Somo la 9: Msingi wa Serikali ya Mungu
Somo la 9: Msingi wa Serikali ya Mungu
(Waebrania 9, Ufunuo 12, Warumi 7-8)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Neno “Lexrex” limekuwa likiandikwa kwenye kibao cha namba za usajili wa magari yangu kwa miongo kadhaa. Je, kibao cha usajili wa gari langu kinamhusu Lex Luthor, mhalifu katika sinema ya Superman? Hapana. “Lex” ni neno la Kilatini likimaanisha sheria, na “rex” ni neno la Kilatini likimaanisha mfalme. Linapaswa kutafsiriwa, “Sheria ni Mfalme.” Vibao vya namba za usajili ni vya muhimu kwangu kwa sababu mimi ni mwanasheria na kwa sababu ya imani yangu kwenye umuhimu wa Amri za Mungu katika Ufalme wa Mungu. Je, sheria ni msingi wa serikali ya Mungu, au upendo ndio msingi? Je, upendo hautakuwa na maana bila uwapo wa sheria? Linapokuja suala la kufundisha umuhimu wa sheria, kasoro inakaribiana sana na ukweli. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kukiona kuhusu ukweli kuhusiana na umuhimu wa sheria!
I. Ndani ya Sanduku la Agano
A. Soma Waebrania 9:3-5. “Vibao vya agano” ni Amri Kumi. Angalia Kumbukumbu la Torati 10:2-5. Kwa nini hazimo tu ndani ya patakatifu, sio tu Patakatifu pa Patakatifu, bali kimsingi ndani ya Sanduku la Agano?
1. Kwa nini fimbo ya Haruni na mana pia vimo ndani ya Sanduku? Vyote vina jambo gani lenye kufanana? (Hesabu sura ya 16-17 inaandika kuwa kuchipuka kwa fimbo ya Haruni ulikuwa msingi wa kukomesha uasi na kuanzisha uongozi wa Musa na Haruni. Mana, kimsingi, ni chakula alichokitoa Mungu ili kuwalisha watu katika safari ya wana wa Israeli kutoka Misri. Hizi, pamoja na Amri Kumi, ni ishara ya uongozi na uangalizi wa Mungu.)
B. Soma Kutoka 25:16. Mungu anakiita “ushuhuda” kile kilichowekwa kwenye Sanduku. Kwa nini? (Ilikuwa ni kuwakumbusha watu uangalizi wa Mungu kwao. Walikuwa mashahidi wa uangalifu wake.)
C. Waebrania sura za 8-10 ni ufafanuzi wa sababu ya kwa nini patakatifu pa duniani pamoja na kafara zake za wanyama zilikuwa ni aina ya unabii kuhusu ujio wa Yesu na kafara yake ya hadhi ya juu ya kujitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu. Hii inaashiria kuwa sababu ni ipi ya Amri Kumi kuwekwa kwenye Sanduku katika Patakatifu pa Patakatifu? (Inaashiria mambo mawili. Kwanza, sheria ni ya muhimu sana kwa Mungu. Yesu alikufa ili kutimiza matakwa ya sheria kwa niaba yetu. Pili, sheria inatuambia dhambi ni kitu gani, na dhambi husababisha mauti. Hivyo, Yesu alikuja kuiokoa sheria na sisi. Warumi 6:23.)
II. Je, Sheria ni Mfalme?
A. Soma Ufunuo 12:9-12. Nini kimemtokea Shetani na washirika wake? (Wamefukuzwa kutoka mbinguni na kutupwa duniani.)
1. Je, hilo ni jambo jema kwa watu wanaoishi mahali ambapo Shetani alitupwa? (Kimsingi hapana. “Ole” ni neno lililotumika kuelezea jinsi tunavyopaswa kujisikia.)
1. Je, ni n2ksi kuwa mahala ambapo Shetani alitua? (Hii sio ajali au nuksi. Wanadamu walimkaribisha Shetani kuishi hapa tulipomchagua Shetani dhidi ya Yesu katika Bustani ya Edeni. Angalia Mwanzo 3.)
B. Soma Ufunuo 12:17. Shetani anamlenga nani na hasira yake? (Wale wazishikao amri za Mungu na kuwa na ushuhuda wa Yesu.)
1. Ikiwa Shetani hana hasira nasi, unadhani hiyo inamaanisha nini? (Inamaanisha sisi sio wapinzani wake. Hatusababishi tatizo lolote kwenye ufalme wake wa kiovu.)
a. Hii inazungumzia nini kuhusu sheria? (Ni ya muhimu sana kwenye pambano kati ya wema na uovu. Utaona kwamba, kama ilivyo kwa sheria kuwa ndani ya Sanduku, hii inasisitiza umuhimu wa sheria.)
b. Inamaanisha nini kuwa na ushuhuda wa Yesu? (Angalia tena Ufunuo 12:11. Hawa ni wale ambao wanashuhudia kwamba Yesu ni Mungu na wanautegemea wokovu kwa njia ya neema. Damu ya Yesu inafunika dhambi zao.)
C. Soma Wakolosai 2:11-14. Jambo gani liligongomelewa msumari msalabani? (“Hati iliyoandikwa ya kutushtaki kwa hukumu zake.”)
1. Vifungu vinaporejelea “hukumu zake,” je, hiyo ni rejea ya sheria? (Ndiyo. Tulikuwa tumekufa kwa sababu sote tuliikiuka sheria. Hukumu zetu dhambini ndizo zilizogongomelewa msalabani.)
