Somo la 11: Pambano Linalokaribia
Somo la 11: Pambano Linalokaribia
(2 Wathesalonike 2, Ufunuo 13, Mwanzo 1)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Kitabu cha Ufunuo kimejaa taswira ya wanyama wa kutisha na ishara zinazofikisha ujumbe kuhusu siku zijazo. Taswira na ishara nyingi zinazua mjadala juu ya kile zinachomaanisha na muda wa kutimia kwake. Hata hivyo, huo sio unabii pekee unaopatikana katika Agano Jipya. Unabii mmoja ambao kimsingi haupatikani kwenye kitabu cha Ufunuo uko bayana na ni vigumu kuukataa. Unabii huo ndio tutakaouzingatia juma hili. Pia unaendana na mtazamo wa dini tatu za Ibrahimu: Ukristo, Uyahudi na Uislam. Unabii huu unatuambia kuhusu pambano linalokaribia linaloendelea kabla ya ujio wa Yesu Mara ya Pili. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!
I. Onyo
A. Soma 2 Wathesalonike 2:1. Mada gani inajadiliwa katika mjadala unaofuata? (Ujio wa Yesu Mara ya Pili na wafuasi wake kwenda mbinguni. Tunapowafundisha wanasheria namna ya kujenga hoja mahakamani, huwa tunawaambia kwanza waandae “mpango (roadmap).” Ifanye mahakama ifahamu kuwa utajenga hoja. Kifungu cha kwanza ni mpango.)
B. Soma 2 Wathesalonike 2:1-3. Nini kinachojaliwa kuhusu ujio wa Yesu Mara ya Pili? (Kwamba watu watajaribu kuwadanganya wafuasi wa Yesu.)
1. Tunapaswa kutazamia nini ili kuepuka kudanganywa? (Uasi utakuja kwanza.)
2. Hebu subiri, tulikuwa na uasi dhidi ya Mungu tangu wakati Kaini alipomuua Habili. Hii inatusaidiaje?
C. Soma 2 Wathesalonike 2:4. Mambo gani muhimu kwenye uasi huu yanautofautisha na uasi mwingine? (Muasi huyu anatangaza kuwa yeye ni Mungu, na anachukua kiti chake “katika hekalu la Mungu.”)
1. Sasa hebu tuongezee muktadha. Mpango (roadmap) unatuambia nini kuhusu muktadha? (Unabii huu unahusu kuufanya bandia ujio wa Yesu Mara ya Pili.)
D. Soma Mathayo 24:23-27. Yesu anaonya kuwa nini kitatokea kabla ya ujio wake Mara ya Pili? (Makristo wa uongo wakitenda ishara kubwa na maajabu yatakuja.)
1. Ni njia gani moja ya uhakika ya kuutofautisha ujio bandia wa Mara ya Pili na ule wa kweli? (Kila mtu atauona. Utakuwa kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi. Angalia pia Ufunuo 1:7 – “kila jicho litamwona.”)
E. Soma 2 Wathesalonike 2:9-10. Nani anayeutia nguvu Upinga Kristo? (Shetani.)
1. Uthibitisho uliotumiwa na huyu muasi bandia una ushawishi kiasi gani? (Uwezo mkubwa na ishara za ajabu zinaunga mkono madai haya.)
F. Soma 2 Wathesalonike 2:8. Hii inatuambia nini kuhusu kipindi cha utawala wa Mpinga Kristo? (Kwamba ujio wa Yesu Mara ya Pili pekee ndio unaomuua. Matukio haya mawili yanaonekana kutokea katika kipindi kinachokaribiana.)
G. Je, unafahamu kuwa imani kwa masihi wa uongo pia inaaminika kwa Waislam? (“Mdanganyi” (al-Dejjal) ni masihi wa uongo katika fundisho la Kiislam kuhusu nyakati za mwisho. Kwa mujibu wa fundisho hilo, Mdanganyi atatawala kwa kipindi chenye ukomo kabla hajaangamizwa na Mahdi au Yesu. Angalia orodha ya Britannica kwa al-Dejjal yote.)
