Somo la 3: Wito wa Mungu Kwenye Utume

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Matendo 1 & 2, Mwanzo 9, 11 & 12
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
4
Lesson Number: 
3

Somo la 3: Wito wa Mungu Kwenye Utume

(Matendo 1 & 2, Mwanzo 9, 11 & 12)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Mara ngapi umeshiriki kwenye “kikao cha taasisi” ili kupokea maelekezo juu ya kutimiza lengo la taasisi? Kwa kiwango cha chini, ni mara ngapi umekaa chini na kutafakari kwa namna gani bora utekeleze jambo jipya? Nakumbuka hiki kilikuwa chanzo cha kutokubaliana kati yangu na kaka yangu tulipokuwa tukifanya kazi pamoja kwenye kampuni ya ujenzi. (Alikuwa bosi.) Alikuwa akiwaambia wafanyakazi, “Hebu tupeleke zana hizi za ujenzi pale.” Nami nilimjibu, “Hebu subiri kwanza, tuangalie njia rahisi na yenye ufanisi ya kutekeleza jambo hili.” Baadhi ya kazi hazihitaji kufikiri kwingi, lakini jukumu tunalojifunza leo tunahitaji kupokea maelekezo kutoka kwa Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia!

I.  Kupatia

A.  Soma Matendo 1:1-2. Wanafunzi walielekezwaje? (Yesu mwenyewe aliwafundisha, na kisha akawafundisha kupitia kwa Roho Mtakatifu.)

B.  Soma Matendo 1:3-5. Ni nini msingi wa hili fundisho la mwisho kutoka kwa Yesu?  (Lilihusu “Ufalme wa Mungu.”)

C.  Soma Matendo 1:6. Muktadha, kama tunavyoona katika Matendo 1:9, ni kwamba Yesu anainuliwa ili kurejea mbinguni. Swali hili linatufunulia jambo gani? (Inaonekana wanafunzi hawakujifunza chochote. Wanadhani kuwa Yesu atawashinda Warumi na kuirejesha Israeli kwa Wayahudi. Kwa msingi huo ni kwamba, watakuwa viongozi katika urejeshwaji huu.)

1.  Tafakari miaka 3.5 ya mafundisho ya Yesu ya moja kwa moja na mafundisho yake ya mwisho katika siku zake arobaini za mwisho kuhusu “Ufalme wa Mungu.” Inawezekanaje wanafunzi bado walikuwa na dhana potofu?

a.  Hiyo inatuambia nini kuhusu kuelewa maelekezo yetu yanayoendana na hayo? (Ni vigumu kwa mawazo ya kale kufa. Wanafunzi walimuhitaji Roho Mtakatifu ili aendelee kufanya nao kazi.)

D.   Soma Matendo 1:7-8. Yesu anajibuje swali hili lenye kukatisha tamaa sana lililoulizwa na wanafunzi? (Anatoa jibu zuri zaidi kuliko vile ambavyo tungeweza kujibu. Kilichojikita kwenye jibu lake ni uwezo wa Roho Mtakatifu.)

1.  Je, Yesu anasema kuwa jukumu la kwanza kabisa la wanafunzi ni kuwa viongozi wa ufalme mpya? (Hapana. Anasema jambo tofauti kabisa – watakuwa mashahidi.)

2.  Mashahidi wanatoa ushuhuda. Wanashuhudia jambo gani? (Anasema, “nanyi mtakuwa mashahidi wangu.” Kiini cha ushuhuda wao ni Yesu.)

3.  Angalia mpangilio wa juhudi za ushuhudiaji. Unauelezeaje? (Kwanza, ni mahali walipo. Kisha katika Uyahudi yote, halafu Samaria, kisha sehemu nyingine za dunia zilizosalia.)

a.  Je, bado hii inahusika kwetu? (Eneo mahsusi la kijiografia ni tofauti, lakini inaleta mantiki kwamba tunapaswa kuanzia mahali ambapo tunawafahamu watu na utamaduni wao.)

b.  Nilisoma pendekezo linalosema kwamba tunapaswa kwenda mahali ambapo hatuna utulivu (we are not comfortable.) Je, hilo ni wazo jema? (Yesu anafafanua suala la ushuhudiaji kama mtu atupaye jiwe kwenye dimwi – mawimbi yanatawanyika kwenda mbali. Inaonekana kuwa na mantiki kufanya kazi mahali ambapo unaelewa utamaduni wao vizuri na hoja gani itakuwa ya kufurahisha na ipi haitawafurahisha watu.)

c.  Ninaashiria kuzingatia mantiki. Je, hicho ndicho alichokipendekeza Yesu? (Hapana. Yesu aliashiria kuwa tuutegemee uwezo wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu atayaongoza mawazo yetu.)

II.  Mashuhuda Wasiokusudiwa

A.  Baadha ya gharika, hili lilitokea. Soma Mwanzo 11:2-4. Ni nini lengo la mkutano huu? (Kujenga mnara, kuwa maarufu, na kuwa pamoja.)

1.  Kwa nini watake kujenga mnara ili “kilele chake kifike mbinguni?” Kwa nini isiwe bustani nzuri? Uwanja? Kasri? Nyumba nzuri kwa ajili yao? (Jibu linaonekana kuwa dhahiri – walikuwa na wasiwasi juu ya gharika nyingine. Jambo baya zaidi ni kwamba hawakumwamini Mungu pale aliposema kuwa hataleta tena gharika jingine litakaloifunika dunia yote. Angalia, Mwanzo 9:15.)

B.  Soma Mwanzo 11:7-9. Kwa nini Mungu alifanya hivi? Je, ni kutokana na kiburi chao? Tofauti na kutokuamini kwa dhahiri katika ujenzi wa mnara, kulikuwa na ubaya gani na lengo hili?

