Somo la 8: Nuru Kutoka Patakatifu
Somo la 8: Nuru Kutoka Patakatifu
(Waebrania 8-10)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Juma lililopita tulijadili unabii wa siku 2,300. Sehemu ya unabii huo imethibitishwa kuwa sahihi kabisa, lakini mwisho wake, kama alivyouelewa William Miller, haukuwa sahihi bali uongo kabisa. Miller na rafiki zake waliamini unabii huo ulitabiri mwisho wa dunia kuwa mwaka 1844. Ningekuwa nikiishi katika kipindi hicho, ningekubaliana na ukokotoaji wa Kibiblia wa Miller. Vipi kama alipatia kwenye ukokotoaji wake, lakini akawa amekosea kuhusiana na tukio? Vipi kama kifungu cha Danieli 8:14 kinapaswa kusomwa na kueleweka kama kilivyoandikwa, kiasi kwamba kinaposema “patakatifu patakapotakaswa [au kurejeshwa katika hali yake ya kawaida],” kinamaanisha patakatifu na sio dunia? Tatizo la dhahiri kwenye hitimisho hilo ni kwamba patakatifu palipokuwepo kwenye Hekalu la Pili paliangamizwa na Warumi mwaka 70 BK. Ama kwa hakika hapawezi kutakaswa baada ya kuangamizwa. Fumbo jingine! Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!
I. Patakatifu
A. Soma Kutoka 25:8-9. Sura hii inaanza kwa Mungu kutoa maelekezo kwa Musa kuhusu namna ya kujenga hekalu la Mungu jangwani wakati wa safari ya wana wa Israeli kutoka Misri. Mungu amempa nini Musa cha kumsaidia kutengeneza patakatifu/tabenakulo? (Bombwe/Mpangilio (pattern).)
1. “Bombwe” (Pattern) ni neno lisilo la kawaida kutumika hapa. Tunapozungumzia juu ya kuweka mipango tunairejelea kama michoro au ramani. Je, utaiita ramani ya usanifu majenzi (architectural plan) kama bombwe/mpangilio? (Hapana. Tunatumia neno bombwe (pattern) tunapoona au tunapotafuta kurudia jambo. Bombwe hurudia ubunifu. Unapotoa nakala ya kitu unatumia bombwe (pattern).)
B. Soma Waebrania 8:5. Hivi punde tu tumejifunza kuhusu bombwe/mpangilio (pattern) na maelekezo kwa Musa? (Kuna tabenakulo mbinguni! Alichoelekezwa kukitengeneza Musa kilikuwa na mwelekeo na tabenakulo lililopo mbinguni.)
C. Soma Waebrania 9:1-4. Ubunifu wa tabenakulo la duniani ukoje? (Lilikuwa na vyumba viwili, “Patakatifu” na “Patakatifu pa patakatifu.”)
D. Soma Waebrania 8:1-2. “Mahali patakatifu” panarejelewaje hapa? (Kifungu hiki kinaweka bayana. Hapa ni mbinguni. Hii ni “ile hema ya kweli ambayo Bwana aliiweka,” na sio hema ambayo ilitengenezwa na Musa na wasaidizi wake.)
II. Patakatifu pa Patakatifu
A. Soma Waebrania 9:7 na Mambo ya Walawi 16:32-34. Hizi ni rejea za Siku ya Upatanisho, taratibu ambazo zimefafanuliwa kwa kina kwenye Mambo ya Walawi 16. Ni nini lengo la Siku ya Upatanisho? (Mambo ya Walawi 16:30 inatuambia kuwa iliwatakasa. Katika kipindi cha mwaka, watu walipeleka kafara hekaluni kwa ajili ya msamaha wa dhambi zao. Kisha mara moja kwa mwaka dhambi zote zilizokuwa zimejilimbikiza (accumulated) hekaluni zilitakaswa katika Siku ya Upatanisho.)
