Somo la 3: Bwana Anatawala
Somo la 3: Bwana Anatawala
(Zaburi 8, 75, 105 & 119)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2024, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Inamaanisha nini, kiuhalisia, kumwamini Mungu mwenye enzi? Mtazamo wako wa kiulimwengu na matendo yako vingekuwaje kama kweli unamwamini Mungu aishiye mwenye nguvu? Kwanza, utaamini kile anachokisema. Kama Mungu anasema kuwa aliumba kila kitu, na unaona vitu (kwa mfano wewe mwenyewe) ambavyo huwezi kuvielezea kikamilifu, basi unapaswa kumwamini. Ikiwa Mungu anasema kuwa kama Muumba ana mpango kwa ajili ya maisha mazuri, basi tunapaswa sio tu kumwamini, bali kuufuata mpango wake. Ikiwa Mungu anasema kuwa kanuni zake ni za muhimu kwa ajili ya kuendelea kuwapo kwa wanadamu, na kwamba ataleta hukumu kwa wale wanaoasi dhidi yake, tunapaswa kumwamini na kujaribu kutii na sio kuasi. Mambo yote haya yamo kwenye somo letu la Zaburi juma hili. Hebu tuzame kwenye somo letu na tujifunze zaidi!
I. Mungu Muumbaji
A. Soma Zaburi 8:3-4. Nani aliyeumba mbingu? (Mungu!)
1. Hiyo inaashiria nini kuhusu upendo wa Mungu kwa ajili yetu? (Kama kifungu cha nne kinavyouliza, kwa nini mtu huyo mwenye nguvu, ambaye ana kila aina ya uumbaji, ajali kuhusu uumbaji wake mmoja?)
2. Miaka mingi iliyopita nilinunua gari ambalo mimi na kijana wangu tuliliona tulipokuwa matembezini. Nililinunua kwa dola 200. Bahati iliyoje! Baadaye, nilisikia habari za binti mmoja kanisani aliyehitaji gari. Kwa kusita sana niliamua kuwa lazima nimuuzie binti huyu gari lile. Jibu lake linaakisi kifungu cha 4: hakutaka gari langu la hali ya chini, na alitaka kujua kwa nini mwanasheria anunue gari kama hilo? Niliendesha gari hilo kwenda kazini kwa miaka mingi baada ya tukio hilo. Je, hii inaashiria jibu la sababu ya Mungu kutujali? (Nilikuwa na vichache kwenye gari lile, Yesu aliwekeza kila kitu kwetu. Swali halisi ni kwamba, “Kwa nini Mungu afanye hivyo?” Jibu ni kwamba Mungu anatupenda. Ninapenda “deals!”)
B. Soma Zaburi 8:5-8. Mungu wetu Muumbaji ameamua nini kuhusiana na mpangilio wa utawala wa uumbaji wake? (Sio tu kwamba Mungu anatujali, bali ametufanya kuwa watawala juu ya uumbaji wake. Kwa umahsusi, ametufanya tutawale juu ya dunia na wanyama.)
C. Soma Zaburi 100:3-4. Tunapaswa kuwa na mwitiko (reactions) gani mwingine kwa Mungu Muumbaji wetu? (“Sisi tu watu wake.” Tuna hisia za kumilikiwa. Tunapaswa kuwa na hisia za shukrani.)
II. Mungu wa Agano
A. Soma Zaburi 105:7-10. Agano gani linafanyika na Ibrahimu, Isaka na Yakobo? (Soma Zaburi 105:11. Mungu aliwapatia Kanaani.)
1. Hiyo inasema nini kuwahusu wale ambao leo wanatamani kuiangamiza Israeli?
B. Soma Wagalatia 3:27-29. Nani ambaye ni mnufaika wa hili agano la kale? (Kila “aliyebatizwa katika Kristo.”)
1. Je, hiyo inamaanisha kuwa tunaipata nchi? Kwamba Kanaani ni yetu, pia? (Hebu tuendelee kusoma katika Zaburi 105.)
C. Soma Zaburi 105:16-19. Ni kwa jinsi gani njaa na Yusufu kufanywa kuwa mtumwa vinakuwa sehemu ya agano? (Soma Zaburi 105:20-24. Tunaanza kuona taswira ya kwamba kuwa na nchi ni sehemu tu ya agano na Mungu. Mungu anabuni njia ya kuwalinda watu wake dhidi ya njaa.)
1. Ungesema nini kuhusu agano kama ungekuwa Yusufu? (Zaburi 105:19 inasema kuwa Mungu alimjaribu Yusufu. Mwisho wa jambo hili ni kwamba Yusufu alikuwa “mtawala wa vyote alivyovimiliki [Farao].”)
2. Kama unakifahamu kisa, unadhani ni haki kusema kwamba “Mungu alimjaribu” Yusufu? Je, ni haki kusema kuwa Mungu alileta njaa? (Soma Mwanzo 37:26-28. Shetani kuwajaribu ndugu wa Yusufu kutenda uovu ndio sababu ya jaribu la Yusufu. Njia sahihi ya kuliangalia jambo hili ni kwamba Mungu aliruhusu Yusufu atendewe vibaya kwa kipindi kifupi ili kutafuta suluhisho la tatizo la njaa. Mungu alibadili kuwa ushindi kile alichokipanga Shetani kuwa uovu.)
D. Soma Zaburi 119:97-100. Agano la Mungu linatoa jambo gani jingine? (Linatufanya tuwe na hekima kuliko wale wasiozingatia sheria ya Mungu.)