C.  Soma Mwanzo 9:1. Je, unadhani watu wa Babeli walifahamu juu ya maelekezo haya kutoka kwa Mungu? (Nina uhakika walifahamu. Walikuwa wanampinga Mungu kwa namna zote. Ukisoma Mwanzo 1:27-28 utaona huu ulikuwa mpango wa awali wa Mungu. Bila shaka walifahamu.)

1.  Unadhani raia hawa wa zamani wa Babeli walipeleka habari gani katika pande nyingine za dunia walizoweka makazi yao? (Nadhani walikuwa wamisionari wa namna fulani kwa uwezo wa Mungu.)

D.  Soma Matendo 8:1 na Matendo 8:4. Uwezo gani upo nyuma ya jambo hili? Je, hicho ndicho kinachomaanishwa kwa kutoka nje ya utendaji wetu wa kawaida wa kila siku tuliouzoea (comfort zone)? (Hii ni nguvu ya uovu. Lakini, kama Warumi 8:28 inavyotuambia, Mungu anachukua mambo mabaya na kuyatumia kutimiza jambo jema.)

III.  Mashuhuda wa Hiari

A.  Soma Mwanzo 12:1-3. Tafakari jinsi Abramu alivyoelewa jambo hili na vile ambavyo Mungu alikusudia alielewe. Je, vinafanana? (Nina uhakika kwamba Abramu, kama ilivyo kwetu sote, aliliangalia hili kwa kuzingatia maslahi yake binafsi. Kwa kuangalia jambo hili hii ni baraka kubwa kwa Abramu. Atakuwa tajiri, atabarikiwa (atakuwa taifa), na atalindwa. Tunafahamu kwamba kazi ya Mungu katika jambo hili ni kubwa zaidi.  Mungu sio tu kwamba ataanzisha taifa lake katika nchi ya ahadi, bali analianzisha taifa ambamo Yesu alizaliwa.)

1.  Unadhani kwa nini Mungu aliwasilisha hili kama jambo ambalo litakuwa baraka kubwa kwa Abramu?

2.  Kwa nini maelekezo kwa wanafunzi (Matendo 1:8) hayakujawa na baraka kwa ajili yao? (Hili ni swali linalopotosha. Utakumbuka kwamba wanafunzi walikuwa wanatafuta mamlaka ya kidunia. Yesu anawaambia katika Matendo 1:8 kuwa watapokea nguvu ya Roho Mtakatifu.)

B.  Soma Matendo 2:1-4. Kwa nini wazungumze “kwa lugha nyingine?” (Soma Matendo 2:5-6 na Matendo 2:9-11. Hii iliwafanya wanafunzi kuzungumza kwa lugha ya watu wa pande zote za dunia waliokusanyika Yerusalemu.)

1.  Hii inatufundisha nini kuhusu kuwa mashuhuda ulimwenguni kote? (Roho Mtakatifu anaweza kuuleta ulimwengu wote kwetu. Watu hawa walirejea katika mataifa yao ili kupeleka habari njema za Yesu.)

2.  Teknolojia imefanya nini kuuruhusu ulimwengu kutujia? (Hivi punde nilikuwa kwenye tukio ambalo, kwa sehemu fulani, lilitoa heshima kwa Dwight Nelson. Sifa zake zilibainisha ugunduzi wa teknolojia ya satilaiti ili kusambaza ujumbe wake wa injili. Muda mrefu huko nyuma kabla Dwight Nelson hajaanza kufanya hivi, Pat Robertson alileta ujumbe wa Yesu kwa ulimwengu kwa njia ya satilaiti.))

IV.  Hitimisho kwa Wito Wetu

A.  Hebu tupitie tena Matendo 8:1, kifungu kilichofafanua safari za wamisionari wasiokusudiwa. Kwa nini mitume hawakuondoka?

B.  Swali la awali ni gumu. Lakini hebu litafakari kutokana na hitimisho la jumla kwamba tunapaswa kuwafikia watu kwa kuzingatia vifungu ambavyo tumejifunza hadi kufikia hapa. Ni nini kanuni ya kwanza ya wito wetu wa utume? (Kumfuata Roho Mtakatifu. Katika kila mfano wetu, tunaye Mungu akinena au akichukua hatua kushinikiza mwelekeo wa utume. Hiyo inaashiria kuwa jibu sahihi la kwa nini mitume walibaki ni kwamba Roho Mtakatifu hakuwaelekeza kuondoka. Baadhi ya watu wanajenga hoja, zenye mantiki, kwamba bado walikuwa wanaitii Matendo 1:8 iliyowaambia kwanza waanzie Yerusalemu.)

C.  Rejea kwenye sehemu ya utangulizi ambapo tulijadili kikao cha taasisi. Kama ungekuwa kwenye mradi uliojadiliwa kwenye kikao, na hukuwa na uhakika jinsi gani unapaswa kusonga mbele, je, utawasiliana na waandaaji wa mradi? (Naam. Hiyo inaleta mantiki kabisa. Kwa kuwa Mungu ndiye mratibu wa utume wetu, na kwa kuwa mara zote Roho Mtakatifu yupo ili kutuelekeza, basi tunapaswa kuutafuta mwongozo wa Roho Mtakatifu. Ninaamini mitume walisalia Yerusalemu kwa sababu Roho Mtakatifu aliwaambia wabaki na kuwaongoza wengine kwa kuwa viongozi makini.)

D.  Rafiki, je, utamwomba Roho Mtakatifu akusaidie uwe makini na msikivu zaidi kwa uongozi wake? Kwa nini usifanye hivyo sasa hivi?

V.  Juma lijalo: Kushiriki na Wengine Utume wa Mungu.