Somo la 9: Mji Unaoitwa Machafuko
Somo la 9: Mji Unaoitwa Machafuko
(Ufunuo 17 & 18, Mwanzo 11, Yeremia 50)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2023, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Watu wengi hawapendi kufanya chaguzi ngumu. Tunapendelea kuendana na ulimwengu jinsi ulivyo na kutumaini kuwa mambo yatakuwa mazuri. Kuutegemea utepetevu ni uamuzi mbaya kabisa. Tutakabiliana na chaguzi kati ya nguvu zilizo kinyume na Mungu na wale wanaotangaza ibada kwa Mungu. Somo letu la Biblia juma hili linaashiria kuwa tunapaswa kuchukua uamuzi huu haraka iwezekanavyo, kwa sababu kujiingiza kwenye kambi ya wapinga Mungu inamaanisha kuwa fikra yetu ya kawaida imedhoofu. Hiyo inafanya uchaguzi sahihi kuwa mgumu zaidi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!
I. Wanawake Wawili
A. Soma Ufunuo 17:1-2 na Ufunuo 14:8. Kahaba mkuu ni ishara ya jambo ambalo kwa dhahiri sio jema. Unadhani anawakilisha nini? (Ukimlinganisha na Ufunuo 14:8 unamfanya aonekane kama Babeli Mkuu. Babeli ni mamlaka ambayo kihistoria yako kinyume na watu wa Mungu.)
B. Soma Ufunuo 12:1 na Ufunuo 12:5. Mwanamke huyu ni ishara ya nini? Je, ni mwema au mbaya? (Hapo awali tulipomjadili mwanamke wa Ufunuo 12:1 tulihitimisha kuwa anawakilisha wale wanaomfuata Yesu kwa sababu mwanamke huyu “alimzaa” Yesu. Hivyo, hili ni kundi la kidini linaloendana na Mungu wa kweli.)
1. Kwa kuwa mwanamke wa Ufunuo 12:1 anawawakilisha wale wanaomfuata Yesu, hiyo inazungumzia nini kuhusu asili ya kahaba mkuu wa Ufunuo 17:1? (Pia anawakilisha kundi la kidini ambalo sio zuri. Haliendani na Mungu wa kweli.)
2. Tunaambiwa kuwa viongozi wa kisiasa “wamezini” na kahaba mkuu na kwamba watu wa kawaida “wamelewa” mtazamo wake. Unadhani hiyo inamaanisha nini? (Inamaanisha kuwa watu katika nyanja zote za maisha wanashiriki mtazamo wake.)
C. Soma Warumi 1:21. Hii inatuambia nini kuhusu wale wanaomkataa Mungu? (Fikra yao inakuwa “haina maana” na mioyo yao “ikatiwa giza.” Huyu anaonekana kama mlevi. Huu ni uthibitisho zaidi kuwa mvinyo wa kahaba mkuu ambao watu wanaunywa katika Ufunuo 17:2 ni kumkataa Mungu wa kweli.)
D. Angalia tena Ufunuo 17:1. Inamaanisha nini kusema kwamba kahaba huyu “ameketi juu ya maji mengi?” (Soma Ufunuo 17:15. Kahaba huyu ana ushawishi mkubwa sana kwa ulimwengu. Lazima haya yatakuwa mamlaka ya kidunia ambayo ni adui wa Mungu.)
1. Utaelezeaje kwa ujumla mtazamo wa kiteolojia wa kundi la kahaba? (Viongozi wa kisiasa na watu kwa ujumla wanakubaliana na mtazamo wake wa ukana-Mungu.)
E. Unapowatafakari wanawake hawa wawili, hiyo inaashiria kuwa wale wanaoishi duniani wanakabiliana na nini? (Wanawake hawa wawili wanawakilisha mamlaka zinazopingana. Tunapaswa kufanya uchaguzi kati ya mamlaka hizo mbili.)
II. Babeli Mkuu
A. Soma Mwanzo 11:2-4 inayoelezea maisha ya watu baadha ya Gharika. Lengo la watu hawa ni lipi? (Wanataka kuwa maarufu na wanataka kujikinga na gharika.)
B. Soma Mwanzo 9:11. Mungu alitoa ahadi hii kwa wanadamu baada ya gharika. Ahadi hii inatuambia nini kuhusu aina ya wajenzi wa mnara? (Hawakumwamini Mungu. Hawakumtegemea Mungu. Bali waliitegemea mipango yao wenyewe na uwezo wao.)
1. Soma Mwanzo 11:6. Mungu anafikiria nini kuhusu umoja huu wa malengo ya kiovu? (Mungu anasema umoja maana yake ni kwamba hakuna kisichowezekana kwao.)
C. Soma Mwanzo 11:7-9. Ni nini tiba ya nguvu ya umoja? (Uanuwai! Mungu anawapatia lugha tofauti na wanatawanyika duniani kote.)
D. Mungu anapaitaje mahala hapa panapojengwa mnara? (Babeli.)
E Haya ndio matumizi ya kwanza ya neno Babeli katika Biblia. Unapotafakari kisa hiki, Babeli inawakilisha nini? Je, ni vuguvugu la kidini? (Babeli inawakilisha kumkataa Mungu na kubadilisha uwezo wa kibinadamu. Ni la “kidini” kwa maana ya kwamba kwa mahsusi inampinga Mungu na inajikita katika kumbadilisha Mungu kuchukua nafasi ya wanadamu. Hii ndio nadharia ya msingi iliyo nyuma ya uabudu sanamu.)
