Somo la 14: Waefeso Moyoni
Somo la 14: Waefeso Moyoni
(Waefeso 1-6)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Kabla ya kufanya mtihani wa mwisho wanafunzi wangu hupenda kupitia upya somo lote walilolisoma. Hiyo inaonekana kama kile tunachokifanya juma hili – kupitia upya kitabu chote cha Waefeso. Hebu tuzame kwenye somo letu ili tujikumbushe ushauri wa Paulo kwetu uliovuviwa na Roho Mtakatifu!
I. Msingi wa Maisha Yetu
A. Soma Waefeso 1:3-4. Jambo gani lipo kwa ajili yetu? (Kila baraka ya kiroho!)
1. Ni nini lengo la hii zawadi? (Kwamba ili tuwe watakatifu na tusio na hatia.)
B. Nimefika katikati kwenye kitabu cha Ron Duffield kiitwacho “The Return of the Latter Rain.” Katika kitabu hicho mwandishi anakumbukia mtafaruku uliotokea mwaka 1888 katika kanisa langu kuhusu kuhesabiwa haki kwa imani. Baadhi ya viongozi walikuwa wanajenga hoja kwenye kile ninachokichukulia kama jambo maarufu la “wokovu kwa njia ya matendo,” wakati wengine walikuwa wanajenga hoja juu ya “kuhesabiwa haki kwa imani.” Unaaminije kuwa tunakuwa “watakatifu na watu wasio na hatia,” kama anavyosema Paulo? (Soma Waefeso 1:7-8. Vifungu hivi vinasema kuwa tunasamehewa na kukombolewa kwa njia ya damu ya Yesu.)
1. Duffield anabainisha kuwa wale wanaojenga hoja ya kuhesabiwa haki kwa imani pia walikuwa wanajenga hoja kwamba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu tunaweza kuishinda dhambi. Kushinda huku hakukuwa kwa lengo la kuokolewa, bali kumheshimu Mungu. Unalionaje hili?
II. Kufufuka Pamoja na Kristo
A. Soma Waefeso 2:1-3. Maisha yetu ya zamani yanaelezewaje?
B. Soma Waefeso 2:4-5. Hii inaangaziaje mtazamo wetu juu ya kuhesabiwa haki kwa imani na utii? (Inatuambia kuwa wakati bado tulipokuwa katika maisha yetu ya zamani (“wafu kwa sababu ya makosa”), Mungu alituokoa kwa neema. Hiyo inamaanisha kuwa hoja ya kwamba hatuwezi “kuokolewa katika dhambi zetu” haiko sahihi.)
C. Soma Waefeso 2:8-10. Je, ni lengo la Mungu kwamba “tuokolewe katika dhambi zetu?” (Hapana. Kifungu cha kumi kinaelezea bayana lengo la Mungu kwa ajili ya maisha yetu, “tunapaswa kuenenda” katika “matendo mema.”)
III. Siri ya Umoja
A. Soma Waefeso 3:2-6. Ni siri ipi inayojenga msingi wa kazi ya Paulo maishani? (Kifungu cha sita kinatuambia kuwa “Mataifa ni warithi pamoja nasi” kanisani na katika injili.)
1. Ni nini umuhimu wa ufunuo huo? “Kama m-Mataifa, hiyo ni habari ya kufurahisha sana!)
B. Soma Waefeso 3:8-10. Ni nini lengo letu katika umoja wetu mpya na Wayahudi? (Kuibainisha hekima ya Mungu kwa “falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho.”)
1. Hizo falme na mamlaka ni akina nani? (Kwa kiasi fulani Paulo atakuwa anawarejelea malaika wa mbinguni na malaika walioanguka (wapotovu). Hii pia inaweza kuurejelea ulimwengu mwingine.)
2. Hebu tuchukulie kwamba angalao hadhira ni malaika wapotovu na Shetani. Unatarajia wawe na mwitikio gani kwenye habari hii? (Eneo la mbele kwenye pambano la vita kati ya wema na uovu limekuwa kubwa zaidi.)
3. Unapaswa kuwa na mwitiko gani kwenye eneo la mbele la vita lililopanuka zaidi? (Hii inatuambia kuwa pambano halituhusu peke yetu, bali linahusu jamii kubwa ya Wakristo.)
C. Soma Waefeso 3:16-17. Roho Mtakatifu na upendo wa Mungu vinahusianaje? (Msingi wetu unajengwa juu ya upendo wa Mungu kwanza kwa kafara yake kwa ajili yetu, na pili, kwa sababu ya kipawa cha Roho Mtakatifu.)
1. Litafakari hili kidogo. Mungu alijitoa kafara kubwa kuja duniani ili kutuokoa. Je, kafara hiyo inafanana na ile ya Roho Mtakatifu kutumia muda wake kutusaidia sisi sote? Alikuwa anafanya nini kabla hajatumwa kuja kutusaidia?
D. Soma Waefeso 3:18-19. Tukijawa na Mungu, je, tunajawa upendo?
1. Kama umejibu kuwa, “ndiyo,” je, hilo ni jepesi kwako? (Kwenye pambano dhidi ya uovu, ni vigumu kwangu kuwa na mtazamo chanya kwa watu wanaofanya madhara mengi. Mtazamo wangu unatakiwa kurekebishwa.)
