Somo la 11: Utume kwa Wasiofikika: Sehemu ya 2

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
1 Wafalme 11, Mathayo 15, Matendo 10
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
4
Lesson Number: 
11

Somo la 10: Utume kwa Wasiofikika: Sehemu ya 2

(1 Wafalme 11, Mathayo 15, Matendo 10)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, huwa unakubaliana na mitazamo ya marafiki wako? Ikiwa hukubaliani nayo, je, wataendelea kuwa marafiki wako? Sote tunashawishiwa na utamaduni wetu, marafiki wetu, na kile tunachokisoma na kukitazama. Kwa kuwa tu jambo fulani ni maarufu (au sio maarufu) hiyo haimaanishi kuwa tunapaswa kukubaliana nalo au kuepukana nalo. Badala yake, mara zote tunatakiwa kutumia Biblia na mwongozo wa Roho Mtakatifu kama kiongozi wetu. Zingatia somo letu lililopita kumhusu Yona. Yona alikuwa mzalendo, na alikuwa maarufu kwa watu wake. Huo ndio mwelekeo ambao Mungu alimwongoza kuufuata. Lakini baadaye Mungu alimwongoza kwenye mwelekeo wenye kuleta ubishani (controversial) na wa hatari zaidi. Yona alipata ugumu na jambo hilo. Hebu tuzame kwenye Biblia na tuangalie jinsi tunavyotakiwa kuwa makini kuhusu kuwasikiliza marafiki wetu na utamaduni pale tunapopeleka injili kwa wengine!

I. Sulemani

A. Soma 1 Wafalme 11:1-2. Je, umewahi kuwasikia watu wakisema, “upendo ni upendo?” Je, Sulemani aliamini kuwa upendo ulikuwa wa muhimu zaidi kuliko neno la Mungu? (Kifungu cha pili kinasema dhahiri kuwa Mungu alikataza ndoa na wanawake waliobainishwa katika kifungu cha kwanza. Kifungu cha pili kinatuambia kuwa Sulemani alikiuka katazo la Mungu kwa sababu “aliambatana nao kwa kuwapenda.”)

B. Soma 1 Wafalme 11:3-4. Ndoa na wanawake hawa iliathirije maisha ya Sulemani?

C. Soma 1 Wafalme 11:6-8. Sulemani alikuwa mmojawapo wa watu maarufu sana duniani. Jambo gani lilitokea kwenye ushawishi wake miongoni mwa wapagani? (Hana tena ushawishi kwa mambo mema. Badala yake, anashawishi mambo maovu. Badala ya Sulemani kuwa na ushawishi kwa upande wa Mungu wa kweli, wake zake wa kipagani wanamshawishi Sulemani dhidi ya Mungu wa kweli.)

D. Soma 1 Wafalme 11:9-11. Ni athari gani binafsi anayoipata Sulemani kwa kufuata mitazamo yake ya upendo na kupuuzia alichokiamrisha Mungu kuhusu uhusiano wa kingono? (Mungu alimgeuka Sulemani.)

II. Mkananayo

A. Soma Mathayo 15:22-23. Kwa nini Yesu hakumjibu mwanamke Mkananayo? Je, Yesu anafuata njia sahihi ya Kibiblia ambayo Mfalme Sulemani alishindwa kuifuata?

B. Soma Mathayo 15:24-26. Hii inatuambia sababu iliyomfanya Yesu asizungumze na mwanamke Mkananayo ni ipi? (Hakuwa “wa nyumba ya Israeli,” kwa hiyo alikuwa “mbwa.”)

1. Je, Yesu alikuwa anazingatia chuki kubwa za wakati huo? (Ndivyo inavyoonekana. Yesu anaonesha chuki kwa kumwita mwanamke huyo mbwa.)

C. Soma Mathayo 15:27-28. Sasa mambo yote yako bayana. Je, Yesu anakuwa mkweli kwa kumwita mwanamke yule mbwa na kusema kuwa hakutumwa duniani ili kumsaidia? (Hapana. Anamjaribu imani yake. Anamwambia kuwa “imani yako ni kubwa,” na kisha anatenda muujiza kwa binti yake.)

1. Kuna nini cha kujifunza hapa? Angalia Mathayo 15:23. Wanafunzi walikuwa kwenye mizania gani ya chuki? (Walikuwa upande wa Yesu kutomjibu mwanamke yule.)

2. Tunajifunza nini kutoka kwa mwanamke? (Kama wewe ni mwathirika wa ubaguzi na chuki, unatakiwa kusonga mbele katika imani yako ya dini.)

3. Je, ni haki kusema kuwa mwanamke Mkananayo aliweka msingi wa kusihi kwake kwenye imani yake ya dini? (Angalia tena Mathayo 15:22. Anamwita Yesu “Mwana wa Daudi” na “Bwana,” ambapo maoni ya Barnes yanasema kuwa mwanamke alidhani Yesu ni Masihi.)

III. Kornelio

A. Soma Matendo 10:1-2. Je, Kornelio ni Myahudi? Au yeye ni aina fulani hivi ya “mbwa?” (Kornelio ni akida wa Kiitalia mwenye jina la Kirumi. Uwezekano ni mdogo kwamba Kornelio ni Myahudi, hata kama anaitwa “mtauwa, mchaji wa Mungu” na anaelezewa kuwa anamcha Mungu na kumwomba Mungu daima.)

