Somo la 9: Kuishi kwa Hekima

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
Waefeso 5:1-20
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
3
Lesson Number: 
9

Somo la 9: Kuishi kwa Hekima

(Waefeso 5:1-20)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, unawafahamu watu wanaoonekana kuishi maisha mazuri zaidi kuliko wewe? Je, ungependa kuishi maisha bora na kwa hekima? Jibu limo ndani ya Biblia. Kuishi kama Wakristo kunatutaka sio tu kukumbatia utambulisho mpya katika Kristo, bali pia kuenenda kwa namna inayoakisi utambulisho huo. Manufaa yake ni kwamba maisha yetu yanaboresheka! Paulo anatumia taswira thabiti ya maneno, kama vile kuenenda katika upendo na nuru, kutuongoza katika mwenendo wetu wa kila siku. Hebu tuzame kwenye somo la Biblia la juma hili na tujifunze jinsi ya kutumia dhana hizi ili kuishi maisha mazuri!

I.  Kumuiga Mungu

A.  Soma Waefeso 5:1-2. Paulo anamaanisha nini anapotutaka “tuenende” kama Mungu? Tunawezaje kumuiga Mungu mkuu wa mbinguni? (Tunapojifunza zaidi habari za Mungu, tunatakiwa kupangilia tabia zetu, mitazamo yetu, na thamani zetu kwa kumfuata Mungu.)

1.  Je, hilo linawezekana? (Kwenye masomo yetu katika majuma mawili yalioyopita tulijifunza kuwa Roho Mtakatifu anafanya mambo yasiyowezekana yawezekane.)

2.  Angalia tena kifungu cha 1 kwa ajili ya kidokezo muhimu. Kinaturejelea kama watoto wa Mungu. Chukulia kwamba ulikuwa na wazazi wazuri, je, uliwaiga?

B.  Angalia tena Waefeso 5:2. Tulikua na wazazi wetu hivyo tulijua jinsi walivyoenenda. Nani ambaye ni mfano wetu kwa ajili ya kumuiga Mungu? (Yesu.)

1.  Alitutolea mfano gani? (Kujitoa, msamaha, kufundisha, uponyaji, miongonbi mwa mambo mengine.)

II.  Kuishi Maisha Sahihi

A.  Soma Waefeso 5:3-5. Kama ungetakiwa kuandika kwa ufupi vifungu hivi vitatu, ungeandikaje? (Paulo analaani uasherati na tamaa. Anasifia na kutupendekezea shukrani.)

1.  Je, uasherati na tamaa ndizo dhambi kubwa hapa duniani? Vipi kuhusu dhambi za kanisa? Vipi kuhusu dhambi zako?

2.  Je, dhambi hizi (tamaa na uasherati) zinahusiana? (Nilipokuwa mtu mzima niligundua mwelekeo fulani miongoni mwa washirika wa kibiashara wa kiume waliofanikiwa. Utajiri wao ulipoongezeka, kwanza walinunua gari zuri, kisha nyumba nzuri, halafu wakatafuta mke kijana zaidi. Ilikuwa kama ramani ya wanaume wenye mafanikio.)

a.  Paulo anauita huu kama uabudu sanamu. Je, unaweza kulifafanua hilo? Kamwe sikuwahi kuwaona washirika hawa wa kibiashara wakizisujudia sanamu. (Kuabudu sanamu ni kitendo cha kipumbavu cha kusujudia kitu ulichokitengeneza kwa mikono yako mwenyewe. Kama wanaume hawa wangetambua kuwa Mungu ndiye mwanzilishi wa mafanikio, na sio wao wenyewe, wangejifungamanisha zaidi na malengo ya Mungu.)

i.  Je, kununua kile unachokitaka ni tatizo la dhambi?

3.  Kwa nini Paulo anatoa msisitizo mkubwa kiasi hicho kwenye uasherati na tamaa? (Dhambi hizi zinaathiri sana uhusiano na uadilifu wetu.)

4.  Paulo anatoa onyo gani la kutisha? (Hatuna urithi wa Mungu tukienenda katika uasherati na kutamani.)

5.  Paulo anasema maneno yasiyo ya kawaida katika Waefeso 5:3. Anasema uasherati na tamaa “usitajwe kwenu kamwe.” Unadhani hii inamaanisha nini? (Katika mwongozo wa kimaadili kwa wanasheria tunaona onyo sio tu la kuepuka tabia isiyo ya kimaadili, bali pia hata kuonekana kuwa na mwenendo usiofaa. Ninadhani hicho ndicho anachokimaanisha Paulo hapa.)

B.  Soma Waefeso 5:6. Kifungu hiki kinazungumzia “hasira ya Mungu.” Je, Mungu anawaangamiza waasherati na wenye kuwaka tamaa? (Nimegundua mwenendo mwingine maishani. Wanaume hawa walipowapata wake vijana zaidi, walipoteza nyumba zao nzuri na sehemu kubwa ya fedha zao. Uwezekano mkubwa ni kuharibika kwa uhusiano na watoto wao. Kama ambavyo mke wa kwanza alizeeka, vivyo hivyo kwa mke mdogo baada ya kipindi fulani kupita. Huenda walijikuta baadaye maishani wakilea watoto tena. Huenda kwa kadiri walivyozidi kuzeeka wake zao wadogo walipata waume wapya, vijana zaidi. Ninadhani “hasira ya Mungu” inajitekeleza yenyewe. Chaguzi mbaya huleta matokeo mabaya.)

