Somo la 4: Bwana Anasikia na Kutenda
Somo la 4: Bwana Anasikia na Kutenda
(Zaburi 17, 123, 139 & 1 Wakorintho 10)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Visa viwili vinapamba somo letu juma hili. Kisa kimoja kinamhusisha mshiriki wa kanisa ambaye alikuwa na uhakika kuwa Mungu angemponya ugonjwa wa saratani. Mshiriki huyu alikuwa mwanamke. Wakati fulani mshiriki huyu alipata mshtuko alipotambua kuwa atakufa. Niliweza kuona masikitiko yake makuu machoni mwake. Miongo kadhaa imeshapita, lakini bado ninakumbuka mwitiko (reaction) wake kabla hajafariki. Kisa kingine kinatoka kwa mhubiri maarufu. Nilimsikia akisema kuwa anamwomba Mungu kwa ajili ya kumpatia nafasi nzuri ya kuegesha gari – na kweli anapata nafasi nzuri. Kwa nini mwanamke mmoja mwaminifu anafariki wakati mwingine anazawadiwa nafasi nzuri ya kuegesha gari – jambo dogo/hafifu? Hebu tuzame kwenye somo letu la Zaburi na tujifunze zaidi!
I. Anaona na Kusikia
A. Soma Zaburi 139:1-5. Je, unadhani uhusiano huu wa karibu ni kwa sababu tu Mfalme Daudi ni mtu wa muhimu sana?
1. Je, Mungu anawasaidia watu wa muhimu kupata eneo la kuegesha gari na watu wadogo wanakufa kwa saratani?
B. Soma Zaburi 139:6. Daudi ananena jambo gani la msingi linalojibu maswali niliyouliza? (Daudi anaandika kuhusu uwezo wa Mungu usio wa kawaida. Mungu anajua kila kitu kumhusu. Mungu anajua kila anachokiwaza Daudi na kile anachotaka kukisema. Kuelewa maarifa haya ya Mungu mwenye uwezo wote ni jambo la “juu.” Kama ilivyo kwa Daudi tunapata taabu kufikia kiwango cha kulielewa jambo hilo!)
1. Je, kuna sababu yoyote ya Mungu kutenda jambo hili kwa Mfalme Daudi na sio kwako? (Hii inasisitiza juu ya udhaifu katika fikra ya mwanadamu: kwamba uwezo wa Mungu una ukomo. Ikiwa uwezo wa Mungu hauna ukomo basi hana haja ya kugawa msaada wake. Hana haja ya kufanya uamuzi juu ya nani wa kumsaidia kwa sababu haweza kumsaidia kila mtu kwa wakati mmoja. Hiki ndicho ambacho Daudi anakiita “Maarifa [ambayo] ni ya ajabu sana kwangu; yako juu; siwezi kuyafikia.”)
C. Soma Zaburi 139:7-12. Je, ungependa kuukimbia uwapo wa Mungu?
1. Kwa nini mtu anajibu, “Ndiyo?” (Sababu pekee itakuwa ni endapo mtu huyo alijihusisha na mambo ambayo Mungu hayaidhinishi.)
a. Jambo gani la muhimu ambalo kimantiki linatokana na hili? (Ufahamu wa Mungu wa hali yetu hautokani na endapo tu watiifu. Hatuwezi kumkimbia hata kama tupo kuzimu.)
2. Hebu turejee kwa mshiriki mwenzangu wa kanisa aliyeshtushwa kutambua kwamba Mungu hatamsaidia. Unadhani alikuwa anawaza nini kuhusu sababu za Mungu? (Kimantiki itakuwa ni kwamba hakustahili. Hakuwa mtiifu kwa namna fulani.)