IV. Kutembea Katika Umoja
A. Soma Waefeso 4:2-6. Ni nini linalopaswa kuwa lengo la Mkristo? (Kuwa na umoja na waamini wenzake.)
1. Madhehebu yote tofauti-tofauti yalitokeaje? Kanisa lako linasema nini kuhusu makanisa mengine? (Tunatakiwa kuepuka kuwashambulia Wakristo wenzetu. Kama haukubaliani na hili, unalielewaje fundisho la Paulo hapa?)
B. Soma Waefeso 4:15-16. “Kusema kweli katika upendo” kunafanyaje kazi kwenye suala la umoja na makanisa mengine? (Bila shaka hili ndilo jambo la msingi kabisa. Kama hatukubaliani juu ya kipi ni cha kweli, tunapata matatizo katika kujenga mwili mmoja.)
V. Watoto wa Nuru Gizani
A. Soma Waefeso 5:8-10. Ukiangalia katika maeneo yanayokuzunguka na ukakasirika au kukatishwa tamaa na uovu wote unaokuzunguka, unapaswa kufanya nini? (Hakikisha kuwa unaenenda katika nuru. Kwa nini? Kwa sababu matokeo yake ni “katika wema wote na haki na kweli.”)
B. Soma Ezekieli 9:4-6. Hiki ni kifungu kinachohusu hukumu. Inaonekana kuwa haikuwa kwamba miaka mingi iliyopita ningesoma jambo hili nikijalisha mtazamo wangu. Je, “nilishusha pumzi na kugumia” dhidi ya dhambi? Au nilivutiwa na majaribu? Siku hizi kiukweli ninaweza kusema kwamba “ninashusha pumzi na kugumia” juu ya “machukizo.” Vipi kuhusu wewe?
1. Kama uzoefu wako unafanana na wangu, je, unadhani ulimwengu umebadilika au wewe ndiye uliyebadilika? (Lengo letu ni, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kutembea kikamilifu nuruni. Lakini nina uhakika kuwa ulimwengu umebadilika sana na kuwa mbaya zaidi.)
VI. Kuweka Wazi Matendo ya Giza
A. Soma Waefeso 5:11-14. Ni kwa jinsi gani kuufichua uovu kunasaidia katika pambano kati ya wema na uovu? (Kuleta giza nuruni hupunguza uwezo wake kwa kuwaruhusu watu kuuelewa uovu vizuri zaidi. Hii ni hatua ya kwanza ya kuuruhusu ukweli na haki kushinda.)
B. Kwa sasa ninasoma kitabu cha Douglas K. Murray, “The Madness of Crowds.” Kitabu chake kinaelezea mfano baada ya mfano wa wale ambao ama kwa makusudi waliusimamia ukweli au walisema ukweli kwa kughafilika (bila kuwa waangalifu) na kazi zao zikaangamia. Licha ya hayo Murray ana ujasiri wa kufichua hilo nuruni. Murray ananifundisha mambo mapya. Je, hiyo ni sawa na Waefeso 5:14 kwamba tunafanana na “wasinziao” tunaoamshwa na watu majasiri?
1. Katika idara ya “nuru” lazima nikuambie kuwa Murray ni mkanamungu (atheist) na basha/msenge (homosexual). Je, hiyo inamzuia kuileta nuru? (Ningependa kujadili suala hili kwa kina zaidi. Kwa kutambua histoaria yake inanisaidia kutathmini maoni yake. Anakosa taswira ya Kibiblia katika mambo yote haya. Kwa mfano, nimesoma maoni yake kwamba mitafaruku juu ya ngono, mbari (race), na jinsi (gender) kwa sasa inatisha sana kiasi kwamba kama itaendelea kutokea basi dunia itahitaji kumtafuta mtu mwenye nguvu na ushawishi mkubwa atakayetutatulia mitafaruku hiyo. Ninafikiria kuhusu mpinga Kristo, Murray sio mpinga Kristo.)
VIII. Silaha ya Mungu
A. Soma Waefeso 6:13. Lengo letu la msingi ni lipi kama askari katika pambano kati ya wema na uovu? (Kusimama imara. Kwani mgongano wa muhimu zaidi haukuhusu wewe na familia yako? Wajibu wetu wa kwanza ni kusimama.)
B. Soma Waefeso 6:18. Maombi yanaungaje mkono ulinzi wetu wa kiroho na makosa yetu? (Maombi yanatuunganisha na Mungu moja kwa moja, chanzo cha nguvu yetu, hekima yetu, na mwongozo wetu katika kila pambano.)
C. Rafiki, kitabu cha Waefeso kinatuongoza kuelewa asili ya vita yetu ya kiroho. Kuendeleza amani sio jambo linalotokea lenyewe kimyakimya; linahusisha kusimama imara katika utambulisho wetu, kuuendeleza umoja, kutembea katika upendo, kung’aa kama nuru gizani, na kuvaa silaha ya Mungu. Tunapokabiliana na vita za kiroho hebu msingi wetu ukaendelee kujengwa katika kitabu cha Waefeso, huku tukikumbatia uwezo wa Mungu katika kuendeleza na kutangaza amani ya kweli. Je, utakubali, sasa hivi, kukitumia kitabu cha Waefeso kama mwongozo wako kwenye pambano kati ya wema na uovu?
Juma lijalo: Mfululizo mpya kuhusu “Utume wa Mungu – Utume Wangu.”