Somo la 12: Thawabu ya Uaminifu

Mathayo 25, Waebrania 11, Warumi 8
Swahili
Year: 
2023
Quarter: 
1
Lesson Number: 
12

Somo la 12: Thawabu ya Uaminifu

(Mathayo 25, Waebrania 11, Warumi 8)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kila ninapofanyiwa uchunguzi wa macho, madaktari huwa wanachunguza ili kuona kila upande wa jicho langu unaweza kuona kwa umbali gani ninapoangalia mbele. Baadhi ya watu wana madhara au ugonjwa unaowafanya wawe na uoni hafifu. Fikra yangu ni kwamba Wakristo wengi wana uoni hafifu sana linapokuja suala la “Thawabu ya Uaminifu.” Wanaona thawabu wanapokwenda mbinguni tu, na hilo husababisha mkanganyiko kuhusu uhusiano kati ya matendo na wokovu. Ingawa ni kweli kwamba baadhi yao wataiona thawabu yao mbinguni pekee (angalia Waebrania 11), kwa Wakristo wengi huu uoni hafifu unafanana na ugonjwa. Unawafanya wasizione thawabu za dhahiri zitokanazo na uaminifu, zinazotujia sasa hivi hapa hapa duniani kama matokeo ya kumtii Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na unaweza kuamua kama ninaliangalia suala hili kwa usahihi!

I.  Talanta na Mbingu

A.  Soma Mathayo 25:14. Yesu anasema kuwa “ni” mfano wa mtu atakaye kusafiri. “Ni” ni kitu gani? Mada ya kisa hiki ni ipi? (Soma Mathayo 25:13. Yesu anaelezea mifano (mafumbo) kuhusu ujio wake Mara ya Pili. Kutokuijua siku wala saa inarejelea muda wa kuja kwake.)

B.  Soma Mathayo 25:15-18. Unadhani “talanta” zinawakilisha nini katika mfano huu? (Uwezo tuliopewa na Mungu. Hata hivyo, utaona kwamba kifungu cha 14 kinarejelea talanta kama “mali” za bwana.)

C.  Soma Mathayo 25:19-21. Bwana anasema kitu kile kile kwa mtumwa aliyepewa talanta mbili. Unadhani inamaanisha nini “kuingia katikaa furaha ya bwana wako?” (Kwa muktadha huo, lazima hii imaanishe kuingia mbinguni.)

1.  Je, hiyo inamaanisha Wakristo wenye “uoni hafifu” wako sahihi? Thawabu yetu ya uaminifu ni uzima wa milele?

D.  Katika Mathayo 25:24-27 mtumwa aliyepewa talanta moja anamfedhehesha bwana wake kwa kumwita “mtu mgumu” na kuashiria kwamba yeye ni mlafi. Bwana anamwambia mtumwa yule kwamba ni “mbaya na mlegevu.” Soma Mathayo 25:28-29. Je, maoni haya yanahusu wokovu? (Inawezekana. Je, unaweza kuokolewa zaidi ya mara moja? Je, mtu mwenye talanta kumi anapata tiketi ya kwenda mbinguni kwa ajili ya watu wengine? Yesu anawezakuwa anasema kwamba alikuwa na talanta kumi na moja atakazopewa mbinguni. Hilo linawezekana. Lakini, hii inaonekana kama Yesu anaweza kuwa anazungumzia jambo fulani la hapa duniani – hususan kwa kuwa ongezeko la talanta mara mbili lilitokea hapa duniani.)

E.  Soma Mathayo 25:30. Je, hii ni rejea ya kuikosa mbingu? (Ndiyo. Hilo liko wazi.)

1.  Je, hii rejea ya dhahiri ya kuikosa mbingu inatufundisha kuwa tunaikosa mbingu kwa kutokuwa na matendo? (Kama tusingemsikia mwenye talanta moja akimbatiza bwana wake majina, na kushambulia hulka yake, tunaweza kufikia hitimisho hilo. Lakini, kwa kuwa tunajua kile alichokisema, tunaelewa kwamba mtazamo wake kwa bwana wake haukuwa sahihi, na hicho ndicho kilichomfanya asitende jambo lolote.)

F.  Hebu tupitie jibu lililotangulia. Nilikuuliza kwamba talanta hizi zinawakilisha nini na nikapendekeza jibu lilikuwa “talanta zitolewazo na Mungu.” Soma Mathayo 25:7. Kifungu hiki kinasema kuwa talanta ni ipi? (Kinasema kuwa ni “fedha.” Yesu analiweka jambo hili kuwa wazi zaidi kwa kurejelea kuiweka katika benki na kupokea riba.)

1.  Hiyo inatufundisha nini juu ya mahali tunapopokea thawabu yetu? (Kwa kuwa tunajua hii ilikuwa fedha, na alipewa mtu mwenye talanta kumi, tunaona kwamba alipata fedha nyingi zaidi. Kwa kuwa hatuwezi kwenda na fedha mbinguni, pendekezo lenye ushawishi zaidi, kwa mara nyingine, ni kwamba kwa sehemu fulani tunazungumzia thawabu zinazotujia hapa duniani.)

II.  Nuhu na Hapa Duniani

A.  Soma Waebrania 11:6. Uhusiano chanya na Mungu unahitaji nini? (Lazima tuamini kwamba Mungu yupo na kwamba anawapa thawabu wale wanaomtafuta.)

1.  Je, ni muhimu kupatia kwa usahihi sehemu ya “thawabu?” (Hii inatuambia kuwa ni muhimu sana! Imani impendezayo Mungu ni imani ya uwepo wake na kwamba anatoa thawabu.)