E. Soma Zaburi 119:101-105. Mtunga Zaburi anaposema kuwa neno la Mungu “ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu,” hilo linamaanisha nini kiuhalisia? (Neno la Mungu linatusaidia kuepuka maanguko na matatizo katika maisha. Linatusaidia kuepuka kuaibishwa.)
F. Soma Zaburi 119:114. Je, hii inafanana na Mungu kuwapatia watu wake nchi yao? (Anawafanya wawe salama mbele ya taabu.)
G. Soma Zaburi 119:173-176. Mtunga Zaburi anaifurahia sheria ya Mungu. Kwa nini anaifurahia? (Anajua kwamba kuzishika sheria za Mungu humsaidia.)
1. Je, uelewa huu wa baraka zinazotokana na sheria ya Mungu unamfanya mtunga Zaburi kuishika sheria kikamilifu? (Sio nyakati zote kwani anakiri “kutanga-tanga.”)
2. Mtunga Zaburi anasema kuwa Mungu atafanya nini atakapotanga-tanga? (Mungu “atamtafuta” mtumishi wake.)
H. Utaelezeaje kwa ufupi manufaa ya kuishika sheria ya Mungu? Ya kuingia agano na Mungu?
I. Tunapozungumzia juu ya kuzishika sheria za Mungu, je, tunazungumzia kuhusu ufunguo wa wokovu? (Soma Zaburi 51:1-2, na Zaburi 51:7-10. Zaburi hii kwa dhahiri inazungumzia kuhusu neema ya Mungu.)
J. Soma Zaburi 103:1-6, Zaburi 103:13-14, na Zaburi 103:17-19. Taswira gani ya haki ya Mungu kwa ajili yetu inaonekana kwenye vifungu hivi?
K. Soma Waefeso 2:8-10. Hii inatuambia nini kuhusu wokovu kwa njia ya neema pekee? (Zaburi haziko wazi kuhusu neema kama yalivyo maandiko ya Paulo. Hilo linatarajiwa kutokana na nyakati (timing) za Agano la Kale na Agano Jipya.)
III. Mungu wa Hukumu
A. Soma Zaburi 75:1-3. Mungu anasema kuwa atahukumu “kwa haki” katika muda atakaouchagua. Unadhani kwa nini kinachofuata Mungu anajadili kuhusu kutokuwa imara kwa dunia? (Ninachokiona ni kwamba Mungu anaingilia kati ili kusahihisha mambo. Mungu anaimarisha mambo.)
B. Soma Zaburi 75:4-7. Mifumo gani miwili ya mamlaka inalinganishwa hapa? (Kwa upande mmoja ni watu wenye nguvu na majivuno ambao wako kinyume na Mungu. “Pembe yako” inawakilisha mamlaka – kama ilivyo katika dunia ya wanyama. Kwa upande mwingine ni hukumu ya Mungu ambayo inamwinua mmoja na kumshusha mwingine.)
1. Je, hukumu ni nzuri? (Hatutaki wenye majigambo na wenye nguvu watawale kwa kuwa hapatakuwepo na viwango vya kimaadili. Badala yake, Mungu anatuambia kuwa atatoa hukumu kwa mujibu wa jinsi mambo yanavyopaswa kuwa.)
C. Soma Zaburi 75:8. Waovu wameandaliwa nini? (Mungu anawafanya wanywe “mvinyo unaotoka povu ... naye huyamimina.”)
1. Je, hilo ni jambo jema? (Mojawapo ya jinsi neno hili linavyosomeka ni mvinyo “unaotoka povu.” Hili sio jambo zuri.)
2. Utaona kwamba mvinyo “umechanganywa vizuri.” Unadhani hiyo inamaanisha nini? (Nadhani hukumu imerekebishwa ili kufikia uovu unaofanywa na mtu aliyepotea. Hii ni hoja nyingine dhidi ya kuungua milele kwa wote waliopotea. Je, unadhani kosa lolote lililotendwa na mwanadamu linahalalisha kuungua milele? Binafsi sidhani hivyo.)
3. Kifungu kinaposema mvinyo unaotoka povu hufyonzwa na kunywewa, hiyo inamaanisha nini? (Hukumu kamili. Wanapata kile wanachostahili.)
D. Soma Zaburi 75:9-10. Mpangilio wote huu mpya wa pembe unamaanisha nini? (Waovu wanapoteza uwezo wao na wenye haki sasa wako madarakani.)
E. Angalia tena Zaburi 75:9. Hizi ni habari njema kwa waliookolewa ambao wananyanyaswa na waovu! Je, hii inaonesha upendo wa Mungu? (Inaonesha upendo wake kwa wale wanaomchagua na upendo wa Mungu kwa ajili ya haki.)
F. Soma Zaburi 25:15. Unadhani inamaanisha nini kutolewa katika nyavu? (Unaokolewa kutoka kwenye kitu kilichokukamata.)
G. Soma Zaburi 25:16-18. Jambo gani lipo kwa ajili ya waovu linaloonesha upendo mkuu wa Mungu kwa kuzingatia hukumu inayokuja? (Mungu atatusamehe dhambi zetu zote. Mungu anatupatia njia kutokana na hukumu.)
H. Soma Zaburi 25:19-22. Watu wabaya wanawachukia watu wa Mungu. Tunapaswa kufanya nini kuhusiana na hilo? (Tunamwomba Mungu atulinde wakati tukiendelea kumngojea.)
I. Rafiki, hizi ni habari njema! Mungu wetu Muumbaji anatawala! Sio tu kwamba atakuwa pamoja nasi, bali pia atatupatia ushindi na kutawala huku akitupatia upendeleo katika hukumu yake. Wakati huo huo, je, utawapa hizi habari njema wale ambao pengine hawazijui?
IV. Juma lijalo: Bwana Anasikia na Kutenda.