Somo la 12: Esta na Mordekai

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Esta 2-8
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
4
Lesson Number: 
12

Somo la 12: Esta na Mordekai

(Esta 2-8)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, una haja ya kuwa makini juu ya kile unachokisema kuhusiana na imani yako ya dini? Miaka michache iliyopita, wakati masomo yalipohusisha ulinganifu wa Uislamu na Ukristo, mmojawapo wa watafsiri wangu aliniambia kuwa anapaswa kuwa na tahadhari juu ya kile anachokiandika kuhusu Uislamu. Kwa dhahiri, nilichokiandika kwenye somo kilikuwa na utata! Kwa kuwa nimeishi maisha yangu yote nchini Marekani, na katika kipindi chote hicho nimekuwa mwanasheria ninayetetea uhuru wa maoni wa Wamarekani, ninakataa dhana ya kuhatarisha (compromise) haki yangu ya kusambaza injili. Sio kila asomaye somo hili anao uhuru kama huu. Hata nchini Marekani haki ya uhuru wa dini kwa sasa inashambuliwa. Vyuo vikuu vyenye wasomi havilindi tena uhuru wa maoni, na baadhi ya majimbo yamekuwa yakifanya kazi kwa nguvu kukandamiza uhuru wa maoni. Tunatakiwa kujifunza kile Biblia inachotufundisha kuhusu kushiriki imani yetu na watu wengine katika mazingira yenye uhasama. Hebu tuanze sasa hivi!

I. Mordekai

A. Soma Esta 2:5-6. Hii inatufundisha nini kumhusu Mordekai? (Mordekai ni Myahudi. Yeye (au mababu zake) walikuwa sehemu ya kundi lililochukuliwa na kupelekwa Babeli wakati Nebukadreza alipoiteka Yerusalemu.)

1. Soma Danieli 1:6-7. Fikiria kile unachokijua kuhusu kisa cha Danieli na uzoefu wake kama mateka mpya. Je, watu wa Babeli walikuwa wanajaribu kuhifadhi utamaduni na imani za kidini za Kiyahudi? (Hapana. Walibadili majina ya mateka wao kama sehemu ya juhudi za kuwafanya waendane na kukubali utamaduni na imani za Kibabeli.)

B. Soma Esta 2:7. Hii inatuambia jambo gani jingine kuhusu Mordekai? (Anaamini katika familia. Anamhurumia Esta ambaye ni yatima. Anamchukua nyumbani kwake na kumtendea kama binti yake.)

C. Hebu turukie chini hadi Esta 2:19. Je, Mordekai alikuwa mzururaji tu? Au hii inatuambia jambo muhimu kumhusu? (Hiki ni mojawapo ya vifungu vitatu vinavyotuambia kuwa Mordekai aliketi mlangoni pa Mfalme. Hii inaashiria kuwa yeye ni afisa wa mahakama katika serikali.)

II. Esta

A. Soma Esta 2:7-8. Tunajifunza habari gani kumhusu Esta? (Ni mwanamke mzuri sana. Mzuri sana kiasi kwamba mawakala wa mfalme wanamchukua kutokana na uzuri wake.)

B. Soma Esta 2:9, Esta 2:12-13, na Esta 2:15. Sio tu kwamba Esta ni mrembo, tunagundua jambo gani jingine kumhusu? (Ana hulka ya ushindi. Anatawala hisia (she has emotional intelligence).)

C. Isipokuwa tu kama unafahamu historia ya kisa hiki, unaweza kushangaa jambo gani linamtokea Esta. Je, serikali inawachukua wanawake wazuri mara kwa mara na kisha kuwafanya kuwa warembo zaidi? Soma Esta 1:10-12 na Esta 1:17 na Esta 1:19-20. Kwa nini kuna nafasi ya wazi kwa Malkia wa Waajemi? (Malkia Vashti hamtii Mfalme. Kinachoumiza akili miongoni mwa wanaume ni kwamba kitendo hiki kinaweza kuamsha uasi miongoni mwa wake (wives) wote. Vashti anaondolewa kwenye nafasi yake, na Esta ni sehemu ya utafutwaji unaofanyika kwa ajili ya malkia mpya.)