B.  Soma Waebrania 11:7. Kwa nini Nuhu alionywa juu ya mwisho wa ubinadamu unaokuja? (Kwa sababu alikuwa na imani.)

1.  Je, hii ni thawabu iliyotengwa kwa ajili ya mbingu? Ujio wa Mara ya Pili? (Hapana! Matokeo ya imani ya Nuhu ni kwa yeye kuonywa na kupewa fursa ya kujiokoa yeye na familia yake. Thawabu hii ilitokea hapa hapa duniani.)

III.  Ibrahimu na Hapa Duniani

A.  Soma Waebrania 11:8-9. “Urithi” gani unarejelewa hapa? (Nchi (ardhi)!)

B.  Soma Waebrania 11:10. Thawabu gani nyingine ilimvutia Ibrahimu? (Mbingu!)

C.  Soma Waebrania 11:11-12. Thawabu hii inatolewa wapi? (Hii ni thawabu iliyopo duniani. Thawabu ni kuwa na ardhi na uzao mwingi.)

D.  Soma Waebrania 11:13. Kifungu hiki kinaposema kuwa “wasijazipokea zile ahadi,” kinazungumzia jambo gani? (Kinazungumzia ahadi kwa ujumla wake. Ibrahimu aliishi katika nchi aliyoahidiwa na aliuona uzao mwingi. Lakini, kamwe hakuuona utimilifu kamili wa hii thawabu.)

1.  Tunaweza kuwaambia nini kwa ujasiri Wakristo wenye “uoni hafifu?” (Imani kwa Mungu, utii kwa Mungu, hutupatia thawabu wakati wa uhai wetu, baada ya uhai wetu, na mbinguni.)

IV.  Mateso Hapa Duniani

A.  Soma Waebrania 11:36-39. Je, watu hawa waaminifu walipokea thawabu hapa duniani? (Hapana. Biblia inatutaarifu kuwa hili linaweza kutokea. Ingawa kwa ujumla thawabu za Mungu hutujia kwa sehemu fulani katika kipindi cha maisha ya uaminifu, kwa sehemu nyingine thawabu hizo hazitujii hadi tufike mbinguni.)

1.  Litafakari hili. Kama mtu aliyekatwa vipande viwili kwa msumeno akisoma kile tulichojifunza hadi kufikia hapa, mtu huyo atakuwa na mjibizo (reaction) gani? (Ninahofia kuwa atakatishwa tamaa. Tunatakiwa kuwa makini kwa wale walio miongoni mwa kundi dogo wanaoonekana kuwa na thawabu mbinguni pekee.)

B.  Soma Waebrania 11:40. Inamaanisha nini kusema “ili wao wasikamilishwe pasipo sisi?” (Hii inatuambia kuwa waaminifu katika Agano la Kale walimtazamia Masihi aje na kuwapatia uzima wa milele. Hii inaunga mkono zaidi hitimisho kwamba sehemu ya muhimu ya thawabu ya uaminifu ni mbingu.)

1.  Je, kinyume chake ni kweli? Kwamba tofauti na Agano la Milele hatuwezi kufanywa kuwa wakamilifu? (Agano la Kale ni muhimu kwa ajili ya uelewa sahihi wa Mungu.)

C.  Soma Warumi 8:16-17. Hii inazungumzia mateso ya namna gani? Yesu alisulubiwa. Je, hicho ndicho kinachorejelewa?

D.  Soma Warumi 8:18-19. Je, vifungu hivi viwili vina uhusiano? Je, kifungu cha 19 kinaelezea aina ya mateso yanayorejelewa katika kifungu cha 18? (Nadhani vifungu hivi vinahusiana.)

E.  Soma Warumi 8:20-23. Mateso ya namna gani yanabainishwa hapa? (Haya ni mateso ambayo kila mtu anayapitia kama matokeo ya dhambi. Uumbaji wote unayapitia. Lakini yanaishia katika ujio wa Yesu Mara ya Pili.)

1.  Je, Yesu alijiingiza kwenye mateso ambayo sisi na uumbaji wote tunayapitia? (Ndiyo. Na kwa kuongezea, aliteseka kwa namna nyingine mbaya zaidi na kuishia katika mateso yenye maumivu makali wakati wa kifo chake.)

F.  Soma Warumi 8:28. Mungu anafanya nini pale tunapokabiliana na mateso? (Anayafanyia kazi kwa manufaa yetu.)

1.  Unadhani inawezekana kwamba Mungua anaandaa na kuweka mipangilio kabla kwa “manufaa yetu?” (Tafakari taswira pana. Sote tunateseka kwa sababu ya dhambi. Hata hivyo, Mungu kwa upendo wake alitupatia amri zake ili tuweze kuepuka kutenda dhambi na hivyo kuepuka matokeo ya kutenda dhambi.)

2.  Hiyo inazungumzia nini kuhusu uhusiano kati ya mateso na amri za Mungu? (Amri ni dawa ya kutukinga dhidi ya mateso. Kufuata kanuni za Mungu hutupatia thawabu sasa hivi hapa hapa duniani.)

G.  Rafiki, usiwe na uoni hafifu. Kwa kiasi kikubwa Mungu anawapa thawabu watu wake sasa hivi na mbinguni. Kwa nini usifanye uamuzi sasa hivi wa kudhamiria kuzifuata kanuni za Mungu na kufurahia thawabu za uaminifu zinazopatikana sasa hivi na baadaye!

V.  Juma lijalo: Tunaanza mfululizo mpya wa masomo unaoitwa, “Ujumbe kwa Ulimwengu.” Ikiwa ulimwengu unakukanganya zaidi na zaidi, masomo yetu yajayo yatasaidia kukufafanulia kinachoendelea.