F. Soma Yeremia 50:33-34. Hapa tunagundua nini kuhusu Babeli? (Mgongano kati ya watu wa Mungu na babeli. Babeli imewakandamiza na kuwachukua mateka watu wa Mungu.)
G. Katika Yeremia 50:35-38 Mungu anaahidi kuwa atatumia silaha na asili kuishinda Babeli kwa maana ni “nchi ya sanamu za kuchongwa ... “wameingiwa wazimu kwa ajili ya sanamu.” Soma Yeremia 50:39-40. Ni nini ulio mustakabali wa Babeli? (Umeangushwa na kukimbiwa.)
1. Ikiwa hali ndio hiyo, kwa nini tunaiona Babeli Kuu inayorejelewa katika kitabu cha Ufunuo? Kwa nini ujumbe wa malaika wa pili kati ya wale malaika watatu (Ufunuo 14:8) ni maoni kuhusu kushindwa kwa Babeli? Je, malaika wa pili kati ya wale malaika watatu anatupatia habari za kale sana? (Ufunuo ni kitabu cha ishara. Kahaba mkuu anayeenenda kama Babeli ni ishara ya mtazamo wa kidunia. Mtazamo unaokataa kumtegemea Mungu na kumwabudu Mungu, na kuubadilisha na fikra ya kibinadamu. Fikra ambayo imevurugwa kutokana na kuilinganisha na mvinyo.)
H. Hebu turejee kwenye Ufunuo 17 na tufuate njia ya kahaba mkuu. Soma Ufunuo 17:5. Tunapaswa kuhitimisha nini kuhusu “Babeli mkuu” kuandikwa kwenye kipaji cha uso cha kahaba mkuu? (Anaukumbatia kikamilifu ukana-Mungu, mtazamo wa kibinadamu ambao awali uliibuka katika Mnara wa babeli.)
1. Je, kuna umuhimu wowote wa yeye kuitwa “kahaba” ambaye ni “mama wa makahaba?” (Hii ni sababu nyingine kwa nini watu wa Mungu na kikundi cha wakana-Mungu wanaelezewa kama wanawake. Je, ni waaminifu kwa Mungu baba yetu au la? Wale wasio waaminifu ni makahaba.)
I. Soma Ufunuo 17:6. Ni nini ulio mtazamo wa Babeli dhidi ya wafuasi waaminifu wa Mungu? (Anataka kuwaua.)
J. Soma Ufunuo 17:7-9. Unadhani inamaanisha nini kusema kuwa kahaba mkuu “anachukuliwa” na mnyama mwenye vichwa saba “atakayepanda kutoka kuzimu?” Kuzimu ni kitu gani? (Soma Ufunuo 20:1-3. Ni mahali ambapo Shetani anafungwa. Hii inamaanisha kuwa kahaba mkuu “anachukuliwa” na Shetani.)
1. Utaona kwamba Ufunuo 17:9 inasema kuwa kahaba mkuu “amekaa” juu ya “milima saba.” Unadhani hiyo inamaanisha nini? (Katika maeneo kadhaa kwenye Agano Jipya neno la Kiyunani lililotafsiriwa kama “mlima” linatumika kufafanua “mlima Sinai.” Angalia, kwa mfano, Matendo 7:38. Ninapoandika masomo haya kwa ujumla huwa ninatumia maoni ya kale. Maoni ya kale kabisa ya kiprotestanti yanaeleza kuwa milima hii inapaswa kuchukuliwa kama vilima, na kwamba Rumi inakaa juu ya milima saba.)
2. Dhana ya Babeli kama mamlaka ya kiovu yanaanzia katika kitabu cha Mwanzo na kuishia katika kitabu cha Ufunuo. Mtazamo gani mpana wa kihistoria unaweza kuwakilishwa na hii milima saba? (Baadhi ya watu wanaamini kuwa “milima” ni maeneo ya ushawishi. Kwa mahsusi ni katika familia, dini, elimu, vyombo vya habari, burudani, biashara na serikali.)
a. Ikiwa Babeli ni mkana-Mungu, falsafa ya kibinadamu (na iko hivyo) je, tunaiona Babeli kwenye maeneo haya ya ushawishi?
III. Ushindi
A. Soma Ufunuo 17:14 na Ufunuo 14:8. Pambano kati la wanawake hawa wawili linaishaje? (Tunaungana na Yesu, Mwana-Kondoo. Anamshinda mnyama.)
1. Wafuasi wa Yesu wanaelezewaje katika Ufunuo 17:14? (“Walioitwa, wateule, na waaminifu.)
B. Rafiki, unapewa wito wa kumfuata Yesu. Amekuchagua. Je, utamchagua? Je, utakuwa mwaminifu kwa Yesu kwa kukataa kutegemea nguvu za kibinadamu na badala yake kuutegemea uwezo wa Mungu? Kwa nini usichukue uamuzi huo sasa hivi?
IV. Juma lijalo: Udanganyifu wa Mwisho wa Shetani.