D. Soma Esta 2:10. Je, ingekuwa tatizo kwa Mfalme kumchagua malkia wa Kiyahudi? (Kwa dhahiri, Mordekai alidhani hivyo.)

1. Una maoni gani kuhusu uaminifu wa kile ambacho Mordekai na Esta wanakifanya? (Hakuna chochote kwenye kifungu kinachosema kuwa Esta alidanganya kuhusu ukoo wake katika kujibu maswali. Badala yake, hakujitolea kutoa taarifa. Huu ndio ushauri ambao huwa ninawapatia wateja mara kwa mara pale wanapoulizwa maswali chini ya kiapo. Hawana haja ya kujitolea kutoa taarifa.)

III. Hamani

A. Soma Esta 3:1-2 na Esta 3:5. Unadhani kwa nini Mordekai alikataa kumheshimu Hamani? (Soma Esta 3:3-4. Mordekai alipoulizwa swali hilo alijibu kuwa “yeye ni Myahudi.”)

1. Unadhani hiyo inamaanisha nini? (Kwa hakika Mordekai aliamini kuwa ni makosa kumwabudu mwanadamu. Angalia Kutoka 20:3-5. Maoni ya “The Bible Knowledge Commentary” yanajenga hoja kwamba suala sio kuabudu bali kuonesha heshima kwa Hamani. Hii haifanani na kisa cha Danieli 3 ambapo ibada halisi ya sanamu ilihusika.)

2. Baadhi ya watu wanajenga hoja kwamba kama Myahudi, Mordekai angepinga kuonesha heshima kwa mtu aliyetoka kwa Agagi, Mfalme wa Waamaleki. “The Bible Knowledge Commentary” inabainisha kuwa Agagi aliishi miaka 600 kabla, hivyo uhusianisho na Agagi ni jambo lisiloelekea (unlikely). Bali, wanaakiolojia waligundua jimbo katika Ufalme wa Waajemi lililoitwa Agagi, na kuna uwezekano mkubwa kwamba Hamani alitoka katika jimbo hilo. Una maoni gani kuhusu mitazamo hii miwili tofauti?

3. Utaona kwamba Mordekai alimwambia Esta asidhihirishe kuwa yeye ni Myahudi (Esta 2:10), lakini Mordekai anawaambia wale wanaouliza kwa nini anakiuka sheria kwamba yeye ni Myahudi (Esta 3:4). Kwa nini majibu tofauti?

B. Soma Esta 3:5-6 na Esta 3:8-11. Matokeo ya uamuzi wa Mordekai ni kutolewa kwa amri ya kuwaua Wayahudi wote. Je, haya ni matokeo ya mgongano kati ya majivuno ya Hamani na majivuno ya Mordekai? Au, je, haya ni matokeo ya Mordekai kuzifuata Amri Kumi? (Hili ni swali muhimu ambalo kila mmoja wetu anatakiwa kulitafakari. Je, tuna matatizo na wapagani kwa sababu ya majivuno yetu, au kwa sababu ya utiifu kwa Mungu?

1. Angalia tena Esta 3:8. Je, hii inaashiria kuwa hili ni suala la majivuno, au suala la imani ya kidini? (Hamani anataarifu kuwa Wayahudi wanafuata sheria zao. Nadhani uelewa mzuri ni kwamba Mordekai alichukua msimamo wake kutokana na sababu za kidini.)

IV. Wokozi

A. Soma Esta 4:1. Mordekai amefanya nini? (Matendo yake yatasababisha watu wake waangamizwe.)

1. Mordekai na Esta wangeweza kurejea Israeli. Je, wamefanya kosa kukaa katika taifa la kipagani?

2. Unadhani Mungu angesema nini kuhusiana na uamuzi wa kutorejea, “Umechukua uamuzi wako, sasa unatakiwa kuishi kutokana na uchaguzi wako?”