1. Je, Uyahudi una imani kama hiyo? (Naam! Itafakari. Wanamkataa Yesu kama Masihi, na hivyo wanaendelea kuutazamia ujio wa Masihi wa kweli.)
H. Una maoni gani kuhusu ukweli kwamba dini zote tatu za Ibrahimu, ambazo zinawakilisha sehemu kubwa ya imani za kidini za dunia, zinautazamia ujio wa masihi?
II. Mada
A. Soma tena 2 Wathesalonike 2:4. Tofauti na kupatia kwenye utambulisho, kuna suala gani la msingi katika kumpinga muasi Mpinga Kristo anayeufanya kuwa bandia ujio wa Yesu Mara ya Pili? (Ibada. Anajiinua juu ya wengine wote wanaodai kuwa wana haki ya kuabudiwa. Anasema kuwa yeye ni Mungu.)
B. Soma Ufunuo 4:11. Hii inatoa taswira ya mbinguni katika chumba cha ufalme. Sababu gani inatolewa ya kumwabudu Yesu? (Yeye ni Muumbaji wetu. Anawezesha uumbaji.)
C. Soma Ufunuo 14:7. Ni sababu ipi inatolewa kwa Malaika wa Kwanza kati ya Malaika Watatu kusema kuwa tunapaswa kumwabudu Mungu? (Yeye ni Muumbaji.)
D. Ufunuo 13 inatuambia kuhusu wanyama and joka. Soma Ufunuo 13:4 na Ufunuo 13:11-14. Kuna suala gani lililopo kwa joka na wanyama? (Ibada. Angalia rejea za ishara kubwa kutumika katika kudanganya.)
E. Miaka mingi iliyopita, niliamua kufanya utafiti wa hatua kwa hatua wa Biblia ili kuona alichokisema Mungu kuhusu madai yake ya kuabudiwa. Niliona angalao vifungu 100 vya Biblia ambavyo madai yake ya kuabudiwa ni kwamba Yeye ni Muumbaji! Kama ulikuwa unajaribu kumshinda Mungu na kudai kuabudiwa kunakomstahili, ungefanya nini? (Kuhafifisha madai yake kama Muumbaji.)
III. Mada Iliyopo Leo
A. Maoni kadhaa ya Biblia ninayoyatumia mara kwa mara ni ya zamani sana. “Barnes’ Notes” ziliandikwa miaka ya 1830. Maoni ya Adam Clarke yalichapishwa kuanzia mwaka 1810 hadi 1826. Maoni ya Biblia ya Jamieson-Fausset-Brown yalichapishwa mwaka 1871. Maoni haya, miongoni mwa mengineyo, yalinifanya niamini kuwa miaka mia mbili iliyopita kulikuwa na makubaliano ya jumla miongoni mwa wasomi wakubwa wa Biblia wa Waprotestanti kwamba mojawapo ya kichwa cha mnyama wa Ufunuo 13, ambaye kidonda chake kifacho kiliponywa, ni Kanisa Katoliki. Bado kanisa langu linafundisha hivyo, vivyo hivyo kwa Waprotestanti wengine wa zama za leo (wa kisasa). Kanisa langu pia linafundisha kuwa “Mnyama apandaye juu ya Nchi” wa Ufunuo 13:11 ni Marekani. Ninazielewa hoja hizi na kwa ujumla ninazielewa kuwa na mashiko. Hata hivyo:
1. Hoja kuhusu Kanisa Katoliki inakinzanishwa na uhalisia wa leo. Kanisa Katoliki, ambalo linatetea maadili ya msingi hadharani (kama vile kuwalinda watoto ambao hawajazaliwa), linapigwa sana na vyombo vya habari. Waumini wake wanaoshikilia nafasi za kisiasa nchini Marekani ama ni wakanaji wa imani (Bunge la Marekani na matawi yake) au waungaji mkono thabiti wa uhuru wa dini (Mahakama Kuu).