3. Ikiwa kiwango chetu cha utii hakiathiri uelewa wa Mungu wa hali yetu, hitimisho ni lipi la kwa nini Mungu hakumponya mshiriki wa kanisa aliyeamini kuwa Mungu angemponya? (Mungu alifanya uamuzi wa kiutendaji wa kutomponya kwa wakati huo. Mungu aliruhusu afariki na kisha kumponya wakati wa ujio wa Yesu Mara ya Pili.)
D. Soma Zaburi 139:13-16. Mungu alijihusisha nawe kiasi gani kabla hujazaliwa?
1. Mungu alijua nini kuhusu urefu wa maisha yako kabla hujazaliwa? (Mungu ameandika katika kitabu chake idadi ya siku ambazo Daudi angeishi hata kabla Daudi hajaiona siku yake ya kwanza duniani!)
2. Hiyo inazungumzia nini kuhusu Mungu na mshiriki wa kanisa ambaye alikuwa na uhakika kuwa angeponywa? (Mungu alifanya uamuzi wa suala hili kabla “hajaumbwa.”)
3. Tunapaswa kuwa na mwitiko gani juu ya suala hili – wakati ambapo maisha yetu ndio yanayoning’inia kwenye mzani? (Tunatakiwa tu kumwamini Mungu. Mungu hana uzembe kwa upande wake. Amefanya uamuzi wa busara baada ya kujua kweli zote.)
a. Vita ya Shetani kwetu inaathirije swali hili?
E. Soma Zaburi 139:17-19. Je, Mfalme Daudi ana njia ambayo anataka Mungu aichukue? (Ndiyo. Anataka waovu wauawe ili waachane naye. Wakati huo huo Daudi anatambua kuwa mawazo ya Mungu ni makubwa mno. Ni mapana kuzidi uwezo wa Daudi kuyafumbata.)
1. Je, Mungu anaweza kukutafutia nafasi ya kuegesha gari? (Kwa nini asiweze? Hilo halimsumbui Mungu kutokana na uwezo wake. Anajua kila kinachokuhusu. Anaweza kukusaidia kutafuta na kupata ufunguo wa gari lako.)
F. Soma Zaburi 121:6-8. Mshiriki wa kanisa aliyekuwa anakufa kwa saratani anapaswa kuvielewaje vifungu hivi? Saratani ilikuwa uovu uliokuwa unayachukua maisha yake! (Soma Zaburi 121:2-4. Uamuzi wa kuruhusu mwanamke huyu afariki kwa saratani haikuwa kwa sababu Mungu hakuwa na uwezo wa kuponya au kwa sababu hakuwa mzingativu. Mungu atampatia mwanamke huyu uzima wa milele badala ya nyongeza ya muda mfupi wa maisha sasa hivi.)
II. Imani (Confidence)
A. Soma Zaburi 17:6. Daudi anasema kuwa Mungu “ataniitikia.” Ukipitia Zaburi 17:1-5 utaona kuwa Daudi anajenga hoja jinsi alivyokuwa mkuu na mtiifu. Je, tunapaswa kuwa watiifu ili Mungu aweze kutusikia? (Hicho ndicho ambacho tumekijadili hivi punde. Sidhani kama tunatakiwa kuwa watiifu ili Mungu aweze kutusikia.)
1. Ikiwa hilo ni kweli, Daudi anazungumzia jambo gani? (Daudi anaamini kuwa Mungu anapofanya uamuzi wa kiutendaji wa kusaidia, sehemu ya uamuzi unageukia kwenye suala la endapo tumekuwa waaminifu.)
B. Soma Kumbukumbu la Torati 28:1 na Kumbukumbu la Torati 28:15. Je, unadhani hii ni sehemu ya fikra ya Daudi? (Agano la Kale liko wazi kwamba kanuni ya jumla ni kwamba matokeo ya utii ni baraka na matokeo ya kutokutii ni laana. Bila shaka hilo lilisadifu fikra ya Daudi.)
