Somo la 11: Mhuri wa Mungu na Alama ya Mnyama : Sehemu ya 1
Somo la 11: Mhuri wa Mungu na Alama ya Mnyama : Sehemu ya 1
(Waefeso 2, Warumi 8, Ufunuo 7, 13 & 14)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Tumejifunza nini hadi kufikia hapa? Dunia itagawanywa katika makundi mawili. Kundi moja litakuwa aminifu kwa Mungu Muumbaji wetu na kundi jingine litamkataa Mungu na litakuwa aminifu kwa mafanikio ya mwanadamu. Wale wanaomkataa Mungu wanazidi kuwa na hali mbaya zaidi na uwezo wao wa kutafakari unahafifishwa kwa dhahiri kabisa. Tabia bainishi za wale wanaomchagua Mungu, kwa mujibu wa Ufunuo 14:12, ni kwamba wana imani ya Yesu na ni waaminifu kwa amri za Mungu. Ufunuo 14 inaendana kikamilifu na dhana ya kwamba watu waaminifu kwa Mungu wanamtegemea Yesu kwa ajili ya wokovu wao, na si kuyategemea matendo yao wenyewe. Lakini wakati huo huo wanaelewa kuwa kuitegemea imani yao kwa Yesu maana yake ni kuichukulia kwa umakini kafara ya Yesu na maelekezo yake kwa ajili ya maisha yetu. Matokeo gani mengine yanaibuka kutokana na huu mgawanyiko mkubwa? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!
I. Mwendo
A. Soma Waefeso 2:8-10. Je, tunapata wokovu kutokana na matendo yetu? (Hapana! Imani yetu kwa Yesu ndio hutuokoa, na sio matendo yetu. Wokovu ni karama (zawadi) kutoka kwa Mungu.)
1. Kwa nini tuliumbwa? (Ili tutende mambo mema.)
2. Kwa nini Waefeso 2:10 inazungumzia kuhusu kuenenda katika matendo mema? Hiyo inamaanisha nini? (Inamaanisha kuwa mwelekeo wa maisha yetu unaendana na amri za Mungu – ambao aliuandaa kabla.)
3. Nimetoka kusoma makala inayoelezea kuwa wokovu wetu umebadili utiifu wetu kwa sheria. Je, hiyo ni kweli? Au huo ni uzushi? (Kuna msitari mwembamba kati ya masuala haya mawili. Kuchagua kumtegemea Yesu kwa ajili ya wokovu wetu maana yake ni kuchagua kuyategemea maelekezo yake kwa ajili ya maisha yetu. Mwelekeo huu unapatikana kwenye Amri Kumi. Mtazamo huu ni tofauti kabisa na wale wanaoamini kuwa utiifu wao kwa amri za Mungu ndilo takwa la wokovu.)
B. Soma Warumi 8:1-2. “Sheria ya Roho wa uzima” ni nini na inatofautianaje na “sheria ya dhambi na mauti?” (Sio kwa bahati kwamba “Roho” ndio kiini cha sheria yetu. Roho Mtakatifu anatuongoza juu ya kilicho sahihi na kisicho sahihi. Ushindi wa Yesu ndio hutupatia uhuru huo.)
C. Soma Warumi 8:3-4. Sheria inawezaje “kudhaifishwa kwa sababu ya mwili?” Nilidhani iliandikwa (ilichorongwa) kwenye jiwe! (Kuwa dhaifu kwa sababu ya mwili inaturejelea. Hatuwezi kuishika sheria. Yesu ametenda kile tusichoweza kukifanya.)
1. Inamaanisha nini kusema kuwa Yesu “aliihukumu dhambi katika mwili?” (Inamaanisha kuwa alitupatia ushindi dhidi ya dhambi. Alituonesha kwa dhahiri kabisa kile ambacho Shetani anataka kututendea. Maisha yake yalifunua masuala yaliyopo katika pambano kuu kati ya wema na uovu.)