1.  Kwa nini Paulo anaandika “mtu asiwadanganye” kuhusu hasira ya Mungu?

2.  Je, baadhi ya madai kuhusu haki kwa imani pekee ni sehemu ya udanganyifu? (Maoni ya John MacArthur yanasema “Ni udanganyifu wa hatari kwa Wakristo kutoa hakikisho la wokovu kwa muumini ambaye maisha yake yanaongozwa na dhambi ya kujirudiarudia na Mkristo asiyeonyesha fedheha ya dhambi hiyo.”)

C.  Soma Waefeso 5:7-9. Tunalo onyo hili la “kutoshirikiana nao.” Wao ni akina nani? Tamaa na uasherati? Au, “wana wasio watiifu?”

1.  Unadhani Paulo anakusudia ubia wa namna gani? (Nadhani anawazungumzia watu badala ya mitazamo. Sehenu ya kuenenda nuruni ni kuwachagua marafiki sahihi.)

2.  Nimewasikia watu wakimwambia kwa utani mtu aliyesema jambo la kutisha, “ninakaa mbali na wewe kwa sababu sitaki kuwa karibu wakati radi itakapokupiga.” Je, dhana ya jumla nyuma ya utani huo iko sahihi? (Ndiyo. Anachokimaanisha Paulo ni kwamba mambo mabaya yapo kwa ajili ya wana wasio watiifu. Usiwe karibu sana mambo mabaya yanapotokea.)

D.  Soma Waefeso 5:10. Utatendaje jambo hili? (Paulo anatutaka tulitafakari jambo hili. Kulichunguza jambo lenyewe.)

E.  Soma Waefeso 5:11-14. Kuna uovu mkubwa unaotangazwa leo nchini Marekani na serikali, vyombo vya habari, elimu, na hata biashara kubwa. Watu wengi wanainamisha vichwa vyao na kujaribu kuepuka kujiingiza kwenye mvutano. Vifungu hivi vinasema kuwa tunapaswa kufanya nini? (Tuifichue dhambi.)

1.  Tukitumia kanuni hii katika eneo letu la kazi, unadhani inapaswa kutendekaje? (Kesi mashuhuri ilihusisha kampuni ya Hewlett Packard (HP) na mwajiriwa aliyeitwa Peterson. Kampuni ya HP ilibandika bango linalotangaza haki za mashoga kwenye meza ya Peterson na Peterson akabandika vifungu vya Biblia kuhusu usenge. Peterson alikataa kuondoa bandiko lake isipokuwa tu kama kampuni ya HP nayo itaondoa bandiko lake. Peterson alifukuzwa kazi.)

a.  Je, Peterson alikuwa anaifuata Waefeso 5:11?

F.  Soma Mathayo 10:14. Maelekezo ya Yesu yanatumikaje kwenye mazingira ya Peterson? (Kuna tofauti kati ya kuzungumza ukweli na kujiingiza kwenye vita. Peterson hakuwa na haki ya kuelekeza sera kwenye kampuni hii. Yesu aliwaelekeza wanafunzi wake kwamba mji ukiwakataa wasonge tu mbele. Waefeso 5:13 inaashiria kuwa kufichua tu jambo haitoshi. Nuru ina tiba yake yenyewe.)

III.  Kuishi kwa Hekima

A.  Soma Waefeso 5:15-17. Je, vifungu hivi vinahusika kwenye wajibu wetu wa kuufichua uovu nuruni? 

1.  Ikiwa ndivyo, vinatuambia tufanye nini? (Vinatuambia kuwa tutafakari mambo kwa kina. Vinatuambia tutawale hisia zetu. Vinatuambia tuwe na ufanisi. Ninafundisha somo katika shule ya sheria ambapo tunajifunza kesi zinazohusisha waajiriwa wanaozingatia misingi ya dini wanaoingia kwenye matatizo na waajiri wao au vyama vyao kwenye masuala ya imani. Nyingi ya kesi hizi zingeweza kuepukika kwa mwajiriwa kuwa na hekima.)

B.  Soma Waefeso 5:18. Je, mvinyo na Roho Mtakatifu vinafungamana? (Bibi yangu alionewa tena alipokuwa na umri wa miaka ya sitini baada ya kuwa mjane kwa miongo kadhaa. Mumewe alikuwa amemchangamkia sana Mungu, lakini maisha yake ya nyuma yalikuwa ya ulevi wa kupindukia. Aliniambia kuwa alijutia miaka yote aliyoipoteza kwenye ulevi. Nadhani hiyo inafafanua kile anachotuambia Paulo.)

C.  Soma Waefeso 5:19-20. Mimi sio mwimbaji mzuri. Sisi waimbaji wabaya tunafanya nini?  Au, je, hii inahusu uimbaji? (Utaona kifungu kinasema “mkiimba” “mioyoni mwenu.” Kinatuambia tuwe na shukrani. Anachokiashiria Paulo ni kuwa na mtazamo sahihi. Ninapenda kuimba (hata kama ninaimba vibaya) na ninapenda kutoa shukrani.)

D.  Soma Waefeso 5:21. Tumetoka kupitia mambo yote ya kipumbavu tunayopaswa kuyaepuka. Kwa nini “nijitoe” kwa wengine wakati kuna watu wengine wengi wanaofanya uamuzi mbaya? (Maneno ya udhibiti ni “kunyenyekeana katika kicho cha Kristo.” Tunatakiwa kuachana na kiburi, lakini hatutakiwi kuacha uamuzi unaojengwa juu ya ufahamu wa Biblia.)

E.  Rafiki, Biblia inaweka njia ya namna ya kuishi maisha mazuri. Je, utaifanya njia hiyo kuwa ramani ya maisha yako?

IV.  Juma lijalo: Waume na Wake: Pamoja Msalabani.