2. Hoja kuhusu Marekani kulazimisha ibada ulimwenguni kote inasingiziwa na ukweli kwamba inaonekana kutokuwa na ushawishi katika ulimwengu wa Kiislam kutozungumzia chochote kuhusu kuinuka kwa Wachina. Huenda ibada ya uongo ni uovu wenye madhara ambao Marekani inausambaza ulimwenguni kote kupitia kwenye vyombo vyake vya uburudishaji (entertainment media). Hata hivyo, vyombo hivyo vinaonekana kulichukia Kanisa Katoliki.
3. Jambo linalotokea sasa hivi linahusisha shambulio la moja kwa moja kwenye madai ya Mungu kama Muumbaji wetu. Hebu tuangalie matukio ya sasa ambayo yanatia changamoto moja kwa moja madai ya Mungu kuwa Mungu Muumbaji wetu na hivyo kustahili kuabudiwa nasi.
B. Soma Mwanzo 1:1-5. Sehemu iliyosalia ya sura hii inafuata mpangilio huu wa jumla. Mambo ya muhimu ni yepi katika mpangilio huu? (Mungu aliumba kila kitu kutoka kwenye “ukiwa na utupu.” Mungu alitamka na uumbaji ukatokea. Kila kipengele kilitokea baada ya kuamriwa.)
1. Je, kwa sasa madai haya yako chini ya shambulio? (Yapo kwenye shambulio karibia ulimwenguni kote kupitia kwenye nadharia ya uibukaji iliyoasisiwa na Darwin.)
C. Soma Mwanzo 1:26-28. Hii inadhihirisha nini kuhusu wanadamu? (Tumeumbwa kwa mfano wa Mungu. Tulidhamiriwa kuutawala uumbaji. Tuliumbwa ama mwanaume au mwanamke kwa lengo la kuzaliana.)
1. Je, madai haya kwa sasa yako chini ya shambulio? (Kwa sasa tunafundishwa kuwa kuna jinsi nyingi, jinsia sio ya ki-jozi. Tunahakikishiwa kuwa ndoa za jinsi moja, ambazo haziwezi kuzaliana, zina hadhi sawa kwenye mpangilio wa Mungu wa uumbaji.)
2. Vipi kuhusu madai kwamba wanadamu wanatawala uumbaji? (Tunaonywa kwamba wanadamu ni viumbe wa hatari kwenye ulimwengu ulioumbwa na wanadamu wanatakiwa kupunguzwa idadi yao. Tunaambiwa kuwa tunatakiwa kuzingatia mahitaji ya mazingira ambayo yanatutawala.)
D. Soma Mwanzo 2:1-3 na Kutoka 20:8-11. Vifungu hivi vinasema kuwa sababu ya kuabudu siku ya saba ni ipi? (Ni ukumbusho wa Mungu kuumba “mbingu na nchi.”)
1. Je, kwa sasa madai haya yako chini ya shambulizi? (Karibia dunia yote ya Kikristo inaabudu siku ya Jumapili – siku ya kwanza ya juma.)
E. Rafiki, Martin Luther aliandika: “Nikisema kwa sauti kubwa na kufafanua bayana kila sehemu ya ukweli wa Mungu isipokuwa sehemu ndogo ambayo ulimwengu na Shetani vinaishambulia kwa wakati huo, basi simkiri Kristo, hata kama nitaonekana kuwa ninamkiri Kristo kwa nguvu na ujasiri mkubwa.” Nitaona jinsi utimilifu wa Ufunuo 13 unavyojidhihirisha, lakini kwa sasa niko upande wa Martin Luther. Hatuna maana yoyote ikiwa hatupingi kile anachokishambulia Shetani sasa hivi. Je, utakuwa askari mwaminifu katika pambano linaloendelea sasa hivi?
IV. Juma lijalo: Matukio ya Kufunga Historia ya Dunia.