1. Katika muktadha huo, unawaelezeaje Ayubu na Yona? (Kama unavifahamu visa hivi vya Biblia, unafahamu kwamba Mungu alisikia na kujibu maombi ya Yona baada ya uasi wake kuyaweka maisha yake hatarini. Ayubu aliteseka mambo ya kutisha ingawa alikuwa mwaminifu. Nadhani fundisho ni kwamba mara zote Mungu anasikia. Anachokijibu Mungu kinaweza kwa sehemu fulani kugeukia kwenye utii wetu.)
2, Kichwa cha sehemu hii ni “Imani.” Baada ya mjadala huu, unaweza kuwa na imani juu ya jambo gani? (Mara zote Mungu anatupenda na anatusikiliza. Hiyo haimaanishi kwamba Mungu atatenda kile tunachokitaka. Licha ya hayo, tunatakiwa kuuamini uamuzi wake.)
III. Kutokuwa Tayari
A. Soma Mathayo 23:37-38. Hivi punde tumemaliza kujadili endapo msaada wa Mungu unageukia kwenye utii wetu. Yesu anatufundisha nini kuhusu utayari wa Mungu na utayari wetu linapokuja suala la baraka? (Mungu anasikia na yuko tayari kubariki. Sisi ndio tunaomkataa Mungu. Sisi ndio wale ambao hatuko tayari kukusanywa salama chini ya mbawa za Mungu.)
1. Je, watu walioukataa ulinzi na baraka za Mungu walikuwa watu wa dini?
a. Ni kwa jinsi gani sisi ambao ni watu wa dini tunaepuka kuanguka kwenye tatizo hilo hilo? (Kifungu kinaashiria kuwa walikuwa waasi. Waliwapiga mawe na kuwaua manabii. Waliitaka dini yao wenyewe badala ya dini ya Mungu.)
b. Mungu ni mvumilivu kiasi gani kuhusu uasi wetu? (Wewe na mimi tutaacha kutoa msaada baada ya mauaji mamoja! Kwa nini kuwasaidia watu kama hao? Lakini Yesu alikuja kwa watu wake hata kama walimuua! Mungu ni mvumilivu sana kuliko sisi.)
B. Soma 1 Wakorintho 10:1-4. Kundi hili lina faida gani za kiroho?
C. Soma 1 Wakorintho 10:5-6. Ni nini sababu ya kushindwa kwa watu hawa? (Walitamani uovu.)
D. Soma 1 Wakorintho 10:7-10. Uovu umeelezewaje? (Unabainisha mambo manne: uabudu sanamu (ikinukuu Kutoka 32:6 kuhusu ndama wa dhahabu), uasherati (ikirejelea Hesabu 25:1-9), kumjaribu Yesu (yumkini ikirejelea Hesabu 21:5-9), na manung’uniko.)
E. Soma 1 Wakorintho 10:11-13. Je, ujumbe wa wale waliokufa jangwani ni kwa ajili yetu? (Ndiyo! Hiki ndicho tunachotakiwa kukiepuka. Hatupaswi kuchukulia kwamba tuko sawa.)
1. Ahadi gani inatolewa ili kututia moyo? (Mungu hatatupatia jaribu lililo kubwa kupita kiasi. Ataweka njia ya kutokea.)
F. Rafiki, je, unauona mpango wa Mungu wa kukuokoa wenye safu mbili? Kwanza, tunaona kwamba Mungu anasikia na kusaidia. Wasiohusika hapa (exception) ni wale wasio tayari kuwa na uhusiano na Mungu. Lakini hata kwa watu hao, Mungu ana hatua inayofuata, atahakikisha kuwa unakuwa na uwezo wa kuwa na uhusiano naye. Hakuna kinachoweza kukuzuia kumchagua Mungu, tofauti na uhuru wako wa uchaguzi. Je, utafanya uchaguzi, sasa hivi, kuingia ndani ya duara la ulinzi na hekima ya Mungu?
IV. Juma lijalo: Kuimba Wimbo wa Bwana Katika Nchi ya Ugenini.