B. Soma Esta 4:8 na Esta 4:10-12. Kuna tatizo gani kwa Esta kutii amri ya Mordekai? (Angeweza kufa.)

C. Soma Esta 4:13. Je, unakubaliana na Mordekai? Kumbuka kwamba alimwambia Esta asimwambie mfalme kuwa alikuwa Myahudi.

1. Kama ungekuwa Esta, je, ungetafakari kwa kina kwamba unaweza kuepuka amri ya kifo? (Nadhani kuna uwezekano kuwa atakiepuka. Hamani asingemshambulia Malkia. Lakini, kwa hakika atampoteza Mordekai.)

D. Soma Esta 4:14-16. Mordekai na Esta wanakubaliana juu ya jambo gani? (Kwamba Mungu atawasaidia Wayahudi.)

1. Utaona kuwa Esta 4:16 inatoa wito wa kufunga na sio kuomba (prayer). Soma Danieli 9:3 kwa ajili ya kufanya ulinganifu. Je, unadhani kuwa walifanya maombi na kifungu hakibainishi tu maombi hayo? (Kuna shaka kwamba Mordekai na Esta hawakuwa watu wa dini sana. Kwa nini Modekai anarejelea kuokolewa “kutoka mahala pengine” na sio kurejelea Mungu kuwaokoa watu wake?

E. Katika Esta 5 tunaona kuwa Esta anaweka maisha yake rehani na kujitokeza mbele ya Mfalme bila kukaribishwa. Mfalme anamsikiliza (badala ya kuamuru auawe) na Esta anawaalika Mfalme na Hamani katika chakula cha jioni. Soma Esta 5:12-14. Hamani ana mpango gani kwa ajili ya chakula cha jioni kati yake na Mfalme na Esta? (Atahudhuria na kufurahia wazo la Mordekai kunyongwa.)

F. Chakula cha jioni cha kifalme kimeandaliwa! Soma Esta 7:3-10. Je, Hamani amezidiwa ujanja? Je, Mungu amepindua meza? Unayaelezeaje matokea haya? (Kwenye suala la endapo Esta na Modekai ni watu wa dini, matokeo ni ya kupendeza sana kiasi kwamba lazima huu utakuwa mkono wa Mungu. Tunaweza kuuona mkono wa Mungu kuanzia mwanzoni kabisa mwa kisa.)

1. Hii inatufundisha nini kuhusu kuwa waaminifu katika nchi ya kipagani?

G. Soma Esta 8:1-3. Kisasi kimekamilika kwa Hamani na nyumba yake, lakini tishio gani la kutisha bado limesalia? (Amri ya kifo kwa Wayahudi.)

H. Soma Esta 8:11. Una maoni gani juu ya jibu hili? Je, hiki ndicho kinachoendelea sasa hivi kule Gaza?

I. Soma Esta 8:15-17. Je, huu ni ushindi mkubwa kwa Mungu? Je, kuna waongofu wengi kwenye dini ya Kiyahudi (Judaism) kwa sababu ya hofu? (Hatupendi kudhani kuwa tunapaswa kutumia hofu ili kuwaongoa watu wengine, lakini angalia jinsi jambo hili linavyomwinua Mungu Mkuu wa Mbinguni dhidi ya miungu mingine yote katika nchi? Nadhani kuuogopa uwezo wa Mungu wa kweli ndilo jambo linalomaanishwa hapa.)

J. Rafiki, tukio la ajabu kiasi gani kwa Esta na Mordekai! Je, utamtumaini Mungu katika mazingira ya kutisha? Je, utakuwa radhi kujitoa kafara kwa manufaa ya wengine?

V. Juma lijalo: Mwisho wa Utume wa Mungu.