2. Vifungu hivi vinatuambia kuwa Yesu alituokoa kwa kuishika sheria kwa ajili yetu na kwa kufa kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa nini alifanya hivyo? Kwa sababu ya upendo au kwa sababu ya umuhimu wa sheria? (Kama sheria haikuwa mfalme, Yesu angeudai tu “upendo,” na kupuuzia kushindwa kwetu kuishika. Yesu aliishika sheria NA alikufa badala yetu kwa sababu sheria ni kiini cha ufalme wake na anatupenda kwa namna isiyoweza kupimika. Nadhani hilo linaifanya sheria kuwa mfalme.)
III. Kuhusiana na Lex Rex
A. Soma Warumi 7:3-6. Paulo anatuambia kuwa tumewekwa huru dhidi ya sheria – kama ambavyo tunawekwa huru dhidi ya viapo vyetu vya ndoa mwenza wetu anapofariki. Je, Mfalme amefariki?
B. Soma Warumi 7:7-8. Baadhi ya watu wanajenga hoja kwamba sheria iliyokufa ilikuwa ni ile ya mapokeo na sio Amri Kumi. Vifungu hivi vinatufundisha kuwa ni sheria gani inayojadiliwa? (Vifungu hivi vinadhihirisha kuwa sheria ambayo kwayo tunawekwa huru ni Amri Kumi na sio sheria ya mapokeo. Amri dhidi ya kutamani ni Amri ya Kumi.)
1. Kama torati ilikuwa ya muhimu sana kiasi cha Yesu kuifia, kwa nini awekwe huru dhidi ya torati? Kwa nini Shetani awachukulie maadui wake wa kweli kuwa wale wanaozishika amri?
C. Soma Warumi 7:22-25. Paulo anasema kuwa mtazamo wake dhidi ya sheria ya Mungu ni upi? (Anaifurahia! Anaitumikia “sheria ya Mungu” kwa akili yake. Tatizo ni kwamba mwili wake hautoi ushirikiano.)
D. Angalia tena Warumi 7:24 na usome Warumi 8:1-4. Matakwa ya sheria yanatimizwaje ndani yetu – ambao tuna tatizo la kuishika sheria? (Kwa njia ya Yesu. Aliitii kwa ajili yetu.)
E. Soma Warumi 8:4-6. Je, Paulo amebadili uelekeo? Ametuambia kuwa alitaka kutenda lililo jema lakini hakuweza (Warumi 7:19). Lakini sasa anatuonya kuwa tutakufa ikiwa mawazo yetu yatawekwa “juu ya mambo ya mwili.” Unalielezeaje hili? (Tafakari kidogo kile tulichojifunza hadi kufikia hapa. Amri Kumi zilikuwa ndani ya Sanduku kwa sababu amri hizo ni ushuhuda juu ya mwongozo na upendo wa Mungu. Yesu alikufa juu ya sheria ili tuweze kuishi. Hakusema (kama ambavyo angeweza kusema) “Achaneni na sheria. Upendo wangu kwenu utayashinda matakwa yote haya bandia.” Badala yake alikufa ili kuitunza sheria na sisi. Huu ni ushuhuda mkuu kwenye umuhimu wa sheria ya Mungu.)
F. Soma Warumi 8:12-14. Vifungu hivi vinasema kuwa tunawezaje kuzishika amri? (Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.)
1. Unalitafsirije hili? Je, sisi tuna nguvu kuliko Paulo? (Hatuwezi kuishika sheria kwa sababu sisi ni wadhambi na mwili wetu ni dhaifu, lakini Roho Mtakatifu anayabadilisha yote hayo.)
G. Soma tena Warumi 8:4. Maneno ya msingi ni “usienende kwa kufuata mambo ya mwili.” Tunasoma katika Warumi 8:5 kwamba hili linahusiana na jinsi “tunavyoyaweka mawazo yetu.” Anachokitaka Mungu kwetu ni mtazamo wa utii. Anatutaka tufurahie katika sheria. Anataka utii uwe mwelekeo wa jumla wa maisha yetu. Hatarajii utii ulio mkamilifu – hiyo ilikuwa kazi yake!)
IV. Kuiandaa Akili
A. Soma Ufunuo 14:6-7. Hii inaitwa “injili ya milele.” Kwa nini? (Tunamtii na kumwabudu Mungu kwa sababu yeye ni Muumbaji na Hakimu wetu.)
1. Mtazamo wetu wa Mungu kama Hakimu unazungumzia nini kuhusu mtazamo wetu dhidi ya Amri Kumi?
B. Soma Kutoka 20:8-11. Kuishika Sabato kuna athari gani kwenye mtazamo wetu kwa Mungu kama Muumbaji wetu? (Ni ukumbusho wa kila juma kwamba Mungu ni Muumbaji wetu. Unauhabarisha mtazamo wetu kila juma.)
C. Soma Mathayo 12:40. Wakristo wengi wanaamini kuwa Yesu alisulubiwa siku ya Ijumaa, akapumzika kaburini siku ya Jumamosi, na akafufuka katika uzima wa milele siku ya Jumapili. Kwa nini Yesu aliitunza Sabato hata akiwa amekufa? (Sabato sio tu ukumbusho wa Uumbaji, sasa pia ni ukumbusho wa wokovu wetu kwa njia ya neema pekee. Yesu aliishinda dhambi kwa niaba yetu. Alitupatia zawadi ya uzima wa milele. Tunapaswa kulikumbuka hilo siku ya Sabato. Hii ni sehemu ya muhimu ya “kuiandaa akili.”)
D. Rafiki, sheria ni ya msingi kwenye pambano kati ya wema na uovu. Yesu alikufa ili kuilinda sheria na Shetani anawalenga wale wanaoishika sheria. Je, utachagua upande gani? Ukichagua kufurahia katika sheria Roho Mtakatifu atakusaidia kutimiza hilo. Fanya uchaguzi leo!
V. Juma lijalo: Umizimu Wafichuliwa.