II. Alama
A. Soma Ufunuo 13:15. Hapo awali tulifuatilia historia ya Babeli na mwasisi wake, Shetani. Lengo la Shetani ni kutufanya tumwabudu na falsafa yake ya maisha ya ukanaji-Mungu. Ni nini sehemu ya lengo hilo? (Kuwaua wale wanaokataa kukubali mtazamo wake wa maisha. Kuwaua wale wanaokataa kumkana Mungu Muumbaji wao. Watakatifu hawa waaminifu wanadhihirisha uchaguzi wao kwa kushikilia imani zao zinazozingatia imani ya msingi (downstream) iliyopo katika kitabu cha Mwanzo. Hapo awali tulijifunza kuwa imani hizi za msingi ni Uumbaji, Sabato, ndoa, na ujinsia.)
B. Soma Ufunuo 13:16-17. Matokeo gani mengine hutokea kutokana na kuikataa alama ya utiifu kwa Shetani na washirika wake? (Mgomo wa kiuchumi. Hatuwezi kuuza kile tunachokizalisha, na hatuwezi kununua kile tunachokihitaji.)
1. Je, hilo linatokea leo? Je, wale wanaoamini katika maelezo ya kitabu cha Mwanzo kuhusu ndoa na ujinsia wanapoteza kazi zao?
C. Soma Ufunuo 13:5-7 na Danieli 7:25. Kipindi hiki cha miaka mitatu na nusu, au siku 1,260 ni kibainishi mahsusi kabisa. Ukiongezea na muktadha wa muda wa Danieli 7 tunaona kuwa hii inahusiana na “mnyama wa nne” ambaye ni Ufalme wa Rumi. Hii inaimaanisha mamlaka gani? (Maoni ya Barnes kwenye kifungu hiki, pamoja na maoni mengine ya kale, yanafafanua mafundisho ya msingi ya Kiprotestanti kwamba hii inairejelea Rumi ya Upapa.)
1. Rumi ya Upapa ni Kanisa Katoliki. Ni kwa jinsi gani kundi hili kubwa la waumini wa Kikristo linajumuishwa kwenye falsafa ya Babeli?
D. Soma 1 Timotheo 2:5. Hii inasema kuwa “mpatanishi” kati ya Mungu na wanadamu ni nani? (Yesu.)
1. Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Na. 969, inamrejelea Mariamu kama “Mediatrix” (Mpatanishi). Mariamu anawezaje kuwa mpatanishi kati ya Mungu na mwanadamu wakati Biblia inaeleza kuwa Kristo ndiye mpatanishi pekee? (Hii inabainisha sehemu ya tatizo kubwa la teolojia ya Kikatoliki. Sio tu kwamba Mariamu anachomekwa kati ya mtu na Mungu, lakini pia mapadre wanachomekwa kwa njia ya kitubio. Madai kuhusu mamlaka ya Papa yanapunguza zaidi uhusiano wa moja kwa moja kati ya mtu na Mungu.)
2. Ukinzani huu na 1 Timotheo 2:5 unaendanaje, ikiwa kweli unaendana, na tatizo la kihistoria la kuzitegemea juhudi za mwanadamu badala ya kumtegemea Mungu? (Hiki ni kipengele kingine cha utegemezi kwa wanadamu badala ya kumtegemea Mungu. Waprotestanti wanaoamini kuwa wanaokolewa kwa matendo yao, Wakristo wanaoamini kuwa wanaweza kuzikataa sehemu za Biblia wasizozipenda, wote wanaungana kwenye kasoro ile ile ya kumkataa Mungu kwa kuyategemea matendo na fikra za mwanadamu.)
3. Kuna tatizo gani la dhahiri linalotokana na kujikita kwenye Kanisa Katoliki pale tunapojadili uchaguzi kati ya Alama na Yesu? (Tunao muda mahsusi na wenye ukomo unaohusiana na kuibuka kwa Utawala wa Rumi. Makundi mengi na falsafa nyingi tofauti zinaendana na falsafa stahamilivu za kidini za Babeli.)