B. Kwa nini Danieli 8:14 inarejelea hekalu kutakaswa (mwaka 1844), wakati kimsingi Siku ya Upatanisho hutokea kila mwaka? (Kwa sababu hakuwa akiandika kuhusu Siku ya Upatanisho ya kila mwaka ya hapa duniani.)
C. Soma Waebrania 9:11-12. Tukio hili linatokea wapi? (Hekalu la mbinguni. Tunalifahamu hilo kwa sababu kifungu kinasema hekalu “haikufanyika kwa mikono.”)
1. Yesu anaingia patakatifu mara ngapi? (Mara moja, sio kila mwaka.)
III. Kuhani Wetu Mkuu
A. Hebu tuchunguze anachokifanya Yesu katika patakatifu pa mbinguni. Soma Waebrania 9:13-14. Yesu anafanya nini? (Anaondoa dhambi zetu kwa kafara ya damu yake mwenyewe. Anatutakasa.)
B. Soma Waebrania 9:15, na Waebrania 9:22-24. Je, makuhani katika patakatifu pa duniani walifuata mwelekeo wa kile kitakachofanyika mbinguni baadaye?
C. Soma Waebrania 9:25. Tukio gani mahsusi hapa duniani linarejelewa kwenye kifungu hiki? (Siku ya Upatanisho! Ilifanyika “kila mwaka.”)
D. Soma Waebrania 9:26. Siku ya Upatanisho ya mbinguni inafanyika lini? (“Katika utimilifu wa nyakati.” Hii sio tarehe kamili, lakini inafurahisha kwamba inarejelea “mwisho” wa nyakati.)
1. Ikiwa Siku ya Upatanisho ilikuwa siku kwa ajili ya utakaso wa dhambi za watu, makuhani, na patakatifu, je, inaleta mantiki kwako kwamba Danieli 8:14 inarejelea muda kamili wa Siku ya Upatanisho mbinguni? (Inaendana.)
2. Unadhani kubainisha tarehe ya mwaka 1844 ni muhimu kwa ajili ya wokovu wako au kwenye imani yako kwa Biblia? (Tukio, na sio tarehe mahsusi, ndio suala la msingi. Umuhimu wa mwaka 1844 unaibuka kutokana na suala la uaminifu wetu katika Biblia. Dunia haikukoma mwaka 1844. Hivyo jambo gani lilitokea, ikiwa sio utakaso wa patakatifu pa mbinguni?)
IV. Kupatanisha kwa Muda Gani?
A. Soma Waebrania 10:1-4. Mwandishi wa Waebrania anatoa ulinganifu gani? (Analinganisha sheria na patakatifu pa duniani na kile anachokijadili katika sehemu inayofuata.)
B. Soma Waebrania 10:5-9. Jambo gani limekoma na jambo gani limeanzishwa? (Mfumo wa kale wa kafara umekoma na nafasi yake kuchukuliwa na kile ambacho Yesu atakifanya.)
C. Soma Waebrania 10:10-14. Yesu alitakiwa kutolewa kafara mara ngapi ili kutufanya kuwa wakamilifu? (Mara moja.)
1. Kama Yesu alituokoa kwa kutolewa kafara mara moja, na Siku ya Upatanisho hapa duniani ilikuwa siku moja, Yesu anafanya nini tangu mwaka 1844? Ikizingatiwa kwamba, aliumba ulimwengu kwa juma moja. Jambo gani linaweza kuchukua muda mrefu kiasi hicho?
D. Soma Ufunuo 20:12-13 na Ufunuo 20:15. Nimesikia mara nyingi kwamba Yesu anatumia muda wake mbinguni tangu mwaka 1844 akifanya kazi kama mwanasheria akijenga hoja kwa ajili ya wokovu wa wenye haki. Anajenga hoja kwa kila mmoja wetu. Hilo huchukua muda mrefu. Je, hilo linaendana na vifungu hivi katika kitabu cha Ufunuo? (Hapana. Kazi pekee inayochukua muda mrefu ni kuwahukumu wale wote waliopotea kwa kufanya mapitio ya “kile walichokitenda” katika kipindi cha uhai wao. Kwa wenye haki ni tofauti kabisa. Umakini pekee ni kuangalia kama majina yao yameandikwa kwenye kitabu cha uzima.)
