakatifu, unadhani inamaanisha nini “kutiwa muhuri” na Roho Mtakatifu “hata siku ya ukombozi?”
E. Soma Waefeso 1:13. Hii inaelezea kuwa inamaanisha nini kutiwa muhuri na Roho Mtakatifu? (Ni hatua ya mwisho kuelekea kwenye wokovu. Kwanza tunaisikia injili, kisha tunaiamini injili, halafu tunamwalika Roho Mtakatifu maishani mwetu ili kutusaidia kuishi kwa kufuata mapenzi ya Mungu. Mtu aliyetiwa muhuri ni mtu ambaye amefanya uamuzi wa kushirikiana na Roho Mtakatifu. Watu hao sio waasi.)
F. Soma Ufunuo 7:1-3. Utiwaji muhuri huu unaonekana kuwa tofauti kidogo. Unadhani uko tofauti? (Jambo lenye kufanana ni kwamba kutia muhuri katika vipaji vya nyuso kimantiki huwakilisha fikra ya mwanadamu. Fikra yao inaongozwa na Roho Mtakatifu.)
1. Maishani mwangu mwote nimefundishwa kwamba muhuri wa mwisho ni kuitunza Sabato. Je, hilo lina makosa? (Sidhani kama lina makosa, ni sawa na kusisitiza silabi isiyo sahihi kwenye neno. Sabato sio njia imara ya kutia muhuri, Roho Mtakatifu ndio njia iliyo imara. Kama tulivyojifunza juma lililopita, Sabato ni msingi wa kumwabudu Mungu Muumbaji wetu. Hivyo, kuitunza Sabato itakuwa mojawapo ya matokeo makubwa ya kutiwa muhuri na Roho Mtakatifu. Hebu tugeukie, katika sehemu inayofuata, kwenye ishara nyingine ya mwisho yenye nguvu ya kutiwa muhuri.)
II. Umiminaji wa Sasa
A. Soma Yoeli 2:28-29. Nani ana haki ya kuwa msemaji wa Roho Mtakatifu? (Kila mtu. Hakuna tofauti kulingana na jinsia, hakuna tofauti kulingana na umri, hakuna tofauti kulingana na hadhi katika jamii.)
1. Udhihirisho wa Roho Mtakatifu unafananaje? (Unadhihirishwa kwenye unabii, ndoto, na maono.)
a. Hebu litafakari hili kidogo. Kama kuna mtu katika kundi lako amedai kuwa na unabii, ndoto, au njozi kutoka kwa Mungu, utakuwa na mwitiko gani?
b. Kama umekuwa na mwitiko hasi, je, hiyo inamaanisha kuwa wewe ni muasi, mtu ambaye hajatiwa muhuri na Roho Mtakatifu?
B. Soma Matendo 2:1-4. Wanafunzi wanafanya nini?
1. Roho Mtakatifu anafanya nini?
C. Soma Matendo 2:14-16. Petro analielezeaje jambo hili? (Anasema kuwa huu ni utimilifu wa Yoeli 2!)
D. Soma Matendo 2:17. Tunaishi katika siku gani? (Kama Petro anasema matukio ya Matendo 2 yalikuwa ni utimilifu wa kauli ya Yoeli 2 ya “siku za mwisho,” basi kwa dhahiri tunaishi katika siku za mwisho.)
E. Petro anatusaidia kuelewa asili kamili ya huu utiwaji muhuri. Hebu tuendelee kwa kusoma Matendo 2:19-21. Mkristo aliyetiwa muhuri anatarajiwa kufanya jambo gani jingine? (Utaona kwamba Petro anaendelea kunukuu Yoeli 2:30-32. Petro anasisitiza dhana ya kwamba uwezo wa Roho Mtakatifu unadhihirishwa kwa njia ya maajabu mbinguni na duniani, na ishara za damu, moto, na moshi hapa duniani.)
1. Unadhani “damu, moto, na moshi” vinamaanisha nini? (Soma Ufunuo 8:7-8. Hii inaelezea matukio ya kutisha ya siku za mwisho ambayo ni sehemu ya hukumu za Mungu.)
a. Tunapaswa kuhitimisha nini kuhusu moto chanya wa Pentekoste na moto hasi wa Ufunuo 8? (Tutaona ishara zisizo za kawaida (extraordinary) za uwezo wa Roho Mtakatifu zikitenda kazi kupitia kwetu, na tutaona hukumu za kutisha zisizo za kawaida zinazoendelea.)
2. Hebu tuangalie nyuma kwenye somo letu la juma lililopita. Soma Mathayo 24:23-24. Hii inafanyaje kazi yetu kuwa ngumu zaidi? (Biblia inasema kuwa Kristo wa uongo pia atatenda “ishara kubwa na maajabu.”)
a. Tunawezaje kuutambua ukweli kutoka kwenye uongo? (Tulichokiona juma lililopita ni kwamba Kristo wa uongo anaweka kituo cha ibada hapa duniani. Yesu anapokuja mara ya pili atatuchukua mbinguni. Hatatumia muda wake hapa duniani. Hiyo ni njia mojawapo ya kutofautisha mambo haya mawili.)
F. Soma tena Matendo 2:2-4. Je, uko tayari kwa ajili ya sauti kubwa na moto kuwa sehemu ya ushuhudiaji wako?
G. Soma Matendo 2:19. Je, uko tayari kuwa sehemu ya ishara na maajabu?”
III. Unenaji wa Sasa
A. Soma Ufunuo 18:1. Unadhani maneno “nchi ikaangazwa” yanamaanisha nini kiuhalisia? (Malaika anasambaza ukweli. Dunia inaangazwa na ukweli.)
1. Je, hii ni kazi ya malaika pekee, au hii ni sehemu ya kazi yetu kama mawakala wa Mungu waliotiwa muhuri?
B. Soma Ufunuo 18:2-4. Je, hii inashutumu vitendo vya ngono visivyo vya kimaadili? (Sidhani kama huo ndio ujumbe mkuu hapa. Badala yake, hili ni onyo lile lile lililotolewa katika Ufunuo 14:8. Aina hii ya uzinzi ni kutokuwa waaminifu kwa Mungu. Ni utiifu kwa mamlaka ya kiroho au ya “kiuadilifu” ambayo yanampinga Mungu. Hii inaturejesha kwenye kile tulichojifunza juma lililopita – kumwabudu Mungu wa kweli na kuukataa uongo.)
1. Hii inatupatia maelekezo gani halisi kwa ajili ya kazi yetu kama mawakala wa Mungu “waliotiwa muhuri?” (Tunapaswa kutazamia sio tu ishara kubwa na nguvu, bali zile ishara na nguvu zinaendana na ujumbe wa kumwabudu Mungu wa kweli na kukataa mbadala wa Shetani. Tuna ujumbe wa kusambaza!)
C. Soma Ufunuo 13:14-17. Watu wabaya wanafanya nini wakati tunapoeneza injili? (Wanalazimisha (wanatia chapa mkononi), au wanaushawishi (wanatia chapa katika vipaji vya nyuso) ulimwengu kufuata nguvu ya kiroho ya uongo.)
D. Rafiki, je, utatiwa muhuri na Roho Mtakatifu? Je, utaungana na timu ya kumpambania Kristo na dhidi ya Mpinga-Kristo? Muda wa kufanya uamuzi wa kuwa upande wa Yesu ni sasa!
IV. Juma lijalo: Ushindi wa Upendo wa Mungu.