1. Je, unawafahamu watu muhimu ambao sio washiriki wa kanisa lako? Je, watu hao ni Wakristo makini? (Kazi yangu inanikutanisha na watu wenye nguvu. Nimekuwa nikishangazwa na Wakristo wengi wa dhati wanaofanya kazi katika nafasi za juu serikalini. Mungu ana watu wake waaminifu kila mahali.)

B. Soma Matendo 10:3-5. Je, malaika wanakutokea kwa njia ya maono?

1. Hii inaashiria nini kuhusu mtazamo wa ubora (superiority) dhidi ya washiriki wa makanisa mengine? (Ninakumbuka mtazamo wangu wa kipumbavu nilipokuwa kijana. Mjomba wangu alikuwa mtu wa imani kubwa na afisa katika Jeshi la Wokovu. Nilijihisi kuwa nilikuwa Mkristo wa hadhi ya juu kwa kuwa niliitunza Sabato. Ingawa nilikuwa na uelewa mzuri zaidi wa Biblia, mjomba wangu alikuwa mtu aliyetembea na Mungu.)

C. Soma Matendo 10:9-10. Malaika anamtokea Kornelio na Petro anazimia wakati akiomba. Unadhani ni nini sababu ya ujumbe wa malaika na kuzimia? (Utaona kuwa wote wawili, yaani, Petro na Kornelio, wanaomba. Mungu anawajibu wale wote wanaomtafuta.)

D. Soma Matendo 10:11-16. Hii inaibua suala la muhimu sana la kiteolojia. Unapaswa kufanya nini pale Roho Mtakatifu (au mjumbe wa Mungu) anapokuambia utende jambo linalokinzana na Biblia? (Nitachukulia kwamba Roho Mtakatifu (au mjumbe wa Mungu) hatakinzana na Biblia.)

E. Soma Matendo 10:17. Petro ana maoni gani kuhusiana na mtafaruku wa wazi? (Anatatizika. Anaona mtafaruku na hakubaliani na ujumbe aliouona alipozimia.)

F. Soma Matendo 10:19-20. Kwa nini Roho Mtakatifu anamwambia Petro aende na watu wale? (Soma Matendo 10:28-29. Hii inafumbua siri. Petro asingemtembelea akida wa Kirumi. Lakini maono aliyoyaona darini sasa yanawekwa bayana. Hayakurejelea ulaji wa wanyama, yalirejelea kujihusisha na watu.)

G. Soma Matendo 10:34-36. Je, Kornelio angemwendea Petro bila maelekezo kutoka kwa Mungu?

1. Je, Petro angemtembelea Kornelio bila maelekezo kutoka kwa Mungu?

2. Je, tunapaswa kusubiri maelekezo kutoka kwa Mungu ili kupeleka injili kwa watu wasiostahili? (Maelekezo ya sisi kufanya hivyo yanapatikana katika Matendo 10:34-35.)

H. Soma Matendo 10:43-47. Jambo gani linatokea linalothibitisha ujumbe wa awali uliotolewa kwa Kornelio na Petro? (Uwezo wa Roho Mtakatifu unawashukia watu wa Mataifa kiasi kwamba wananena kwa lugha.)

IV. Matumizi Maishani

A. Kwa nini kisa cha Sulemani ni sehemu ya somo letu pamoja na kisa cha Kornelio? (Tunatakiwa kuwa makini na mwongozo wa Mungu. Kushikamana na wapagani (kwa upande wa Sulemani kuwaoa) kunaweza kutupotosha. Kwa upande mwingine, tunaweza na tunapaswa kuwaongoa wapagani kwenye injili.)

1. Kwa nini Sulemani alishindwa kuwaongoa wake zake wapagani? (Alikataa maelekezo ya Mungu. Linganisha hili na Kornelio na Petro waliofuata maelekezo ya Mungu. Ukitaka kuwaongoa wapagani, tofauti na kuongolewa na wapagani, unatakiwa kuyazingatia mapenzi ya Mungu kwa ukaribu.)

B. Kornelio na mwanamke Mkananayo wana jambo gani linalofanana? (Angalao mambo mawili. Kwanza, walimwamini Mungu wa kweli. Pili, walikuwa tayari kuwa na uhusiano mzuri na Mungu hata kama walikuwa waathirika wa chuki na ubaguzi.)

1. Kuna uwezekano mdogo kwamba Yesu anawaita waulizaji (inquirers) makini “mbwa,” lakini alifanya hivyo. Kuna fundisho gani katika hili? (Kuushinda ubaguzi uliojengwa juu ya mbari (race) na utaifa una mambo mawili. Kwanza, hatupaswi kuonesha ubaguzi na chuki. Pili, tukikabiliwa na ubaguzi na chuki tunabeba mzigo wa kukataa kuikumbatia fadhaa. Kujaribu kuidhibiti chuki kwa kutumia chuki sio njia ya Biblia.)

C. Je, kuna vizingiti vya ubaguzi na chuki ambavyo vinaweza tu kukabiliwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu?

D. Rafiki, je, uko tayari kuweka kando madhara ya chuki zisizo na sababu ili kuutangaza Ufalme wa Mungu? Kama unapambana na suala hili, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, akuponye tatizo hili la dhambi maishani mwako?

V. Juma lijalo: Esta na Modekai.