1. Je, Yesu anaenenda kama Kuhani Mkuu mbinguni kwa ajili ya waliopotea? (Hicho sicho kilichofanyika katika patakatifu pa duniani katika Siku ya Upatanisho.)
2. Ukosoaji wa tarehe ya mwaka 1844 ni kwamba haina mantiki yoyote. Yesu anaweza kuwa anafanya nini kama Kuhani Wetu Mkuu ikiwa suala la hukumu ni endapo tu jina letu limeandikwa katika Kitabu cha Uzima?
E. Soma Waebrania 4:14-16. Kifungu hicho kinasema kuwa Yesu anafanya nini Mbinguni kwa niaba yetu? (Anatutia moyo.)
F. Soma Waebrania 3:1-2. Utaona kwamba Yesu analinganishwa na Musa, ambaye hakuwa kuhani achilia mbali Kuhani Mkuu. Hii inatuambia nini kumhusu Yesu?
G. Soma Waebrania 3:3-6. Musa aliwafanyia nini watu wa Mungu waliposafiri kupitia jangwani? (Musa alikuwa mpatanishi kati ya Mungu na watu. Musa aliwaongoza watu na kuwatia moyo kutenda yaliyo sahihi.)
H. Tunaposoma katika Waebrania 4:15-16 kuhusu Yesu kutuonea huruma kutokana na udhaifu wetu na kutupatia ujasiri katika neema, utalinganishaje hilo kwenye ulinganifu na Musa? (Musa alikuwa mwanadamu aliyewaongoza watu katika nchi ya ahadi. Alikuwa mwakilishi wa Mungu kwa watu. Yesu, kutokana na kafara yake kwa niaba yetu, anaifungua nchi ya ahadi mbinguni kwetu. Tunatiwa moyo kila mara kwa neema, kile Yesu alichotutendea.)
I. Soma Waebrania 1:3. Kifungu hiki kinasema kuwa Yesu alikaa lini mkono wa kuume wa Mungu? (“Akiisha kufanya utakaso wa dhambi.”)
1. Je, hapo ni pale alipopaa mbinguni siku ya Jumapili baada ya mateso, au mwaka 1844? (Ninadhani kuna hoja ya nguvu kwa mwaka 1844. Sehemu kubwa ya Waebrania imejikita kuzungumzia kuhusu Yesu kama Kuhani Wetu Mkuu mbinguni. Ingawa kafara zilitolewa kila siku katika patakatifu pa duniani, utakaso kamili ulifanyika Siku ya Upatanisho pekee.)
2. Kwa nini kusubiri hadi 1844? Kwani tarehe hiyo inaleta mantiki yoyote? (Haitakuwa na mantiki kama hukubaliani na unabii wa siku 2,300 na kauli ya Danieli 8:14 kwamba katika tarehe maalumu patakatifu patatakaswa. Utaona kwamba unabii wa siku 2,300 HAUWEKI tarehe kwa ajili ya utakaso katika kipindi cha kusulubiwa kwa Yesu.)
3. Hebu turejee kwenye ulinganifu kati ya kazi ya Yesu na kazi ya Musa. Kwa nini Mungu alisubiri mamia ya miaka ili kuwaokoa watu wake kutoka Misri? Je, muda (timing) huo unaleta mantiki yoyote kwako? (Tunatakiwa kupokea kile ambacho Mungu ametufunulia na sio kukikataa kwa msingi wa mantiki yetu.)
J. Rafiki, usipotee kwenye mjadala wa muda (timing). Furahi kutokana na ukweli kwamba Yesu alishinda dhidi ya dhambi na kifo na anafanya kazi kwa niaba yako mbinguni sasa hivi. Je, utampokea na kumkiri kama Mwokozi wako? Kwa nini usifanye hivyo sasa hivi?
V. Juma lijalo: Msingi wa Serikali ya Mungu.