III. Mhuri na Vazi
A. Soma Ufunuo 7:2-3. Mhuri huu ni upi? (Ni alama kwenye kipaji cha uso kwa wale wanaomtumikia Mungu.)
B. Soma Ufunuo 7:4. Je, idadi ya wale waliotiwa mhuri ina ukomo? (Kifungu kinasema ni watu 144,000.)
C. Soma Ufunuo 7:9-10. Je, idadi ya wale waliovaa mavazi meupe ina ukomo? (Hapana! Ni wengi sana kiasi kwamba hawawezi kuhesabika.)
1. Tunapaswa kuhitimisha nini kutokana na hili kuhusu wale wanaookolewa? (Wale waliomchagua Mungu ama wametiwa mhuri au wamevaa vazi jeupe.)
D. Soma tena Ufunuo 7:4 kisha usome tena Ufunuo 7:9. Je, wale waliotiwa mhuri na wale wanaovaa mavazi ukomo wao unatokana na kabila lao? (Ufafanuzi katika Ufunuo 7:4-8 ukomo wake unaishia kwa “wana wa Israeli.” Wakati Ufunuo 7:9 inadhihirisha kuwa “kila taifa, na kabila, na lugha, na jamaa” wanavaa vazi jeupe.)
E. Soma Waefeso 1:13-14. Kifungu hiki kinasema kuwa mhuri wa Mungu ni upi? (Roho Mtakatifu.)
1. Hebu tuviangalie vifungu hivi kwa kina zaidi ili tuone jinsi vinavyohusiana na Ufunuo 7 na mjadala wetu wa Alama ya Mnyama. Tunaupataje mhuri wa waefeso 1:13? (Tunamwamini “Yeye” na “injili ya wokovu wako.”)
2. Je, hii inahusiana na mhuri na mavazi ya Ufunuo 7? (Ndiyo! Mhuri katika kipaji cha uso unaakisi imani yetu katika wokovu kwa njia ya neema pekee. Vazi jeupe la haki ni Yesu akitufunika kwa matendo yake ya haki. Angalia mfano wa vazi la harusi katika Mathayo 22:1-14, Zekaria 3:1-4, na Isaya 61:10. Lakini angalia Ufunuo 19:8.)
F. Hebu tuendelee na mhuri ulioelezewa katika Waefeso 1:14. Ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu ni mdhamana wa mustakabali wa urithi wetu mbinguni? (Tutakapokuwa mbinguni tutakaa na Mungu. Roho mtakatifu, kama sehemu ya Utatu Mtakatifu, anakaa na wale wanaomwalika maishani mwao. Kuishi kwa mujibu wa maelekezo ya Roho Mtakatifu sio tu kwamba inatutenga na wale wanaofuata mamlaka ya mwanadamu, bali inatupatia uzoefu wa mbinguni.)
G. Unaweza kuwa umeona rejea yangu ya “Lakini angalia” ya Ufunuo 19:8. Soma Ufunuo 19:7-8. Bibi harusi anapataje hili vazi safi? (“Anapewa.” Siamini kwamba hii inamaanisha kuwa vazi la haki ni matokeo ya matendo yetu. Vinginevyo, Wafilipi 3:9 na warumi 3:25-26 zisingekuwa kweli. Muhimu zaidi, taswira pana ni kwamba waliookolewa wanakataa utegemezi kwa dhana ya kwamba tunazingatia juhudi za kibinadamu. Badala yake, Ufunuo 19:8 inasisitiza dhana ya kwamba uchaguzi wetu una matokeo kwa namna tunavyoenenda.)
1. Soma Mathayo 22:10-12. Mtu huyu alikuwa amevaa mavazi gani? (Mavazi yake mwenyewe. Alikataa kubadili na kuvaa mavazi yaliyotolewa na Mfalme.)
a. Hii inatufundisha nini kuhusu mavazi ya Ufunuo 19:8? (Inahitimisha dhana ya kwamba mavazi yetu yanakubalika, achilia mbali “kitani nzuri na safi.”)
H. Rafiki, je, itakuwa ipi? Alama ya Mnyama au Mhuri au Vazi la Mungu? Kwa nini usimpokee Yesu, sasa hivi, kama Mtu ambaye utamfuata?
IV. Juma lijalo: Mhuri wa Mungu na Alama ya Mnyama: Sehemu ya 2.